Mahakamani kwa kuisabababishia serikali hasara ya mabilioni

0

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Carlos Gwamagobe na watendaji watano wa halmashauri hiyo wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Geita kwa tuhuma za kughushi nyaraka,utakatishaji fedha na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi bilioni mbili nukta nane.

Watendaji hao wamesomewa mashtaka matano mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Geita Jovita Kato.

Kutokana na kosa la nne la  utakatishaji fedha kuwanyima dhamana watuhumiwa hao wamerudishwa rumande baada ya kesi yao kuahirishwa hadi tarehe 22 ya mwezi huu.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya makosa hayo kati ya mwezi  Januari  mwaka 2016 hadi mwezi Juni  mwaka huu.

Marufuku kuingiza mifugo mapori ya Biharamulo, Buligi na Kimisi

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepiga marufuku wananchi kuingiza mifugo katika mapori ya akiba ya Biharamulo, Buligi na Kimisi.

Waziri Mkuu ambaye yuko ziarani mkoani Kagera amesema mapori hayo kwa sasa yapo katika hatua za mwisho kutangazwa kuwa mbuga za wanyama, hivyo kuifanya wilaya hiyo kuwa miongoni mwa wilaya za kitalii nchini.

Katika mkutano wa hadhara Biharamulo, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja anayesimamia mapori hayo, Bigilamungu Kagoma kuhakikisha mapori hayo yanalindwa na hakuna mifugo inayoingizwa.

Amesema shilingi bilioni 70 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji safi na salama katika wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.

Rais Kenyatta atoa rambirambi ya shilingi Milioni 125

0

Rais Dkt. John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Kenya hapa nchini Dkt. Dan Kazungu na kupokea hundi ya shilingi Milioni 125 kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ikiwa ni rambirambi ya ajali ya MV Nyerere iliyotokea tarehe 20 Septemba 2018 katika ziwa Victoria.

Akizungumza baada ya kukabidhi rambirambi hiyo kwa Rais Magufuli, Balozi wa Kenya nchini amesema Wananchi wa Kenya wanaungana na Watanzania katika majonzi ya kuwapoteza watu 228 na wengine kujeruhiwa.

Kwa upande wake Rais Dkt. Magufuli amemshukuru Rais Kenyatta na wananchi wa Kenya kwa kuguswa na ajali hiyo na ameahidi kuwa fedha hizo zitaelekezwa kuwasaidia wananchi wa visiwa vya Ukerewe ikiwa ni pamoja na kujenga hospitali kubwa yenye hadhi ya Wilaya.

“Mwambie Mhe. Rais kuwa nashukuru sana, tulipanga fedha tulizopata tujenge wodi za wagonjwa lakini sasa tumeamua tujenge hospitali kubwa yenye hadhi ya Wilaya, na kwa mchango huu tunaweza kuamua wodi moja tukaiita Wodi ya Kenyatta” amesisitiza Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika  – SADC Dkt. Stergomena Tax.

Dkt. Stergomena Tax amesema amekutana na Rais Magufuli kumpa taarifa rasmi kuwa Mkutano wa 38 wa SADC uliofanyika tarehe 17 – 18 Agosti mwaka huu mjini Windhoek Namibia umemteua Rais Magufuli kuwa Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 2018 hadi Agosti 2019, na kwa maana hiyo Rais Magufuli ndiye atakuwa Mwenyekiti ajaye wa SADC kwa kipindi cha mwaka 2019/2020.

Kwa upande wake Rais Dkt. Magufuli amempongeza Dkt. Tax kwa kuteuliwa kwa mara ya pili kuwa Katibu Mtendaji wa SADC na pia amempongeza kwa kazi nzuri anazofanya katika Jumuiya hiyo.

Rais Magufuli amesema amepokea kwa heshima kubwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa SADC na kwamba yupo tayari kushirikiana na viongozi wenzake wa Jumuiya hiyo katika kutekeleza jukumu hilo.

