Askari wa usalama barabarani wapongezwa

0

Rais John Magufuli amewapongeza askari wa usalama barabara kwa juhudi zao za kusimamia usalama wa barabarani licha ya changamoto m mbalimbali wanazokabiliana nazo.

Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo Septemba 23 alipokutana na kunywa chai na baadhi ya askari hao Ikulu jijini Dar es salaam, muda mfupi baada ya kutoka katika ibada ya jumapili iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

“Nawapongeza Trafiki wote kwa kazi mnazofanya, nafahamu mnakabiliwa na changamoto nyingi, mnafanya kazi zenu kwenye jua na mvua, na wakati mwingine mnakwazwa na watumia barabara lakini mnaendelea na kazi.“Nataka kuwatia moyo, chapeni kazi, wanaovunja sheria za barabarani wachukulieni hatua, msitishwe na mtu yeyote lakini na nyie msimuonee mtu yeyote” amesisitiza Rais Magufuli.

Askari hao wamemshukuru Rais Magufuli kwa kuwaalika Ikulu kupata nao chai ya asubuhi na kuzungumza nao na wamemhakikishia kuwa wataendelea kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa ili kuhakikisha usalama barabarani unazidi kuimarika chini ya kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.

“Tunakushukuru sana Mhe. Rais kwa upendo wako kwetu, umetutia moyo sana na tunakuhakikishia tutachapa kazi kwa nguvu zetu zote” amesema Mkuu wa Trafiki wa Wilaya ya Kipolisi ya Kati Inspekta Neema Mvungi.

Mapema asubuhi, Rais Magufuli ameshiriki misa takatifu iliyoongozwa na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Oysterbay Padre Bathlomeo Bachoo ambaye katika maombezi yake amewaongoza Waumini kuwaombea Marehemu wote wa ajali ya kivuko cha MV Nyerere walale mahali pema peponi na majeruhi wapone haraka.

Wanamichezo, Wasanii kuombeleza

0

Waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo Dkt Harrison Mwakyembe ameagiza mabaraza ya michezo na sanaa ya taifa na mashirikisho husika kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia taifa liko kwenye maombolezo.

Waziri Mwakyembe amewataka wachezaji na watazamaji wa michezo mbalimbali kusimama kwa dakika moja kabla ya michezo kuanza ili kuwaombea marehemu na majeruhi wa ajali ya kivuko cha mv nyerere iliyotekea tarehe 20 septemba mwaka huu katika ziwa viktoria.

Pia amevitaka vyombo husika vya michezo kuhakikisha kila mchezaji anafunga kitambaa cheusi kwenye mkono, ishara ya wanamichezo kuomboleza msiba huo.

Aidha Waziri huyo wa habari, utamaduni, sanaa na michezo ameliagiza baraza la sanaa la taifa lihakikishe kuwa wamiliki wa kumbi za wazi za starehe wanadhibiti kelele za shamrashamra na upigaji muziki usiozingatia kipindi cha maombolezo kitakachohitimishwa septemba 24 mwaka huu.

Mazishi ya waliokufa maji yanafanyika Ukara

0

Mazishi ya Kitaifa ya watu waliokufa maji katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere yanaendelea hivi sasa katika kisiwa cha Ukara.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ndiye anayeongoza mazishi hayo ambayo pia yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Akizungumza na TBC mapema hii leo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kuwa kazi ya kuokoa miili ya watu waliokufa maji katika ajali hiyo ya kivuko cha MV Nyerere inatarajiwa kukamilika leo.

Idadi ya watu waliokufa kwenye ajali hiyo imeongezeka na kufikia 224 huku walio okolewa wakiwa hai ikiwa ni 41.

Miili ya watu 172 yatambuliwa Ukara

0

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema miili ya watu 172 waliokufa maji baada ya kivuko cha MV Nyerere kuzama Septemba 20 mwaka huu imetambuliwa hadi majira ya saa 11 jioni ya leo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kisiwa cha Ukara mkoani Mwanza Waziri Kamwelwe amesema miili ya watu 112 imekwishachukuliwa na ndugu zao na miili ya watu 37 bado haijatambuliwa.Idadi ya miili ya watu iliyoopolewa imefikia 209.

