Nurmagomedov sasa amtaka Myweather

0

Bingwa wa uzani wa juu katika mchezo wa masumbwi Khabib Nurmagomedov wa Russia amesema yupo tayari kuzichapa na mbabe wa Kimarekani Floyd Myweather muda wowote atakapohitajika kufanya hivyo.

Nurmagomedov amesema kuwa anataka kushinda kitu alichoshindwa mpinzania wake Conor McGregor na kuongeza kuwa siku zote mfalme wa pori ni mmoja tu.

Mapema mwezi huu Mrussia huyo alimnyuka Mcgregor ambaye alikuwa hajapanda ulingoni katika uzani wa juu tangu alipotwangwa na Myweather mwezi Agosti  mwaka  2017 na kutanua wimbi la ushindi katika rekodi zake kufikia mapambano 27 huku akiwa hajapoteza pambano hata moja.

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa  instagram,  Nurmagomedov ameonekana akisema kuwa ni wakati wa kupigana na Myweather huku Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Mayweather Promotions akisema kuwa wababe wawili ambao hawajapoteza pambano hata moja kwanini wasipigane.

Myweather hajapanda ulingoni tangu alimpomshinda McGregor kwa knockout katika raundi ya  kumi mwezi Agosti mwaka  2017 katika pambano ghali zaidi duniani huku akiwa na rekodi ya kucheza mapambano hamsini na kushinda yote.

Uingereza,Ujerumani na Ufaransa zataka uchunguzi kuhusu Khashoggi

0

Uingereza,Ujerumani na Ufaransa zimetaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina kufuatia kutoweka kwa mwandishi maarufu wa wa habari wa Saudia Arabia, – Jamal Khashoggi.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo wamesema kuwa iwapo mtu yoyote atabainika kuhusika na kutoweka kwa mwandishi huyo awajibike.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, – Jeremy Hunt amesema kuwa mambo yote yanayoendelea hivi sasa yanaihusu Saudi Arabia licha ya nchi hiyo kukanusha kuhusika na kutoweka ama kuuawa kwa Khashoggi katika ubalozi wake huko Instanbul nchini Uturuki.

Khashoggi aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Saudia Arabia alitoweka tangu Oktoba Pili mwaka huu baada ya kuingia katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Instambuli nchini Uturuki.

Naye Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa litakua ni jambo la kusikitisha endapo itabainika Saudi Arabia imehusika na kutoa maagizo ya kuuawa kwa Khashoggi

Uchaguzi Simanjiro, Serengeti Disemba pili

0

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza tarehe mbili Disemba mwaka huu kuwa siku ya uchaguzi mdogo katika majimbo ya Simanjiro lililopo mkoani Manyara, Serengeti lililopo mkoani Mara na kwenye kata 21 katika maeneo mbalimbali nchini.

Mwenyekiti wa NEC Jaji Semistocles Kaijage amesema kuwa  fomu za uteuzi  wa  wagombea zitatolewa kati ya  Oktoba 28  na Novemba Tatu mwaka huu na kufuatiwa na kampeni za uchaguzi zitakazofanyika kuanzia tarehe Nne Novemba hadi Disemba mosi  mwaka huu.

“Tunapenda kuvikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha uchaguzi huu mdogo,” amesema Jaji Kaijage.

Serikali kuendelea kuuenzi Mwenge wa Uhuru

0

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo.

Dkt Shein ametoa wito huo jijini Tanga, wakati wa kumbukumbu ya miaka 19 ya kifo cha Baba wa Taifa, Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na hitimisho la wiki ya Vijana Kitaifa.

Amesema kuwa Hayati Mwalimu Nyerere alikua anajali na kusisitiza umoja siku zote za maisha yake, hivyo ni vema Watanzania wakaendeleza umoja huo ili Taifa liweze kupata maendeleo kwa haraka.

Kuhusu rushwa, Dkt Shein ametoa wito kwa Watanzania wote bila kujali tofauti zao, kupiga vita vitendo vya rushwa kwa kutoa
taarifa za watu wanaojihusisha na vitendo hivyo ili kumuenzi Baba wa Taifa ambaye aliichukia rushwa.

Kwa upande wa Mwenge wa Uhuru, Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesisitiza kuwa serikali zote mbili zitaendelea kuzienzi na kuzithamini mbio za Mwenge wa Uhuru.

Amewataka wale wote ambao wamekua wakiubeza Mwenge huo wa Uhuru waache mara moja kwa kuwa umekua ukihamasisha uendelezaji wa miradi mbalimbali nchini kote.

