Maporomoko ya udongo yasababisha vifo Uganda

0

Zaidi ya watu thelathini wamethibitika kufa baada ya kutokea kwa maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika eneo la mashariki la Uganda.

Idadi hiyo ya watu waliokufa inatarajiwa kuongezeka kwa kuwa bado watu kadhaa hawajulikani walipo.

Habari kutoka nchini Uganda zinasema kuwa vikosi vya uokoaji vipo katika maeneo yaliyoathiriwa na maporomoko hayo ya udongo na matumaini ni kuwapata watu kadhaa wakiwa hai.

Katika wilaya ya Bududa, watu wengi wamekufa baada ya kufukiwa na vifusi vya udongo pamoja na mawe yaliyosombwa kutoka maeneo ya milimani, ambayo pia yamesababisha kuharibiwa kwa nyumba zote zilizopo kwenye vijiji vitatu vya wilaya hiyo.

Mwaka 2010, takribani watu mia moja walikufa katika tukio kama hilo la maporomoko ya udongo katika wilaya hiyo ya Bududa, huku tukio kama hilo likiripotiwa kutokea kila mwaka katika wilaya hiyo na kusababisha vifo, majeruhi pamoja na uharibifu wa mali.

Marekani yasema haioni sababu ya kutoiuzia silaha Saudi Arabia

0

Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa haoni sababu ya kusimamisha mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia kwa sababu ya kutoweka kwa mwandishi wa habari wa Saudi Arabia Jamali Khashoggi.

Trump amesema kuwa Marekani inaweza kusaidia katika uchunguzi ili kubaini kilichomfika Khashoggi ambaye ni mkosoaji maarufu wa sera za Saudi Arabia.

Kashoggi alionekana mara ya mwisho akiingia katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul nchini Uturuki oktoba pili mwaka huu.

Vyanzo vya habari nchini Uturuki vinasema kuwa vinaamini Khashoggi aliuawa ndani ya jengo la ubalozi huo na baadaye mwili wake kuondolewa madai ambayo Saudi Arabia inayakanusha na kusema kuwa hayana msingi.

NBA kutimua vumbi karibuni

0

Nchini Marekani imechezwa michezo mitatu ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu ya kulipwa ya mpira wa kikapu nchini humo – NBA itakayoaanza kuunguruma rasmi Oktoba 16 mwaka huu.

New Orlan Pelicans wakiwa nyumbani Smoothie King Center- Los Angeles wamekula kichapo kwa kunyukwa alama 134 kwa 119 na Toronto Raptors katika mchezo ambao Pascal Siakami ameibuka shujaa kwa kuifungia timu yake ya Raptors alama 21 na kucheza mipira iliyorudi yaani Rebounds 12.

Licha ya nyota wa Pelicans, – Antony Davis, Julius Randle na Nikola Mirotic kwa pamoja kufunga alama 71 bado hazikutosha kuipa timu yao ushindi mbele ya Raptors waliotawala sehemu kubwa ya mchezo huo.

Huko Golden One Center mjini Sacramento – California, wenyeji Sacramento Kings wamekiona cha moto baada ya kutandikwa alama 132 kwa 93 na Utah Jazz.

Rudy Gobert amefunga alama 18 na kucheza Rebounds saba zilizochagiza ushindi wa Jazz wakiwa ugenini na kuibua matumaini kwa mashabiki wa timu hiyo kufanya vema kwenye msimu unaokuja.

Mchezo wa mwisho umechezwa kwenye dimba la Stapeles mjini Los Angeles – California,  kwa timu ya Haifa Macabi kuchezea kichapo baada ya kula mweleka wa alama 124 kwa 76 kutoka kwa wenyeji Los Angeles Clippers.

Boban Marjanovic ameifungia Clippers alama 18 na kucheza Rebounds 12 zilizochagiza ushindi huo mbele ya Maccabi iliyokuwa ikiongozwa na Roman Sorkin aliyefunga alama 12 na kucheza Rebounds tatu.