Amesema wadau mbalimbali wameendelea kujitokeza kuchangia fedha kusaidia shughuli za uokoaji, misaada na rambirambi kwa waliofiwa ikiwemo Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo iliyotoa shilingi Milioni 150, Jumuiya ya Shia Dar Es Salaam imetoa shilingi Milioni 10 na zaidi ya katoni elfu tatu za maji, Wakala wa Ufundi na Umeme – TEMESA umeahidi kutoa mafuta kwa ajili ya kusafirisha miili ya marehemu na kutoa vifaa vitakavyotumika kunyanyua kivuko hicho kilichozama.

Serikali yafungua akaunti maafa Mv Nyerere

0

Serikali imefungua akaunti maalum baada ya kivuko cha MV Nyerere kuzama Septemba 20 mwaka huu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema watanzania wanaweza kutuma rambirambi zao katika akaunti hiyo itakayokuwa ikiratibiwa na ofisi ya maafa mkoa wa Mwanza chini ya usimamizi wa Ofisi ya maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Akaunti hiyo ya maafa inaitwa Maafa MV Nyerere yenye namba 31110057246 katika Benki ya NMB tawi la Kenyatta Road mkoani Mwanza.

Waziri Mhagama amesema wale wote watakaoguswa kuchangia watume fedha katika akaunti hiyo.

Kazi ya uokoaji yaelekea ukingoni

0

Mkuu wa majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo amesema wanajitahidi kuhakikisha kazi ya kuwaokoa watu waliozama kufuatia kupinduka kwa kivuko cha MV Nyerere inakamilika hii leo ili kazi ya kuhifadhi miili ianze.

Akizungumza na tbc kutoka katika eneo kilipozama kivuko hicho, Jenerali Mabeyo amesema kuwa kwa wale ambao watakuwa hawajatambuliwa na ndugu zao wataomba kibali cha serikali ili wahifadhiwe karibu na eneo ilipotokea ajali hiyo.

Mapema hii leo, fundi mkuu wa kivuko hicho cha MV Nyerere ameokolewa akiwa hai wakati zoezi la uokoaji likiendelea.

Mhandisi Augustino Charahani ni miongoni mwa wafanyakazi Wanane wa kivuko cha MV Nyerere ambaye alikuwemo ndani ya kivuko wakati ajali hiyo inatokea.

Hadi kufikia mchana wa leo miili ya watu 60 imeopolewa na kufanya idadi ya watu waliokufa kufikia 197.

Fundi Mkuu wa MV Nyerere aokolewa akiwa hai

0

Fundi Mkuu wa kivuko cha MV Nyerere ameokolewa akiwa hai wakati zoezi la uokoaji likiendelea katika kisiwa cha Ukara wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.

Mwandishi wa TBC aliyeko kisiwani Ukara anaripoti kwamba Fundi huyo Augustino Charahani ni miongoni mwa wafanyakazi wanane wa kivuko cha MV Nyerere ambaye alikuwemo katika kivuko hicho wakati ajali ikitokea.

Fundi huyo alikuwa amejifungia katika chumba cha injini ya kivuko hicho tangu ajali ilipotokea Septemba 20 mwaka huu.

Kazi ya uokoaji inaendelea ambapo mapema leo miili ya watu 25 imeopolewa.

Kufuatia msiba huo kwa taifa kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom imetoa shilingi Milioni kumi kwa serikali ili zitumiwe na wafiwa kusaidia katika mazishi ya wapendwa wao.

Rais Magufuli atangaza siku nne za maombolezo

0

Rais Dkt. John Magufuli ametangaza siku nne za maombolezo kuanzia leo kufuatia vifo vya watu zaidi ya 130 vilivyotokana na kuzama kwa kivuko vya MV Nyerere.

Akihutubia taifa kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania –TBC, Rais Magufuli amewataka wanasiasa kutotumia msiba huu kupata umaarufu.

Rais Magufuli ametoa pole kwa watanzania wote hususan waliofiwa na ndugu na jamaa zao na kuwatakia majeruhi kupona haraka.

Aidha bendera zitapepea nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia kesho, Septemba 22 mwaka huu 2018.

Akizungumza jijini Dodoma kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi ameagiza watu wote wanaohusika na shughuli za uendeshaji wa kivuko cha MV Nyerere kukamatwa na kuhojiwa na watakaokutwa na hatia wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.