Waziri Mkuu kuanza ziara Kagera

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Oktoba Sita mwaka huu anatarajia kuanza ziara ya kikazi ya  siku nne mkoani Kagera.

Akiwa mkoani humo, Waziri Mkuu Majaliwa atatembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo zile za kilimo, afya, elimu na viwanda.

Taarifa iliyotolewa na mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti imewataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kumpokea kiongozi huyo.

Wakati wa ziara yake mkoani Kagera, Waziri Mkuu Majaliwa atatembelea wilaya za Bukoba, Kyerwa, Karagwe, Muleba na Biharamulo.

 

Wagonjwa 36 wafanyiwa upasuaji wa moyo

0

Jumla ya wagonjwa 36  wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na bila kufungua kifua katika kambi maalum ya matibabu inayofanyika katika Taasisi ya Moyo  Jakaya Kikwete (JKCI).

Upasuaji huo unafanywa na madaktari bingwa wa moyo wa taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Albalsam  Care & Care la nchini Saudi Arabia ambapo wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa kufungua kifua ni kumi na bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab kwa njia ya kutoboa tundu dogo katika  paja ni 26.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa JKCI, -Bashir Nyangasa amesema kuwa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji hali zao zinaendelea vizuri na wengine wameshatoka katika chumba cha uangalizi maalum na kurudi wodini kwa ajili ya kufanya mazoezi pamoja na matibabu.

“Tunafanya upasuaji wa kubadilisha valvu kwa wagonjwa ambao  valvu zao hazifanyi kazi vizuri, kubadilisha  mishipa ya moyo inayosafirisha damu kutoka mishipa mikubwa kwenda kwenye mzunguko wa moyo na kuziba matundu kwenye moyo kwa watu waliozaliwa na matundu hayo”, amesema Dkt Nyangasa.

“Katika kambi hii tumemfanyia upasuaji wa kupandikiza mshipa wa damu kutoka kwenye mguu na kuuweka kwenye moyo mgonjwa aliyekuwa na maradhi mawili ya moyo ambayo  ni kuziba kwa mishipa ya damu na mlango mkubwa wa moyo”, ameongeza Dkt Nyangasa.

Kwa upande wake  daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Shirika la Albalsam Care and Care la nchini Saudi Arabia,- Emad Bukhari ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kuwekeza  katika vifaa vya kisasa vya matibabu ya moyo.

“Kuwepo kwa mashine hizi za kisasa, wataalam pamoja na huduma nzuri  za kibingwa katika Taasisi hii, kumeifanya  kutambulika kimataifa na  hivyo kuzifanya taasisi zinazotibu magonjwa ya moyo Duniani kuja mahali hapa kutoa huduma kwa wananchi”, amesema Dkt Bukhari.

Kambi hiyo maalum ya matibabu inayofanyika katika Taasisi ya Moyo  ya Jakaya Kikwete, inafanyika kwa pamoja na utoaji wa elimu na ubadilishanaji wa ujuzi wa kazi ambao umewajengea uwezo madaktari, wauguzi pamoja na wataalamu wa mashine za moyo.

 

 

Wadau watakiwa kujitokeza kuishangilia Stars

0

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe  ameendelea kuwasisitiza wadau wa michezo  nchini kukata tiketi kwa ajili ya kwenda Cape Verde kuishangilia timu ya Taifa ya  mpira wa miguu -Taifa Stars ambayo itasafiri na ndege ya Dreamliner kwa ajili ya mchezo wa kufuzu kwa fainali za AFCON, mchezo utakaochezwa Oktoba 12 mwaka huu mjini Pria.

Akizungumza katika kipindi cha Meza ya Michezo kitachotangazwa na TBC I, Waziri  Mwakyembe amesema kuwa  tiketi za ndege zitauzwa kwa dola 1, 500 za Kimarekani na nyingine kwa dola 2000 za kimarekani kwa safari ya kwenda na kurudi.

Waziri  Mwakyembe amesema kuwa ili kuhakikisha safari hiyo inafanikiwa, serikali imetoa ndege hiyo ya Dreamliner ambayo itabeba wachezaji wa timu ya taifa na viongozi wake kuelekea Cape Verde kwa ajili ya mechi hiyo na kuongeza kuwa mchezo huo ni muhimu kwa Taifa Stars, hivyo nguvu ya mashabiki wa kuishangilia inahitajika.

“Kwa kweli serikali yetu imeonyesha nia kwa kutoa ndege ya kisasa ya Dreamliner yenye uwezo wa kubeba watu 250 ambapo kikosi cha wachezaji kina watu 31, hivyo wanahitajika watu zaidi ya 200 kukamilisha idadi kamili ya abiria”amesema Dkt Mwakyembe.

Ameongeza kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) limelipa dola  elfu  69 za kimarekani  kwa ajili ya kusafirisha timu hiyo, huku nafasi zilizobaki ni kwa ajili ya wadau wa michezo walio tayari kuungana na Taifa Stars kuelekea Cape Verde.

“Kitendo cha timu kushuka Cape Verde na Dreamliner tena ndege ya nyumbani tayari tumekwishapiga goli mbili, hizo zingine namuachia Amunike na benchi la ufundi waongezee” ameongeza Dkt Mwakyembe.

Mchezo wa marudiano kati ya Taifa Stars na timu ya Taifa ya Cape Verde utafanyika siku tatu baadae yani oktoba 16.

Mara ya mwisho Tanzania kucheza fainali za AFCON ilikuwa mwaka 1980.

 

 

 

 

 

 

Rais Magufuli apokea hati za utambulisho za mabalozi

0

 

Rais John Magufuli kwa nyakati tofauti hii leo amepokea hati za utambulisho za mabalozi wapya watano wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Hafla ya kupokea hati hizo za mabalozi wapya wa Ubelgiji, Norway, Sweden, Palestina na Kuwait imefanyika Ikulu jijini Dar es salaam.

