China yafungua daraja refu zaidi duniani

0

Rais Xi Jinping  wa China amefungua daraja refu zaidi duniani lenye urefu wa kilometa 55 linaloyaunganisha maeneo mawili ya Hong Kong na Macau.

Sherehe za ufunguzi wa daraja hilo zimepambwa na burudani mbalimbali na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa miji ya Hongkong na Macau.

Ujenzi wa daraja hilo lililovunja rekodi umeigharimu China Dola bilioni  Ishirini za Kimarekani na umechukia muongo mmoja kumaliza ujenzi wake.

Daraja hilo ambalo limejengwa kuhimili matetemeko makubwa ya ardhi na vimbunga, linajumuisha njia ya urefu wa kilimota 30 iliyopita kwenye mlango wa Mto Pearl na linajumuisha pia visiwa viwili vidogo vya kujengwa na binadamu.

Ufunguzi wa daraja hilo unaelezwa kuwa utapunguza muda wa safari kutoka Hong Kong hadi China kwa hadi dakika 30 badala ya saa nne, jambo ambalo China imesema kuwa itakuwa kiungo muhimu kwa ukuaji wa uchumi katika siku zijazo.

 

 

Erdogan atoa maelezo kuhusu mauaji ya Khashoggi

0

Rais Recep Tayyip Erdogan  wa Uturuki ametoa maelezo ya kwanza rasmi juu ya mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul na kudai kuwa mauaji hayo yalipangwa.

Rais Erdogan amesema kuwa mpango wa mauaji hayo ulianza kuandaliwa Septemba 29 mwaka huu na kwamba aliuawa Oktoba pili.

Amesema kuwa kamera za ubalozini hapo ziliondolewa kabla ya mauaji hayo na siku moja kabla ya mauaji wataalamu wa uchunguzi wa jinai waliwasili mjini Istanbul na baada ya Khashoggi kuuawa mmoja wa wataalamu hao alivaa nguo zake na kutoka ubalozini hapo ili aonekane kuwa mwandishi huyo alitoka.

Rais Erdogan ameutaka utawala wa kifalme wa  Saudi Arabia uwataje wote waliohusika na mauaji ya Khashoggi ambao pia walirekodi kila kitu kilichofanyika.

Rais huyo wa Uturuki ametaka watuhumiwa 18 waliokamatwa nchini Saudi Arabia kwa kuhusika na mauaji hayo wapelekwe nchini Uturuki kujibu mashtaka yao na kuongeza kuwa  hana mashaka na uadilifu wa mfalme wa Saudi Arabia lakini anachotaka ni uchunguzi wa uwazi.

 

Rais Magufuli akutana na Dkt Kikwete

0

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Kikwete  Ikulu jijini Dar es salaam.

Baada ya mazungumzo yao, Rais Mstaafu Kikwete amesema kuwa wamekutana kwa utaratibu wa kawaida wa kusalimiana na kutakiana heri katika majukumu.

Aidha, Rais Mstaafu Kikwete amebainisha kuwa Rais Magufuli anafanya kazi nzuri na amemtaka aendelee hivyo hivyo.

Nimekuja kumsalimia na kumtakia kila la heri, anafanya kazi nzuri, aendelee tu kuchapa kazi na sisi tupo kwa namna yoyote ya kumpa nguvu, tupo tayari kumsaidiaamesema Rais Mstaafu Kikwete.

 

Kongamano la kimataifa la uwekezaji laendelea Uswisi

0

Tanzania ni  miongoni mwa nchi 160 duniani zinazoshiriki katika kongamano la kimataifa la uwekezaji (World Investment Forum) linaloendelea Geneva, -Uswisi.

Kongamano hilo la siku Tano limebeba kaulimbiu inayosema kuwa uwekezaji kwa maendeleo endelevu na lina lengo la kuimarisha uwekezaji kwenye nchi hizo.

Pamoja na mambo mengine, washiriki wa kongamano hilo lililoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) wanajadili changamoto za uwekezaji katika mazingira mapya ya utandawazi na mapinduzi ya viwanda.

Kongamano hilo limekua likiandaliwa na UNCTAD kila baada ya miaka miwili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya uwekezaji ambapo kwa mwaka huu kuna zaidi ya  washiriki elfu Tano kutoka nchi hizo 160 duniani ambapo ujumbe wa Tanzania unaoongozwa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Dkt. James Msekela.

Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC)  nacho kinashiriki katika kongamano hilo ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho  Geoffrey Mwambe anashiriki katika vipindi, midahalo na majadiliano mbalimbali kwa lengo la kuinadi Tanzania hasa  katika  fursa za uwekezaji.

