Wasomi waelezea msimamo wa Marekani dhidi ya ICC

0

Wasomi mbalimbali nchini wamepokea kwa mtazamo tofauti hatua ya Marekani ya kutishia kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu – ICC endapo itawashitaki askari wake wanaodaiwa kufanya vitendo vya uhalifu nchini Afghanstan.

Miongoni wa wasomi hao ni Profesa wa sheria  kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Chris Peter Maina na mhadhiri wa chuo cha Diplomasia, – Abbas Mwalimu.

Profesa Maina ambaye amekuwa katika kamisheni mbalimbali za sheria za kimataifa amesema kuwa haoni nguvu yoyote ya Marekani katika kuathiri utendaji kazi wa ICC.

Naye Abbas Mwalimu ameukosoa uamuzi huo wa Marekani na kusema kuwa kuna umuhimu kwa mahakama hiyo ikaangalia upya hasa katika kipindi hiki ambacho haiungwi mkono na mataifa mengi hasa yale makubwa.

Hivi karibuni Marekani ambayo ni moja ya nchi ambazo haiiungi mkono mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu imetishia kuweka vikwazo dhidi ya mahakama hiyo endapo itaendelea na mikakati yake ya kuwashtaki raia wa nchi hiyo.

Mshauri wa masuala ya usalama ya kitaifa wa Marekani, -John Bolton amedai kuwa ICC  sio halali na kuapa kuwa nchi hiyo itafanya kila liwezekanalo kuwalinda raia wake.

Mahakama hiyo  ya Kimataifa ya Uhalifu  ambayo makao makuu yake yapo The Hague nchini Uholanzi, kwa sasa inafanya tathmini ili kuwafungulia mashtaka askari wa Marekani kwa madai ya kuwatesa wafungwa nchini Afghanistan.

 

Waliokufa Afghanistan wafikia 68

0

Idadi ya watu waliokufa baaada ya kutokea kwa shambulio la kujitoa muhanga nchini Afghanistan imeongezeka na kufikia 68.

Polisi nchini Afghanistan  wamesema kuwa shambulio hilo ambalo limetokea katika jimbo la Nangarhar lililopo karibu na Pakistan ni baya kuwahi kutokea katika miezi ya karibuni nchini humo.

Katika tukio hilo watu wengine 165 wamejeruhiwa.

Mpaka  sasa hakuna kikundi chochote kilichodai kuhusika na shambulio hilo la kujitoa muhanga, lakini inadhaniwa kuwa wanamgambo wa Kiislam ndio wametekeleza tukio hilo kwa kuwa wamekua wakifanya mashambulio mengi ya kujitoa muhanga katika jimbo hilo.

Mamia ya raia wa Afghanistan wameuawa katika mashambulio yaliyotokea kwenye kipindi hiki ambacho nchi hiyo inajiandaa kufanya uchaguzi wa Wabunge mwezi Oktoba mwaka huu.

Serikali ya Afghanistan  imeonya kuwa mashambulio mengi yatatokea katika mikutano mbalimbali ya kampeni, hivyo ni muhimu kwa raia wa nchi hiyo kuchukua tahadhari.

 

Sheria mpya kuanza kutumika Morocco

0

Sheria mpya ambayo inafanya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia kuwa ni uhalifu itaanza kutumika nchini Morocco hivi karibuni.

Sheria hiyo ambayo inajumuisha upigaji marufuku wa ndoa za kulazimishwa,  inafuatia kuongezeka  kwa vitendo  vya udhalilishaji dhidi ya wanawake katika miaka ya hivi karibuni.

Habari  kutoka nchini Morocco zinasema kuwa wanawake Sita kati ya Kumi wa nchi hiyo wamepitia vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji.

Chini ya sheria hiyo, watu wote watakaotiwa hatiani kwa makosa ya kudhalilisha iwe kwa kutumia maneno  ama ishara yoyote atakabiliwa na hukumu ya kifungo cha kuanzia mwezi mmoja hadi Sita jela na pia faini ya fedha taslimu.

