Bao la Samatta laipa ushindi Genk

0

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Mbwana Samatta amefunga bao la pili katika ushindi wa mabao mawili kwa bila waliopata timu ya Genk dhidi ya Malmo FC huko nchini Ubelgiji.

Leandro Trossad alianza kuifungia Genk bao la kwanza katika dakika ya 37 kabla ya Samatta kuihakikishia ushindi katika dakika ya 71 kwa kupachika bao la pili na kuzima matumaini ya Malmo ya kupata walau alama moja ya ugenini.

Katika matokeo mengine ya ligi ya Yuropa, Sevilla wameitandika Standard Lieg mabao matano kwa moja, Ludogorets wamepokea kipigo cha mabao matatu kwa mawili kutoka kwa Bayer 04 Leverkusen na Dinamo Zagreb wenyewe wameinyuka Fenerbahce mabao manne kwa moja.

Nao Olyimpic Marseile wamekiona cha moto nyumbani baada ya kutandikwa mabao mawili kwa moja na Eintraincht Frankfurt

Idadi ya waliokufa kwenye kivuko yaongezeka

0

Idadi ya watu waliokufa maji kufuatia kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere imeongezeka na kufikia zaidi ya mia moja.

Miili zaidi imepatikana kufuatia kazi ya uokoaji inayoendelea hivi sasa katika eneo kilipozama kivuko hicho.

Kivuko cha MV Nyerere kinachotoa huduma zake kati ya Bugorora na Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza kilizama Alhamisi Septemba 20 mwaka huu kikiwa katika safari zake za kawaida.

Rais John Magufuli ametuma salamu za pole kwa Watanzania wote kufuatia ajali hiyo na kuwataka kuwa watulivu katika kipindi hiki wakati shughuli za uokoaji zikiendelea.

Kivuko cha Mv Nyerere chazama

0

Kivuko cha MV Nyerere kinachofanya safari zake kati Bugorola na Ukara katika Kisiwa cha Ukerewe mkoa wa Mwanza kimezama.

Wakati tukio hilo linatokea kivuko hicho kilikua na abiria kadhaa pamoja na mizigo.

Tutaendelea kukuletea taarifa zaidi kuhusiana na tukio hilo kadri zitakavyopatikana.

Baadhi ya tozo zafutwa kuchochea uchumi wa viwanda

0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema kuwa serikali imefuta baadhi ya ada na tozo zisizoondoa wajibu wa muajiri kulinda afya za wafanyakazi ili kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Waziri Mhagama ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo mengine ameelezea mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa katika Mamlaka ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) kwa lengo la kutekeleza azma ya serikali ya kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji.

Amesisitiza kuwa lengo la kufuta tozo na ada hizo ni kuboresha mazingira ya biashara, kupunguza gharama za uendeshaji kwa wawekezaji pamoja na waajiri.

“Tumefuta ada mbalimbali ikiwemo ada ya fomu ya usajili ambayo ilikuwa shilingi elfu mbili kwa lengo la kupunguza gharama, tumefuta ada ya usajili wa maeneo ya kazi kwa kuzingatia ukubwa wa eneo ambayo ilikuwa ikitozwa kwa kiasi cha shilingi elfu hamsini hadi shilingi milioni moja na laki Nane kulingana na eneo, hivyo usajili kwa sasa ni bure” amefafanua Waziri Mhagama.

Ameongeza kuwa serikali imefuta ada ya leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi iliyokuwa ikitozwa shilingi laki mbili kwa mwaka kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara ambapo kwa sasa leseni hiyo itatolewa bure huku tozo ya siku ya ushauri wa kitaalam wa usalama na afya kwa kuzingatia idadi ya wafanyakazi ya shilingi laki Nne na Nusu ikifutwa kwa lengo la kupunguza gharama ili kutoa elimu kwa wahitaji wengi zaidi.
Hata hivyo Waziri Mhagama amesema kuwa OSHA imejikita katika utoaji wa elimu kwa wadau kuhusu takwa la kisheria la kulinda afya za wafanyakazi nchini mahala pa kazi katika kanda mbalimbali na kusimamia mifumo ya utendaji wa watumishi wa mamlaka hiyo ili kuondoa mianya ya rushwa na kukuza uzalendo na uwajibikaji.

Balozi Mstaafu Siwa Mwenyekiti mpya bodi ya NSSF

0

Rais John Magufuli amemteua balozi mstaafu Ali Idi Siwa kuwa Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Uteuzi wa balozi Mstaafu Siwa unaanza Septemba 20 mwaka huu.

Makubaliano ya Korea Kaskazini na Korea Kusini yaungwa mkono

0

Rais Donald Trump wa Marekani ameunga mkono makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa Korea Kaskazini na Korea Kusini katika mkutano wao uliofanyika mjini Pyongyang.

Trump amesema kuwa makubaliano yaliyofikiwa na viongozi hao kuhusu Korea Kaskazini ni hatua nzuri kwa kuwa awali ilionekana kama Marekani na nchi hiyo zitaingia katika mgogoro kutokana na mpango wake wa nyuklia.

“Tumerejeshewa wafungwa wetu, tunarejeshewa mabaki ya wapiganaji wetu,lakini la muhimu hakuna tena majaribio ya makombora, majaribio ya silaha za nyuklia na sasa wanataka kuomba kuandaa mashindano ya olimpiki, tuna mambo mengi mazuri yanayoendelea,” amesema Rais Trump.

