Rais John Magufuli ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Lamadi na kufungua barabara za mji wa Lamadi katika wilaya ya Busega mkoani Simiyu ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani humo.
Akiwa katika mkoa huo wa Simiyu, Rais Magufuli pia amefungua jengo la wagonjwa wa nje la hospitali ya rufaa ya mkoa huo na ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Maswa – Bariadi.
Mradi wa maji wa Lamadi utakaozalisha lita milioni 3.3 za maji kwa siku ambayo ni mara mbili ya mahitaji ya lita milioni 1.8 ya wakazi wa mji huo kwa sasa, utatatua kero ya miaka mingi ya uhaba wa maji kwa wakazi hao ambao kwa sasa wanapata maji kwa asilimia 23 tu ya mahitaji yao.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa amemueleza Rais Magufuli kuwa ujenzi wa mradi huo ambao umepangwa kukamilika mwezi Mei mwaka 2019, utagharimu shilingi bilioni 12.83 na ni sehemu ya mpango wa uboreshaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira wa ziwa Victoria unaotekelezwa katika miji ya Mwanza, Musoma, Bukoba, Magu, Misungwi na Lamadi kwa gharama ya shilingi bilioni 276.
Fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo zimetolewa kwa mkopo nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Serikali ya Tanzania.
Nao ujenzi wa barabara za mji wa Lamadi zenye jumla ya kilomita 6.26 umegharimu shilingi bilioni 9.192 ambapo barabara hizo zimewekewa taa, mifereji, njia za waenda kwa miguu na eneo la kuegesha magari lenye ukubwa wa mita 900.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amemueleza Rais Magufuli kuwa pamoja na barabara hizo, serikali itajenga kituo cha mabasi na kilomita nyingine 1.5 za barabara, kununua gari la taka na kuandaa ramani ya mpango mji katika mji wa Lamadi kwa gharama ya shilingi Bilioni 6.47 na kwamba mradi kama huo unatekelezwa katika miji mingine 17 hapa nchini kwa gharama ya shilingi bilioni 561 ikiwa ni fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia.
Jengo la wagonjwa wa nje la hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Simiyu limejengwa katika eneo la Nyaumata kwa ghamara ya shilingi Bilioni 1.8 na ni sehemu ya mradi mzima wa ujenzi wa miundombinu ya hospitali hiyo uliopangwa kugharimu shilingi Bilioni 11.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa serikali imetenga shilingi bilioni Tatu kwa ajili ya kujenga miundombinu mingine ya hospitali hiyo katika kipindi cha miezi Sita na kwa kuunga mkono ukamilishaji wa haraka wa hospitali hiyo Rais Magufuli ameahidi kuongeza fedha nyingine shilingi bilioni 4.
Ujenzi wa barabara ya Maswa – Bariadi yenye urefu wa kilomita 49.7 utagharimu shilingi bilioni 88.877 na barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Mwigumbi – Maswa – Bariadi – Lamadi yenye urefu wa kilomita 171.8.
Akizungumza katika miradi hiyo Rais Magufuli amezishukuru taasisi zote za kimataifa zilizotoa mikopo nafuu kwa Tanzania kwa lengo la kufanikisha miradi hiyo na ameahidi kuwa serikali itahakikisha miradi hiyo inatekelezwa vizuri na inaleta manufaa yanayotarajiwa kwa wananchi.
Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Simiyu kwa kupata miradi hiyo na ametoa wito kwa Watanzania wote kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kuwaletea maendeleo, ikiwa ni pamoja na kulipa kodi kwa kuwa fedha za kugharamia miradi hiyo zinatokana na kodi zao.
Amempongeza mkuu wa mkoa wa Simiyu,- Anthony Mtaka, viongozi na wakulima wa mkoa wa Simiyu kwa juhudi kubwa walizofanya katika kuongeza uzalishaji wa zao la pamba ambapo katika msimu uliopita kati ya kilo milioni 226 zilizozalishwa nchini, kilo milioni 120 zimezalishwa katika mkoa wa Simiyu.