Viongozi wa Korea Kaskazini na Korea Kusini wakutana tena

0

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in amewasili Korea Kaskazini kwa ajili ya mkutano wake wa tatu na kiongozi Kim Jong Un wa Korea Kaskazini.

Akiwa nchini humo, Moon ameelezea matumaini yake ya kufufua mazungumzo ya Marekani yenye lengo la kuishinikiza Korea Kaskazini kuachana na silaha za nyuklia.

Ziara ya Moon pia inalenga kuziongezea nguvu jitihada za nchi yake za kuimarisha  uhusiano kati ya Korea ya Kusini na Korea Kaskazini.

Katika uwanja wa ndege wa Pyongyang, Moon na Kim walikumbatiana, kitendo kilichoshangiliwa  na umati wa raia wa Korea Kaskazini.

Kiongozi huyo wa Korea Kusini ameandamana na ujumbe mzito wa wafanyabiashara wakiwemo wakuu wa kampuni kubwa.

Marekani kupunguza idadi ya wahamiaji

0

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani, – Mike Pompeo amesema kuwa nchi hiyo ina mpango wa kupunguza idadi ya wahamiaji wanaoruhusiwa kuingia nchini humo ifikapo mwaka 2019.

Pompeo amesema kuwa idadi hiyo itapunguzwa kutoka wahamiaji elfu 45 kwa mwaka huu wa 2018 hadi kufikia elfu 30 mwaka 2019.

Kwa mujibu wa waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Marekani, idadi ya wahamiaji wanaoingia nchini humo inapunguzwa ili kutekeleza sheria mpya ya uhamiaji iliyoanza kutumika.

Dkt Bashiru aitembelea TBC

0

Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt Bashiru Ally amewashauri wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuhakikisha wanawaunganisha Watanzania.

Dkt Bashiru ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kwanza  kuifanya TBC akiwa na wadhifa huo ambapo ametembelea vitengo mbalimbali kwa lengo la kujionea utendaji kazi wa vitengo hivyo.

Akiwa TBC, pamoja na mambo mengine, Dkt Bashiru ameelezea kufurahishwa na hazina kubwa ya kumbukumbu katika maktaba ya shirika hilo.

Pia amewahimiza Watanzania wote kuungana badala ya kugawanyika na kuvitaka vyama vya siasa nchini vibadilike ili viondokane na kutawaliwa na wapenda anasa na vyeo.

Kuhusu wanaohamia CCM kutoka vyama vingine, Katibu Mkuu huyo wa CCM amesema kuwa wanavutiwa na utekelezaji wa ilani ya chama hicho kupitia huduma za jamii na mambo mengine mengi mazuri.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt Ayoub Rioba amesema kuwa ziara ya Dkt Bashiru TBC ni faraja kwa shirika hilo.

Ameongeza kuwa pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo TBC, ni wajibu wa shirika hilo kumulika matatizo ya Watanzania ili yapatiwe ufumbuzi.

Miili ya waliouawa Songwe yapatikana

0

Miili ya watu watatu wanaodaiwa kuuawa imepatikana kando ya Mto Mlowo wilaya ya Mbozi mkoani Songwe.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Songwe, – Mathias Nyange amewataja watu hao waliouawa kuwa ni Lucas Umri na mke wake Bahati Mohamed pamoja na mdogo wake maarufu kwa jina la mama Bina, ambapo inadaiwa watu waliotekeleza mauaji hayo walitumia vitu vizito.

Kamanda Nyange amesema kuwa ndugu mmoja wa marehemu hao ambaye walikuwa wanaishi naye ametoweka baada ya kutokea kwa mauaji hayo na kwamba jeshi la polisi mkoani Songwe linaendelea kumtafuta pamoja na kuendelea na upepelezi zaidi kuhusu tukio hilo.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Songwe, – Brigedia Jenerali Nichodemus Mwangela amewaomba wakazi wa mkoa huo kuwa watulivu wakati jeshi la polisi mkoani humo likiendelea na uchuguzi wake.