Akizungumzia wiki ya vijana Kitaifa, Dkt Shein amesema kuwa imekua na manufaa makubwa kwa kutoa mafunzo ya aina mbalimbali kwa vijana.

Amewataka vijana nchini kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo na kujiepusha na vitendo viovu ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.

Rais Magufuli ashiriki ibada maalum kumuombea Baba wa Taifa

0

Rais John Magufuli na mke wake Mama Janeth Magufuli wameungana na waumini wengine katika Ibada maalum ya kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Ibada hiyo imefanyika katika Kanisa la Mtakatifu Petro Oysterbay jijini Dar es salaam ikiwa ni miaka 19 tangu kifo cha Baba wa Taifa.

Mara baada ya Ibada hiyo, Rais Magufuli na mke wake Mama Janeth walimtembelea Mjane wa Baba wa Taifa, – Maria Nyerere nyumbani kwake Msasani jijini Dar es salaam.

Kuchauka arejea kwenye kiti

0

Mgombea ubunge katika jimbo la Liwale mkoani Lindi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zuberi Kuchauka ametangazwa kuwa mshindi wa kiti hicho.

Kuchauka ameshinda baada ya kupata kura 34, 532 ambazo ni sawa na asilimia 84.81 ya kura zote zilizopigwa.

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Liwale, -Luiza Mlelwa amempongeza Kuchauka kwa kuaminiwa na Wakazi wa jimbo hilo na hivyo kuamua kumchagua ili aendelee kuwatumikia.

Katika uchaguzi huo mdogo wa ubunge kwenye jimbo la Liwale mkoani Lindi waliojiandikisha kupiga kura ni 55, 777, waliojitokeza kupiga kura ni 40706 na kura halali zilikuwa 40, 301.

Kamati ya muda kuiongoza Ndanda FC

0

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, -Gelasius Byakanwa ametangaza kuuweka pembeni uongozi wa timu ya mpira wa miguu ya Ndanda FC ya mkoani humo.

Kufuatia hatua hiyo Byakanwa ambaye pia ni mlezi wa timu hiyo ameunda kamati ya muda itakayoisimamia timu hiyo katika mechi 29 zilizobaki katika msimu huu wa Ligi Kuu.

Amesema kuwa pamoja na kuunda kamati hiyo ya muda itakayosimamia timu ya Ndanda FC, mkoa wa Mtwara uko katika mkakati wa kutafuta mfadhili atakayeweza kuisaidia timu hiyo ambayo kwa sasa inashika nafasi ya 16 katika msimamo wa Ligi Kuu.

Kamati hiyo ya watu kumi inaongozwa na Laurent Werema.

Byakanwa amesema kuwa ameamua kufanya hivyo ili kuinusuru timu hiyo ambayo hivi karibuni ilishindwa kusafiri kutoka mkoani Singida kurudi Mtwara kutokana na kukosa fedha za nauli.

Hali hiyo ilisababisha msanii wa kizazi kipya (Bongo Fleva) Hamonize ambaye anatokea mkoani humo na pia ni Balozi wa timu hiyo kuichangia shilingi milioni 3.5 ili iweze kusafiri na kurudi Mtwara.

Viongozi wa Afrika wapewa somo

0

Viongozi wa Bara la Afrika  wametakiwa kuhakikisha chaguzi mbalimbali zinazofanyika katika mataifa yao zinafanyika kwa kuzingatia kanuni na sheria.

Wito huo umetolewa jijini Dar es salaam na baadhi ya wasomi na wanasiasa wakati wa mdahalo wa wazi wa kumbukizi ya  miaka 19 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambapo miongoni mwa mada zilizojadiliwa ni ile inayohusu mienendo ya chaguzi na mustakabali wa mataifa ya Afrika.

Akifungua mdahalo huo, Mwenyekiti wa Kigoda  cha Mwalimu Nyerere, Profesa Rwekaza Mukandala amesema kuwa nchi nyingi za Bara la  Afrika  zimekuwa zikifanya chaguzi ambazo hazileti tija katika mataifa yao bali kuchochea migogoro ya kisiasa.

Amesema kuwa jambo kubwa ambalo mataifa ya Afrika  yanatakiwa kufahamu ni kuendeleza  yale yaliyoasisiwa na waasisi wa mataifa hayo ambao walikuwa na mwelekeo wa kuimarisha  demokrasia iliyoleta tija ndani ya mataifa yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu  Nyerere, -Joseph Butiku  amesema kuwa Watanzania wanatakiwa  kufahamu kuwa amani ni jambo la kuzingatiwa katika kipindi cha uchaguzi ili taifa liendelee kuwa na amani na utulivu.