Dunia kushuhudia ligi ya NBA

0

Msimu mpya wa ligi ya kulipwa ya mpira wa kikapu nchini Marekani (NBA) unaanza alfajiri ya Oktoba 17 mwaka huu kwa kupigwa michezo miwili,  ambapo bingwa mtetezi Golden State Warriors watamenyana na Oklahoma City Thunder.

Thunder wanaingia kwenye mchezo huo bila huduma ya nyota wake  Russell Westbrook  ambaye anauguza jeraha la goti alilofanyiwa upasuaji mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu.

Inakadiriwa kuwa nyota huyo atakuwa nje kwa wiki nne kuuguza jeraha lake ambapo kocha wa Oklahoma City Thunder, –  Billy Donovan amekiri kuwa mwanzo wa msimu utakuwa mgumu bila ya nyota wake huyo.

Warriors wao wanaingia kwenye msimu mpya wakiwa na morali baada ya kikosi chake kutokuwa na majeruhi huku pia ikiwa ndio bingwa mtetezi wa ligi hiyo.

Wapenzi wa ligi ya kulipwa ya mpira wa kikapu nchini Marekani  wanasubiri kuona ni nini atafanya nyota wa mchezo huo Lebron James akiwa na timu yake mpya ya Los Angeles Lakers baada ya kufanya vyema kwenye timu aliyotoka ya Cleveland Caveliers.

Mchezo mwingine utakaopigwa alfajiri ya kesho Oktoba 17 unawakutanisha Boston Celtics wanaowakaribisha Philadelphia 76ERS kwenye dimba la TD Garden mjini Boston,- Miami.

 

 

 

Siku ya chakula Duniani yaadhimishwa

0

Tanzania leo inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya Chakula Duniani ambapo kitaifa sherehe hizo zinafanyika katika kijiji cha Chamanangwe wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba.

Siku ya Chakula Duniani ilitokana na kuanzishwa kwa Shirika la Chakula Duniani (FAO) Oktoba 16 mwaka 1945 huko Roma nchini Italia, lengo likiwa ni kusimamia haki ya kupata chakula pamoja na haki ya kila mtu kutokumbwa na njaa.

Katika kufanikisha lengo hilo, nchi tajiri duniani zimekua zikitoa ruzuku kwa wakulima wao na kuwatafutia soko la mazao yao.

Siku ya Chakula Duniani inaadhimishwa huku takwimu zikionyesha kuwa kwa upande wa  nchi zinazoendelea na hasa zilizo kusini mwa jangwa la Sahara Barani Afrika, suala la kutojitosheleza kwa chakula bado ni changamoto kubwa.

Katika kukabiliana na changamoto  hiyo,  kila nchi imeanzisha miongozo, sera, kanuni, sheria na kampeni mbalimbali zenye lengo la kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo.

Kwa upande wa Tanzania, kumekuwa na kampeni katika vipindi mbalimbali ikiwemo ile ya Mapinduzi ya Kijani, Kilimo ni Uti wa Mgongo na Kilimo Kwanza, lengo likiwa ni kujitosheleza kwa chakula na kutumia kilimo kama njia ya kuwainua wakulima kiuchumi na taifa kwa ujumla.

Kauli mbiu ya siku ya chakula duniani kwa mwaka huu ni Juhudi zetu ndio hatma yetu, Dunia bila ya njaa inawezekana ifikapo mwaka 2030.

England yapata ushindi wa kwanza ugenini

0

England imepata ushindi wa kwanza ugenini dhidi ya Hispania ndani ya kipindi  cha miaka 31 baada ya kuwabwaga wenyeji wao Hispania kwa mabao matatu kwa mawili kwenye mchezo wa hatua ya makundi katika michuano ya ligi ya mataifa ya Ulaya.

England ndio walikuwa wa kwanza kupata mabao ambapo ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza waliandika mabao hayo matatu na kuwaduwaza wenyeji wa mchezo huo ambao iliwalazimu kusubiri kupindi cha pili kupata mabao yao mawili.

