Ajali ya ndege yaua 19 Sudan Kusini

0

Watu 19 wamekufa baada ya ndege ndogo ya abiria kuanguka kwenye ziwa Yirol wakati ikijaribu kutua huko Sudan Kusini.

Watu wanne tu, wawili wakiwa watoto wamenusurika katika ajali hiyo.

Habari kutoka Sudan Kusini zinasema kuwa wakati ajali hiyo inatokea, ndege hiyo ilikua na watu 23 ambao ni wafanyakazi pamoja na abiria.

Ndege hiyo ndogo ilikua ikisafiri kutoka mji wa Juba kuelekea mji wa Yirol na chanzo cha ajali hiyo kinaelezwa kuwa ni hali mbaya ya hewa kwani kulikua na ukungu.

Rubani wa ndege hiyo alijaribu kutua katika eneo salama ikashindikana na badala yake ndege hiyo ikaanguka katika ziwa Yirol eneo ambalo ni karibu na mji wa Yirol ambapo ndege hiyo ilitakiwa itue.

Mmiliki wa lori lililosababisha ajali Mbeya kukamatwa

0

Serikali imeagiza kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, mmiliki wa lori lililosababisha ajali hivi karibuni mkoani Mbeya na kusababisha vifo vya watu Kumi na Watano na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Agizo hilo la serikali limetolewa mkoani Mbeya na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Yusuf Masauni alipotembelea eneo ilipotokea ajali hiyo.

Katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo lenye mteremko la mlima wa Igawilo, lori hilo linadaiwa kupata hitilafu katika mfumo wa breki na kusababisha kuyagonga magari mengine matano.

Lori hilo ni mali ya kampuni ya Azania Group.

Mhandisi Masauni amesema kuwa serikali haiko tayari kuona magari mabovu yanatembea barabarani na kusababisha vifo wakati wamiliki wake hawachukuliwi hatua zozote.

Katika ziara yake ya kutembelea eneo hilo la ajali mkoani Mbeya, Naibu Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ya Nchi aliongozana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elias Kwandikwa.

Upotevu wa dawa wamkera Naibu waziri

0

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile ameiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Nachingea mkoani Lindi, Mganga Mkuu wa Mkoa pamoja na wa wilaya kufanya uhakiki wa dawa katika hospitali ya wilaya ya Nachingwea.

Dkt Ndugulile ametoa agizo hilo baada ya kutembelea hospitali hiyo na kubaini mapungufu katika usimamizi wa dawa na kusababisha dawa nyingi kupotea.

Amesema kuwa changamoto ya upotevu wa dawa si kwa wilaya ya Nachingwea pekee, bali ni kwa wilaya nyingi zilizopo maeneo ya pembezoni.

Akisoma taarifa yake kwa Dkt Ndugulile, Mkuu wa wilaya ya Nachingwea, -Rukia Muwango amesema kuwa tayari wilaya hiyo imepokea fedha kwa ajili maboresho ya vituo vya afya na hospitali ya wilaya.

Akiwa katika wilaya hiyo ya Nachingwea, Naibu Waziri huyo wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amehitimisha kampeni ya upimaji wa virusi vya Ukimwi kwa ngazi ya wilaya na kutumia nafasi hiyo kuagiza mikoa na wilaya ambazo bado hazijafanya kampeni hiyo kufanya mara moja.

Serikali kuendelea kushirikiana na madhehebu ya dini

0

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali inatambua mchango wa madhehebu ya dini katika kuwaletea Watanzania maendeleo.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa sherehe za kusimikwa wakfu Askofu Mkuu Msaidizi pamoja na Maaskofu wanne wa majimbo wa Kanisa la Pentekoste Motomoto,- Mwanga mkoani Kigoma.

“Serikali imeweka mazingira rafiki kwa madhehebu ya dini nchini kuweza kutoa huduma za kijamii hususan elimu na afya” amesema Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kanisa kujiepusha na migogoro ya kiutawala ndani ya Kanisa na pia liepuke kuchanganya dini na siasa.

