Korea Kaskazini na Korea Kusini zafungua ofisi ya ushirika

0

Korea Kaskazini na Korea Kusini imefungua ofisi ya Ushirika ambayo itawaruhusu kuwasiliana mara kwa mara ikiwa ni mara ya kwanza tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ofisi hiyo ambayo ipo upande wa Kaskazini mwa mpaka wa nchi hizo itachukua wafanyakazi 20 kutoka kila upande.

Waziri wa Muungano huo Cho Myoung-Gyon amesema pande hizo mbili za KOREA zitaweza kujadiliana mambo mbali mbali wakati wote.

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-In na Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un watakutana wiki ijayo katika kilelele cha mkutano wa tatu.

Tangu Rais Donald Trump afanye mazungumzo na Kiongozi wa Korea Kaskazini mwezi June mwaka huu Korea imekubali kuacha matumizi ya nyuklia ambapo pia Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini amemuomba Rais Trump kukutana kwa mara ya pili.

Kenyatta apunguza kodi ya mafuta

0

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amekubali kupunguza kodi ya mafuta kwa asilimia nane.

Akihutubia taifa hilo Rais Kenyatta amesema amepunguza kodi hiyo kwa wafanyabiashara wote ili kuwawezesha kunufaika zaidi.

Takribani miaka miwili iliyopita Rais Kenyatta alipandisha kodi kwa wafanyabiashara wa mafuta nchini humo.

Mkutano wa 12 wa Bunge waahirishwa

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kuwa ndio mambo muhimu kwa Taifa kukua kiuchumi.

Akiahirisha mkutano wa 12 wa Bunge jijini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa vita ya kiuchumi alioianzisha Rais John Magufuli itafanikiwa endapo kutakuwa na mazingira ya amani na utulivu ambayo yataruhusu kufanyika kwa shughuli za kiuchumi.

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu amewahimiza Watanzania kutumia mvua za vuli zilizoanza kunyesha kwenye baadhi ya maeneo nchini kulima mazao mbalimbali ili kujitosheleza kwa chakula na kupata ziada.

Amesema kuwa kwa upande wake, serikali itahakikisha pembejeo zinawafikia wakulima, huku akiwasisitiza mawakala waliopewa dhamana ya kufikisha pembejeo kwa wakulima kuzifikisha kwa wakati.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, serikari pia itaendelea kusimamia vyama vya ushirika na kuhakikisha vinawanufaisha Watanzania na si kuwanyonya na kuonya kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa watu wote watakaobainika kufanya ubadhirifu katika vyama hivyo vya ushirika.

Bunge limeahirishwa hadi Novemba Sita mwaka huu.

Manchester City yasema safari yake haijakamilika

0

Mwenyekiti wa klabu ya Manchester City ya nchini England, – Khaldoon Al Mubarak amesema kuwa safari ya klabu hiyo bado haijakamilika licha ya kutoa taarifa ya mapato ya klabu hiyo yenye faida ya Pauni Milioni 500 kwa msimu uliopita.

Taarifa ya iliyotolewa na klabu hiyo imesema kuwa hadi kufikia June 30 mwaka huu, klabu hiyo imetengeza faida ya Pauni Milioni 500 zinazoifanya City kuwa klabu ya pili kwenye ligi ya England nyuma ya Manchester United kuweka rekodi ya kutengeza kiasi kikubwa cha fedha.
Taarifa hiyo pia inaonyesha kuwa huu ni msimu wa Nne mfululizo klabu hiyo inatengeneza faida ambapo kwa mwaka huu imepata faida ya Pauni Milioni 10.4 huku mapato yatokanayo na mishahara ikiwa ni asilimia 52.

Taarifa hiyo inakuja ikiwa miezi minne imepita tangu Man City watwae taji la ligi ya England wakiwa timu ya kwanza kuweka rekodi ya kuvuna alama 100 na Al Mubarak amesema kuwa safari haijakamilika kwa kuwa wana malengo makubwa zaidi huku wakihitajika kufanya vizuri kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya.

Real Madrid, Barcelona, Bayern Munich na Manchester United ndiyo vilabu vinavyotengeneza faida kubwa duniani kuliko Man City ambao wameongeza ukubwa wa uwanja wao wa Etihad kufikia uwezo wa kubebea watazamaji Elfu 55.

Tiketi za mpambano wa watani wa Jadi kuanza kuuzwa Septemba 20

0

Shirikisho Soka Nchini (TFF) limesema kuwa tiketi za mchezo baina ya watani wa jadi Simba na Yanga utakaopigwa Septemba 30 mwaka huu, zitaanza kuuzwa mapema ambapo kiingilio cha juu kwenye mtanange huo kikiwa ni Shilingi elfu 30 na cha chini kikiwa ni Shilingi elfu Saba.