 

Taifa Stars uso kwa uso na Cape Verde

0

Timu ya Taifa ya mpira wa miguu – Taifa Stars jioni ya leo inateremka dimbani huko mjini Praia kuikabili Cape Verde katika mchezo wa tatu wa hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2019 nchini Cameroon.

Kuelekea mchezo huo,  kocha mkuu wa Taifa Stars, -Emmanuel Amunike amesema kuwa kikosi chake kipo tayari kuwapa furaha watanzania katika mchezo huo dhidi ya wenyeji Cape Verde.

Amunike amesema kuwa huu ni wakati wa wachezaji wake kufanya jambo jema kwa nchi yao kwa kupata ushindi na kutengeneza njia ya kufuzu kwa fainali za AFCON kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980 huku Mkurugenzi wa Michezo kutoka wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Yusuph Singo akisema kuwa wachezaji wapo tayari kwa mchezo huo.

Taifa Stars inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi lake la L nyuma ya vinara Uganda wenye alama Nne, huku Lesotho wakiwa katika nafasi ya pili wakiwa na alama mbili sawa na Stars na Cape Verde inaburuza mkia.

 

 

Uchaguzi mdogo wa Ubunge Liwale Oktoba 13

0

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewasihi wapiga kura wote waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na wanaoishi kwenye jimbo la Liwale mkoani Lindi na kata nne za Tanzania Bara kujitokeza kupiga kura Jumamosi Oktoba 13 mwaka huu ili kuwachagua viongozi wanaowataka wawaongoze kwa kipindi cha takribani miaka miwili ijayo.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage  na kuwataka wapiga kura hao kutokua na hofu, woga ama wasiwasi wa aina yoyote.

Mbali na wito huo, Jaji Kaijage  pia amewataka wakazi wa jimbo hilo la Liwale na wa kata hizo nne, vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kushirikiana ili kuhakikisha kuwa viashiria vya kuvunjika kwa amani na utulivu vinaepukwa ili uchaguzi utakaofanyika uwe huru, wazi na wa haki.

“Wananchi waheshimu sheria za nchi wakati wote wa upigaji, kuhesabu, kujumlisha kura na kutangaza matokeo, pale panapokuwa na malalamiko yoyote ya ukiukwaji wa sheria na taratibu za uchaguzi, malalamiko hayo yafikishwe kwenye mamlaka inayohusika kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria.”, ameongeza Jaji Kaijage.

Amesisitiza kuwa ni wajibu wa vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo  mdogo kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia na kujumlishia kura kwa utaratibu ambao umekuwa ukitumika katika chaguzi za hivi karibuni.

Uchaguzi huo mdogo wa bbunge katika Jimbo la Liwale mkoani Lindi  na udiwani katika kata nne za Tanzania Bara unafanyika kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujiuzulu kwa mbunge na madiwani wa kata hizo na utahusisha zaidi ya wapiga kura elfu 69  walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura na kutakuwa na vituo vya kupigia kura 192.

Wenye maeneo ya uwekezaji watakiwa kushirikiana na TIC

0

Watanzania wenye viwanja na maeneo makubwa nchini ambayo yanafaa kwa uwekezaji wameshauriwa kwenda katika Kituo cha Uwekezaji nchini – TIC ili kuona ni kwa namna gani wataweza kuyatumia maeneo hayo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.

Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wawekezaji kutoka TIC, –  Ayoub Sizya wakati alipotembelea na kukagua eneo la ukanda wa uwekezaji na mauzo ya ndani na nje ya nchi la Kilua lililopo  katika kijiji cha Disunyala kata ya Mlandizi wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.

TIC imeingia makubaliano na mmiliki wa  eneo hilo lenye zaidi ya ekari elfu moja ambalo ni maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.

