Rais Trump amuomba radhi Jaji Kavanaugh

0

Rais Donald Trump wa Marekani amemuomba radhi kwa niaba ya raia wa nchi hiyo, Jaji mpya wa Mahakama Kuu Brett Kavanaugh kwa kile alichokiita ni kampeni chafu za kisiasa zilizolenga kuharibu sifa zake kwa kumsingizia mambo ya uongo.

Trump ametoa kauli hiyo wakati wa sherehe za kuapishwa kwa Jaji Kavanaugh, sherehe zilizofanyika katika Ikulu ya Marekani.

Mchakato wa kumthibitisha Kavanaugh katika uteuzi wake, uligubikwa na kashfa za udhalilishaji anaodaiwa kuufanya mwaka 1980.

Rais Trump amewaeleza watu walioshuhudia sherehe za kuapishwa kwa  Kavanaugh kuwa tangu awali alisikia madai kutoka chama cha Democratic kupinga uteuzi wa Jaji huyo ambaye binafsi amemuita kuwa ni mtu makini na ambaye hana jambo lolote baya alilolifanya, na kwamba madai hayo ni jitihada za kutaka kumchafua.

Kauli hiyo ya Rais Trump ameitoa wakati wa kiapo hicho ambacho ni cha awali kwa Kavanaugh kilichosimamiwa na Jaji wa mahakama Kuu anayemaliza muda wake Anthony Kennedy huku akiwa amebakiwa na kiapo cha mwisho kutoka kwa Rais.

 

UDART yatakiwa kuzingatia usalama barabarani

0

Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani Nchini Fortunatus Musilimu amewataka watendaji na wasimamizi wa mradi wa usafiri wa  mabasi yaendayo haraka jijini Dar es salaam (UDART)  kuzingatia sheria na taratibu zote za usalama barabarani.

Kamanda Musilimu ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam baada ya kukagua usalama barabarani kwa mabasi hayo yaendayo haraka katika eneo la Kimara.

Amesema kuwa mabasi hayo yanatakiwa kutopakia abiria wengi tofauti na uwezo wake, kuzingatia mwendo unaotakiwa katika kusafirisha abiria pamoja na kuzingatia alama za vivuko vya waenda kwa miguu zilizopo katika njia za mradi huo wa mabasi yaendayo haraka.

Naye mmoja wa viongozi wa UDART, –  Joe Beda amesema kuwa watazingatia maelekezo yote waliyopatiwa na Kamanda Musilimu, ili kuhakikisha usafiri wa  mabasi yaendayo haraka jijini Dar es salaam unakuwa salama na mfano wa kuigwa  katika kutekeleza sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazotokana na uzembe.

Nao baadhi ya wakazi walioshuhudia ukaguzi huo, wamekipongeza  Kikosi cha Usalama barabarani Nchini kwa kukumbusha kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani kwa wadau wote wa usafirishaji ili kuepuka na ajali zinazosababisha vifo na majeruhi.

 

Benki ya Dunia kufadhili miradi zaidi ya elimu

0

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia hapa nchini Bella Bird, mazungumzo yaliyohusu maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na benki hiyo.

Baada ya mazungumzo hayo Bella Bird amesema kuwa miradi inayotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia nchini  Tanzania imefikia thamani ya shilingi Trilioni 10.186 na kwamba maendeleo ya miradi hiyo ni mazuri.

Ameongeza kuwa kwa sasa wanakamilisha maandalizi ya ufadhili wa miradi mingine inayohusu sekta ya elimu hasa elimu ya awali na sekondari itakayogharimu shilingi Trilioni 1.357 na kwamba maandalizi hayo yatakamilika mwezi Novemba mwaka huu.

“Kwa hiyo nimekutana na Mheshimiwa Rais Magufuli kuzungumzia maendeleo ya miradi hiyo na kwa ujumla maendeleo ni mazuri” amesema mkurugenzi mkazi huyo wa Benki ya Dunia hapa nchini Bella Bird.

