Mradi wa uboreshaji wa bandari ya Dar es salaam umefikia asimilia 42 ya ujenzi wake hadi hivi sasa huku ukitarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2020.
Hayo yamebainika wakati Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye alipotembelea mradi huo kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wake.
Mradi huo ambao umelenga kuifanya Bandari ya Dar es salaam kuwa ya kisasa zaidi na kuongeza uwezo wake wa kuhudumia meli kubwa kwa wakati mmoja, unahusisha ujenzi wa gati maalum ya kushushia magari, gati namba moja mpaka namba saba, kuongeza kina cha maji katika magati hayo pamoja na kutanua lango la kuingia meli bandarini.
“Nimefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huu ambao hadi sasa umefikia asilimia 42, matarajio yetu mradi huu utaisha kwa wakati uliopangwa,” amesema Mhandisi Nditiye.
Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) Mhandisi Karim Mattaka amesema kuwa mradi huo wa uboreshaji wa bandari ya Dar es salaam, bado upo ndani ya wakati pamoja na changamoto kadhaa zilizojitokeza wakati wa ujenzi wake.
Mhandisi Mattaka amesema kuwa kulikuwa na changamoto kadhaa wakati wa zoezi la kuhamisha mchanga ambapo ilibainika kuwa kuna mchanga laini upo kwenye eneo litakalojengwa gati ya kushushia magari, na hivyo kulazimika kuendelea na ujenzi wa gati namba moja wakati zoezi la kutibu mchanga huo laini likiendelea.
“Ujenzi wa gati namba moja umefikia pazuri kwani unatarajiwa kukamilika mwishoni wa mwezi Disemba mwaka huu na hivyo kuanza kutumika rasmi kabla ya kuhamia gati namba mbili ,” amesema Mhandisi Mattaka.
Ujenzi wa gati maalum ya kushushia magari unatarajiwa kuanza mara zoezi la kutibu mchanga laini litakapokamilika.
Mradi wa uboreshaji bandari ya Dar es salaam waendelea vizuri
Uchaguzi wa Babati Mjini na Ukerewe nao kufanyika Disemba Pili
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo kwenye majimbo mawili na kata 26 za Tanzania Bara.
Majimbo hayo ni Babati Mjini lililopo halmashauri ya mji wa Babati mkoani Manyara na jimbo la Ukerewe katika halmashauri ya wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza
Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji Mbarouk Salum Mbarouk amesema kuwa uchaguzi huo utafanyika pamoja na uchaguzi wa jimbo la Simanjiro mkoani mkoani Manyara na Serengeti mkoani Mara pamoja na kata 21 za Tanzania Bara uliotangazwa awali.
“Nafasi hizo wazi zimetokana na waliokuwa Wabunge wa majimbo hayo Joseph Mkundi (Ukerewe) na Pauline Gekul (Babati Mjini) kujiuzulu kutoka kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),” amesema Jaji Mbarouk.
Jaji Mbarouk amesema kuwa fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya tarehe 28 mwezi huu na tarehe tatu Novemba mwaka huu, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe tatu Novemba mwaka huu, kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe nne Novemba hadi Disemba Mosi na siku ya uchaguzi ni tarehe Pili Disemba mwaka huu.
Ametoa wito kwa wadua wa uchaguzi nchini kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha uchaguzi huo mdogo.
Mawakala wa utalii watembelea Mafia
Mawakala wa utalii kutoka mataifa mbalimbali duniani wapo katika kisiwa cha Mafia mkoani Pwani kwa lengo la kuangalia vivutio vya utalii vinavyopatikana katika kisiwa hicho.
Wakiwa katika kisiwa hicho cha Mafia, Mawakala hao pamoja na mambo mengine wataishauri Bodi ya Utalii Nchini (TTB) namna ya kuweka mpango maalumu wa kutangaza vivutio hivyo vya utalii ambavyo baadhi yake havipatikani mahali popote Barani Afrika isipokuwa Mafia pekee.
Mawakala hao wameyataja maeneo ambayo yakitangazwa vizuri yanaweza kuvutia watalii wengi kutembelea kisiwa cha Mafia kuwa ni ni pamoja na lile analopatikana samaki mkubwa aina ya Potwe ambaye katika Bara la Afrika hupatikana katika kisiwa hicho cha Mafia peke yake.
Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya bahari Dkt Jean de Villiers amesema kuwa samaki aina ya Potwe ni kivutio kikubwa kinachopendwa kuonwa na watalii wengi, hivyo ni wajibu wa Bodi ya Utalii Nchini kuona kivutio hicho kama fursa pekee inayoweza kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea kisiwa cha Mafia na kuchangia pato la Taifa.
Kwa mujibu wa Bodi hiyo ya Utalii Nchini, mafanikio makubwa yanatarajiwa kupatikana baada ya Mawakala hao wa utalii kutoka mataifa mbalimbali duniani kutembelea maeneo matano makubwa yenye vivutio vikubwa vya utalii nchini kikiwemo kisiwa cha Mafia na Zanzibar.
Kaneria akiri kufanya udanganyifu michezoni
Mcheza Kriketi maarufu wa Kimataifa raia wa Pakistan, – Danish Kaneria amekiri kuwa alikuwa akitumia udanganyifu wakati wa mchezo huo na kuisababishia timu yake ushindi.
Kaneria amewaomba radhi Raia wa Pakistan na wapenzi wa mchezo wa Kriketi kwa udanganyifu huo ingawa kwa muda wa miaka Sita amekuwa akikanusha kuhusika na tukio hilo.
Kaneria alifungiwa kucheza mchezo wa kriketi miaka Sita iliyopita lakini amekiri makosa yake baada ya kuwa na mahojiano na kituo cha televisheni cha Al Jazeera.
Hamas wadai kurusha makombora
Wanamgambo wa Hamas kutoka Mamlaka ya Palestina wamedai kurusha makombora kuelekea nchini Israel ikiwa ni hatua ya kupinga kitendo cha nchi ya Misri kutiliana saini mkataba wa amani na Israel.
Kombora hilo lilirushwa kutoka katika Ukanda wa Gaza na kuangukia eneo la kusini mashariki mwa nchi hiyo ya Israel.
Israel nayo ilijibu mashambulio kwa kurusha makombora katika maeneo Ishirini yanayodhibitiwa na Wanamgambo hao wa Hamas na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Uchunguzi wafanyika kubaini kilichompata Kashoggi
Wachunguzi kutoka nchini Uturuki walioingia katika makazi mawili ya maafisa ubalozi wa Saudi Arabia kuchunguza matukio wanayoweza kubaini kilichomtokea mwandishi wa habari wa nchi hiyo Jamal Kashoggi wamemaliza kazi yao.
Wachunguzi hao wamesema kuwa wamepata sampuli mbalimbali zitakazowasaidia kufanya kazi waliyokuwa wametumwa kufanya kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia.
Wameongeza kuwa gari lililokuwa ndani ya ubalozi huo mdogo katika kipindi ambacho Kashoggi aliingia kwenye ubalozi huo na baadaye kuendeshwa katika makazi ya kiongozi mkuu wa ubalozi, linaweza kusaidia kutoa picha kamili ya kile kilichokuwa kikiendelea siku ya tukio.
Wachunguzi hao walilazimika kuchelewa kufanya uchunguzi wao kwa karibu saa 24 katika makazi hayo baada ya kukamilisha uchunguzi katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul kwa kuwa walikosa ushirikiano kutoka kwa maafisa hao wa ubalozi.
Wakati huohuo, wabunge kutoka chama cha Democrat nchini Marekani wanamshinikiza Rais Donald Trump wa nchi hiyo kuchukua hatua dhidi ya Saudi Arabia baada ya Kashoggi kupotea.
Naye Rais wa Bunge la Umoja wa nchi za Ulaya, – Antonia Tajan amesema kuwa anafuatilia kwa karibu tukio la kutoweka katika mazingira ya kutatanisha la mwandishi huyo wa habari wa Saudi Arabia,- Jamal Kashoggi.
Antonia amesema kuwa yeye mwenyewe akiwa kama mwandishi wa habari wa zamani, anafurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na watu hao na jinsi wanavyotoa muhanga maisha yao kwa ajili ya ustawi wa jamii wanayoitumikia.
