Makamu wa Rais akutana na viongozi mbalimbali

0

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Dkt Alex Mubiru ambaye alifika ofisini kwa Makamu wa Rais kujitambulisha.

Wakati wa mazungumzo yao, Makamu wa Rais amesema kuwa AfDB imeahidi kuendelea kushirikiana na kuisaidia Tanzania kutokana na hatua kubwa ya kimaendeleo ambayo imeonyesha.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi huyo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt Alex Mubiru amesema kuwa wawakilishi wa AfDB wapo nchini kwa lengo la kuisaidia serikali pamoja na watu wake.

Wakati huo huo Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na balozi wa Kenya nchini Dan Kazungu ambaye alifika ofisini kwa kwake kwa lengo la kujitambulisha.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pia amekutana na balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshida ambaye amemaliza muda wake nchini.

Katika mazungumzo yao, Makamu wa Rais amemshukuru balozi Yoshida kwa ushirikiano wote alioutoa kwa kipindi chote alichokuwa hapa nchini.

Naye Balozi Yoshida ameishukuru serikali pamoja na raia wote wa Tanzania kwa ushirikiano mzuri waliompa kwa kipindi chake alichohudumu kama balozi wa Japan hapa nchini.

Wafanyakazi wa afya kuanza kutoa huduma

0

Wafanyakazi wa afya ambao wamekua wakiwasaidia wagonjwa wa Ebola katika mji wa Beni uliopo kwenye Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wameanza tena kutoa  huduma,  baada ya kusitisha kwa muda wa siku mbili kufuatia shambulio la waasi lililosababisha vifo vya watu 18.

Wafanyakazi hao wameanza kutoa huduma hizo za afya kufuatia onyo lililotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa kuendelea kusitishwa kwa huduma hizo kunaweza kusababisha madhara zaidi.

Katika taarifa yake, WHO  imesema kuwa jitihada za kukabiliana na Ebola ni lazima ziendelee kwa kuwa kwa kutofanya hivyo kunaweza kusababisha kuenea kwa ugonjwa huo hadi katika eneo la mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Uganda.

Kwa sasa Wafanyakazi hao wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wataendelea kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Ebola na kutafuta watu walioambukizwa virusi vinavyosababisha ugonjwa huo ili waweze kupatiwa matibabu.

 

Cosby ahukumiwa kifungo jela kwa udhalilishaji

0

Mahakama moja huko Pennsylvania nchini Marekani imemuhukumu kifungo cha kati ya miaka mitatu na kumi jela mchekeshaji Bill Cosby kwa kosa la udhalilishaji.

Cosby mwenye umri wa miaka 81, pia ameorodheshwa kuwa mtu mwenye tabia ya udhalilishaji kwa kuwa amekua akitenda vitendo hivyo mara kwa mara.

Wakati kesi yake ikiendelea, mchekeshaji huyo alikataa kuongea chochote licha ya kupewa nafasi ya kufanya hivyo.

Mwezi Aprili mwaka huu wakati kesi hiyo ikisikilizwa, Cosby alikutwa na hatia ya makosa matatu ya udhalilishaji kwa kumpatia kilevi na kumdhalilisha Andrea Constand mwaka 2004.
Ombi la Cosby la kutaka kuachiliwa kwa dhamana akisubiri kusikilizwa kwa rufaa yake limekataliwa.

Mchekeshaji huyo alitapa umaarufu miaka ya 1980 aliposhiriki katika kipindi cha televisheni kuhusu familia ya Kimarekani yenye asili ya Afrika iliyokuwa ikiishi Brooklyn, New York, umaarufu uliofikia kupewa jina la America’s Dad.

Dkt Ndumbaro Naibu Waziri mpya Mambo ya Nje

0

Rais John Magufuli amemteua Dkt Damas Ndumbaro kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Dkt Ndumbaro ambaye ni Mbunge wa Songea mjini mkoani Ruvuma anachukua nafasi ya Dkt Susan Kolimba ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Wakati huo huo Rais Magufuli amemteua Dkt Faraji Mnyepe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Dkt Mnyepe anachukua nafasi ya Profesa Adolf Mkenda ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Profesa Mkenda amechukua nafasi ya Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi ambaye amestaafu.

Uteuzi wa viongozi hao umeanza leo Septemba 26 na tarehe ya kuapishwa kwao itatangazwa baadaye.

Mwili uliozikwa watambuliwa

0

Mwili mmoja kati ya minne ya watu waliokufa kwenye ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza na kushindwa kutambuliwa na baadaye kuzikwa, umetambuliwa na ndugu zake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema kuwa mwili huo ambao ni wa mwanamke umetambuliwa baada ya kufanyika kwa vipimo vya vinasaba (DNA).