Pia ametoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa kuhusu mauaji hayo atoe taarifa hizo kwenye vyombo vya sheria.

Ligi ya mabingwa Barani Ulaya kutimua vumbi

0

Msimu mpya wa ligi ya mabingwa barani Ulaya unaanza kutimua vumbi usiku wa Septemba 18 kwa kupigwa michezo nane ya makundi Aaa mpaka Dee.

Katika michezo inayotazamiwa kuwa na mvuto mkubwa ni pamoja na ule utakaowakutanisha majogoo wa jiji Liverpool na Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa katika mchezo wa kundi Che.

PSG ina matumaini ya nyota wake NEYMAR kuanza kwenye mchezo huo baada ya kupumzishwa kwenye mchezo uliopita wa ligi daraja la kwanza pale nchini Ufaransa.

Liverpool wao wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa hawana uhakika wa asilimia mia kama nyota wao, Mbrazil Roberto Firmino anayeugulia maumivu ya jicho baada ya kuchokolewa na mlinzi wa Tottenham – Jan Vertonghen kwenye mchezo ligi kuu ya England wikiendi iliyopita.

Liverpool inaanza kampeni ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya ikiwa na kumbukumbu ya kushindwa kutwaa taji hilo ilipofika fainali ya michuano hiyo msimu uliopita baada ya kunyukwa na REAL Madrid mabao matatu kwa moja.

Katika mchezo mwingine wa kundi Che, Napoli ya Italia itakuwa ugenini kumenyana na Redstar Belgrade ya Serbia.

Michezo mingine ni pamoja na ile ya kundi Aaa ambapo Club Brugge ya Ubelgiji inaialika Borussia Dortmund ya Ujerumani huku Monaco ya Ufaransa itakuwa mwenyeji wa bingwa wa Uefa Europa League msimu uliopita, Atletico de Madrid ya Hispania.

Kwenye kundi Be, Barcelona ya Hispania itakuwa nyumbani kwenye dimba la Camp Nou kukipiga na Psv Eindhoven ya Uholanzi na Tottenham Hotspurs itakuwa ugenini kwenye dimba la Giuseppe Meazza kupepetana na Football Club Internazionale Milano maarufu kama Inter Milan.

Na kwenye kundi De, Galatasaray ya Ugiriki inamenyana na Lokomotiv Moscow huku Schalke 04 ya Ujerumani ikikipiga na FC Porto ya Ureno.

Ligi hiyo itaendelea tena kwa kupigwa michezo mingine nane ya makundi Eee hadi H ambapo kwenye kundi Eee Ajax ya Uholanzi itakuwa mwenyeji wa AEK Athens ya Ugiriki huku Benfica ya Ureno ikifungua dimba kwa kuwaalika Bayern Munich ya Ujerumani.

Machester City ya England itapepetana na Lyon ya Ufaransa katika mchezo wa kundi F huku Shakhtar Donetsk kutoka nchini Ukraine wakimenyana na TSG Hoffenheim ya Ujerumani katika mchezo mwingine wa kundi F.

Nako kwenye kundi G, bingwa mtetezi wa ligi hiyo, Real Madrid itaanza kampeni ya kulitetea tena taji lake kwa kumenyana na AS Roma ya Italia kwenye dimba la Santiago Bernabeu huku Viktoria Plzen ya Jamhuri ya Czech ikikipiga na CSKA Moscow ya Russia.

Na kwenye kundi H, Juventus ya Cristiano Ronaldo itakuwa ugenini nchini Hispania kukipiga na Valencia huku Mashetani Wekundu, Manchester United ya England ikisafiri hadi nchini Switzerland kumenyana na Young Boys.

Brazil yakamata mali za Teodorin Obiang

0

Serikali ya Brazil imekamata fedha taslimu pamoja na saa za thamani, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya dola milioni 16 za Kimarekani kutoka kwa watu waliofuatana na Makamu wa Rais wa Equatorial Guinea, – Teodorin Nguema Obiang.

