NIDA yapata Mkurugenzi Mkuu mpya

0

Rais John Magufuli amemteua Dkt Arnold Kihaule kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Uteuzi wa Dkt Kihaule unaanza leo Oktoba tatu.

Kabla ya uteuzi huo Dkt Kihaule alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU).

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango aitembelea TBC

0

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James ametembelea Shirika la Utangazaji Tanzania -TBC jijini Dar Es Salaam na kusema serikali inatambua changamoto zinazoikabili TBC na kuahidi kuzifanyia kazi.

Akizungumza na wafanyakazi wa TBC, Dotto amewapongeza wafanyakazi wa shirika hilo kwa kufanya kazi kwa ustahimilivu na kuahidi kutatua changamoto zinazoikabili TBC ili ifanye kazi kwa ufanisi.

 Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba ameshukuru kwa ujio wa Katibu Mkuu James na kusema Shirika la Utangazaji Tanzania litaendelea kuwatumikia watanzania wote.

Hii ni ziara ya kwanza kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango kutembelea TBC.

Misaada yaendelea kutolewa Indonesia

0

Misaada mbalimbali imeendelea kutolewa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi  na tetemeko la chini ya bahari – Tsunami nchini Indonesia.

Misaada hiyo ambayo ni pamoja na ile ya chakula, maji na mafuta ya kula inasambazwa na wafanyakazi wa kutoa msaada ambao wamekua wakisindikizwa na vikosi vya ulinzi na usalama.

Taarifa kutoka nchini Indonesia zinasema kuwa zaidi ya watu elfu moja na mia tatu wamethibitika kufa hadi sasa, na idadi ya waliokufa itaendelea kuongezeka.

Tetemeko lenye ukubwa wa 7.5 kwenye vipimo vya matetemeko ya ardhi – Richta lilikipiga kisiwa cha Sulawesi na kusababisha tetemeko jingine chini ya bahari katika pwani ya mji wa Palu.

Ofisi ya shirika la msalaba mwekundu nchini Indonesia imesema kuwa miili 34 ya wanafunzi imepatikana katika kanisa moja ikiwa imefukiwa na kifusi.

Wanafunzi hao ni miongoni mwa wanafunzi 86 walioripotiwa kuwa hawajulikani walipo katika shule ya biblia ya Jonooge iliyopo katika kanisa hilo na kwamba hadi sasa wanafunzi wengine 52 hawajulikani walipo.

Mashirika yatakiwa kutia saini mikataba ya utendaji kazi

0

Ofisi ya Msajili wa Hazina imetoa muda wa mwezi mmoja kwa mashirika na taasisi za umma ambazo hazijakamilisha taratibu za kutia saini  mikataba ya utendaji kazi kwa mwaka 2018/2019 kufanya hivyo haraka iwezekanavyo.

Akizungumza jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya utendaji kazi kwa taasisi na mashirika ya umma themanini kwa mwaka 2018/2019, Msajili wa Hazina, – Athuman Mbuttuka amesema kuwa mikataba ya utendaji kazi ni utekelezaji wa sheria na kwamba serikali itaendelea kusimamia taasisi na mashirika hayo ili yaweze kufikia malengo yaliyojiwekwa.

Amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2017/2018, serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina iliwekana saini na taasisi pamoja na mashirika ya umma 105 mikataba ya utendaji kazi na kuzitaka taasisi zilizobaki kukamilisha taratibu hizo kabla ya serikali haijaanza kuzichukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Rais Magufuli atimiza ahadi yake, fedha zakabidhiwa

0

Rais John Magufuli leo Oktoba Pili ametekeleza ahadi yake ya kutoa shilingi milioni Ishirini kwa ajili ujenzi wa ofisi ya wavuvi wadogo (UWAWAKI) waliopo katika eneo la Feri wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam.

Rais Magufuli alitoa ahadi hiyo Oktoba Mosi hapo jana alipokutana na wajasiriamali hao wakati akifanya mazoezi ya jioni pamoja na mke wake Mama Janeth Magufuli ambaye pia ametekeleza ahadi yake ya kutoa shilingi milioni Tano kwa akina mama wajasiriamali wanaofanya biashara ndogo hasa ya Mamalishe katika eneo hilo.

Fedha hizo zimekabidhiwa na Katibu wa Rais Ngusa Samike kwa Makamu Mwenyekiti wa UWAWAKI, – Amir Amani na kiongozi wa akina Mama wajasiariamali Ashura Nanjonga na kushuhudiwa na mkuu wa wilaya ya Ilala, – Sofia Mjema na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, – Tulusubisya Kamalama.

Kabla ya kukabidhi fedha hizo, Ngusa amesema kuwa pamoja na kutoa fedha hizo Rais Magufuli ameiagiza manispaa ya Ilala impelekee taarifa ya mapato na matumizi ya soko la samaki la Feri haraka iwezekanavyo na amemuagiza Mkuu wa wilaya na Manispaa ya Ilala kushughulikia kero za wavuvi na wajasiriamali wa eneo hilo ikiwemo ushuru wenye kero na tatizo la vyoo.

Makamu Mwenyekiti wa UWAWAKI, -Amir Amani na kiongozi wa akina mama wajasiriamali wa Feri, – Ashura Nanjonga wamemshukuru Rais Magufuli kwa kuwasaidia fedha hizo na kwa kuwajali wao pamoja na Watanzania wengine hasa wanyonge.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, -Sofia Mjema amemshukuru Rais Magufuli kwa kutembelea soko la Feri na kuwasaidia wajasiriamali wa soko hilo na amesema kuwa yeye na timu yake ya viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Ilala wataanza mara moja kushughulikia kero za wajasiriamali hao.

