Soko la mitumba laungua Mwanza

0

Soko la mitumba Mlango Mmoja lililopo jijini Mwanza limeungua moto alfajiri ya leo na kusababisha hasara ya mali kwa wafanyabiashara wa soko hilo.

Moto huo ulioanza majira ya alfajiri ya leo unadaiwa kusababishwa na shughuli za mama lishe wanaowahi asubuhi kuandaa vyakula sokoni hapo.

Kazi ya kuzima moto huo bado inaendelea.

Kazi ya kunasua kivuko cha MV Nyerere yaendelea

0

Zoezi la kukinasua kivuko cha MV Nyerere kilichozama ziwa Victoria katika kisiwa cha Ukara mkoani Mwanza limeendelea ambapo mchana huu kivuko hicho kimevutwa kuelekea ufukweni.

Katika zoezi hilo ambalo linaendeshwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania – JWTZ kwa kushirikiana na wataalam kutoka taasisi mbalimbali kivuko hicho cha MV Nyerere kimevutwa kwa kutumia matingatinga huku wataalam wakitoa maji nje ya kivuko hicho.

Marwa aihama CHADEMA

0

Mbunge wa jimbo la Serengeti mkoani Mara kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Marwa Ryoba Chacha amejivua uanachama wa chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Marwa amesema kuwa amefikia uamuzi huo ikiwa ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya Rais John Magufuli katika kuwatumikia na kuwaletea maendeleo Watanzania.

Rais Magufuli akutana na mjukuu wa Malkia Elizabeth II

0

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mjukuu wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza, -Prince William Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo Prince William ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uingereza na amemshukuru Rais Magufuli kwa kupata nafasi ya kuzungumza nae.

Prince William amezungumzia juhudi anazozifanya katika uhifadhi wa wanyamapori na amemuomba Rais Magufuli kuendelea kushirikiana nae katika kukabiliana na vitendo vya ujangili hasa wa Tembo.

Kwa upande wake Rais Magufuli amemkaribisha Prince William kuja Tanzania wakati wowote na amemuhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Uingereza hasa katika uhifadhi wa wanyamapori.

“Naomba ufikishe salamu zangu kwa Malkia Elizabeth II, mwambie Watanzania tunaipenda Uingereza na tutaendeleza na kuuimarisha zaidi ushirikiano wetu mzuri kwa manufaa yetu sote” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameongeza kuwa serikali ya awamu ya tano imefanya juhudi kubwa za kukabiliana na ujangili hasa wa Tembo ambapo kwa sasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba anatarajia Prince William ataunga mkono juhudi hizo ili kukomesha kabisa ujangili katika hifadhi zote za wanyamapori nchini.

Prince William atakuwa nchini kwa muda wa siku nne hadi Septemba 29 mwaka huu.

Vigogo sita bodi ya wakulima wa chai Mponde mahakamani

0

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini -TAKUKURU imewafikisha mahakamani vigogo sita wa bodi ya wakurugenzi wa kiwanda cha wakulima wa chai cha MPONDE kwa tuhuma za uhujumu uchumi.

Watuhumiwa hao wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Mkoa wa TANGA na kusomewa mashtaka mawili yanayohusu uhujumu uchumi.

Waliofikishwa mahakamani hapo ni Nawab Mulla, Shahdad Mulla, William Shellukindo,Richard Mbughuni, Richard Madandi na Rajab Msagati.

Akisoma hati ya mashitaka, mwanasheria wa serikali, Seth Mkemwa akisaidiana na Magubo Waziri wameieleza mahakama kuwa kati ya mwaka 2000 na 2013 watuhumiwa wote kwa pamoja walikula njama na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni 30.

Mkemwa alieleza kosa la kwanza la watuhumiwa hao kuwa kati ya January 2000 hadi desemba 2013 washtakiwa walikula njama na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni 30.

Kosa la pili ni kuwa watuhumiwa hao mnamo Januari mwaka 2000 na Desemba 2013 kwa nia ovu wameidanganya Mamlaka ya Mapato Nchini -TRA kutaka msamaha wa kodi katika vifaa mbalimbali walivyodai kuviingiza kwa ajili ya wakulima wadogo wa chai jambo ambalo si kweli.

Mkutano Mkuu wa ALAT wafunguliwa Dodoma

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kuboresha maeneo ya utawala kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo na kuongeza uwezo wa halmashauri kujiendesha zenyewe.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT).

Kauli hiyo ya Waziri Mkuu ameitoa baada ya kuwepo kwa maombi mengi ya kuanzisha maeneo mapya ya utawala nchini.

Amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2014/2015, jumla ya halmashauri 66 na mkoa mmoja wa Songwe vilianzishwa pamoja na vijiji 1,949, mitaa 1,379 na vitongoji 8,777.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, hadi sasa maeneo hayo hayajaweza kuwa na miundombinu, vifaa na watumishi wa kutosha ili kuwezesha wananchi kupata huduma iliyokusudiwa.

Ametolea mfano mkoa wa Songwe ambapo halmashauri zake zote hata halmashauri ya wilaya ya Mbozi ambapo ndiyo makao makuu ya mkoa bado haujafikia vigezo vya kuwa Manispaa.

“Baadhi ya halmashauri zinaendelea na ujenzi wa ofisi wakati nyingine kama Mafia, Rufiji, Handeni na Ludewa zipo kwenye magofu na huwezi kuamini kama ni Ofisi za Halmashauri” amesema Waziri Mkuu.

