Tume ya Madini yatembelea machimbo ya Mpwapwa

0

Mwenyekiti wa Tume ya Madini nchini Profesa Idris Kikula ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Afisa Madini na Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Dodoma kumaliza mgogoro kati ya wachimbaji wadogo na Mwekezaji kwenye machimbo ya Winza yaliyopo wilayani Mpwapwa, mgogoro uliodumu kwa takribani miaka Kumi.

Profesa Kikula ametoa muda huo baada ya kupata malalamiko ya
wachimbaji hao wadogo ya kushindwa kuendelea na shughuli za uchimbaji kutokana na mgogoro uliopo baina yao na mwekezaji katika eneo hilo, hali ambayo pia inaikosesha serikali mapato.

Wachimbaji hao wadogo wametoa malalamiko hayo kwenye Tume hiyo ya Madini nchini inayoongozwa na Profesa Kikula ambayo imefanya ziara katika machimbo mbalimbali wilayani Mpwapwa ili kujionea shughuli za uchimbaji wa madini na namna serikali inavyoweza kufaidika na shughuli hizo za uchimbaji.

Wakizungumza na wachimbaji hao, baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo ya madini nchini wamewashauri wachimbaji hao wadogo kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria wakati malalamiko yao yakifanyiwa kazi

Wajumbe wa Tume hiyo ya madini nchini wanaendelea na ziara yao katika wilaya za Mpwapwa na Kongwa mkoani Dodoma.

Japan yafuta mchezo wake dhidi ya Chile

0

Japan imefuta mchezo wake wa kirafiki dhidi ya Chile uliotakiwa kuchezwa Septemba Saba mwaka huu, kufuatia tetemeko la ardhi kukikumba kisiwa cha Hokkaido.

Mchezo huo wa kirafiki dhidi ya Chile ulitakuwa kuchezwa kwenye mji wa Sapporo Dome.

Chama Cha Soka cha Japan (JFA) kimesema kuwa kimefikiria kuhusu suala hilo na kuamua kuchukua maamuzi ya kuufuta mchezo huo.

Taarifa iliyotolewa na JFA imesema kuwa kutokana na tetemeko hilo la ardhi wameona ni vema kuufuta mchezo huo.

Rais wa JFA, -Tashima Kohzo amesema kuwa wote kwenye chama cha soka pamoja na wachezaji wamesikitishwa na tukio hilo na wapo pamoja na wakazi wa Hokkaido.

Mchezo dhidi ya Chile ungekuwa wa kwanza kwa kocha mpya wa timu ya Taifa ya Japan, – Hajime Moriyasu ambaye ameanza kuinoa timu hiyo mara baada ya kumalizika kwa michuano ya kombe la Dunia.

Japan pia imepanga kucheza mchezo mwingine dhidi ya Costa Rica Septemba kumi na moja mwaka huu kwenye mji wa Osaka.

Stars yajiandaa na mchezo wake dhidi ya Uganda

0

Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania, -Taifa Stars imewasili jijini Kampala nchini Uganda tayari kwa mchezo wao wa kufuzu kwa michuano ya Afrika dhidi ya timu ya Taifa ya nchi hiyo utakaochezwa siku ya Jumamosi Septemba Nane.

Msafara wa Taifa Stars una wachezaji 23 na makocha watatu wakiongozwa na kocha mkuu Emmanuel Amunike ambae mchezo dhidi ya Uganda utakuwa mchezo wake wa kwanza akiwa kocha wa timu hiyo.

Kikosi hicho cha Taifa Stars kina wachezaji tisa wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wakiongozwa na nahodha Mbwana Samatta anaecheza soka kwenye timu ya Genk ya Ubelgiji.

Akizungumza kabla ya kuondoka nchini, kocha Amunike amesema kuwa wanaenda Uganda huku wakiwa na matarajio ya kurejea na matokeo chanya ili kuweza kuibua matumaini ya kufuzu kwa michuano ya Afcon.

“Tuna hakika tutapata matokeo chanya kwenye mchezo huo wa Jumamosi dhidi ya Uganda na huo ndio mpango wetu” amesema Amunike.

Pia kocha huyo amesema kuwa amefurahi kuweza kuwa na wachezaji wote wanaocheza soka nje ya nchi na wale wanaocheza soka hapa nchini.

“Tunaenda Uganda kusaka ushindi, hivyo tutajitahidi kushambulia na wakati huohuo kulinda lango letu ili tusiruhusu kufungwa” amesema kocha huyo Mnigeria.

Kwa upande wake nahodha Mbwana Samatta amesema kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kwa sababu ni mchezo wa majirani, lakini wao wanenda kupambana ili kuibuka na ushindi.
“Kama nilivyosema huu ni mchezo wa majirani, hivyo lazima utakuwa mgumu na tunawajua wachezaji wa Uganda kwa sababu tumecheza nao mara nyingi na siku zote mchezo wetu dhidi yao unakuwa mgumu” amesema Samatta.

Pia Samatta amesema kuwa mipango yao sio kwa Uganda tu bali kwenye michezo yote ya kundi lao la L katika kufuzu kwa michuano ya Afrika ya mwaka 2019 itayofanyika huko nchini Cameroon.

Huu ni mchezo wa pili kwa Taifa Stars wa kufuzu kwa michuano hiyo ya Afcon baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja na Lesotho mwaka 2017 hapa nchini, hivyo Taifa Stars inatakiwa kushinda mchezo huo dhidi ya Uganda ili kuweza kuibua matumaini yao ya kufuzu kwa michuano hiyo ya Afcon.