Baadhi ya raia wa Morocco wamepongeza hatua ya kuwepo kwa sheria hiyo mpya huku wengine wakiikosoa kwa madai kuwa haitoi maana kamili ya unyanyasaji majumbani au marufuku katika vitendo vya udhalilishaji ndani ya ndoa.

Katika taarifa yake ya mwaka 2015, Shirika la Haki za Binadamu nchini Morocco lilisema kuwa zaidi ya asilimia Ishirini ya wanawake nchini humo wamekumbwa na matukio ya udhalilishaji japo mara moja katika maisha yao.

Serikali yajipanga kutekeleza ahadi zake

0

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali ya awamu ya tano imejipanga kutekeleza ahadi zake na kuwatahadharisha wananchi kuwa macho na matapeli wanaopita vijijini kuchangisha fedha kwa madai ya kuwapa kipaumbele katika mgao wa shilingi milioni hamsini kwa kila kijiji.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Muzeze wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.

Amesema fedha hizo hazijaanza kutolewa kutokana na kipaumbele kuelekezwa kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi.

Akiwa wilayani Buhigwe Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pia amezindua shamba la miti katika kijiji cha Muzeze na kuwataka watanzania kutunza mazingira.

Makamu wa Rais amehitimisha ziara yake ya siku nne mkoani Kigoma.

Mwili wa Annan waagwa Accra

0

Mwili wa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan unaagwa leo katika mji mkuu wa Ghana, Accra.

Mwili wa Annan uliwasili Jumatatu jioni katika uwanja wa ndege wa kimataifa ulioko mjini Accra ukitokea nchini Uswisi. Mazishi rasmi ya Annan yanatarajiwa kufanyika siku ya Alhamis wiki hii.

Annan alifariki dunia tarehe 18 Agosti mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Amefariki dunia nchini Uswisi akiwa na umri wa miaka 80 .

Polisi kusaka waganga wa jadi

0

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limetangaza kuanza msako dhidi ya waganga wa jadi wanaojihusisha na upigaji ramli chonganishi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana ametangaza msako huo kufuatia ongezeko la mauaji hususani ya wanawake yanayodaiwa kusababishwa na imani za kishirikina.

Kamanda Shana ametangaza msako huo alipokutana na wakuu wa polisi, wakuu wa upelelezi wa wilaya na wakuu wa vituo vya polisi mkoani humo.

Amesema msako huo utahusisha pia wanaotoa vibali kwa waganga hao huku akitangaza kiama kwa maofisa na askari polisi wanaodaiwa kuwabambikizia kesi wananchi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza amewataka askari polisi kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Shilingi Bilioni 8.6 kulipa fidia

0

Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 8.6 kulipa fidia wananchi wanaopisha upanuzi wa Ikulu ya Chamwino na Kiwanja cha Ndege cha Dodoma.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge katika mkutano na maafisa wa viwanja vya ndege na Wakala wa Majengo Nchini TBA.

Mkurugenzi Idara ya Miliki Wakala wa Majengo Nchini -TBA, Baltazari Kimanyamo amewahakikishia wakazi wa Chamwino kuwa hakuna atakaye chukuliwa ardhi yake bila kulipwa fidia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini – TAA, Richard Mayongela amesema kuna changamoto katika kiwanja hicho cha ndege hali inayosababisha ndege kushindwa kutua nyakati za usiku mkoani Dodoma.

Uhakiki wachelewesha nyongeza ya mishahara

0

Serikali imesema inatambua kuwa wafanyakazi wanahitaji nyongeza ya mishahara lakini zoezi hilo limekwama kutokana na zoezi la uhakiki la mwaka 2016/17 na kwamba kwa sasa wafanyakazi wanaingizwa kwenye kanzi data baada ya uhakiki.

Akijibu swali bungeni mjini Dodoma Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Anthony Mavunde amesema nyongeza ya mishahara itafanyika baada ya zoezi la kanzi data kukamilika.

Katika hatua nyingine Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama ameliambia Bunge kwamba serikali imekuwa ikitenga shilingi bilioni kumi na tano kwa ajili ya kufanya tafiti na kutoa ujuzi kwa wananchi ili kufanikiwa katika ujenzi wa viwanda.