Wafanyabiashara wa Tanzania na Ubelgiji kukutana

0

Kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Ubelgiji linatarajiwa kufanyika jijini Dar es salaam Oktoba 25 hadi 27 mwaka huu na kushirikisha zaidi ya kampuni arobaini na wafanyabiashara wakubwa takribani mia mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam,  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa  Afrika  Mashariki Dkt Damas Ndumbaro amesema kuwa kongamano hilo lina lengo la kujenga uzoefu na kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo kati ya mataifa hayo.

Amesema kuwa Tanzania na Ubelgiji zimekuwa na ushirikiano mkubwa wa masuala ya uwekezaji, hivyo kufanyika kwa kongamano hilo kunazipa fursa nchi hizo kuimarisha uhusiano wao uliodumu kwa muda mrefu.

“Serikali za Tanzania na  Ubelgiji  zinatekeleza miradi  32 ya biashara na uwekezaji  katika sekta mbalimbali  ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji yenye thamani ya dola 902.01 za Kimarekani  ambayo itatengeneza ajira kwa watanzania zaidi ya 1814”, amesema Dkt Ndumbaro.

Akizungumzia sekta ya utalii,  Dkt Ndumbaro amesema kuwa hivi sasa Tanzania na Ubelgiji  wameanza kujadili mikataba mbalimbali ya utalii na endapo itasainiwa itakuwa na manufaa makubwa kwa kuongeza pato la Taifa, ambapo takwimu zinaonyesha kuwepo kwa ongezeko la watalii elfu sita kutoka 7,057 mwaka 2012 hadi kufikia watalii 12,253 mwaka 2017.

Kwa upande wake balozi wa Ubelgiji nchini, Peter Van Acker amesema kuwa kongamano hilo litaipatia fursa nchi yake ya kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kibiashara na Tanzania, kwa kuwa wafanyabiashara wengi wa nchi hiyo wamekuwa na mwamko mkubwa wa kuzifahamu fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania.

“Mkutano huu utaimarisha mahusiano yetu ya kidiplomasia na kibiashara, hivyo tuna mategemeo makubwa kwa wafanyabiashara hawa wakikaa pamoja watabadilishana uzo

Tanzania haina ukandamizaji wa uhuru wa habari

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania hakuna ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari wala taasisi zisizo za kiserikali.

Amesema kuwa jambo hilo linadhihirishwa na uwepo wa jumla ya vituo vya redio 152, ambavyo kati yake ni vituo vitatu tu ndivyo vinavyomilikiwa na serikali.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee.

“Tunapenda kuwahakikishia kuwa, Serikali ya Tanzania inaongozwa na katiba na sheria za nchi ambazo zinatoa uhuru wa kujieleza na kupata habari,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Amesema kuwa mwananchi yeyote atakayeenda kinyume na sheria, serikali itamuwajibisha kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, serikali imeridhia mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na ule wa haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni.

Ameongeza kuwa pamoja na kusimamia haki hizo, serikali imeendelea kutekeleza wajibu wake katika kuiwezesha jamii kuishi salama kwa amani na utulivu kwa kuzingatia sheria za nchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa zoezi la kuwarejesha wakimbizi wa Burundi nchini kwao lilikuwa ni la hiari na limetekelezwa baada ya hali ya amani kurejea nchini humo.

Amesema kuwa hakuna sababu ya kuendelea kuwahifadhi wakimbizi ambao kwa hiari yao wameamua kurejea nchini kwao ili wakaendelee na shughuli za kulijenga Taifa lao.

“Nasisitiza kuwa zoezi hili ni la hiari, tangu mwezi Septemba mwaka jana Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Burundi na UNHCR imekuwa ikiwarejesha wakimbizi hao kwao,”amesema Waziri Mkuu.

Amefafanua kuwa zoezi hilo limekuwa likifanyika kwa kuzingatia usalama na utu wa wakimbizi hao.

Wakimbizi 52,283 wa Burundi wamerejea nchini kwao kati 81,281 waliokwisha jiandikisha.

Waziri Mkuu Majaliwa amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada baadhi ya nchi kuishutumu serikali kwa namna ilivyoendesha zoezi hilo.