“Nimepokea kwa heshima kubwa na nipo tayari kufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na wenzangu” amesema Rais Magufuli.

Hali ya kawaida yarejea Indonesia

0

Siku kadhaa baada ya tetemeko la ardhi kuikumba Indonesia watoto katika mji wa Palu wameanza kurejea shule kufanya usafi kwenye baadhi ya vyumba vya madarasa ambavyo havikupata madhara.

Mkuu wa shule moja huko Kasiludin amewataka walimu wote kuhudhuria shule hii leo na kutoa taarifa za wanafunzi walioanza kuhudhuria masomo na taarifa za wale ambao wamefariki dunia.

Tetemeko hilo la ardhi limeua watu zaidi ya 1900, wengine 2500 wamejeruhiwa na 5000 hawajulikani walipo na zoezi la kuwatafuta watu wengine linatarajiwa kusitishwa Alhamisi wiki hii.

Trump na Kim kukutana tena

0

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amesema Rais Donald Trump wa Marekani na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un watakutana kwa mara ya pili hivi karibuni.

Marekani inataka muendelezo wa mazungumzo kuhusu kusitisha matumizi ya silaha za nyuklia.

Kim amemwambia Pompeo kuwa mazungumzo yake na Trump yatafanyika hivi karibuni na yupo tayari kusikiliza makubaliano watakayoyafikia.

Mara ya kwanza Kim alikutana na Trump mwezi June  mwaka huu ambapo walizungumzia kusitisha matumizi ya silaha za kinyuklia.

Pompeo yupo barani Asia ambapo amefanya ziara ya kikazi ya siku tatu katika nchi ya Japan na Korea Kaskazini ambapo hii leo pia atafanya mazungumzo na viongozi wa juu wa China.

Mwandishi wa habari Bulgaria auawa

0

Mwandishi wa habari za kiuchunguzi wa runinga nchini Bulgaria Victoria Marinova amebakwa na kisha kuuawa.

Mwili wa mwandishi huyo mwenye umri wa miaka 30 ulikutwa katika bustani moja ya mapumziko huko Ruse ambapo simu yake, funguo za gari na nguo zake hazijaonekana.

China Kuchunguza Mashtaka ya Rushwa Yanayomhusu Meng

0

Serikali ya China imevunja ukimya na kusema inachunguza  mashtaka ya rushwa ambayo wanayahusisha na kupotea kwa kiongozi wa shirika la Polisi duniani Interpol, Meng Hongwei.

Mke wa Meng amesema anahisi mumewe yupo China na atakuwa kwenye hali ya hatari kwani baada ya kumkosa mumewe alipiga simu katika ofisi za Shirika hilo huko Ufaransa.

Meng hajapatikana tangu Septemba 25 alipoondoka kwenda China kwa ziara binafsi ambapo taarifa za kupotea kwake zilianza kusikika wiki  iliyopita.

Taarifa zinasema Meng aliachia nafasi ya urais wa Shirika hilo la Polisi lenye makao makuu yake nchini Ufaransa katika mji wa Lyon.

Rais Uturuki kufuatilia kupotea mwandishi wa Saudi Arabia

0

Serikali ya Uturuki imesema inachukulia suala la kupotea kwa mwandishi wa habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi kama kesi ya mauaji na Rais wa  nchi hiyo Reccep Tayyip Erdogan ametangaza kuifuatilia kesi hiyo.

Umoja wa Mataifa umetaka wachunguzi wa kujitegemea kufuatilia kupotea kwa mwandishi huyo siku ya Jumanne iliyopita.

Mfalme wa Saudi Arabia amesema Uturuki inaweza ikachukua hatua ya kumtafuta mwandishi huyo katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Istanbul kwani hawana chochote cha kuficha.

Khashoggi amekuwa akiandikia magazeti tofauti ikiwemo gazeti la Washington Post.

Rafiki wa kike wa Khashoggi amesema Khashoggi aliingia katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul na amekuwa akiandika habari za kuikosoa serikali ya Saudi Arabia.