“Kazi kubwa ya Kanisa iwe kuhubiri amani kwa waumini wake na wananchi kwa jumla” amesema Makamu wa Rais huku akinukuu neno la Mungu katika Waebrania 12:14 ambalo linasema “tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote”.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza kuwa eneo jingine ambalo serikali inalitegemea Kanisa ni katika kujenga maadaili mema ya jamii, hivyo ameliomba Kanisa hilo kusaidiana na serikali katika kupiga vita tamaduni zisizofaa ili kujenga Taifa lenye maadili ya Kitanzania.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa hilo la Pentekoste Motomoto,- Mwanga mkoani Kigoma, -Ezra Mtamya ameipongeza serikali kwa juhudi zake za kuijenga Tanzania yenye maendeleo na kwamba kama Kanisa wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya jamii na utunzaji wa mazingira.

Ameiomba serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kuwapatia wataalam wa mazingira pamoja na wale wa ufugaji nyuki ili waweze kuwaelekeza njia bora za utunzaji wa mazingira na ufugaji nyuki.

Watumishi wa afya watakiwa kuendelea kufanya kazi

0

Serikali imewataka watumishi wa sekta ya afya nchini kuendelea kufanyakazi ya kuwatumikia Watanzania kwa upendo wakati ikiendelea kushughulikia matatizo yao mbalimbali.

 

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Rais John  Magufuli katika  hospitali ya wilaya Meatu mkoani Simiyu ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani humo yenye lengo la kukagua na kuzindua miradi mbalimbali pamoja na kuzungumza na wakazi wa mkoa huo.

 

Amesema kuwa serikali kwa upande wake inaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ya watumishi hao wa sekta ya afya nchini ikiwa ni pamoja na kuongeza vitendeakazi  na kuongeza watumishi zaidi.

 

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, serikali pia italipa madai yote halali wanayodai watumishi hao wa sekta ya afya nchini.

 

Akiwa katika hospitali hiyo ya wilaya ya Meatu, Rais Magufuli pia amewashukuru wadau wote wa sekta ya afya ambao wamekua wakishirikiana na serikali katika kusogeza karibu na Wananchi huduma bora za afya.

 

Rais Magufuli bado anaendelea na ziara yake katika mkoa huo wa Simiyu.

Wasira na Limbu wateuliwa

0

Rais John Magufuli amemteua Stephen Wasira kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Wasira anachukua nafasi ya Profesa Mark Mwandosya.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amemteua Dkt Festus Limbu kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Dkt Limbu anachukua nafasi ya Dkt John Jingu ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Uteuzi wa viongozi hao umeanza Septemba Tisa mwaka huu.

Queen Elizabeth Miss Tanzania 2018

0

Mrembo Queen Elizabeth Makune ambaye ni Mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo cha Uhasibu kutoka jijini Dar es salaam amevikwa Taji la Miss Tanzania baada ya kuwabwaga warembo wengine katika shindano lililofanyika Septemba Nane mwaka huu.

Kufuatia ushindi huo, Queen Elizabeth ataungana na warembo wengine kutoka sehemu mbalimbali duniani kushiriki shindano kubwa la urembo la Dunia yaani Miss World litakalofanyika huko Sanya nchini China Disemba Nane mwaka huu.

Warembo walioingia Tano bora katika kinyang’anyiro hicho ni Queen Elizabeth Makune kutoka Dar es salaam, Nelly Kalikanzi kutoka Dar es salaam, Linda Samson kutoka Dar es salaam, Sandra Loren kutoka Kanda ya Kaskazini na Sharon Headlam kutoka Kanda ya Ziwa.

Washiriki wa shindano hilo ambalo mgeni rasmi alikua Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe walionesha aina mbalimbali ya mavazi likiwemo lile la kanga na la ubunifu.

Kinyang’anyiro hicho kilishirikisha walimbwende Ishirini kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Makamu wa Rais aanza ziara Kigoma

0

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameanza ziara ya kikazi ya siku Nne mkoani Kigoma.

Katika siku yake ya kwanza ya ziara hiyo, Makamu wa Rais amepokea taarifa ya maendeleo ya mkoa wa Kigoma iliyosomwa na Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga .

Akiwa mkoani Kigoma pamoja na mambo mengine, Makamu wa Rais atatembelea na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile ya afya, elimu na mazingira.

Jumapili Septemba Tisa, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan atashiriki sherehe za kuwekwa wakfu Askofu Mkuu Msaidizi na Maskofu Wanne wa majimbo katika Kanisa la Pentekoste Mwanga lililopo katika Manispaa ya Kigoma – Ujiji.