TPA yatakiwa kuharakisha ufungaji wa Flow Meters

0

 

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt  Philip Mpango ameiagiza Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) kuharakisha mchakato wa kufunga mita za kupima mafuta – Flow Meters katika bandari ya Tanga na kuharakisha urasimishaji wa bandari bubu nne katika mwambao wa bahari wa Tanga ili kudhibiti magendo na upotevu wa mapato ya serikali.

Dkt Mpango ametoa agizo hilo alipotembelea bandari ya Tanga kwa lengo la kujionea utendaji kazi wa bandari hiyo inayotajwa kuwa moja ya eneo muhimu na chanzo kikubwa cha mapato ya serikali lakini mchango wake hauonekani ipasavyo.

Amesema kuwa mchakato wa kumpata mzabuni wa kufunga mitambo hiyo umechukua muda mrefu licha ya kwamba uongozi wa juu wa serikali ulitoa maelekezo ya kufungwa mara moja kwa flow meter hizo.

Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, -Donald Ngaile amemweleza Dkt Mpango kuwa mfumo wa kupima mafuta kwa njia ya flow meter haufanyikazi tangu ufungwe miaka mitatu iliyopita kwa sababu ya uchakavu.

Dkt Mpango pia ameuhimiza uongozi wa TPA kuharakisha urasimishaji wa bandari nne bubu zilizoko bahari ya hindi katika mwambao wa Tanga kwenye wilaya za Muheza, Pangani na Mkinga ili kudhibiti biashara ya magendo inayoikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi.

 

Ujenzi wa meli MV Mbeya II wafikia asilimia 80

0

Ujenzi wa meli mpya ya abiria ya MV Mbeya II inayotarajiwa kutatua changamoto za usafiri wa abiria pamoja na mizigo katika mwambao wa ziwa Nyasa umefikia asilimia 80.

Meneja wa bandari katika ziwa Nyasa,- Abed Gallus amesema kuwa meli hiyo itakayokua ya kwanza ya kisasa ya abiria itaunganisha mikoa mitatu ya Mbeya, Njombe na Ruvuma pamoja na nchi jirani za Malawi na Zambia.

Gallus amesema kuwa ujenzi wa meli hiyo unaofanywa na kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine ni moja ya juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) katika kuboresha shughuli za usafirishaji wa abiria pamoja na mizigo majini.

“Ujenzi wa meli hii ya abiria, ni sehemu ya utekelezaji wa ujenzi wa meli tatu za TPA katika ziwa Nyasa zinazolenga kutatua changamoto za usafiri wa abiria na mizigo majini,” amesema Gallus.

Ameongeza kuwa,  TPA ilianzisha mradi wa meli tatu zikiwemo mbili za mizigo zenye uwezo wa kubeba tani elfu moja na moja ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200.

Ujenzi wa meli hiyo ya abiria ya MV Mbeya II unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni tisa.

Meli hiyo mpya ya MV Mbeya II inatarajia kufanya safari zake katika bandari mbalimbali kongwe na nyingine mpya zitakazoanzishwa na TPA katika mwambao wa ziwa Nyasa, lengo likiwa ni kuleta ufanisi katika usafirishaji wa abiria na mizigo.

 

 

Idadi ya waliokufa Indonesia yaongezeka

0

Zaidi ya watu 840 wamethibitika kufa baada ya tetemeko la ardhi na tetemeko chini ya bahari – Tsunami kupiga katika maeneo kadhaa nchini Indonesia.

Habari kutoka nchini Indonesia zinasema kuwa juhudi za kuwatafuta watu walionusurika katika tetemeko hilo zinaendelea huku idadi ya watu waliokufa ikitarajiwa kuongezeka.

Idadi ya watu waliokufa katika tetemeko hilo nchini Indonesia inatarajiwa kuongezeka kwa kuwa mpaka sasa maeneo mengi hasa ya vijijini  yaliyokumbwa na tetemeko hilo hayajafikiwa na vikosi vya uokoaji.

Katika mji wa Palu, vikosi vya uokoaji vinajaribu kuwafikia mamia ya watu ambao wanadhaniwa kuwa wako hai huku wakiwa wamefukiwa kwenye vifusi vya miundombinu mbalimbali.

Akizungumza mara baada ya kutembelea mji huo wa Palu,  Rais Joko Widodo wa Indonesia amewaagiza viongozi wa mji huo kushirikiana na serikali kuu kutoa mahitaji yote muhimu kwa wakazi wa mji huo pamoja na kufanya matengenezo ya miundombinu iliyoharibiwa.

Kwa mujibu wa Shirika la msalaba mwekundu, takribani watu milioni moja nukta sita wameathiriwa na tetemeko hilo la ardhi pamoja na tetemeko la chini ya bahari –  Tsunami na kwamba madhara ya tetemeko hilo yanaweza kuwa makubwa zaidi.

Nyamilandu mjumbe mpya Baraza Kuu FIFA

0

Rais wa chama cha soka cha nchini Malawi,- Walter Nyamilandu amechaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) atakayeliwakilisha Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).

Katika uchaguzi huo uliofanyika nchini Misri, Nyamilandu amepata kura 35 na kumshinda Danny Jordaan ambaye ni Rais wa chama cha soka nchini Afrika Kusini aliyepata kura 18 baada ya mizunguko miwili ya upigaji kura kukamilika.

Katika uchaguzi huo kulikuwa na mizunguko mitatu ya upigaji kura ambapo katika mzunguko wa kwanza walikuwepo wagombea watatu akiwemo aliyekuwa rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), – Leodgar Tenga ambaye aliondolewa katika raundi ya kwanza.