NECTA yafuta matokeo kwa baadhi ya shule

0

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza kufuta matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi uliofanyika tarehe Sita na Saba mwezi Septemba mwaka huu katika shule zote za msingi za halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma.

Shule nyingine za msingi zilizofutiwa matokeo hayo ni Hazina na New Hazina zilizopo katika manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es salaam, Aniny Nndumi na Fountain Joy za Ubungo jijini Dar es salaam, shule za msingi za Alliance, New Alliance na Kisiwani za mkoani Mwanza, pamoja na Kondoa Integrity iliyopo wilayani Kondoa mkoani Dodoma.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt Charles Msonde amesema kuwa Baraza hilo limefikia uamuzi huo kutokana na kuwepo kwa vitendo vya wizi na uvujaji wa mitihani hiyo vilivyofanywa na baadhi ya watumishi waliopewa dhamana ya kuilinda mitihani hiyo, vitendo vilivyobainika katika shule na vituo vya kufanyia mitihani.

Dkt Msonde amesema kuwa kufuatia kufutwa kwa matokeo ya mtihani huo, mitihani ya shule zote zilizofutiwa matokeo itarejewa tarehe Nane na Tisa mwezi huu.

Ameongeza kuwa NECTA pia imefuta vituo vya mitihani vya shule za msingi za Hazina, New Hazina, Aniny Nndumi, Fountain Joy, Alliance, New Alliance, Kisiwani na Kondoa Integrity hadi hapo Baraza la Mitihani Tanzania litakapojiridhisha kuwa havitakiuka tena kanuni za mitihani.

Tayari NECTA imeziarifu mamlaka za ajira na za usimamizi wa sheria kuwachukulia hatua kali watumishi wote na mtu yeyote aliyebainika kujihusisha na kuvujisha mtihani huo kwa mujibu wa kanuni za utumishi na sheria za nchi.

Waliopotosha mipaka Kilosa kukiona

0

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekabidhi taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa kijiji cha Mabwegere na vijiji saba vya wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro na kuagiza wote waliohusika kupotosha mipaka ya eneo hilo kuchukuliwa hatua za kisheria.

Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo mkoani Morogoro wakati akikabidhi taarifa ya uchunguzi wa mgogoro huo kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe Stephen.

“Wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine katika process yote ambayo kwa kiasi fulani imeigharimu serikali fedha nyingi na kuipa maumivu serikali katika suala hilo ni lazima wachukuliwe hatua kali” amesema waziri Lukuvi.

Uchunguzi wa mgogoro huo uliofanywa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacob Mwambegele umebaini kuwa chanzo cha mgogoro huo ni kukosekana kwa ushirikishwaji wa vijiji jirani katika kuainisha na kuweka mipaka ya kijiji cha Mabwegere na hivyo kusababisha kijiji hicho kiwe na eneo lenye ukubwa wa hekta 10,234.

Hata hivyo  Waziri Lukuvi amesema kuwa serikali haijakifuta kijiji cha Mabwegere bali ni kutekeleza taarifa ya uchunguzi ya kufuta mipaka ya kijiji hicho ambapo kwa sasa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na wilaya ya Kilosa itatakiwa kuanza mchakato wa kuandaa upya mipaka ya vijiji hivyo kwa njia shirikishi.

Katika taarifa yake, Jaji Mwambegere amependekeza kwa nia ya kuboresha utendaji kazi, weledi, maadili, umakini na uwezo wa kulinda na kutunza kumbukumbu katika idara ya upimaji na ramani na ofisi ya kamishna wa ardhi, hatua za kinidhamu zichukuliwe ili kuzuia migogoro ya ardhi.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Mendeleo ya Makazi  ilikosea katika zoezi la upimaji kwa kuanzisha kijiji cha Mabwegere lakini wilaya ya Kilosa itakuwa na jukumu la kuanza mchakato upya wa upimaji katika vijiji hivyo.

Amesisitiza kuwa shughuli za binadamu kama vile ufugaji hazihusiani na masuala ya mipaka,  hivyo wilaya ya Kilosa pamoja na kushughulikia suala la mipaka lazima iandae mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuanza  kupendekeza maeneo ya ufugaji kwa vijiji vyote saba na kwamba ni lazima busara itumike katika kushughulikia jambo hilo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Tamisemi, -Joseph Kakunda amesema kuwa uanzishwaji wa kijiji cha Mabwegere haukufuata sheria na kuwataka wataalamu kuacha kuwa na  nidhamu ya woga na kuzingatia kanuni na sheria katika kutekeleza maj

Siku ya wazee duniani yaadhimishwa

0

Rais Mstaafu  wa awamu ya pili mzee Ali Hassan Mwinyi amesema kuwa serikali inatambua matatizo na changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee nchini na inafanya jitihada kubwa katika kuzitatua changamoto hizo.

Mzee Mwinyi ametoa kauli hiyo mkoani Arusha wakati wa maadhimisho ya siku ya wazee duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani humo, ambapo amemwakilisha Rais John Magufuli.

Kwa mujibu wa mzee Mwinyi, wazee nchini  wana changamoto nyingi zinazotakiwa kushughulikiwa kwa haraka ikiwa ni pamoja na namna ya kupata huduma bora za afya na ulinzi dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyotokana na imani za kishikirina.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo ya siku ya wazee duniani, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, -Ummy Mwalimu amesema kuwa tayari serikali imeshaandaa sheria itakayosimamia maslahi ya wazee nchini.

Siku ya wazee duniani huadhimishwa Oktoba Mosi ya kila mwaka  ambapo kauli mbiu kwa  mwaka huu  ni kuwaenzi watetezi wazee wa haki za binadamu kwa kuimarisha haki zao, kuzidisha utambuzi wao katika jamii na kutatua changamoto wanazopitia.