Baraza la Wadhamini wa CCM lakutana

0

Baraza la Wadhamini wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) limewaagiza watendaji na viongozi wote wa chama hicho na Jumuiya zake wa ngazi mbalimbali kuhakikisha katika maeneo yao hakuna mali yoyote ya  chama au Jumuiya inayouzwa, kukodishwa, kumilikishwa au kuhaulishwa kwa mtu yeyote au chombo kingine bila idhini ya baraza hilo.

Agizo hilo limetolewa na Baraza hilo chini ya Mwenyekiti wake Anna Abdalla lilipokutana  katika ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM Lumumba jijini  Dar es salaam, ikiwa ni mara ya kwanza tangu liteuliwe Julai Kumi mwaka huu.

Pamoja na mambo mengine, Baraza  hilo la Wadhamini wa CCM limeipitia kwa kina na kuanza kuifanyia kazi ripoti ya Tume ya kuhakiki mali za chama na Jumuiya zake  kwa lengo la kuchambua na kuzifanyia kazi changamoto na mapendekezo yote ya tume yanayohusu mali za CCM.

Kwa mujibu wa katiba ya CCM ya mwaka 1977, Baraza la Wadhamini wa CCM ndilo lenye jukumu la kumiliki na kusimamia mali zote zinazoondosheka na zisizoondosheka za Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake.

Baraza hilo limeelezea kubaini  uwepo  wa mikataba isiyo na tija, uuzaji, uporaji na uvamizi wa mali za CCM kinyume na katiba ya  chama hicho na hivyo kuwaonya watendaji na viongozi wote kuacha mara moja vitendo hivyo.

Kufuatia hali hiyo, Baraza la Wadhamini wa CCM limeziagiza mamlaka zote husika za chama hicho na Jumuiya zake kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watendaji na viongozi wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uuzaji wa mali za chama hicho ama Jumuiya zake bila kibali.

Rooney amtetea Mourinho

0

Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Manchester United, – Wayne Rooney amesema kuwa kocha wa timu hiyo Jose Mourinho sio mlengwa namba moja kwenye kufanya vibaya kwa timu hiyo bali wachezaji wake wanatakiwa kupambana.

Mourinho amekuwa na wakati mgumu baada ya Manchester United kuwa  na mwanzo mbaya  kwenye ligi kuu ya England na imefika wakati kuzushiwa kuwa anaweza kutimuliwa kazi.

Rooney amesema kuwa anajua fika kuwa  Mourinho yupo kwenye wakati mgumu hivi sasa lakini wachezaji lazima wasimame imara na kuifanya kazi yao ipasavyo.

Nyota huyo anayecheza soka nchini Marekani kwa sasa kwenye klabu ya D.C United ameongeza kuwa kocha anaweza kufanya kila kitu lakini atakuwa nje ya uwanja,  sasa kazi inabaki kwa wachezaji ambao ndio wanashuka dimba hivyo nao lazima waonyeshe nini wanafanya.

 

 

 

FIFA kuongeza idadi ya wanawake wanaocheza Soka

0

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) linataka hadi ifikapo mwaka 2026 wanawake milioni sitini wawe wanacheza mpira wa miguu duniani kote.

Katika kuhakikisha suala hilo linafanikiwa, FIFA imepanga kuanzisha mashindano mapya ya soka kwa wanawake ya klabu bingwa ya Dunia kama ilivyo ile ya klabu bingwa ya dunia ya wanaume iliyoanzishwa mwaka 2000.

Hiyo ni sehemu ya mipango ya FIFA katika kuboresha soka la wanawake duniani kote,  ambapo mashindano hayo mapya ni sehemu ya tathmini ya FIFA katika kuboresha soka la wanawake.

Katibu Mkuu wa FIFA, Fatma Samba Diouf Samoura ambaye ni mwanamke wa kwanza kuongoza shirikisho hilo amesema kuwa  amejisikia faraja kuzinduliwa kwa mpango huo na kwamba watakuwa karibu na wanachama wao wote ili kuhakikisha mpango huo unafanikiwa

Watanzania watakiwa kufanya kazi kwa bidii

0

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ametoa wito kwa Watanzania kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Profesa Ndalichako ametoa wito huo jijini Dar es salaam wakati wa kongamano la kumbukizi ya miaka 19 ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Profesa Ndalichako ameongeza kuwa kupitia kongamano hilo ni vema elimu kuhusu uzalendo na uadilifu ikatolewa, kwa kuwa mipango ya taifa kuwa na uchumi wa viwanda haitafanikiwa bila kuwa na vijana waadilifu.

Akichangia mada kuhusu umuhimu wa Azimio la Arusha katika kustawisha viwanda, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt Ayub Rioba amesema kuwa miongoni mwa malengo yaliyowekewa msisitizo zaidi katika azimio la Arusha ni kufanya kazi kwa bidii.