Ametaka kufanyika kwa jitihada zaidi ili hatma ya Kashoggi iweze kufahamika.
Henry kufanya mambo Monaco
Kocha mpya wa klabu ya AS Monaco, – Thierry Henry amesema kuwa kocha wa Manchester City, – Pep Guardiola atakuwa motisha kubwa kwake katika majukumu yake mapya ya ukocha nchini Ufaransa.
Henry ambaye alianza maisha yake ya soka la kiushindani kwenye klabu ya Monaco, amerejea kwenye klabu hiyo kama kocha baada ya klabu hiyo kumtimua kocha wake Leonardo Jardim kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo kwenye ligi.
Nyota huyo wa zamani wa Arsenal ambaye amewahi pia kuichezea FC Barcelona chini ya Guardiola amesena kuwa Pep ni muongozo mzuri kwake kutokana na mbinu alizonazo wakati mchezo ukiendelea na hata kabla ya mchezo.
Alipoulizwa kuhusu Mfaransa mwenzake Arsene Wenger ambaye chini yake alicheza kwa mafanikio makubwa, Henry amesema kuwa siku zote Wenger atabaki kuwa mtu muhimu kwake aliyemfanya kujua nini maana ya soka la ushindani na wanamahusiano mazuri na kuna baadhi ya vitu kutoka kwake atavitumia kwenye kazi yake ya ukocha.
Henry ambaye alikuwa kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Ubelgiji, amesaini mkataba wa miaka mitatu na Monaco utakaofanya kuhudumu hadi mwezi June mwaka 2021 na mwaka 1997 aliisaidia Monaco kushinda taji la ligi ya Ufaransa na sasa anakibarua cha kuinasua timu hiyo kutoka mkiani na mchezo wake wa kwanza utakuwa dhidi ya Strasbourg Oktoba 20 mwaka huu kabla ya kumenyana na Club Brugge siku nne baadae kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya.
Wenger kurejea kibaruani Januari
Aliyekuwa kocha wa washika mtutu wa jiji la London Arsenal, Mzee Arsene Wenger amesema kuwa anatarajia kurejea kibaruani kuanzia Januari Mosi mwaka 2019 na amepokea ofa kutoka kila kona ya dunia.
Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 68 alisitisha huduma yake ya miaka 22 ndani ya kikosi cha Arsenal msimu uliopita na mpaka sasa bado hajajua kazi yake mpya itakuwa wapi ingawa amesema kufanya kazi na chama cha soka, timu ya taifa au kurejea Japan ambapo aliwahi kuifundisha timu ya Nagoya Grampus Eight, mojawapo linawezekana.
Wenger amesema kuwa amepumzika vya kutosha, na sasa yupo tayari kufanya kazi tena ingawa hajajua ni wapi na kuongeza kuwa miaka 22 aliyohudumu Arsenal imempa uzoefu wa kutosha na mezani kwake ana ofa za kutosha kutoka sehemu mbalimbali duniani, hivyo ni yeye tu kuchagua wapi pa kwenda.
Wenger alianza kazi ya ukocha kwenye klabu ya Nancy kabla ya kujiunga na Monaco ambapo alidumu nayo kwa miaka Saba na kushinda taji la Ufaransa katika msimu wa kwanza akiwa na timu hiyo na baadae kutimkia Japan ambapo alihudumu kwa muda mfupi kabla ya kujiunga na Arsenal mwaka 1996 na kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu ya England, na saba ya kombe la FA.
Katika hatua nyingine, Wenger amesema kuwa timu ya taifa ya Ujerumani bado inahitaji huduma ya kiungo Mesut Ozil ambaye alitangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya kukwaruzana na chama cha soka cha nchi hiyo siku chache baada ya kutolewa kwenye fainali za kombe la FIFA la dunia zilizofanyika nchini Russia.
Wenger ameongeza kuwa anaamini Ujerumani inamhitaji Ozil na anategemea kocha wa timu hiyo Joachim Low atamshawishi mchezaji huyo kurejea kwenye kikosi hicho kwani kiungo huyo ni mchezaji wa daraja la juu na siku zote anapenda kuona akicheza na asipochezea timu ya taifa kuna vitu atapoteza.