Rais wa shirikisho la soka nchini Kenya, -Nick Mwendwa na yule wa chama cha soka nchini Seychelles,- Elvis Chetty walijitoa katika kinyang’anyiro hicho mapema kabla ya upigaji kura katika mzunguko wa kwanza.

Baraza Kuu la FIFA ndilo lenye dhamana ya kuendesha na kusimamia shughuli zote za mpira wa miguu duniani na wajumbe wake hutoka katika mashirikisho ya soka kwenye mabara yote.

Uchaguzi huo umefanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa rais wa chama cha soka nchini Ghana, -Kwesi Nyantakyi aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya kupokea rushwa ya dola elfu 65 za kimarekani kutoka kwa mwandishi wa habari aliyejifanya ni mwekezaji wa soka.

 

Vettel ajitapa kushinda

0

Dereva wa kampuni ya Ferari, -Sebastian Vettel amesema kuwa bado ana nafasi ya kushinda taji la mbio za langalanga msimu huu licha ya kuachwa kwa tofauti ya alama hamsini na mpinzani wake mkubwa Lewis Hamilton.

Hamilton amejiweka katika nafasi nzuri ya kushinda taji la tano la mbio za langalanga baada ya kuibuka kinara katika michuano ya Russian Grand Pri iliyofanyika mjini Sochi.

Ushindi huo unamfanya Hamilton kufikisha alama 306 katika nafasi ya kwanza kwenye msimamo, huku Vettel akiwa katika nafasi ya pili akiwa na alama 256.

Vettel amesema kuwa anajua si kazi rahisi kupindua matokeo hayo lakini atafanya kila analoweza kuwashangaza wengi mwisho wa msimu.

Mpaka sasa yamebaki mashindano matano kukamilisha msimu yatakayofanyika katika nchi za Japan, Marekani, Mexico, Brazil na Abu Dhabi.

Ligi kuu Bara kuendelea leo

0

Ligi kuu Tanzania Bara inaendelea kutimua vumbi leo Jumatatu kwa michezo Sita kuchezwa katika viwanja tofauti.

Vinara wa ligi hiyo Mbao FC wenye alama 14 wanasafiri hadi kwenye dimba la Mabatini pale Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani kumenyana na wenyeji Ruvu Shooting wenye alama tano huku maafande wa JKT Tanzania wakiwa nyumbani kwenye dimba la Jenerali Isamuhyo kuwaalika African Lyon.

Michezo mingine,  chama la wana Stand United watakuwa nyumbani kwenye dimba la Kambarage mjini Shinyanga kukipiga na Mbeya City wakati wakulima wa alizeti Singida United wakiwa kwenye dimba la Namfua mjini Singida kuwaalika wanapaluhengo Lipuli FC ya Iringa.

Wagosi wa kaya Coastal Union wenyewe wana kibarua cha kukabiliana na Mwadui FC,  mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Mkwakwani jijini Tanga wakati wana tamtam Mtibwa Sugar wakiwa katikati ya mashamba ya miwa huko Turiani wilayani Mvomero mkoani Morogoro wakiwakaribisha Biashara United ya Mara kwenye dimba la Manungu Complex.

Katika mchezo pekee wa ligi hiyo uliochezwa jana kwenye dimba la Taifa jijini Dar es salaam, watani wa jadi Simba na Yanga wameshindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu katika mchezo ambao kwa kiasi kikubwa ulitawaliwa na Simba walioshindwa kuzitumia nafasi walizopata kufunga huku mlinda mlango wa Yanga, Beno Kakolanya akiibuka shujaa wa mchezo huo.

 

Kivuko cha MV Nyerere chanasuliwa

0

Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe amesema zoezi la kukinasua kivuko cha MV Nyerere kilichozama kwenye ziwa Victoria katika kisiwa cha Ukara mkoani Mwanza limekamilika rasmi hii leo.

Akizungumza na TBC Waziri Kamwelwe amesema zoezi hilo lililoendeshwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania -JWTZ kwa kushirikiana na wataalam wa taasisi mbalimbali limehitimishwa rasmi hii leo.

Amesema kwa sasa wakazi wa eneo hilo watatumia kivuko cha MV Ukara chenye uwezo wa kubeba abiria 70 tu bila mizigo.

Amesema hadi kufikia leo zaidi ya shilingi milioni mia tisa zimepatikana na zoezi la michango litasitishwa ifikapo kesho Septemba 29 saa saba mchana.

Kivuko cha MV Nyerere kilizama Septemba 20 mwaka huu mita 50 kufika kwenye gati.

Kivuko cha MV Ukara chaanza kufanyiwa majaribio

0

Wakati kivuko cha MV Nyerere kikiendelea kuvutwa ili kufika mwaloni, kivuko cha MV Ukara ambacho kilikuwa kikifanyiwa matengenezo kimeanza kufanyiwa majaribio ili kutoa huduma ya kusafirisha watu kati ya kisiwa cha Ukara na Bugorola wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Mwandishi wa TBC aliyeko kisiwani Ukara amesema kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba watu 70, kitaanza kufanya kazi pindi wataalam watakapojiridhisha kwamba kiko tayari kutoa huduma.

Kivuko hicho kitatumika wakati huu ambapo serikali inaendelea na mchakato wa kupata mzabuni atakayetengeza kivuko kipya kwa ajili ya wakazi wa maeneo hayo.