Katuni inayomkejeli Serena yazua zogo

0

Umoja wa kitaifa wa waandishi wa habari weusi nchini Marekani umeilaani vikali katuni iliyochapwa na gazeti la Herald Sun la Australia jana Jumatatu, iliyomchora katika namna ya kuchekesha mcheza tennis nyota duniani, Serena Williams, alipokuwa akimshambulia kwa maneno ‘umpire’ Carlos Ramos, katika mchezo wake na Naomi Osaka, Jumamosi iliyopita.

Umoja huo umesema katuni hiyo imebeba ubaguzi wa rangi na ukandamizaji wa kijinsia dhidi ya wanawake (sexism), tuhuma ambazo pia zilitamkwa na Serena wakati akimshambulia Ramos.

Katuni huyo imemchora Serena akiwa na umbo linalochekesha, huku akiruka ruka karibu na ‘racket’ iliyovunjika, ambapo pia mdomo wake ulikuwa umekuzwa na kuwa mkubwa na pua yake ikifanana na michoro iliyokuwa ikiwabagua watu weusi nchini marekani miaka ya zamani.

Mpinzani wa Serena katika mchezo huo Naomi Osaka amechorwa akiwa mwembamba kupita kiasi na akimsikiliza Ramos anayemwambia “kwa nini usimwachie ashinde tu?”

Katuni hiyo ‘imeshambuliwa’ huko Marekani baada ya baadhi ya watu nchini Australia kuisambaza katika mitandao ya jamii. Imeelezwa kuwa washabiki wa Serena walioko nchini Australia pia wameilaani vikali katuni hiyo.

Hata hivyo katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne, gazeti la Herald sun limesema kuwa katuni hiyo haikubeba dhana zozote za ubaguzi wa rangi wala jinsia.

Shilingi Milioni Mia tatu zakusanywa kwa mwezi mmoja

0

Zaidi ya shilingi milioni mia tatu zimekusanywa jijini Dar Es Salaam katika kipindi cha mwezi mmoja ikiwa ni faini kutoka kwa watu waliokutwa na makosa ya uchafuzi wa mazingira.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa usafi wa mazingira Mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda amesema zoezi la usafi si la mkuu wa mkoa bali ni la kila mkazi wa jiji hilo.

Makonda amewaambia wadau wa usafi kwamba hali ya usafi imeimarika na kusema zaidi ya watu 11,000 wamepatikana na makosa yanayohusu uchafu wa mazingira.

Aidha wadau wa uzoaji taka wamekubali hoja ya kuzoa taka nyakati za usiku.

Kigoma watakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya Ebola

0

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wakazi wa mkoa wa Kigoma hususani wanaoishi katika maeneo ya mipakani na mwambao wa ziwa Tanganyika kuchukua tahadhari za kiusalama dhidi ya ugonjwa wa Ebola.

Akizungumza kwenye mikutano ya hadhara katika kata za Mwakizega na Kazuramimba wilayani Uvinza mkoani Kigoma,  Makamu wa Rais pamoja na mambo mengine  amewataka wakazi hao kuacha tabia ya kupokea na kuwahifadhi wageni kutoka nchi jirani.

Kuhusu lishe Makamu wa Rais amewataka watendaji wa sekta ya afya pamoja na wazazi hususani akina mama  kutimiza wajibu wao.

Aidha Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wavuvi na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi katika ziwa Tanganyika kujiunga kwenye vikundi  ili kuunganisha nguvu katika uendelezaji wa shughuli zao.

Katika wilaya ya UVINZA Makamu wa Rasi pia amekagua mradi wa ukarabati wa kituo cha afya cha Uvinza.

Katibu Mkuu Wizara ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatama ametumia fursa ya ziara ya Makamu wa Rais mkoani Simiyu, kutangaza kuanza kwa oparesheni ya kuwasaka wavuvi haramu katika ziwa Tanganyika.

Serena atozwa faini Dola 17,000 za Marekani

0

Nyota wa mchezo wa Tennis duniani mkongwe Serena Williams ametakiwa kulipa faini ya dola za Marekani 17,000 sawa na zaidi ya Shilingi milioni 38 kwa makosa mbali mbali aliyoyafanya usiku wa juzi jumamosi Septemba 08 kwenye mchezo wa fainali ya mashindano ya wazi ya marekani (US OPEN) dhidi ya Mjapani Naomi Osaka.

Faini hiyo inahusu makosa kadhaa ikiwemo lile la kumuita mwamuzi wa mchezo huo muongo na mwizi wa alama zake, kupokea maelekezo kutoka kwa kocha wake wakati mchezo ukiendelea kinyume cha sheria za mchezo huo pamoja na kuvunja ‘racket’ yake kwa makusudi wakati wa mchezo.

SERENA alionekana kujawa na jazba hasa baada ya muamuzi Umpire kumkata alama katika mchezo huo dhidi ya Naomi ambapo alipoteza kwa kipigo cha seti mbili kwa bila za ushindi wa 6-2 na 6-6 hivyo kumfanya Naomi kushinda Grand Slam yake ya kwanza kutoka kwenye mikono ya aliyekuwa Role Model wake.

Ushindi wa Naomi mbele ya Serena unamfanya kupanda katika viwango vya ubora kutoka nafasi ya 19 aliyokuwepo awali hadi nafasi ya 7 huku nyota wa zamani wa mchezo huo kutoka nchini Japan Kimiko Date akisema Mjapan mwenzake huyo anastahili kuwa nambari moja kwenye viwango vya ubora kwa sasa.