Rais huyo wa Marekani amerejea kauli yake kuwa utawala wake umekuwa chachu ya kuleta mazingira tulivu yanayoonekana hivi sasa.

”Kumbuka hili, kabla ya kuwa rais watu wengi walifikiri kuwa tunakwenda vitani lakini sasa mahusiano mazuri yamejengwa, nawaambia kwa mawazo yangu, mahusiano ni mazuri, hali imekuwa ya utulivu, kwa sasa tunapoongea hali imetulia, amekuwa mtulivu, nimekuwa mtulivu hivyo tutaona mambo yatakavyokuwa” ameongeza Rais Trump.

Hivi karibuni Rais Kim Jong-un wa Korea Kaskazini alikutana na mwenzake wa Korea Kusini, – Moon Jae-in katika mji wa Pyongyang, mkutano ambao ni wa tatu kwa viongozi hao.
Wakati wa mkutano huo Kim alitangaza kuzima moja ya mitambo yake mikubwa ya nyuklia na majaribio ya makombora wa Tongchang-ri, tukio litakaloshuhudiwa na wataalam wa nyuklia kutoka mataifa mbalimbali.

City wapoteza kwa Lyon

0

Kampeni ya Manchester City kwenye mashindano ya klabu bingwa barani Ulaya imeingia dosari baada kuanza vibaya kama mabingwa watetezi wa ligi kuu England kwa kupoteza mbele ya Lyon katika uwanja wa Etihad kwa kuchapwa mabao mawili kwa moja.

Maxwel Cornet aliifungia Lyon goli la kwanza baada ya makosa ya Fabian Delph ya kushindwa kuutoa mpira nje baada ya krosi iliyopigwa na Fekir.

City ambao wanapewa nafasi ya kufanya vizuri kwenye klabu bingwa walijikuta wakiongozwa kabla ya mapumziko.

Nahodha wa Lyon, -Fekir alifunga goli la pili umbali wa mita 25 baada ya makosa kutoka kwa Fernandinho.

Bernardo Silva aliwapa matumaini City baada ya kufunga goli akisaidiwa na Leroy Sane, lakini wenyeji walikosa bahati ya kupata mabao na hivyo kushindwa kuepuka kupoteza mchezo wao wa kwanza kwenye mashindano hayo makubwa Ulaya.

Pamoja na majaribio kadhaa kutoka kwa beki Aymerici Laporte, Gabriel Jesus na Sergio Aguero walishindwa kupata magoli kutokana na ubora wa mlinda mlango wa Lyon,- Anthony Lopes.

City ilionekana ikosa maelekezo muhimu kutoka kwa kocha mkuu Pep Guardiola kutokana na adhabu anayoitumikia.

Kocha wa Manchester city alikuwa anaushuhudia mchezo huo akiwa jukwaani akitumikia adhabu yake aliyoipata msimu uliopita katika hatua ya robo fainali dhidi ya Liverpool.

Kocha msaidizi Mikel Arteta ambaye pia ni kiungo wa zamani wa Arsenal alichukua majukumu ambayo hata hivyo yalionekana kumzidi.

City ilionekana kama wangeendelea kutawala soka la Ulaya baada ya kufanikiwa kupata alama mia moja katika msimu uliopita kwenye ligi kuu England, lakini hata hivyo watahitaji kupambana kwa hali na mali ili waweze kuongoza kundi lao kama walivyofanya msimu uliopita.

Makatibu Wakuu wa wizara watakiwa kuzingatia sheria

0

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amewataka makatibu wakuu wa wizara na makatibu tawala wa mikoa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria , kanuni, taratibu na miongozo inayotolewa na serikali kila wanapofanya maamuzi.

Akifungua kikao kazi cha siku tatu kwa viongozi hao jijini Dodoma, Balozi Kijazi amesema kuwa makatibu wakuu wa wizara na makatibu tawala wa mikoa wana jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wanazingatia taratibu zote ili azma ya kujenga uchumi wa viwanda ifikiwe kwa wakati na kuwanufaisha Watanzania.

“Nafasi zenu ni za maamuzi, hivyo msipofanya maamuzi sahihi na kwa wakati mtakwamisha shughuli za maendeleo na huduma muhimu kwa wananchi,” amesisitiza Balozi Kijazi.

Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuwa jukumu kubwa la washiriki wa kikao hicho ni kuhakikisha wanafanyia kazi masuala yote yatakayoazimiwa katika kikao kazi hicho kinacholenga kuongeza tija kwenye ngazi ya wizara na mikoa kwa kuzingatia azma ya serikali ya kuleta mageuzi makubwa katika nyanza zote hasa katika huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Amesema kikao kazi hicho kina umuhimu mkubwa na kitakuwa kikifanyika kila mwaka ili kuwapa fursa makatibu wakuu na makatibu tawala kubadilishana uzoefu, kubaini changamoto zilizopo na kuweka utaratibu mzuri wa kuzitatua kwa maslahi ya wanachi.

Kauli mbiu ya kikao kazi hicho kinachoshirikisha makatibu wakuu wa wizara na makatibu tawala wa mikoa ni Uongozi makini na wa pamoja unaozingatia uzalendo, uwajibikaji, utawala bora na kusimamia rasilimali zetu ni nyenzo muhimu katika kuifikisha Tanzania katika uchumi wa Kati.