 

Matokea ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi yatangazwa

0

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA ) limetangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE ) uliofanyika tarehe Tano  na Sita mwezi Septemba mwaka huu ambapo jumla ya watahiniwa 733, 103 kati ya 943,318 wamefaulu mtihani huo.

Katibu Mtendaji wa NECTA Dkt Charles Msonde amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuwa watahiniwa hao waliofaulu wamepata alama 100 na zaidi kati ya alama 250 zinazohitajika  na kwamba idadi hiyo ya waliofaulu ni sawa na asilimia 77.72.

Kwa mujibu wa Dkt Msonde, mwaka 2017 watahiniwa walifaulu kwa asilimia 72.76, hivyo kuna ongezeko la ufaulu kwa asilimia 4.96.

Kwa upande wa ufaulu kimasomo, Dkt Msonde amesema kuwa takwimu za matokeo zinaonesha kuwa katika masomo ya kiingereza, maarifa ya jamii, hisabati na sayansi ufaulu umepanda kwa kati ya asilimia 4.03 na 11.92 ikilinganishwa na mwaka 2017 huku kwa somo la kiswahili ufaulu wake ukishuka kwa asilimia 1.44 ikilinganishwa na mwaka 2017.

Katibu Mtendaji huyo wa NECTA Dkt Charles Msonde ameongeza kuwa watahiniwa wamefaulu zaidi katika somo la Kiswahili na katika somo la kiingereza wamefaulu kwa kiwango cha chini zaidi.

Amezitaja shule kumi bora zilizofanya vizuri kitaifa zenye idadi ya watahiniwa zaidi ya arobaini kuwa ni Raskazone ya mkoani Tanga, Nyamuge ya mkoani Mwanza, Twibhoki ya mkoani Mara, Kwema Modern na Rocken Hill za mkoani Shinyanga, St Anne Marie ya mkoani Dar es salaam, Jkibira, St. Achileus Kiwanuka, St. Severine na Rweikiza zote za mkoani Kagera.

Shule Kumi ambazo hazikufanya vizuri kitaifa ni Mangika ya mkoani Tanga, Mwazizi ya mkoani Tabora, Isebanda ya mkoani Simiyu, Malagano ya mkoani Tabora, Magana ya mkoani Mara, Kododo ya mkoani Morogoro, Mtindili ya mkoani Tanga, Lumalu ya mkoani Ruvuma, Chidete ya mkoani Dodoma na Mavului ya mkoani Tanga.

Rais Magufuli ateua wenyeviti wa taasisi tano za serikali

0

Rais Dkt. John Magufuli ameteua wenyeviti wa bodi za taasisi tano za serikali baada ya wenyeviti waliokuwa wakiongoza bodi hizo kumaliza muda wao na wengine kuteuliwa katika nyadhifa nyingine.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, imesema walioteuliwa ni Profesa Charles Mkonyi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mifupa (MOI), Mwamini Malemi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Sukari, Sophia Simba kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dkt. Mwanza Kamata kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) na Dkt. Maria Mashingo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo (TIB).

Uteuzi wa wenyeviti hao wa bodi umeanza leo tarehe 22 Oktoba, 2018.

Utafiti wabainisha Malaria yapungua nchini

0

Utafiti wa viashiria vya ugonjwa wa Malaria kwa mwaka 2017 unaonyesha kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa huo nchini kutoka asilimia 14 ya mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 7.3.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo jijini Dar Es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema utafiti huo umefanyika nchi nzima.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amewataka maafisa afya na mazingira katika halmashauri zote nchini kujikita katika usafi wa mazingira ili kuua mazalia ya mbu wanaosababisha malaria.

Utafiti wa viashiria vya Malaria wa mwaka 2017 nchini umefanyika ili kutoa taarifa zitakazosaidia kufuatilia  hali ya malaria nchini.

Waziri Mkuu asisitiza ushirikiano kwa ajili ya amani

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ushirikiano baina ya taasisi za dini nchini na serikali ni jambo muhimu katika kuimarisha amani.

Waziri Mkuu ameyasema hayo mjini Mwanza akiwa njiani kwenda mkoani Simiyu ambako kesho anatarajia kufungua maonesho ya wajasiriamali.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Mwanza ina wajibu wa kuhakikisha maeneo ya mkoa huo yanaendelea kuwa salama.

Halkadhalika Waziri Mkuu amempongeza Kaimu Sheikh wa mkoa wa Mwanza, Sheikh Hassan Bin Mussa Kabeke kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.