NSSF kukuza uhusiano na benki za NMB, CRDB na UBA

0

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa ya Hifadhi ya Jamii (NSSF) William Erio amekutana na kufanya mazungumzo na menejimenti za Taasisi Tatu za kibenki nchini ambazo ni NMB, CRDB na UBA.

Lengo la mkutano huo uliofanyika jijini Dar es salaam ni kuendeleza na kukuza uhusiano wa kibiashara baina ya NSSF na benki hizo tatu.

Wakati wa mkutano huo masuala mbalimbali yamejadiliwa ambayo lengo lake ni kuimarisha ushirikiano utakaowezesha kukuza maendeleo katika sekta ya uchumi kupitia benki za NMB, CRDB, UBA na shirika hilo la Taifa la Hifadhi ya Jamii.

Wakurugenzi waliokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, -William Erio ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, – Charles Kimei, Usman Imam Isiaka ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya UBA pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa benki ya NMB, – Ineke Bussemaker

Korea Kaskazini kuzima moja ya mitambo yake ya nyuklia

0

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in amesema kuwa Rais Kim Jong-un wa Korea Kaskazini amekubali kuzima moja ya mitambo yake mikubwa ya nyuklia na majaribio ya makombora.

Amesema kuwa Rais Kim amekubali kuzima kabisa mtambo huo unaojulikana kama Tongchang-ri, tukio litakaloshuhudiwa na wataalam wa nyuklia kutoka mataifa mbalimbali.

Moon amesema kuwa baada ya mkutano wao wa tatu katika mji wa Pyongyang, wamekubaliana masuala mbalimbali yanayohusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Kim mwenyewe amesema kuwa mazungumzo yao yamekwenda vizuri na makubaliano waliyofikia yana faida kubwa kwa pande zote mbili na hata mataifa mengine.

Kwa mujibu wa Rais huyo wa Korea Kaskazini, atafanya ziara Korea Kusini hivi karibuni ikiwa ni ziara ya kwanza kwa kiongozi wa Korea Kaskazini katika taifa hilo.

China na Marekani zaendeleza vita ya kibiashara

0

China imesema kuwa italipiza kisasi kwa kutoza ushuru wa dola bilioni sitini za Kimarekani kwa bidhaa za kutoka Marekani, baada ya rais Donald Trump kutangaza kiwango cha ushuru wa ziada kwa bidhaa zinazoingia kutoka China.

China imefikia uamuzi huo baada ya Marekani kutangaza kuwa ushuru wa ziada wa bidhaa kutoka nchini China kuingia nchini humo utakua dola bilioni 200 za Kimarekani.

Mvutano huo ni matokeo ya vita ya kibiashara kati ya China na Marekani, nchi zenye uchumi mkubwa.

Wizara ya Fedha ya China imesema kuwa inalipiza kile ilichokiita ajenda ya Marekani ya kutazama upande mmoja na biashara yenye ushindani usio wa usawa.

Rais Trump ametahadharisha kuwa atalipa kisasi ikiwa wakulima, wafugaji na wafanyakazi wa nchini Marekani watalengwa kwenye uamuzi wa China na kwamba milango ipo wazi endapo China itataka kujadiliana na Marekani kuhusu jambo hilo.

” Tumekuwa na biashara isiyo na uwiano sawa na China, mwaka jana tulipoteza kiasi cha zaidi ya dola bilioni mia tano kwa China, hatuwezi kufanya hivyo” amesema Trump.

Wizara ya mambo ya nje ya China imesisitiza kufanyika kwa mazungumzo kati ya China na Marekani, mazungumzo yenye usawa, kuaminiana na kuheshimiana ikiwa ni njia pekee ya kumaliza mvutano wa kiuchumi na kibiashara kati ya mataifa hayo mawili na kuongeza kuwa kinachofanywa hivi sasa na Marekani hakionyeshi ukweli wala nia njema.

Lahyani asimamishwa kuchezesha tenisi

0

Muamuzi wa mchezo wa tenisi Mohamed Lahyani raia wa Sweden amesimamishwa kuchezesha mashindano mawili yajayo ya China Open na Shanghai Masters yatakayofanyika mwezi Oktoba mwaka huu baada ya kupatikana na kosa la kumsaidia mcheza Tenisi,-Kick Kyrgios wa Australia kwenye mashindano yaliyopita ya US Open.

Lahyani alisikika wakati wa mapumziko akimwambia Kyrgios kuwa nataka kukusaidia wakati wa mpambano wake na Pierre – Hugues Herbert wa Ufaransa na baada ya kauli hiyo Kyrgios aliweza kutoka nyuma hadi kuibuka mshindi.

Waandaaji wa mashindano ya US Open wamemtuhumu muamuzi huyo kwa kusema kuwa alienda kinyume na taratibu za mashindano hayo, lakini wamempa tena nafasi ya kuchezesha kwenye mashindano hayo mwaka 2019.

Lahyani atakuwa huru kuchezesha tena mashindano ya tenisi kuanzia mashindano ya Stockholm Open.