Waziri Mhagama amesema kuwa vipimo hivyo vimefanyika baada ya ndugu wa marehemu huyo ambao ni pamoja na mume na watoto kufika kisiwani Ukara wakitokea wilayani Muleba mkoani Kagera na kusema kuwa ndugu yao ni miongoni mwa watu waliokufa maji katika ajali hiyo.

Amesema kuwa baada ya vipimo kuthibitisha kuwa marehemu huyo ni ndugu yao, familia hiyo imeonyeshwa kaburi la ndugu yao na kwamba wako huru kufanya taratibu nyingine zozote kama zile za kiimani, kimila na kikabila endapo watahitaji.

Waziri huyo wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu amesisitiza kuwa utaratibu mzuri umewekwa ambao utasaidia kutambua miili mingine mitatu ambayo nayo ilizikwa wakati wa mazishi ya kitaifa, na endapo ndugu watajitokeza itafanyiwa vipimo na baadae ndugu hao wa marehemu wataonyeshwa makaburi ya wapendwa wao.

Wakati wa mazishi hayo ya kitaifa yaliyofanyika kisiwani Ukara, miili Tisa ilizikwa, mitano ni baada ya kutambuliwa na ndugu zao kuridhia izikwe katika eneo hilo, huku mingine minne ikizikwa baada ya kutotambuliwa.

Michango zaidi yaendelea kutolewa

0

Michango zaidi inaendelea kutolewa na taasisi pamoja na watu mbalimbali kufuatia kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere Septemba 20 mwaka huu katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Akizungumza na TBC kutoka kisiwani Ukara, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi  na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kuwa mpaka sasa akaunti ya maafa imepokea jumla ya shilingi milioni 557.

Amesema miongoni mwa michango iliyopokelewa hii leo, ni pamoja na shilingi milioni 125 kutoka benki ya KCB na shilingi milioni kumi kutoka Benki ya Posta.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kamwelwe, kwa siku ya leo pekee akaunti hiyo ya maafa  imepokea jumla ya shilingi milioni 160.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesisitiza kuwa fedha hizo zitatumika kama ilivyokusudiwa.

Kuhusu kazi ya kunasua kivuko hicho cha MV Nyerere, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa kazi hiyo iko katika hatua ya mwisho ambayo ni kukinyanyua na kwamba kitanyanyuliwa muda mfupi ujao.

Trump kukutana tena na kiongozi wa Korea Kaskazini

0

Rais Donald Trump  wa Marekani amesema kuwa anatarajia kukutana kwa mara ya pili na Rais Kim Jong-un  wa Korea Kaskazini  katika siku za hivi karibuni.

Akizungumza na Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini mjini New York nchini Marekani, Trump  amesema kuwa mambo mazuri yamekwishafikiwa toka akutane kwa mara ya kwanza na kiongozi huyo wa Korea Kaskazini nchini Singapore.

Kwa mujibu wa Trump, uhusiano kati ya Marekani na Korea Kaskazini umezidi kuimarika hasa baada ya mkutano wake na Rais Kim mwezi June mwaka huu, mkutano ambao ameuita kuwa ulikua ni wa kihistoria.

Amesema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo ataandaa mkutano mwingine kati yake na kiongozi huyo wa Korea Kaskazini hivi karibuni bila kueleza utafanyika wapi.

Modric mchezaji bora wa mwaka wa Fifa

0

Kiungo wa kimataifa wa Croatia,-Luca Modric ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Fifa baada ya kuwashinda Cristiano Ronaldo na Mohamed Salah.

Nyota huyo anayechezea Real Madrid aliisaidia klabu hiyo kushinda mataji matatu mfululizo ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya pamoja na kulisaidia taifa lake la Croatia kufika fainali ya kombe la Fifa la dunia.

Hii ni mara ya kwanza baada ya miaka kumi kupita tuzo kubwa duniani kunyakuliwa na mchezaji tofauti ya Ronaldo na Messi ambapo mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2007 pale Mbrazil Ricardo Kaka aliposhinda tuzo ya Balon d’or.

Kwa upande wa goli bora la mwaka,  tuzo imeenda kwa Mohamed Salah wa Liverpool ambapo bao lake alilofunga dhidi ya Everton mwezi Disemba mwaka jana limeteuliwa kuwa goli bora la mwaka.

Ushindi huo hata hivyo umeibua mjadala hasa kutokana na ubora wa magoli mawili yaliyoshindwa likiwemo lile la Cristiano Ronaldo dhidi ya Juventus na lile la Gareth Bale dhidi ya Liverpool katika michuano ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya.

Tuzo ya kocha bora wa mwaka imeenda kwa Didier Deschamp wa Ufaransa wakati tuzo ya mchezaji bora wa kike ikienda wa Marta wa Brazil na tuzo ya mashabiki bora imeenda kwa mashabiki wa timu ya Taifa ya Peru.