Raheem Sterling wa England amepachika mabao mawili dakika za 16 na 38 huku bao lingine likitiwa kimiani na Marcus Rashford kwenye dakika ya 30 na Francisco Alcacer akifunga katika dakika ya 58 na nahodha wa Hispania, – Sergio Ramos akipachika bao la pili kwa Hispania katika dakika ya 97.

Mara ya mwisho kwa England kupata bao na ushindi wakicheza ugenini dhidi ya Hispania ilikuwa mwaka 1987 ambapo nyota wa England kwa wakati huo Gary Lineker alipofunga mabao yote manne kwenye ushindi wa mabao manne kwa mawili.

Kwa upande wa Hispania,  wenyewe hii ni mara yao ya  kwanza ndani ya kipindi cha miaka 15 kupoteza mchezo wa kimataifa wa kiushindani wakicheza nyumbani  ambapo  walifungwa na Ugiriki mwaka 2003 na kukatisha mfululizo wa michezo 38 bila kipigo.

Mbali na hiyo, hii pia inakuwa mara ya kwanza katika historia ya Hispania kufungwa mabao matatu ama zaidi ndani  kwenye mchezo wa kiushindani wa kimataifa waliocheza nyumbani.

Stars kuamua hii leo

0

Timu ya Taifa ya soka – Taifa Stars leo inacheza mchezo muhimu wa kuwania kufuzu kwa michuano ya mataifa ya Afrika (AFCON 2019) dhidi ya timu ya taifa ya Cape Verde ambayo walicheza nayo Ijumaa iliyopita na kuambulia kichapo cha mabao matatu kwa sifuri.

Mchezo wa leo dhidi ya Cape Verde ndio utakaoamua mustakabali wa Taifa Stars kucheza michuano ijayo ya mataifa ya Afrika hasa baada ya kupoteza mchezo uliopita mjini Praia.

Ili Kuendelea kuwa na matumaini ya kushiriki michuano hiyo mwaka 2019, Taifa Stars inalazimika kushinda mchezo dhidi ya Cape Verde na kufikisha alama tano ambazo zitaiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kwa michuano hiyo nchini Cameroon.

Ili kuongeza nguvu kwenye mchezo wa leo, kocha wa Stars Emmanuel Amunike amemuita mchezaji kiraka wa timu ya Simba,- Erasto Nyoni ambaye ni moja ya wachezaji wazoefu na waliocheza kwa muda mrefu kwenye timu ya Taifa ya Tanzania.

Stars itawakosa wachezaji wake wawili ambao ni mlinzi wa kulia Hassan Kessy Ramadhan na Thomas Ulimwengu ambao wote wanatumikia adhabu ya kuwa na kadi mbili za njano.

Kwenye kundi la L ambalo Taifa Stars ipo, Uganda inaongoza ikiwa na alama saba ikifuatiwa na Cape Verde yenye pointi nne huku Taifa Stars na Lesotho zikiwa na alama mbili kila mmoja na zote hazijashinda mchezo wowote hadi sasa.

Dkt Shein kufungua maonesho ya utalii Zanzibar

0

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein anatarajiwa kufungua maonesho ya utalii yatakayofanyika Zanzibar kuanzia Oktoba 17 hadi 20 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, – Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwa maonesho hayo yatahusisha takribani  kampuni 150 za utalii.

Amesema kuwa lengo la maonesho hayo kufanyika Zanzibar ni kutangaza utamaduni wa Mzanzibar na vivutio vya utalii vinavyopatikana visiwani humo.

Waziri Kombo ametaja nchi zitakazoshiriki maonesho hayo kuwa ni pamoja na Lebanon, China,  Indonesia, Malaysia , nchi za falme za kiarabu na nchi za masharikai ya kati.

 

 

Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano waongeza ukusanyaji mapato

0

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye  amesema kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umeongeza makusanyo ya mapato ya serikali kwenye maeneo ya mipakani mwa Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Mhandisi Nditiye  ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye kituo cha huduma cha pamoja cha Mtukula ambacho kinawezesha usafirishaji wa taarifa, data za wateja na bidhaa kutoka Tanzania kwenda nchi jirani ya Uganda.

