Dkt Dalmas kuongoza bodi TANROADS

0

Rais John Magufuli amemteua Dkt Dalmas Nyaoro kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS).

Dkt Nyaoro ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam anachukua nafasi ya Hawa Mmanga ambaye amemaliza muda wake.

Uteuzi wa Dkt Nyaoro umeanza Oktoba Kumi mwaka huu.

 

Tetemeko jingine laitikisha Indonesia

0

Tetemeko jingine la ardhi limevitikisa visiwa vya Java na Bali nchini Indonesia zikiwa zimepita wiki mbili tu  tangu matetemeko mengine makubwa yalipoitikisa nchi hiyo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu elfu mbili.

Kumekuwa na hali ya wasiwasi baada ya kutokea kwa tetemeko hilo la ardhi, huku waokoaji wakiendelea na zoezi la kuwatafuta watu ambao hadi sasa hawajulikani walipo baada ya matetemeko hayo ya ardhi.

Matetemeko hayo ni tetemeko la kawaida la ardhi na tetemeko la ardhi chini ya bahari  – Tsunami.

Awali serikali ya Indonesia ilitangaza kuwa alhamisi wiki hii ndiyo ingekuwa siku ya mwisho ya kuendelea kuwatafuta watu ambao hawajulikani walipo, lakini waokoaji wameonyesha matumaini ya kuendelea kupata miili zaidi ya watu katika zoezi hilo.

 

 

Kimbunga Michael chasababisha uharibifu Florida

0

Kimbunga Michael tayari kimelipiga jimbo la Florida nchini Marekani na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu ambao haujawahi kutokea katika jimbo hilo katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Kimbunga hicho ambacho hivi sasa kinaelekea katika jimbo la jirani la Georgia huku kikiwa kimesababisha baadhi ya mapaa  katika jimbo la Florida kung’olewa na kutupwa mbali.

Kimbunga Michael pia kimesababisha mafuriko na kung’oa miti mikubwa  ambayo mingine imeangukia barabarani na kutatiza mawasiliano ya barabara katika jimbo hilo.

Marekani yashinikizwa kufanya uchunguzi kuhusu kashoggi

0

Baadhi ya wabunge wa bunge la Seneti la nchini Marekani wameanza kuihamasisha serikali ya nchi yao kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio la kupotea kwa mwandishi wa habari raia wa Saudi Arabia katika ubalozi wa nchi hiyo.

Wabunge hao wanataka serikali ya Marekani kutuma maafisa usalama kuchunguza mahali alipo mwandishi wa habari Jamal Kashoggi ambaye alipotea katika mazingira ya kutatanisha mara baada ya kuingia katika ubalozi wa nchi yake mjini Istanbul, -Uturuki.

Wabunge hao wametaka uchunguzi huo kufanyika baada ya gazeti la The Post la nchini Marekani kuandika kuwa serikali ya Saudi Arabia iliamuru kuwa mwandishi huyo wa habari akamatwe na kupelekwa mjini Riyadh.

Awali serikali ya Uturuki ilitangaza kuwa mwandishi huyo ameuawa ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia, kwani tangu alipoingia kwenye ubalozi huo hajaonekana hadi  hii  leo.

 

Wanafunzi Zanzibar watakiwa kuzingatia elimu

0

Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi, – Ayoub Mohamed Mahamoud amewataka wanafunzi Visiwani Zanzibar kuzingatia elimu ili kutimiza ndoto zao na kuachana na matendo maovu.

Akizungumza na wanafunzi na walimu wa shule ya sekondari ya Bububu, – Mahamoud amesema kuwa  ni wajibu wa kila mwanafunzi kuongeza juhudi katika masomo yake kwa kuwa taifa linawategemea katika siku za baadaye.

Akiwa katika shule hiyo,  pamoja na mambo mengine, Mkuu huyo wa mkoa wa Mjini Magharibi  amekabidhi madawati na matofali kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi wa kufanyia mitihani, vifaa vilivyotolewa na ofisi yake kwa lengo la kuunga mkono maendeleo ya sekta ya elimu.

