Ronaldo na Higuain wamaliza ukame wa magoli

0

Kwenye Seria A nchini Italia, nyota wawili Cristiano Ronaldo na Gonzalo Higuain wamemaliza ukame, baada ya kufunga kwa mara ya kwanza kwenye michezo yao ya ligi tangu kuanza kwa msimu huu.

Kwenye dimba la Allianz mjini Turin, mwanasoka bora duniani Cristiano Ronaldo amemaliza ukame wa mabao baada ya kufunga mabao mawili yaliyoipa Juventus ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Sassuolo.

Ronaldo alizitikisa nyavu katika dakika za 50 na 65 na kumaliza ukame wa kucheza michezo mitatu mfululizo ya ligi ya Seria A bila kufunga bao tangu ajiunge na kibibi kizee cha Turin, akitokea Real Madrid katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.

Huko Sardegna Arena, mshambulaiji mpya wa AC Milan, – Gonzalo Higuain na yeye amefunga goli la kwanza tangu ajiunge na miamba hiyo ya Italia na kufanikiwa kuipa sare ya bao moja kwa moja AC Milan mbele ya Cagliari.

Higuain ambaye hakufunga bao hata moja katika michezo yake miwili ya kwanza tangu atue San Siro kwa mkopo akitokea Juventus, aliisawazishia Milan katika dakika ya 55 baada ya Joao Pedro kuitanguliza Cagliari mapema katika dakika ya nne.

Alama hiyo moja waliyoipata AC Milan inawapandisha hadi katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Seria A wakiwa na alama nne katika michezo mitatu waliyocheza huku wakiwa na mchezo mmoja wa kiporo mkononi.

West Ham wapata ushindi dhidi ya Everton

0

Wagonga nyundo wa jiji la London, – West Ham United wamepata ushindi wa kwanza kwenye ligi ya England msimu huu, wakiwa chini ya kocha Manuel Pellegrini baada ya kuitandika Everton mabao matatu kwa moja kwenye dimba la Goodison Park.

Myukraine, – Andriy Yarmolenko aliifungia West Ham mabao mawili katika dakika za 11 na 31 kabla ya Marco Arnautovic kupigilia msumari wa mwisho katika dakika ya 61, huku bao pekee la kufutia machozi kwa Everton likifungwa na Gylfi Sigurdsson katika dakika ya 45.

Ushindi huo unamaliza ukame wa West Ham kucheza michezo Minne mfululizo bila kupata ushindi, na endapo wangepoteza mchezo huo wangeweka rekodi ya kuwa na mwanzo mbaya zaidi wa msimu katika klabu hiyo.

Katika matokeo mengine ya mchezo wa ligi ya England uliochezwa Septemba 16, Wolverhampton Wenderers wakiwa nyumbani wameibuka na ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Burnley na leo Septemba 17 utachezwa mchezo mmoja ambapo Southampton watakuwa nyumbani kwenye dimba la ST. Marys kuwakaribisha Brighton & Hove Albion.

Taasisi ya PCMC Health Care yawatembelea wagonjwa Vijibweni

0

Wakazi wa manispaa ya Kigamboni jijini Dar es salaam wameipongeza serikali kwa kufanya maboresho katika sekta ya afya, hasa huduma za mama na mtoto na hivyo kuwawezesha akina mama wengi kuwa na uhakika wa kujifungua salama.

Wakizungumza na Mwandishi wa TBC katika hospitali ya wilaya ya Kigamboni,- Vijibweni, walipotembelewa na Taasisi ya Madaktari bingwa ijulikanayo kama PCMC Health Care Limited, baadhi ya akina mama waliojifungua na wanaosubiria kujifungua hospitalini hapo wamesema kuwa uwajibikaji miongoni mwa wahudumu wa afya na upatikanaji wa dawa katika hospitali na vituo mbalimbali vya afya ni wa kuridhisha.

Madakari na wahudumu wa afya kutoka Taasisi hiyo ya PCMC Health Care Limited yenye makazi yake jijini Dar es salaam wamewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wazazi na watoto katika hospitali ya Vijibweni ikiwa ni moja ya njia ya kuonyesha upendo.
Kiongozi Mkuu wa Taasisi hiyo Richard Ulanga amesema kuwa suala la utoaji wa huduma za afya ni mtambua, hivyo halipaswi kuachiwa serikali pekee bali wadau wote wanatakiwa kushirikiana na serikali ili kufanikisha jambo hilo.

Ameongeza kuwa lengo la Taasisi hiyo ya PCMC Health Care Limited ni kutoa huduma bora za afya kwa Wananchi kwa kushirikiana na serikali.

Kwa mujibu wa Ulanga, kila mwaka taasisi hiyo imekua ikifanya matendo ya kihuruma ya utoaji huduma za upimaji afya bila malipo, kutembelea vituo mbalimbali vya watoto yatima, kutembelea wagonjwa waliolazwa katika hospitali mbalimbali na kuwapatia zawadi za aina tofauti.