 

Waamriwa kuondoka katika maeneo yao

0

Zaidi ya watu Laki Tano wameamriwa kuondoka haraka katika makazi yao yaliyopo kwenye eneo la kusini mashariki  nchini Marekani ili kuepusha madhara yanayoweza kujiyokeza katika kipindi hiki ambacho kimbunga Michael kinakaribia kulikumba eneo hilo.

Watu hao ni wa majimbo ya Alabama, Florida na Georgia ambapo pia majimbo hayo yametangaza hali ya hatari.

Watabiri wa hali ya hewa nchini Marekani wamesema kuwa kimbunga hicho cha Michael kwa sasa kimekwishaingia katika hatua ya tatu na kuongeza kasi yake kadri kinavyopita kwenye ghuba ya Mexico kuelekea  majimbo ya Florida, Alabama na Georgia.

Wamesema kuwa kimbunga hicho ambacho ni hatari zaidi kinasababisha upepo mkali ambao unakwenda kwa kasi ya kilomita mia mbili kwa saa.

Ajali yaua hamsini Kenya

0

Watu hamsini wamekufa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutumbukia bondeni kwenye barabara kuu ya Nairobi – Kisumu nchini Kenya.

Vyombo vya habari nchini Kenya vimesema kuwa ajali hiyo mbaya imetokea katika eneo la Fort Ternan lililopo kwenye jimbo la Kericho majira ya alfajiri.

Kamanda wa polisi wa jimbo la Kericho, – James Mogera amesema kuwa dereva wa basi hilo lenye uwezo wa kubeba abiria 67 alishindwa kulimudu na kisha kuvigonga vizuizi vilivyokuwa kando ya barabara na mwisho kutumbukia bondeni.

Awali jeshi la polisi nchini Kenya lilisema kuwa idadi ya watu waliokufa ni arobaini, lakini baadae likasema kuwa idadi hiyo imeongezeka kutokana na majeruhi waliokua na hali mbaya kufariki dunia.

Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo wanatibiwa katika zahanati ya Fort Ternan na wengine kwenye hospitali ya jimbo la Muhoroni.

Taarifa zaidi  kutoka nchini Kenya zinasema kuwa miili ya baadhi ya watu waliokufa katika ajali hiyo imeshindwa kunasuliwa kutoka ndani ya basi hilo.

Wanaovujisha mitihani waonywa

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya maafisa elimu na walimu kutojihusisha na vitendo vya wizi wa mitihani vinavyofanywa kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi kwa kuwa vinawadharirisha.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa onyo hilo baada ya kukabidhiwa vyumba vya madarasa vya shule za msingi Nyakato na Kashozi wilayani Bukoba mkoani Kagera, vyumba vilivyojengwa kwa msaada wa serikali ya Japan baada ya kuathiriwa na tetemeko la ardhi mwaka 2016.

“Kama kweli umemuandaa mtoto huna sababu ya kuiba mitihani na mtoto hawezi kufikiria kuiba mitihani kwa sababu yuko nje ya mfumo,  Walimu heshimuni maadili ya kazi ya ualimu”, amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesema kuwa  tathmini ya elimu katika shule za msingi na sekondari hufanyika kwa kufanya mitihani, hivyo ametaka dosari ya udanganyifu wa mitihani iliyojitokeza katika mitihani ya darasa la saba mwaka huu isijirudie tena.

Hivi karibuni Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) lilifuta matokeo ya mtihani ya darasa la saba kwa shule za msingi zote za halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma na baadhi ya shule katika halmashauri ya Kondoa, Kinondoni, Mwanza jiji na Ubungo kwa kosa la kuvujisha mitihani.

 

 

Kamto adai kushinda Cameroon

0

 

Mgombea wa upinzani katika uchaguzi mkuu  uliofanyika Julai Saba mwaka huu nchini Cameroon, – Maurice Kamto amedai kuwa ameshinda.

Kamto ambaye ni kiongozi wa chama cha upinzani cha Rebirth of Cameroon (MRC) amejitangazia ushindi licha ya serikali ya nchi hiyo  kumtaka asifanye hivyo.

Pamoja na kujitangazia ushindi, Kamto pia ametoa wito kwa rais Paul Biya ambaye ni mmoja wa viongozi wa Afrika waliokaa madarakani kwa muda mrefu kuachia madaraka kwa amani.

Hata hivyo mgombea huyo wa kiti cha urais nchini Cameroon kutoka upande wa upinzani hajatoa matokeo yoyote yanayomuonyesha kuwa yeye ni mshindi.

Mahakama ya katiba nchini Cameroon ndio chombo pekee nchini humo chenye mamlaka ya kutangaza matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu ndani ya kipindi cha muda wa siku 15 tangu kufanyika kwa uchaguzi.