Rais John Magufuli amewaapisha viongozi watatu aliowateua hivi karibuni.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi.
Viongozi walioapishwa ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt John Jingu, Balozi wa Tanzania nchini Uganda Dkt Aziz Mlima na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Diwani Athumani.
Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao Rais Magufuli amemuagiza Dkt Jingu kwa kushirikiana na viongozi wengine wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kufuatilia usajili na utendaji kazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali na kuhakikisha yanafanya kazi kwa kuzingatia sheria ambazo pamoja na mambo mengine zinayataka kuendesha shughuli zao kwa uwazi hususani masuala ya mapato na matumizi ya fedha za ufadhili wa shughuli zake.
Rais Magufuli pia amemtaka Balozi wa Tanzania nchini Uganda Dkt Mlima kusimamia vizuri ushirikiano wa Tanzania na Uganda hasa biashara na uwekezaji unaoendelea kati ya nchi hizo mbili na kuhakikisha Tanzania inanufaika na ushirikiano huo.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, – Diwani Athumani, Rais Magufuli amemuagiza kuongeza kasi ya kushughulikia tatizo la rushwa nchini kwa kuhakikisha wote wanaokabiliwa na tuhuma za kujihusisha na rushwa wanafikishwa mahakamani na sheria inachukua mkondo wake.
Rais Magufuli pia amemtaka Mkurugenzi Mkuu huyo wa TAKUKURU kuangalia upya muundo wa taasisi hiyo ili uweke bayana majukumu ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na kuhakikisha watendaji wa taasisi hiyo wanaoonekana kutofanya kazi kwa tija na kujihusisha na vitendo vya rushwa wanachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuondolewa kazini na kufikishwa mahakamani.
“Nataka ukaisafishe TAKUKURU, kuna baadhi ya wafanyakazi wa TAKUKURU wanajihusisha na rushwa, kawaondoe, nataka kuona TAKUKURU inashughulikia rushwa kwelikweli hasa rushwa kubwakubwa, ukipita huko vijijini wananchi wanateseka sana, wananyanyaswa na kuna dhuluma nyingi sana, na tatizo kubwa ni rushwa” amesisitiza Rais Magufuli.
Viongozi hao walioapishwa na Rais Magufuli pia wamekula kiapo cha uadilifu kwa watumishi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Harold Nsekela na baada ya viapo vyao wamemshukuru Rais kwa kuwateua na wamemuahidi kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na kwa kutanguliza maslahi ya Taifa.