Obiang mwenye umri wa miaka 48 anafahamika kama ni mtu ambaye amekua akiishi maisha ya kifahari na ni mtoto wa rais wa nchi hiyo ya Equatorial Guinea yenye utajiri mkubwa wa mafuta, -Teodoro Obiang Nguema.

Sheria za Brazil haziruhusu mgeni yeyote kuingia nchini humo akiwa na zaidi ya dola elfu mbili na mia nne za kimarekani kama fedha taslimu.

Rais Teodoro Obiang Nguema wa Equatorial Guinea ambaye ni kiongozi wa Afrika aliyekaa madarakani kwa muda mrefu na mtoto wake wamekua wakituhumiwa kwa kutumia vibaya mapato ya fedha za mafuta, huku asilimia 70 ya raia wa nchi hiyo wakiishi katika hali ya umaskini.

Watu 11 waliofuatana na Teodorin Nguema Obiang wamesafiri kwa ndege ya serikali ambapo polisi nchini Brazil wamekuta kiasi hicho cha  fedha pamoja na saa za thamani kwenye mabegi tofauti.

Kesi ya mauaji ya mwanafunzi yahamishiwa Mahakama Kuu

0

Mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi wa Bukoba mkoani Kagera  imeamuru kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa shule ya msingi Kibeta,- Spelius Eradius inayowakabili walimu wawili wa shule hiyo kuhamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba ili kuanza kusikilizwa.

Uamuzi huo umetolewa na hakimu mkazi Mfawidhi John Kapokolo kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kisheria kusilikiliza kesi inayowakabili watuhumiwa hao.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni  mwalimu anayedaiwa kutoa  adhabu ya kipigo kilichosababisha  kifo cha Mwanafunzi ambaye ni Respicius Mutazangira pamoja na mwalimu mwingine anayedaiwa kupotelewa na mkoba uliodaiwa kupokelewa na marehemu,-Herieth Gerald.

Washtakiwa  hao wamerudishwa rumande hadi hapo Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba itakapopanga tarehe ya kusikiliza shauri hilo.

 

Matumizi ya dawa za kulevya yapungua kwa asilimia 90

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa matumizi ya dawa za kulevya nchini yamepungua kwa asilimia 90 baada ya serikali kufanikiwa kudhibiti biashara ya dawa hizo.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam baada ya kufungua mkutano wa 28 wa wakuu wa vyombo vinavyopambana na dawa za kulevya kutoka nchi za Afrika ujulikanao kama 28th HONLEA – Afrika.

Mkutano huo unashirikisha wajumbe zaidi ya 120 kutoka nchi 54 za Afrika na unatarajiwa kutoka na maazimio ya namna ya kutokomeza biashara ya dawa za kulevya katika mataifa hayo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, lengo la mkutano huo ni kubadilishana uzoefu na kupanga mikakati ya pamoja kuhusu udhibiti na mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya katika nchi hizo.

“Ni lazima tuwe na mikakati ya pamoja ya kudhibiti uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya Barani Afrika. Hata hivyo ni muhimu kudhibiti njia zote zinazotumika kusafirisha dawa za kulevya.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Hata hivyo amesema kuwa Tanzania inaendelea na mikakati ya kupambana na uzalishaji wa dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na mirungi na bangi, ambayo inapandwa kwa kuchanganywa na mazao ya chakula.
Waziri Mkuu Majaliwa amewaambia washiriki wa mkutano huo wa 28 wa wakuu wa vyombo vinavyopambana na dawa za kulevya kutoka nchi za Afrika kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza katika Bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kuanzisha vituo vya utoaji wa matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya mwaka 2011.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2017, jumla vituo sita vya kutolea matibabu vilianzishwa, ambapo zaidi ya waathirika Elfu sita na mia tano wa dawa za kulevya aina ya heroin walijiandikisha na kupatiwa matibabu.