Mane,Salah waafrika pekee kikosi cha FIFA

0

Sadio Mane wa Senegal na Mohammed Salah wa Misri ni wachezaji wawili pekee kutoka barani Afrika waliotajwa kwenye orodha ya wachezaji 55 wanaowania nafasi ya nyota 11 watakaounda kikosi bora cha shirikisho la soka duniani FIFA.

Nyota hao wanaocheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Liverpool msimu uliopita walicheza fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya dhidi ya Real Madrid lakini pia waliyawakilisha mataifa yao kwenye fainali za kombe la FIFA la dunia huko Russia ingawa mataifa yao hayakufanya vizuri.

Katika orodha hiyo mabingwa wa dunia Ufaransa wameingiza wachezaji Saba ambao ni Antoine Griezmann, N’golo Kante , Kylian Mbappe, Benjamin Pavard, Paul Pogba, Samuel Umtiti na Raphael Varane huku England ikiwa na wachezaji watatu akiwemo mfungaji bora wa kombe la FIFA la dunia Harry Kane.

Mshambuliaji wa mabingwa wa ulaya Real Madrid, Gareth Bale, hayupo kwenye orodha hiyo licha ya kufunga mabao mawili kwenye mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya dhidi ya Liverpool huku Cristiano Ronaldo aliyetimkia Juventus na mlinda mlango Thibaut Courtois aliyejiunga na Madrid akitokea Chelsea wakiingia kwenye orodha hiyo.

Orodha hiyo imepatikana baada ya majumuisho ya kura zilizopigwa na wachezaji 25,000 kutoka mataifa 65 duniani na orodha ya mwisho itakayotoa wachezaji 11 watakaounda kikosi cha bora cha FIFA itatangazwa September 24 jijini London wakati wa hafla ya utoaji tuzo ya mwanasoka bora wa dunia wa FIFA.

Rais Magufuli ataka ujenzi wa daraja ukamilike kwa wakati

0

Rais Dkt. John Magufuli amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya Hainan kutoka China kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi wa daraja la mto Sibiti ambalo linaunganisha mikoa ya Singida na Simiyu na kuondoa adha wanayopata wananchi hasa kipindi cha mvua.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa daraja la mto Sibiti baada ya kutoridhika na maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo.

Hadi sasa daraja hilo limechukua zaidi ya miaka sita kukamilika licha ya mkandarasi kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya gharama za ujenzi wa daraja hilo ambalo ujenzi wake unagharimu shilingi za kitanzania Bilioni 16.

Rais Magufuli pia amewaagiza watendaji wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano kumsimamia mkandarasi huyo ili akamilishe ujenzi huo kabla ya mwezi Machi mwakani na kama mkandarasi atashindwa kukamilisha kazi hiyo kwa muda uliopangwa basi atachukua hatua zaidi dhidi ya wahusika akiwemo mkandarasi huyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe na Mkuu wa mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi wamesema  daraja hilo ni mkombozi kwa wananchi wa mikoa ya Singida na Simiyu katika uimarishaji wa shughuli za kiuchumi kwenda ukanda huo.

Utalii wa ndege waongezeka msitu wa Amani

0

Idadi ya watalii wanaokwenda kutazama ndege katika hifadhi ya Msitu wa Amani wenye aina za ndege zaidi ya 400 uliopo Muheza Tanga, imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, huku aina ya ndege inayovutia watalii wengi ikiwa ni ‘Kolokolo Domorefu’.

Akizungumza na TBC Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo Mwanaidi Kijazi amesema katikati ya mwaka jana na mwaka huu watalii 782 wamefika hifadhini hapo ambapo zaidi ya 200 kati yao walifika kwa ajili ya kutazama ndege hao adimu duniani na inaosemekana kuwa wapo katika hatari ya kutoweka.

Kutokana na hofu ya kutoweka kwa ndege hao serikali na wadau wa maendeleo ikiwemo taasisi ya Nature Tanzania wamezindua mradi maalum wa kumhifadhi ndege huyo.

Baadhi ya washiriki wa uzinduzi wa mradi huo wamesema kuwa watalii wengi hufika ili kukata kiu ya kumuona ndege huyo kabla hajatoweka duniani.

Imeelezwa kuwa aina nyingine ya ndege inayovutia watalii wengi ni Flamingo, huku ikielezwa kuwa Flamingo wote waliopo katika bara la Afrika asili yao ni Tanzania.

BONDIA ALIEMPIGA MZUNGU ASEMA BADO ANASAKA MAFANIKIO

0

Bondia Mtanzania, Hassan Mwakinyo alieshinda pambano lake huko nchini Uingereza dhidi ya Bondia, Sam Eggington amesema kiu yake ya mafanikio ndio imnayomfanya afanye vizuri kwenye pambano hilo.

Akizungumza na TBC toka jijini Birmingham nchini Uingereza, Hassan Mwakinyo amesema siku  zote yeye ni mtu wa kujituma na anataka kufanikiwa na ndio maana alipopata nafasi hiyo ya kwenda kucheza pambano hilo akajianda vizuri na kutotaka kuipoteza nafasi hiyo.

Meneja wa bondia huyo Rashid Nassoro amesema mteja wake alipata nafasi hiyo ya kwenda kucheza pambano nchini Uingereza baada ya mapromoto wa ngumi kumuona bondia wake kupitia mtandao.

Bondia huyo alimpiga bondia Muingereza, Sam Eggington kwenye raundi la pili ya pambano hilo na kumtengenezea sifa kem kem kwa watanzania na wapenda masumbwi kwa ujumla.