 

 

 

Serikali yaagiza shule kupelekewa walimu

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa  muda wa siku mbili kwa Kaimu Afisa Elimu anayeshughulikia elimu ya msingi wilayani Muleba  mkoani Kagera, – Bukuru Malembo awe amepeleka walimu wawili katika shule ya msingi iliyoko kwenye kitongoji cha Rwenzige kwa kuwa haina mwalimu hata mmoja.

Shule hiyo yenye madarasa wawili na ofisi moja ya mwalimu, ina jumla wanafunzi 216 wa darasa la awali hadi la nne.

Shule hiyo ilijengwa na wananchi ambapo kwa sasa wanafunzi wake wanafundishwa na mwananchi mmoja aliyeamua kujitolea ili kuwapunguzia adha watoto ya kutembea umbali wa kilomita 16 kwenda kusoma katika shule ya kijiji cha Kiteme.

Waziri Mkuu  Majaliwa ametoa muda huo baada ya wanafunzi wa shule hiyo ya msingi iliyoko kwenye kitongoji cha Rwenzige kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ya bango wakati akizungumza na wakazi wa eneo hilo katika mkutano wa hadhara.

“Haiwezekani watoto wadogo wenye umri wa kuanzia miaka mitano wakatembea umbali wa kilomita 16 kwenda shule wakati katika kitongoji chao kuna shule yenye madarasa mawili na chumba kimoja cha ofisi ya mwalimu na Afisa Elimu hadi sasa hajapeleka walimu na kumuachia mwalimu Benson Bukerebe, kijana ambaye si mwalimu ila anajitolea kufundisha akifundisha wanafunzi hao peke yake”, amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa  amemuagiza kaimu Afisa Elimu huyo  anayeshughulikia elimu ya msingi wilayani Muleba  ahakikishe ifikapo Oktoba Kumi mwaka huu saa nne asubuhi awe ameshawapeleka walimu hao wawili katika shule hiyo ya msingi ili waweze kuwafundisha wanafunzi.

Pia amemtaka mkuu wa wilaya ya Muleba, -Mhandisi Richard Ruyango awasilishe taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo ofisini kwake.

Kwa upande wake, Benson Bukerebe  mwenye umri wa miaka 29,  maarufu kama mwalimu Benson amesema kuwa yeye kitaaluma si mwalimu bali ni mhitimu wa kidato cha nne na aliamua kuanzisha darasa kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi hao kwa kuwa alikuwa akiwahurumia kwa sababu baadhi yao hawakuwa na uwezo wa kutembea umbali wa kilomita 16 hadi iliko shule ya msingi ya Kiteme.

Amesema kuwa kwa muda wote huo ameweza kumudu kuwafundisha wanafunzi hao kwa kutumia vitabu vya kuazima kutoka shule mbalimbali za msingi, lengo likiwa ni kuhakikisha watoto wenye umri wa kuanza shule katika kitongoji chao cha Rwenzige wanapata fursa ya elimu ambayo ni haki yao ya msingi.

 

Zama mpya tuzo za Ballon D’or

0

Nyota wa mabingwa wa ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu uliopita  Real Madrid wametawala kwenye orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo ya mchezaji bora duniani inayotolewa na jarida la mchezo wa mpira wa miguu nchini Ufaransa, –  Ballon D’or zitakazotolewa Disemba tatu mwaka huu jijini Paris.

Miamba hiyo ya soka barani Ulaya imeingiza wachezaji nane kwenye orodha hiyo wakiongozwa na Gareth Bale, Karim Benzema, Isco Marcelo, Thibaut Courtois, Sergio Ramos, Raphael Varane na mchezaji bora wa mwaka wa FIFA, – Luka Modric.

Awali, tuzo za Ballon d’Or zilikuwa zikijulikana kama FIFA Ballon d’Or,  lakini tangu Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) lijiengue kwenye tuzo hizo mwaka 2016 na kuanza kutoa za kwake kwa kujitegemea, jarida la Ballon d’Or nalo likaendelea na utoaji wa tuzo hizo kivyake.

Wachezaji wengine waliongia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo hiyo kongwe ni pamoja na mshambuliaji wa England na klabu ya Tottenham Hot Spurs, – Harry Kane, winga wa Chelsea, –  Eden Hazard na Mshambuliaji wa Liverpool, – Mohamed Salah.

