Fedha za pole kuanza kutolewa

0

Malipo ya fedha za pole kwa kila familia iliyopoteza ndugu au jamaa kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere Septemba 20 mwaka huu yanaanza kufanyika hii leo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kuwa malipo ya fedha hizo yanafanyika chini ya usimamizi wa mkuu wa mkoa wa Mwanza,- John Mongela.

Rais John Magufuli ametangaza malipo ya shilingi milioni moja ambazo zitatolewa kwa kila familia kwa ajili ya kila marehemu, fedha ambazo ni tofauti na zile zilizotangazwa kutolewa awali ambazo zilikua ni shilingi laki tano.

Rais Magufuli pia ametangaza malipo ya shilingi milioni moja kwa kila aliyenusurika katika ajali hiyo ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere huko Ukerewe mkoani Mwanza.

Habari zaidi kutoka wilayani Ukerewe zinasema kuwa jitihada za kukinasua kivuko hicho zinaendelea ambapo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa hatua iliyofikiwa ni ya kuridhisha.

 

Salamu za rambirambi zaendelea kutolewa

0

Viongozi mbalimbali wameendelea kutoa salamu za rambirambi kwa Rais John Magufuli kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere iliyotokea Septemba 20 mwaka huu na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 220 katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Salamu hizo ni pamoja na kutoka kwa Rais Vladimir Putin wa Russia, Rais XI Jinping wa China, Rais Brahim Ghali wa Saharawi, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani, Waziri Mkuu wa Israel, – Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Sweden,- Stefan Lofven, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Inmi Patterson na Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini.

Katika salamu zake, Rais XI Jinping wa China ameelezea kushtushwa na taarifa za ajali hiyo na kutuma salamu za pole kwa waliofiwa na walionusurika katika ajali hiyo.

Nayo Ofisi ya Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini imetuma salamu za pole kwa Rais Magufuli, familia za waliofiwa na Watanzania wote kufuatia vifo vya watanzania na kuwatakia manusura nafuu ya haraka na kuipongeza serikali ya Tanzania kwa kuchukua hatua za haraka kushughulikia suala hilo.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwa niaba ya serikali na wananchi wa taifa hilo ametuma salamu za pole kwa wafiwa na kusema kuwa sala na mawazo yao yapo pamoja na watanzania katika kipindi hiki kigumu.

Zabuni ya kutengeneza kivuko kipya kutangazwa

0

Rais John Magufuli ameagiza kutangazwa kwa zabuni ya haraka ya kutengeneza kivuko kingine kipya chenye uwezo wa kubeba tani 50 za mizigo na abiria zaidi ya 200 kitakachotumiwa na Wakazi wa kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kisiwa cha Ukara, ikiwa ni siku chache baada ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere.

“Hili ni agizo la Mheshimiwa Rais, na mimi ninamuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe aitishe zabuni hiyo haraka sana, kazi hiyo ifanywe mara moja ili kivuko kipya kiweze kutengenezwa na kusaidia wananchi wa eneo hili kwa haraka,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa  amesema kuwa  kivuko hicho kipya kikikamilika, kitapangiwa ratiba za safari nyingi zaidi badala ya kwenda mara moja kwa siku ili kuondoka kero iliyokuwa ikiwakabili wakazi wa eneo hilo.

 

 

 

Mtendaji Mkuu wa TEMESA asimamishwa kazi

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza tume ya watu Saba iliyoundwa na serikali itakayochunguza sababu za kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere Septemba 20 mwaka huu na kutoa mapendekezo pamoja na ushauri kwa serikali.

Akitangaza tume hiyo katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa tume hiyo itaongozwa na Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali George Waitara.

Ameitaka tume hiyo inayoshirikisha Wajumbe kutoka sekta mbalimbali akiwemo Mbunge wa Ukerewe, – Joseph Mkundi kufanya kazi yake ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Waziri Mkuu Majaliwa pia ametangaza kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt Mussa Mgwatu, lengo likiwa ni kuiwezesha tume hiyo kufanya kazi kwa uhuru.

Kwa miili ambayo itaendelea kuopolewa kufuatia kuzama kwa kivuko hicho cha MV Nyerere, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa kitakachofanyika hivi sasa ni kuchukuliwa kwa DNA, kwa kuwa miili hiyo huenda itakua imeharibika kutoka na kukaa kwenye maji kwa muda mrefu.

Kuhusu kazi ya kunasua kivuko hicho, Waziri Mkuu Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo kuharakisha kazi hiyo kwani vifaa vyote muhimu vipo ikiwa ni pamoja na wataalam wa kufanya kazi hiyo.

Kivuko cha MV Nyerere kunasuliwa

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa muda mfupi ujao atashuhudia kazi ya kunasua kivuko cha MV Nyerere kilichozama Septemba 20 mwaka huu.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa kazi ya kunasua kivuko hicho haitachukua muda mrefu kwa kuwa kuna vifaa vya kutosha.

Amesema kuwa vifaa vilivyokuwa vikisubiriwa kutoka jijini Dar es salaam vimekwishawasili katika kisiwa hicho cha Ukara kwa ajili ya kazi hiyo.

Bodi ya SUMATRA yavunjwa

0

Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) Mhandisi John Ndunguru na kuivunja bodi hiyo kuanzia leo Septemba 24.

Rais Magufuli amechukua hatua hiyo kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere iliyotokea Septemba 20 mwaka huu na matukio mbalimbali ya ajali za barabarani nchini yanayosababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa mali.

Pamoja na hatua hiyo, kamati ya uchunguzi ambayo itatangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baadaye hii leo itaendelea na uchunguzi wa ajali ya kivuko cha MV Nyerere kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kama ilivyopangwa.

Rais Magufuli avunja bodi TEMESA

0

Kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere iliyotokea tarehe 20 Septemba, 2018 katika ziwa Victoria, Rais Dkt. John Magufuli ameivunja Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme -TEMESA.

Bodi hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti wake Brigedia Jenerali Mstaafu Mhandisi Mabula Mashauri imevunjwa kuanzia leo tarehe 23 Septemba wakati kamati ya uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.

Waziri Mkuu aongoza mazishi ya kitaifa waliokufa ajali ya MV Nyerere

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameongoza wananchi katika mazishi ya kitaifa ya watu waliofariki dunia kwenye ajali ya MV Nyerere iliyotokea Septemba 20, mwaka huu.

Akizungumza katika mazishi hayo yaliyofanyika katika eneo la Bwisya, kisiwa cha Ukara wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza Waziri Mkuu amesema serikali imeanza kuchukua hatua kwa wale wote wanaohusika na shughuli za kivuko hicho wakati uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo ukiendelea.

Waziri Mkuu amesema serikali imechukua hatua ya kuunda tume ya uchunguzi na kuahidi tume hiyo kutangazwa wakati wowote.

Ili kukabiliana na tatizo la usafiri lililopo, Waziri Mkuu amesema meli ya MV Nyehunge imeanza kutoa huduma ya usafiri wa muda badala ya MV Nyerere iliyokuwa ikitoa huduma kati ya bandari ndogo ya Bugolora, Ukerewe na kisiwa kidogo cha Ukara.