Kwa upande wake Katibu wa afya wa hospitali hiyo ya wilaya ya Kigamboni,- Vijibweni, Bernard Makupa amesema kuwa pamoja na kujitahidi kutoa huduma bora za afya, lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya wagonjwa hasa wajawazito wanaofika hospitalini hapo kujifungua.

Nao baadhi ya akinana waliojifungua wamesema wamewashukuru madaktari na wauguzi wote kwa huduma nzuri waliyoipata.

Hospitali ya Vijibweni inazalisha wastani wa akina mama kumi hadi kumi na Watano kwa siku, ikiwa ni wastani wa akina mama Mia Tatu kwa mwezi.

Baraza Wawakilishi kukutana Septemba 19

0

Mkutano wa 11 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar unatarajiwa kuanza Septemba 19 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja, Katibu wa Baraza la Wawakilishi Raya Issa Msellem amesema kuwa wakati wa mkutano huo maswali 154 yataulizwa na kujibiwa.

Ameongeza kuwa miswada mitatu ya Sheria itawasilishwa katika Baraza hilo la Wawakilishi Zanzibar na kusomwa kwa mara ya kwanza.

CCM yaibuka kidedea katika majimbo ya Monduli na Ukonga

0

Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam Jumanne Shauri amemtangaza mgombea wa ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwita Waitara kuwa mshindi katika kinyang’anyiro hicho.

Waitara ameshinda baada ya kupata kura 77,795 ambazo ni sawa na asilimia 89.19.
Uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo hilo la Ukonga na jimbo la Monduli mkoani Arusha ulifanyika septemba 16 mwaka huu.

Katika jimbo la Monduli, CCM imeibuka kidedea katika uchaguzi huo mdogo ambapo mgombea wake Julius Kalanga ameshinda kwa asilimia 95.

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo la Monduli, – Steven Ulaya amesema kuwa Kalanga ameshinda kwa kupata kura 65, 714.

Magari yaonja Fly over Tazara

0

Magari yameanza kupita katika daraja la juu – Fly over eneo la TAZARA wilayani Ilala katika jiji la Dar Es Salaam.

Wakazi wa jiji hilo waliopata fursa ya kutumia barabara hiyo wameelezea furaha yao wakipongeza jitihada za serikali kuboresha miundombinu hapa nchini.

Wamesema kuanza kutumika kwa barabara hiyo ya juu kutapunguza foleni ya magari katika eneo hilo.

Barabara hiyo ya juu inatarajiwa kufunguliwa rasmi mwezi ujao.

Makamu wa Rais ataka bajeti kuadhimisha urithi wetu

0

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza wakuu wa mikoa nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kuadhimisha tamasha la urithi wetu ngazi ya mkoa ifikapo mwezi Septemba kila mwaka.

Amesema hayo katika uzinduzi wa tamasha hilo kitaifa jijini Dodoma, ambapo pia amewaagiza wakuu wa mikoa kuishirikisha sekta binafsi katika maadhimisho ya tamasha hilo.

Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Mali Asili na Utalii kulitangaza tamasha hilo kisheria na kutenga eneo maalum kitaifa kwa ajili ya tamasha hilo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Japhet Hasunga amebainisha kuwa mchango wa sekta ya utalii katika pato la taifa bado hautoshelezi.

Dhoruba zatishia maisha Ufilipino, Marekani

0

Serikali ya Ufilipino imeanza kuhamisha maelfu ya watu, kusambaza idadi kubwa ya wanajeshi na kuweka vituo vya huduma za dharura, ili kukabiliana na kimbunga cha ‘Mangkhut’, kinachotishia maisha ya watu takribani milioni 4, Kaskazini mwa nchi hiyo.

Kimbunga cha Mangkhut, ambacho ni kikubwa kuliko ‘Florence’ kinachoishambulia pwani ya Mashariki ya Marekani kwa sasa hivi, kinatarajiwa kutua katika kisiwa cha Luzon mapema kesho Jumamosi, ambapo kwa sasa kasi ya upepo ni kilomita 285 kwa saa.

Kimbunga hicho kilichotokana na dhoruba kali baharini, kimesababisha tahadhari kutolewa katika nchi zilizoko kwenye eneo lote la Mashariki na Kusini Mashariki mwa bara la Asia. Imeelezwa kuwa dhoruba ya pili iliyopewa jina la ‘Barijat’, pia imeshambulia eneo hilo.

Tayari Mangkhut imeharibu miundombinu huko Guam na visiwa vya Marshall vilivyoko katika bahari ya Pacific, na kusababisha mafuriko makubwa.

Hadi leo Ijumaa sehemu kadhaa za Guam zilikuwa bado hazina umeme.

Huko Marekani zaidi ya watu 100 wameokolewa kufuatia mafuriko yaliyotokana na kimbunga Florence katika mji wa New Bern, jimbo la North Carolina.

Taarifa zimesema kuna watu wengine wasiopungua 150 ambao bado wanasubiri kuokolewa kutoka kwenye maji.

Mji wa New Bern umefunikwa na maji kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

Mamlaka ya Hali ya hewa nchini Marekani imesema kuwa kimbunga hicho kitaleta mvua kubwa zaidi ya kuhatarisha maisha ya watu.