Wengine ni mshambuliaji wa Manchester City, – Sergio Aguero, mlinda mlago wa Liverpool, – Alisson Becker pamoja na washambuliaji wa timu hiyo  Sadio Mane na Roberto Firmino.

Manchester United imeingiza mchezaji mmoja tu kwenye orodha hiyo ambaye ni kiungo Paul Pogba pamoja na Wafaransa wenzake N’golo Kante anayekipiga kwenye klabu ya Chelsea na kipa wa Tottenham, –  Hugo Lloris.

Nyota Cristiano Ronaldo wa Ureno na Klabu ya Juventus aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Real Madrid atakuwa akitetea tuzo aliyotwaa mwaka 2017 pamoja na Lionel Messi, Antoine Griezmann, Kylian Mbape na Neymar.

Orodha hiyo inahitimishwa na Edinson Cavani, Diego Godin, Kevin De Bruyne, Mario Mandzukic, Jan Oblak, Luiz Suarez na Ivan Rakitic.

Hazard aiweka njia panda Chelsea

0

Nyota wa klabu ya Chelsea na timu ya Taifa ya Ubelgiji, – Eden Hazard amesema kuwa bado hana uhakika na mustakabali wake ndani ya klabu ya Chelsea kwa kuwa kujiunga na Real Madrid ni ndoto inayosumbua kichwa chake.

Nyota huyo ambaye amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake wa sasa na klabu hiyo ya London amesema kuwa anaogopa kuahidi kama ataongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia Chelsea halafu mwisho wa siku asiongeze.

Hazard mwenye umri wa miaka 27 alihusishwa kuihama Chelsea kwenye dirisha la usajili lililopita ambapo alinukuliwa akisema ana hamu ya kujaribu jambo jipya.

Pamoja na nia hiyo ya Hazard, timu yake bado inataka kumpa mkataba wa muda mrefu mchezaji huyo huku mwenyewe akionekana kulikwepa jambo hilo.

Hazard amenukuliwa akisema kuwa hataki kudanganya kuwa Real Madrid ni timu kubwa na kuongeza kuwa ni timu ya ndoto yake tangu akiwa mtoto.

 

Stars kuifuata Cape Verde usiku wa leo

0

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inaondoka usiku wa leo Oktoba Tisa kuelekea nchini Cape Verde kwa ajili ya mchezo wa kuwania kushiriki michuano ya mataifa ya Afrika dhidi ya timu ya taifa hilo.

Katika safari ya Stars, kiungo Frank Domayo ndiye mchezaji pekee ambaye anaweza kuukosa mchezo huo kutokana na kukabiliwa na majeraha ambayo aliyapata kwenye siku ya pili ya mazoezi ya Taifa Stars.

Meneja wa  timu hiyo Daniel Msangi amesema kuwa wachezaji wengine ambao waliumia wakati wakizitumikia klabu zao wana uwezekano mkubwa wa kuwepo kwenye safari ya leo usiku tayari kwa mchezo huo utakaochezwa siku ya Jumamosi Oktoba 12.

Msangi ameongeza kuwa mazoezi ya Stars kuelekea kwenye pambano hilo yameimarika hasa baada ya baadhi ya wachezaji wanaocheza soka nje nchi kujumuika na kikosi hicho.

Viongozi wa polisi matatani

0

Rais John Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kagera, – Augustine Ollomi, Kamanda wa polisi wa wilaya ya Kyerwa, – Justine Joseph, mkuu wa upelelezi wa wilaya ya Kyerwa, – Everist Kivuyo na mkuu wa kituo cha polisi cha Kyerwa, – Robert Marwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuhusika katika magendo ya zao la kahawa katika wilaya ya Kyerwa pamoja na tuhuma nyingine.

Rais Magufuli pia amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Jacob Kingu na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Simon Sirro kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika na hatua stahiki zinachukuliwa endapo watabainika kuhusika katika magendo ya kahawa na makosa mengine kwa mujibu wa sheria.

Tuhuma dhidi ya viongozi hao wa polisi katika wilaya ya Kyerwa zimebainika wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wilayani humo.