Messi afanya kweli

0

Lionel Messi amekua mchezaji wa kwanza kufunga goli la kwanza kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya msimu huu na pia kuwa mchezaji wa kwanza kufunga magoli matatu kwenye mchezo mmoja yaani Hat – Trick wakati timu yake ya FC Barcelona ilipoifunga PSV ya Uholanzi kwa bao nne kwa bila.

Messi ambaye kwa sasa ni nahodha wa miamba hiyo ya Catalunya, alianza kufungua milango ya PSV kwenye dakika 31 ya mchezo pale alipofunga kwa mpira wa adhabu ya nje ya kumi na nane na kuongeza magoli mengine mawili kwenye dakika za 77 na 87 na goli lingine la Barcelona lilitiwa kimiani na Ousmane Dembele.

Hadi sasa Messi amefunga Hat – Trick nane kwenye michuano hiyo ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya na kwa msimu huu tu amefunga magoli saba kwenye michezo sita aliyocheza.

Kwa ujumla Messi amefunga magoli 104 kwenye ligi ya mabinwa Barani Ulaya kwa michezo 14 aliyocheza akiwa na timu hiyohiyo ya Barcelona na kufikia rekodi iliyowekwa na nyota wa zamani wa Real Madrid, -Raul Gonzalez.

Ligi Kuu Tanzania Bara yaingia raundi ya Tano

0

Ligi Kuu Tanzania Bara inaingia kwenye raundi yake ya Tano huku timu zingine zikicheza michezo yake ya raundi ya tatu kwenye msimu wa 2018/2019.

Kwenye dimba la Taifa jijini Dar es salaam, mabingwa wa kihistoria Yanga watakuwa wenyeji wa wagosi wa kaya Coastal Union ya Tanga ambayo imerejea msimu huu kwenye ligi kuu baada ya kuikosa kwa misimu miwili.

Yanga ambao mchezo huo dhidi ya Coastal Union utakuwa wa tatu kwao, wameshashinda michezo miwili iliyocheza, huku Coastal Union ikicheza michezo minne na imeshinda mchezo mmoja na kutoka sare michezo mitatu.

Huko Musoma – Mara kwenye dimba la kumbukumbu ya Karume, timu ngeni kwenye ligi kuu Biashara United yenyewe itawaalika matajiri wa Chamazi Azam FC huku wanakuchele Ndanda FC baada ya kutoka sare na mabingwa watetezi Simba safari hii wana kibarua kingine kigumu mbele ya mabingwa wa kombe la Shirikisho, -Mtibwa Sugar.

Kwenye dimba la Samora mjini Iringa, wanapaluhengo Lipuli FC ambayo haijashinda mchezo hata mmoja ikiwa imetoka sare kwenye michezo yake yote minne iliyocheza safari hii, inakipiga na timu inayoburuza mkia kwenye ligi kuu Alliance FC ya Mwanza.

Jijini Mbeya, Wagonga nyundo au watoza ushuru wa jiji hilo Mbeya City watawaalika wazee wa kupapasa Ruvu Shooting na mchezo wa mwisho kwa Septemba 19 utapigwa kwenye migodi ya Almasi huko Mwadui mkoani Shinyanga ambapo wenyeji Mwadui FC watawaalika vinara wa ligi kuu kwa sasa JKT Tanzania.

Usafiri reli ya kati kuboreshwa

0

Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe amewahakikishia wakazi wa mikoa ambayo reli ya kati inapita, kuwa tatizo la usafiri wa njia hiyo linalotokana na uchakavu wa reli ni la muda kwa kuwa tayari serikali imetia saini mkataba wa ujenzi wa reli hiyo.

Waziri Kamwelwe ametoa kauli hiyo mjini Tabora wakati akijibu malalamiko ya wananchi kuhusu ubovu wa njia ya reli ya kati na malalamiko ya wafanyakazi kuhusu vitendea kazi na stahili zao.

Waziri Kamwelwe amemaliza ziara yake ya siku tatu mkoani Tabor

Utandikaji reli SGR waanza

0

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema serikali ipo kwenye mpango wa kukamilisha mradi wa chuma wa Liganga na Mchuchuma ili miradi mbalimbali iweze kutumia bidhaa hiyo na kuacha kuagiza chuma kutoka nje ya nchi.

Waziri Kamwelwe ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam baada ya kushuhudia kuanza kwa zoezi la utandikaji reli katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa -SGR.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Nchini –TRC, Masanja Kadogosa amesema mataruma ya reli hiyo yanatengenezwa hapa nchini na kuwa ni vyuma vya reli tu ndio vinaagizwa kutoka nje ya nchi.

Meneja mradi katika ujenzi huo Mhandisi Maizo Magedzi amesema reli iliyopo hivi sasa itatandazwa umbali wa kilomita 60 na wakati mzigo mwingine unatarajiwa kuwasili mwezi ujao.

Mradi wa reli ya kisasa utakapokamilika utaweza kubeba tani milioni 17 za mizigo kwa mwaka tofauti na reli iliyopo inayobeba tani milioni tano na kupunguza muda wa safari ambapo treni itakuwa ikitembea kwa spidi ya Kilomita 160 kwa saa.