“Taarifa nilizonazo hadi sasa ni kwamba tayari shilingi bilioni 120.7 zimepokelewa kwenye halmashauri mbalimbali kati ya shilingi bilioni 238.8 zinazohitajika kukamilisha ujenzi wa majengo ya halmashauri” ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesema kuwa kiasi kilichobaki kitaendelea kutolewa kupitia bajeti ya serikali na mapato ya ndani ya halmashauri ambapo baadhi yake zitapewa fedha za kukamilisha ujenzi baada ya uhakiki kwa sababu zimekuwa zikipokea fedha kwa muda mrefu.

Kivuko cha MV Nyerere chainuliwa kwa asilimia 85

0

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo amesema zoezi la kukinasua kivuko cha MV Nyerere amesema vikosi vya ulinzi vimefanikiwa kukiinua kivuko hicho kwa asilimia 85 na kazi iliyobaki ni kutoa maji yaliyoingia kwenye kivuko.

Jenerali Mabeyo amesema wataalam wataendelea na kazi ya kutoa maji katika kivuko hicho na kukiweka pembeni kwa ajili ya ukaguzi.

Amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa jinsi vinavyoendelea kuwezesha zoezi hilo huku akilipongeza Shirika la Utangazaji Tanzania –TBC kwa kuhabarisha umma yale yaliyokuwa yakiendelea baada ya kutokea kwa ajali hiyo.

Flyover ya Mfugale yafunguliwa rasmi

0

Rais John Magufuli amefungua daraja za juu katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela eneo la Tazara jijini Dar es salaam (Mfugale Flyover) ambazo zitasaidia kupunguza msongamano wa magari katika barabara hizo, ikiwemo kwenda na kutoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.

Mfugale Flyover imejengwa na kampuni ya ujenzi ya Sumitomo Mitsui Construction Co. Ltd ya Japan kwa gharama ya shilingi bilioni 106.7.

Ujenzi wa Mfugale Flyover umehusisha njia nne za barabara zenye urefu wa kilomita moja, ina uwezo wa kubeba uzito wa tani 180 kwa wakati mmoja, imesanifiwa kuishi kwa miaka mia moja, ina barabara za pembeni, njia za waenda kwa miguu, mfumo wa mifereji ya maji ya mvua, taa za kuongozea magari na umezingatia mradi wa mabasi yaendayo haraka kwa kuacha eneo la mita 12 katikati ya barabara hizo.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema kuwa ujenzi wa Mfugale Flyover umekamilika kabla ya tarehe iliyopangwa ambayo ni Oktoba 31 mwaka huu na kwamba katika juhudi za kukabiliana na msongamano wa magari serikali itajenga Flyover nyingine eneo la Chang’ombe katika makutano ya barabara ya Nyerere na Kawawa.

Kufuatia uamuzi wa Rais Magufuli kuwa Flyover ya makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela iitwe Mfugale Flyover, Mwenyekiti wa bodi ya Usajili wa Wahandisi Mhandisi Profesa Ninatubu Lema amesoma wasifu wa Mhandisi Mfugale na kueleza kuwa ameitumikia nchi akiwa Mhandisi kwa miaka 41 ambapo katika kipindi hicho ameongoza katika kubuni na kusimamia ujenzi wa barabara kilomita 36,258 zikiwemo kilomita 9,951 za lami na amebuni na kusimamia ujenzi wa madaraja makubwa na madogo 1,400 yakiwemo madaraja makubwa ya Mkapa, Umoja, Rusumo, Kikwete, Nyerere, Magufuli na Sibiti.

Katika hotuba yake, Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Japan kwa kutoa mkopo nafuu wa ujenzi wa Mfugale Flyover, amewapongeza wakandarasi kwa kumaliza kazi mapema, ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa usimamizi wake wa karibu na kwa namna ya kipekee amempongeza Mhandisi Patrick Mfugale kwa mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Flyover hiyo, madaraja na barabara mbalimbali nchini.

Rais Magufuli ametoa wito kwa Wahandisi wengine na wataalamu mbalimbali nchini kuiga mfano wa Mhandisi Mfugale wa kutanguliza mbele maslahi ya Taifa badala ya kuwa kikwazo kwa kukosa uaminifu na uadilifu ama kutoa ushauri usio na manufaa kwa Taifa.

Amesema kuwa serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kuboresha miundombinu ya jiji la Dar es salaam kama ilivyoahidi na kwamba pamoja na kujenga Flyover nyingine katika eneo la Chang’ombe pia itajenga Flyover katika eneo la Machinjioni, inajenga barabara za juu katika eneo la Ubungo, inajenga barabara ya njia nane kutoka Kimara jijini Dar es salaam hadi Kibaha mkoani Pwani yenye urefu wa kilomita 19.2.

Rais Magufuli ameagiza mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara uitwao DMDP na ambao umetengewa shilingi bilioni 660 uhamishiwe kwenye Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

Ametoa wito kwa watumiaji wa Mfugale Flyover kuwa makini ili kuepuka ajali zisizo za lazima na ameagiza zifungwe kamera za kurekodi magari katika Flyover hiyo na nyingine zitakazojengwa jijini Dar es salaam.

Sherehe za ufunguzi wa Mfugale Flyover zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wizara, balozi wa Japan nchini anayemaliza muda wake Masaharu Yoshida, Wabunge wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Seleman Kakoso, viongozi wa dini, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa mkoa wa Dar es salaam.

Wakati huohuo Rais Magufuli ameagana na balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshida ambaye amemshukuru kwa ushirikiano mzuri alioupata kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu aliyokuwepo nchini.

Masaharu Yoshida amepongeza uongozi mzuri wa Rais Magufuli na juhudi kubwa anazozifanya katika kujenga uchumi wa Tanzania na ameahidi kuwa balozi mzuri wa Tanzania.