 

Mgodi wa kokoto wa Tan- Turk wafungwa

0

Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko ameufunga mgodi wa kokoto wa Tan- Turk ulipo katika kijiji cha Mindutulieni wilayani Bagamoyo  mkoani Pwani  hadi  hapo mmiliki wa mgodi huo atakapowalipa fidia wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Naibu Waziri Biteko ametangaza kuufunga mgodi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakazi wa kijiji  hicho ambao wamedai kuwa shughuli za ulipuaji wa baruti katika miamba  zinazofanywa katika mgodi zimekua zikisababisha mawe makubwa kuruka na kuangukia  katika makazi ya watu,  jambo linalohatarisha maisha yao.

Akizungumza mara baada ya kukagua mgodi huo wa kokoto wa Tan- Turk , Naibu Waziri Biteko amemuagiza mmiliki wake  kutofanya shughuli zozote hadi hapo atakapozilipa fidia  kaya zaidi ya Thelathini zilizopo katika eneo la mgodi.

Akiwa katika mgodi huo, Naibu Waziri Biteko pia ameelezea kutoridhishwa  na utunzaji wa kumbukumbu za  kiwango cha  kokoto kinachouzwa ndani ya mgodi huo, hali inayosababisha serikali kukosa mapato.

 

Sakata la kutekwa kwa MO, watatu washikiliwa

0

Watu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam kufuatia tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Dewji.

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo, – Paul Makonda amesema kuwa vyombo vya ulinzi vinaendelea kumtafuta mfanyabiashara huyo na kuomba yeyote mwenye taarifa inayoweza kusaidia kupatikana kwake ashirikiane na jeshi la polisi.

Naye Kamanda wa polisi Kanda maalum ya Dar es salaam, –  Lazaro Mambosasa amesema kuwa jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa kina wa tukio hilo na kusema kuwa kipaumbele kwa sasa ni kahakikisha Mohamed Dewji anapatikana akiwa salama.

Kwa mujibu wa Kamanda  Mambosasa, -Mohamed Dewji ametekwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni  raia wa kigeni.

Barabara ya Kongwa, Mpwapwa hadi Kibakwe kujengwa

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema  kuwa serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na michoro ya barabara ya Kongwa, Mpwapwa hadi Kibakwe mkoani Dodoma ili ijengwe kwa kiwango cha lami na kuondoa changamoto ya ubovu wa barabara iliyopo hivi sasa.

Waziri Mkuu Majaliwa amelazimika kutoa kauli hiyo kufuatia ombi la Wabunge wa wilaya ya Mpwapwa wakati wa ziara yake wilayani humo na kuongeza kuwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo zitatengwa katika mwaka ujao wa fedha wa 2018/2019.

Waziri Mkuu  anaendelea na ziara yake mkoani Dodoma  ambayo aliikatisha kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere  katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Akiwa wilayani Mpwapwa, Waziri Mkuu Majaliwa pia amewaagiza watendaji wa vijiji na kata wilayani humo kuwachukulia hatua za kisheria watu wote wanaojihusisha na uharibifu wa vyanzo vya maji na kusababisha wilaya hiyo kuwa na vyanzo vichache vya maji.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema  kuwa serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na michoro ya barabara ya Kongwa, Mpwapwa hadi Kibakwe mkoani Dodoma ili ijengwe kwa kiwango cha lami na kuondoa changamoto ya ubovu wa barabara iliyopo hivi sasa.

Waziri Mkuu Majaliwa amelazimika kutoa kauli hiyo kufuatia ombi la Wabunge wa wilaya ya Mpwapwa wakati wa ziara yake wilayani humo na kuongeza kuwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo zitatengwa katika mwaka ujao wa fedha wa 2018/2019.

Waziri Mkuu  anaendelea na ziara yake mkoani Dodoma  ambayo
aliikatisha kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere  katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Akiwa wilayani Mpwapwa, Waziri Mkuu Majaliwa pia amewaagiza watendaji wa vijiji na kata wilayani humo kuwachukulia hatua za kisheria watu wote wanaojihusisha na uharibifu wa vyanzo vya maji na kusababisha wilaya hiyo kuwa na vyanzo vichache vya maji.