Tanzania haijafuzu kwa muda mrefu michuano ya Afcon ambapo kwa mara ya kwanza na mwisho kufanya hivyo ilikuwa mwaka 1980 yaani miaka 38 iliyopita na sasa kocha Emmanuel Amunike ana kibarua kigumu cha kuipa mafanikio timu hiyo.

Tetemeko la ardhi laikumba Hokkaido

0

Tetemeko kubwa la ardhi limekikumba Kisiwa cha Hokkaido kilichopo Kaskazini mwa Japan na kuharibu makazi ya watu.

Vyombo vya habari katika kisiwa hicho vimeripoti kuwa watu wanane wamekufa na wengine arobaini hawajulikani walipo kutokana na tetemeko hilo.

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 6.7 kwenye kipimo cha mateteko, limesababisha kukatika kwa umeme kwenye nyumba milioni tatu baada ya kituo kikubwa cha kusambaza umeme kuharibiwa.

Tetemeko hilo la ardhi limetokea katika kisiwa hicho cha Hokkaido, siku chache baada ya kimbunga kikali cha Jebi kuyakumba maeneo mbalimbali ya Japan na kusababisha vifo vya watu kumi na kuharibu majengo kadhaa.

Askari 10 Sudan Kusini wahukumiwa kifungo jela

0

Mahakama ya Kijeshi ya Sudan Kusini imewahukumu kifungo cha kati ya miaka Saba na maisha jela, askari kumi wa nchi hiyo baada ya kupatikana na makosa ya kuwadhalilisha wafanyakazi wa kigeni wa kutoa msaada pamoja na mauaji ya mwandishi wa habari wa nchi hiyo.

Habari kutoka Sudan Kusini zinasema kuwa, askari hao walitenda makosa hayo mwaka 2016 baada ya kuvamia hoteli ya Terrain iliyopo katika mji wa Juba, ambapo wafanyakazi hao watano walidhalilishwa.

Mahakama hiyo pia imeagiza kulipwa fidia ya dola elfu nne za Kimarekani kwa kila muathirika wa tukio hilo na kuiagiza serikali kumlipa mmiliki wa hoteli hiyo Mike Woodward ambaye ni raia wa Uingereza zaidi ya dola milioni mbili za Kimarekani.

Wanadiplomasia mbalimbali pamoja na wafanyakazi kadhaa wa kutoa msaada walifika katika mahakama hiyo ya Kijeshi ya Sudan Kusini kusikiliza hukumu ya kesi hiyo.

Pompeo afanya ziara Pakistan

0

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, -Mike Pompeo amefanya ziara ya siku moja nchini Pakistan, ziara yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili.

Katika ziara hiyo Pompeo alitarajiwa kukutana na viongozi wa Pakistan akiwemo Waziri Mkuu Imran Khan ambaye ameingia madarakani hivi karibuni.

Ziara ya Pompeo nchini Pakistan imekuja siku chache baada ya serikali ya Marekani kusitisha msaada wa kijeshi wa zaidi ya Dola Bilioni moja za Kimarekani kwa Pakistan.

Hivi karibuni Marekani ilionesha nia ya kuimarisha uhusiano wake na Pakistan ambao umeendelea kuzorota huku Marekani ikiistutumu Pakistan kwa kushindwa kukabiliana na makundi mbalimbali ya kigaidi ambayo yanafanya shughuli zake nchini humo.

Kimbunga Jebi chaikumba Japan

0

Watu kumi wamekufa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya kimbunga Jebi kuyakumba maeneo mbalimbali nchini Japan.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Japan imesema kuwa kimbunga hicho ni kibaya kuwahi kutokea nchini humo ndani ya kipindi cha miaka 25.

Kimbunga hicho kimesababisha uharibifu mkubwa wa majengo na miundombinu hasa katika miji iliyo Magharibi mwa nchi hiyo ambayo ni pamoja na Kyoto na Osaka.

Habari zaidi kutoka nchini Japan zinasema kuwa njia za usafiri wa anga, treni na vivuko zilisitishwa kwa muda kuhofia madhara ya kimbunga hicho aina ya Jebi.

Hadi sasa zaidi ya watu Mia Tatu wamejeruhiwa kufuatia kimbunga hicho .

Vitabu vya kiada kuendelea kuchapishwa na kusambazwa

0

Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole-Nasha amesema kuwa serikali imejipanga kuchapisha na kusambaza vitabu zaidi ya Milioni Kumi vya kiada kwa shule za msingi nchini ikiwa ni jitihada za kutatua changamoto ya upungufu wa vitabu hivyo.

Akijibu swali bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri Ole-Nasha amesema kuwa tayari serikali imechapisha na kusambaza vitabu Milioni Kumi vya darasa la Kwanza hadi la Tatu na vitabu Elfu Nne vya darasa la Nne.

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dkt Hussein Mwinyi ameliambia Bunge kuwa katika kukabiliana na changamoto ya idadi ndogo ya vijana wanaojiunga na mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa, serikali imejenga kambi mpya ya mafunzo itakayochukua idadi kubwa ya vijana ikilinganisha na siku za nyuma.

Bunge linaendelea na mkutano wake wa Kumi na Mbili jijini Dodoma.