Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za rambirambi mkuu wa mkoa wa Mwanza, – John Mongela kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere na kusababisha vifo pamoja na majeruhi.
Dkt Shein ameeleza kuwa amepokea kwa mshtuko na huzuni taarifa ya ajali ya kuzama kivuko hicho na kuongeza kuwa yeye binafsi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania nzima wana simanzi kubwa kufuatia msiba huo mkubwa wa kitaifa.
“Kwa hakika msiba huu umetugusa Watanzania sote, ni msiba wetu kwa sababu waliofikwa na janga hili ni ndugu zetu, Watanzania wenzetu”, amesema Dkt Shein.
Amesema kuwa kwa vile ajali ni moja kati ya matukio ambayo mwanadamu hana budi nayo, anamuomba Mwenyezi Mungu azijalie roho za wale wote waliopoteza maisha zipumzike mahala pema.
Kwa wale ambao wameweza kuokolewa wakiwa hai, amemuomba Mwenyezi Mungu awape nafuu ili waweze kurudi katika hali zao za kawaida kiafya na waendelee na shughuli zao za kila siku za kujenga nchi yao.
“Watanzania tunatakiwa kuendelea kuwa na utulivu, umoja na mshikamano wakati huu ambapo jitihada za kutafuta miili zaidi ya waliopata ajali hiyo zikiendelea”,ameeleza Dkt Shein.
Kivuko cha MV Nyerere kinachotoa huduma zake kati ya Bugorora na Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza kilizama Alhamisi Septemba 20 mwaka huu kikiwa katika safari zake za kawaida ambapo hadi sasa miili 126 imeopolewa.