Mara baada ya Rais Magufuli kupokea hati hizo za utambulisho, alifanya mazungumzo na mabalozi hao wapya kwa nyakati tofauti, mazungumzo yalioyohusu masuala ya kiuchumi na kisiasa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Augustine Mahiga ambaye naye ameshuhudia mazungumzo hayo amesema kuwa Rais Magufuli na mabalozi hao wapya wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini wamesisitiza kudumishwa kwa uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na mataifa hayo.

Serikali yaokoa shilingi trilioni 3.2 kwa mwaka

0

Serikali imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi Trilioni 3.2 zikiwemo shilingi Trilioni 2.2 zilizookolewa kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii baada ya kufanya uhakiki wa madeni ya serikali, kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti feki.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Doto James amesema timu ya wataalam wanaotengeneza na kusimamia mifumo ya mapato ya serikali, wakaguzi na wataalamu wa bajeti pia imefanikiwa kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za serikali baada ya kuunganisha taasisi 304 katika mfumo unaodhibitiwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Katibu Mkuu huyo amebainisha hayo wakati akiwasilisha taarifa ya uanzishwaji wa mifumo katika taasisi za umma 304 kwa Rais Dkt. John Magufuli Ikulu jijini Dar Es Salaam na kusema fedha hizo zimeokolewa katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi mwaka 2017/18.

Aidha Rais Dkt. John Magufuli amewapongeza wataalamu hao kwa kazi nzuri waliyoifanya na kumuagiza Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kuhakikisha taasisi zote za serikali zinazopaswa kuunganishwa na mifumo ya udhibiti zinaunganishwa haraka iwezekanavyo.

Amesema fedha zilizopatikana baada ya udhibiti wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato zimesaidia kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya 208, ujenzi wa hospitali mpya 67, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa Standard Gauge Railway, madaraja, barabara, kusambaza umeme na maji.

Mhalifu sugu nchini Ufaransa akamatwa

0

Mhalifu sugu nchini Ufaransa ambaye alitoroka gerezani akitumia helikopta iliyokuwa imetekwa nyara Redoine Faid, amekamatwa tena na polisi.

Faid aliyekua akitafutwa  na vikosi vya ulinzi na usalama nchini Ufaransa, amekamatwa kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Paris akiwa na ndugu yake na watu wengine wawili.

Kwa mara ya mwisho, wanaume watatu walimtorosha Faid kutoka gereza moja huko Reau  na kumuingiza kwenye helikopta iliyokua ikiendeshwa na rubani aliyekuwa ametekwa nyara.

Mara kwa mara, mhalifu huyo mwenye umri wa miaka 46 amekua akijinasibu kuwa ni shabiki wa filamu za uhalifu za Hollywood  kama vile Al Pacino thriller Scarface  ambazo zimechangia mfumo wa maisha yake kwa kumfundisha namna ya kufanya uvamizi.

Mwaka 2013 alitoroka  gerezani mara tu baada ya kufikishwa katika gereza hilo  huku akitumia vilipuzi kulipua milango mitano ya gereza na kuwashika walinzi mateka na kuwatumia kama ngao.

Umaarufu wa Faid umechangiwa na kitabu chake alichokiandika mwaka 2009, kitabu kinachosimulia maisha yake akiwa mdogo kwenye mitaa ya Paris na kuibuka kuwa mhalifu.

 

Maeneo yaliyokumbwa na tetemeko Indonesia yafikiwa

0

Vikosi vya uokoaji nchini Indonesia vimesema kuwa vimeweza kuzifikia wilaya zote nne zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi pamoja na tetemeko la chini ya bahari – Tsunami katika kisiwa cha Sulawesi.

Wafanyakazi wa vikosi hivyo wamesema kuwa misaada ya chakula, maji na mafuta ya kula inaendelea kusambazwa katika maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na tetemeko hilo.

Hata hivyo wafanyakazi hao wamesema kuwa wamekua wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kuharibika kwa miundombinu hasa ya barabara, na hivyo kuathiri kazi ya kusambaza misaada hiyo.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa zaidi ya watu laki mbili walionusurika katika tetemeko hilo wanahitaji msaada wa haraka.

Mpaka sasa zaidi ya watu elfu moja na mia tatu wamethibitika kufa kutokana na tetemeko hilo la ardhi na lile la chini ya bahari – Tsunami huku  idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka.

Serikali kushughulikia changamoto za Skauti

0

Rais John Magufuli amesema kuwa serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Chama Cha Skauti nchini ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wakati yanapotokea majanga mbalimbali.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kumuapisha Katibu Mkuu wa wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikikiano wa Afrika Mashariki Dkt Faraji Mnyepe pamoja na Mwantumu Mahiza kuwa Skauti Mkuu wa Tanzania.

Ameongeza kuwa  serikali inatambua changamoto mbalmbali zinazokikabili Chama cha Skauti nchini na kwamba itaendelea kuzishughulikia.

Rais Magufuli ameelezea matumaini yake kwa Chama hicho cha Skauti nchini kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kushughulikia masuala mbalimbali chini ya uongozi wa Skauti Mkuu Mwantumu Mahiza.

Kwa upande wa Dkt Mnyepe, Rais Magufuli amemtaka kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kuleta mabadililiko ndani ya wizara hiyo ya Mambo ya Nje na Ushirikikiano wa Afrika Mashariki.

Amesema kuwa wizara hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi, hivyo ni vema akajipanga vizuri ili kuhakikisha anakabiliana na changamoto hizo.