“Maeneo ya mipakani ndio lango la kuongeza mapato na kukuza uchumi wa nchi yetu, niwatake muendelee na kasi hii ya ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa kutumia Kituo cha pamoja cha huduma ambapo tayari kwa kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka wa fedha wa 2018/2019, mwezi Julai hadi Septemba mwaka 2018 mapato yameongezeka zaidi ya asilimia 100 kwa mwezi na kufikia asilimia 150”, amesema Mhandisi Nditiye.

Kwa upande wake afisa mfawidhi wa forodha wa kituo hicho cha huduma cha pamoja cha Mtukula,- Mohammed Shamte amesema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2018/2019,  malengo yao ni kukusanya shilingi bilioni 15.9 kwa mwaka ambapo tayari imeonekana kiwango hicho kitafikiwa kwa kuwa tayari kwa mwezi wanakusanya shilingi bilioni 1.3.

“Baada ya Serikali kuweka Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, umeongeza spidi na uhakika wa kusafirisha taarifa na data tofauti na hapo awali tulipokuwa tunatumia satelaiti, hivyo mkongo umewezesha ongezeko la mapato”, amesema Shamte.

Naibu Waziri huyo wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye  amefanya ziara hiyo ya kukagua miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye vituo vya mpakani vya Kabanga, Rusumo Mtukula na Biharamulo.

Bilioni Moja atakayefanikisha kupatikana kwa MO

0

Familia ya mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Dewji maarufu kama MO ambaye alitekwa siku chache zilizopita na watu ambao hawajafahamika hadi hivi sasa jijini Dae es salaam imetangaza zawadi ya Shilingi Bilioni Moja kwa mtu yoyote atakayefanikisha kupatikana kwa mfanyabiashara huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, mmoja wa wanafamilia wa mfanyabiashara huyo Azim Dewji amesema kuwa taarifa za mtu atakayefanikisha kupatikana kwa MO zitakua siri.

Azim amesema kuwa mtu yeyote mwenye taarifa hizo awasiliane na familia kupitia namba 0755 030014 na 0717 208478.

Familia ya Dewji pia imeishukuru serikali pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwa jitihada kubwa walizofanya kuhakikisha kuwa MO anapatikana akiwa salama.

Pia imewashukuru Watanzania wote kwa maombi  na dua zao.

 

Koscielny amshukia Deschamps

0

Beki wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Arsenal, – Laurent Koscielny ametangaza kustaafu rasmi soka la kimataifa huku akimkosoa vikali kocha wa timu ya Taifa ya nchi hiyo Didier Deschamps kuwa hakumjali katika kipindi alichokuwa akiuguza jeraha lake.

Koscielny alipata majeraha ya nyama za paja wakati wa mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Yuropa mwezi Mei mwaka huu na kukosa fainali za kombe la FIFA la dunia zilizofanyika nchini Russia na taifa lake kutwaa ubingwa.

Katika taarifa yake, Koscielny amesema kuwa watu wengi wamemfedhehesha wakati akiuguza majeraha yake kitendo ambacho amekifananisha na maumivu makali kwenye kisogo.

Beki huyo ameongeza kuwa wakati ukiwa kwenye kiwango bora unapata marafiki wengi sana lakini ukiwa majeruhi baada ya muda unasahaulika kabisa, na kutolea mfano kocha wake Deschamps kuwa katika kipindi chote amempigia simu mara moja tu wakati wa sikukuu yake ya kuzaliwa na baada ya hapo hakuwahi hata kupata salamu yake.

Koscielny ameichezea Ufaransa katika michezo 51 tangu mwezi Novemba mwaka 2011 na alikuwa kwenye kikosi cha Ufaransa kwenye michuano ya Ulaya ya mwaka 2012 na 2016 pamoja na Kombe la Dunia la mwaka 2014 nchini Brazil.