“Sisi TIC tumeingia makubaliano na Ukanda huu wa uwekezaji wa Kilua,  lengo letu ni kuimarisha shughuli za uwekezaji,tunafanya hivi ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi,kama unavyojua eneo hili linamilikiwa na mtu binafsi,na ni eneo kubwa ,hivyo tukiungana tutaleta wawekezaji wengi zaidi na Tanzania ya viwanda itazidi kusonga mbele”, amesema  Sizya.

Kwa upande wake mmiliki wa eneo hilo la ukanda wa uwekezaji Mohammed Kilua amesema kuwa wanatarajia kujenga zaidi ya viwanda sabini  na kwamba mpaka sasa kiwanda kimoja kimekamilika ujenzi wake huku vingine saba vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.

“Tutajenga viwanda vingi, ni zaidi ya 70 na kwenye eneo hili tayari tumepata maombi ya zaidi ya ujenzi wa viwanda 20 kwa mwaka huu, Tanzania ya Viwanda itafanikiwa tu,lengo letu ni kuunga mkono juhudi za Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli” ameongeza Kilua.

Kampuni ya Kamaka ambayo ni moja ya kampuni zilizowekeza  katika eneo hilo la Kilua imesema kuwa ushirikiano baina ya Kilua na TIC utaleta tija ya uzalishaji wa viwanda na kufikia lengo la serikali la kuwa na uchumi wa viwanda na kufikia uchumi wa kati.

Mpaka sasa, eneo hilo la ukanda wa uwekezaji na mauzo ya ndani na nje ya nchi la Kilua lililopo katika kijiji cha Disunyala kata ya Mlandizi wilaya ya Kibaha mkoani Pwani limetumia zaidi ya shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kuweka miundombinu ya umeme,maji na barabara.

 

Waziri Mkuu ateta na watumishi wa umma

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa vitendo vya udokozi wa mali ya umma havitavumiliwa na serikali na hivyo kuwataka watumishi wa umma kuwa waadilifu na waaminifu wanapotekeleza majukumu yao.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake  mkoani humo.

“Serikali haitamvumilia mtumishi wa umma ambaye si muadilifu, mvivu na mla rushwa, hivyo ni lazima watumishi wawajibike na ambao watashindwa kutekeleza majukumu yao watapa shida kwenye Serikali hii,  hakuna mchezo kwenye serikali hii, watumishi wa umma wanapaswa kulitambua hili” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wahakikishe wanapanga ratiba ya kwenda kuwatembelea wananchi hususani wanaoishi katika maeneo ya vijijini na kushirikiana nao katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili  na si kukaa ofisini.

Ameongeza kuwa  sio kila mtumishi kwenye idara yake anapaswa kwenda kwa wananchi, kama ana siku tano za kufanyakazi kwa wiki basi siku tatu azitumie kwenda kwa wananchi kutatua changamoto zao na kama ana siku sita, siku nne azitumie kwa kufanya jambo hilo.

Waziri Mkuu Majaliwa pia amewasisitiza watumishi wa umma kuzingatia itifaki, mipaka ya madaraka yao pamoja na kuheshimu viongozi na kwamba hata kama ni mkuu wa idara pia anapaswa kumheshimu mtumishi aliyekuwa chini yake.

Awali, Spika wa Bunge  Job Ndugai ambaye ni Mbunge wa jimbo la Kongwa aliishukuru serikali kwa kutatua kero mbalimbali ikiwemo changamoto ya ukosefu wa maji pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mbande hadi Kongwa ambapo aliomba ujenzi huo uendelee hadi Mpwapwa.

Soko la hisa la China lashuka

0

Soko la hisa nchini  China limeshuka kwa asilimia Tano, kiwango ambacho kinaonekana kuwa ni kikubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Wachunguzi wa masuala ya biashara wamesema kuwa mgogoro wa kibiashara kati ya China na Marekani huenda umechangia kushuka kwa soko hilo.

Habari zaidi kutoka nchini China zinasema  kuwa kushuka kwa soko la hisa la nchi hiyo kunaweza kuathiri uchumi wa Taifa hilo kubwa kiuchumi.