Msemaji wa TFF Clifford Ndimbo amesema kuwa tiketi za mchezo huo utakaopigwa kwenye nyasi za dimba la Taifa jijini Dar es salaam zitaanza kuuzwa Septemba 20 huku kukiwa na taratibu mbalimbali za kuingia uwanjani zitakazosaidia kupunguza matatizo yanayoweza kujitokeza.

Watani wa jadi Simba na Yanga watakutana kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2018/2019, ambapo mara ya mwisho zilipokutana kwenye Ligi Kuu Yanga iliambulia kipigo cha bao moja kwa bila.

Vettel akiri adui yake ni yeye mwenyewe

0

Dereva wa kampuni ya Ferari,- Sebastian Vettel amesema kuwa adui yake mkubwa katika kinyang’anyiro cha kuwania taji la mbio za langalanga msimu huu baina yake na dereva wa Marcedes, – Lewis Hamilton ni yeye mwenyewe.

Vettel ambaye yupo alama 30 nyuma ya mpinzani wake Hamilton, amefanya makosa kadhaa msimu huu yaliyotoa faida kubwa kwa Marcedes na amesema bado ana nafasi ya kufanya vema kutokana na ubora wa kampuni ya Ferari inayoongoza kwa kuwa gari lenye kasi zaidi kwenye mbio za langalanga kulinganisha na Marcedes.

Mjerumani huyo amesema kuwa wapo kwenye nafasi nzuri ya kushinda na adui yao mkubwa ni wao wenyewe kama kampuni na si mtu mmoja kama watu wanavyofikiri na kinachohitajika ni umakini wakati wote wa mchezo ili kuepuka makosa yatakayotoa nafasi kwa wapinzani kushinda kama ilivyokuwa kwenye mashindano kadhaa yaliyopita.

Kwa upande wake bingwa mtetezi wa mbio za langalanga, Lewis Hamilton amesema kuwa ufundi wa kwenye usukani ndiyo utadhihirisha nani ni mkali na si maneno ya nje na kuongeza kuwa bado kuna alama nyingi kuelekea kwenye ubingwa.

Vettel na Hamilton ni wapinzani wakubwa kwenye mbio za langalanga na Vettel alianza vema msimu huu kabla ya Hamilton kuzinduka katika mashidano Matano yaliyopita ambapo ameshinda matatu na sasa kila mmoja anapambana kushinda mashindano yanayofuata ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kushinda taji la dunia.

Mnada wa mifugo Pugu Mnadani kuhamishwa

0

Serikali imewaruhusu wakazi wa Pugu Mnadani eneo la Bangulo jijini Dar es salaam kuendelea kuishi katika eneo hilo, na hivyo kumaliza mgogoro wa ardhi wa muda mrefu katika eneo hilo.

Msimamo huo umetolewa leo na mawaziri kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi wakati wa mkutano na wananchi wanaoishi eneo hilo, ili kumaliza mgogoro.

Waziri Mpina amesema serikali imeamua kuwamilikisha eneo hilo wananchi na kwamba itatafuta eneo lingine la kuweka mnada.

Naye waziri Lukuvi amewataka wakazi hao kurasimisha maeneo yao.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda alisema lengo lake ni kumaliza migogoro ya ardhi katika jiji la Dar es salaam ndani ya mwaka huu.

Eneo la Bangulo lililoko wilayani lipo chini ya umiliki wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo iliwamilikisha Tanganyika Parkers mwaka 1939 na kufanywa kuwa eneo la mnada na kuhifadhi Mifugo.

Pacha watano wazaliwa Afrika Kusini

0

Pacha watano wamezaliwa karibu na mji wa Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Watoto hao wamezaliwa katika wiki ya 30 ikiwa ni mapema kwa wiki 10.

Habari kutoka nchini Afrika Kusini zinasema hao ni pacha wa tano kuzaliwa nchini humo tangu mwaka 1960.

Kwa mujibu wa Dkt. Moeng Pitsoe watoto hao wamezaliwa wakiwa na zaidi ya kilo moja kila mmoja hali inayoashiria uwezekano mkubwa wa watoto hao kuendelea vizuri.

Watoto hao waliopewa majina ya Siyanda, Sibahle, Simesihle, Silindile na Sindisiwe wataruhusiwa kuondoka hospitali baada ya kufikisha uzito wa kilo mbili kila mtoto.