Pamoja na kutoa ufafanuzi huo, Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa na washirika wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1967 wa kuwahudumia wakimbizi ili kufanikisha zoezi hilo la kuwarejesha makwao kwa hiari na kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu.

Maadhimisho hayo ya siku ya Umoja wa Mataifa ambao umetimiza miaka 73 tangu uanzishwe, yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Damas Ndumbaro, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), -Alvaro Rodrigues pamoja na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Upasuaji wa aina yake wafanyika Uingereza

0

Madaktari nchini Uingereza wamewafanyia upasuaji wa uti  wa mgongo watoto wawili zikiwa ni zimesalia wiki chake kabla ya watoto hao kuzaliwa.

Upasuaji huo ambao ni wa kwanza na wa aina yake kufanyika nchini Uingereza umefanywa na kundi la madaktari 30 kutoka katika chuo kimoja jijini London.

Watoto hao walikuwa na tatizo lilalojulikana kama Spina Bifida, tatizo ambalo uti wa mgongo hushindwa  kukua inavyotakiwa na unakua na nafasi kwa ndani.

Mara nyingi tatizo hilo hutibiwa baada ya mtoto kuzaliwa lakini kama linatibiwa mapema zaidi mtoto akiwa tumboni,  afya ya mtoto inaimarika zaidi.

Upasuaji huo wa uti  wa mgongo wa watoto wawili ambao bado hawajazaliwa nchini Uingereza  umefanyika kwa muda wa dakika 90 kwa kila mmoja, ambapo madaktari hao walipasua matumbo ya mama zao na kisha kushona pamoja sehemu ya uti wa mgongo wa mtoto iliyokuwa imeachana.

Madaktari kutoka taasisi mbalimbali nchini Uingereza wamesema kuwa upasuaji wa aina hiyo ni hatari, kwa kuwa unaweza kusababisha mama apatwe na uchungu mapema wa kujifungua.

Endapo mama hao wajawazito wasingefanyiwa upasuaji wa  aina hiyo nchini Uingereza, wangelazimika kusafiri na kwenda  katika  nchi za Marekani, Ubelgiji au Uswisi ili kupata huduma hiyo.

Habari zaidi zinasema kuwa zaidi ya watoto mia mbili huzaliwa na tatizo hilo la Spina Bifida duniani kila mwaka duniani kote, tatizo linalotokea wakati kitu kinachoitwa Neural Tube ambacho ni  awamu ya kwanza ya kukua kwa ubongo na uti wa mgongo kukua kwa namna isiyostahili na hivyo kusababisha kuwepo kwa nafasi kwenye uti wa mgongo.

Marekani yaijia juu Saudia mauaji ya Kashoggi

0

Rais Donald Trump wa Marekani ameziita harakati za Saudi Arabia za kuficha ukweli juu ya mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi kuwa ni mbaya zaidi kuwahi kutokea na kwamba za kihistoria.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani, -Trump amesema kuwa mtu yeyote aliyepanga mauaji hayo anatakiwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Walikuwa na wazo duni sana na wakalitekeleza vibaya mno, na kiufupi harakati zao za kuuminya ukweli ndio mbovu zaidi katika historia ya kujaribu kuficha ukweli”, ameongeza Rais Trump.

Marekani imekuwa ikipata shinikizo kutoka Uturuki pamoja na Jumuiya ya Kimataifa la kuwabana washirika wao Saudi Arabia kuhusu mauaji hayo ya Kashoggi yaliyotokea kwenye ofisi za ubalozi mdogo wa nchi hiyo jijini Instanbul, – Uturuki.

Baada ya Rais Trump kutoka kauli hiyo,  Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, –  Mike Pompeo ametangaza kufutwa hati za kusafiri za kuingia  nchini Marekani kwa  zaidi ya watu ishirini wanaotuhumiwa kutekeleza mauaji ya mwandishi huyo wa habari.

Khashoggi anadaiwa kuingia kwenye ofisi hizo za ubalozi mdogo wa Saudi Arabia jijini Instanbul, – Uturuki Oktoba pili mwaka huu kwa lengo la kushughulikia nyaraka binafsi na hakutoka tena.

Awali Saudia walisema kuwa alitoka  na baada ya shinikizo kubwa kutoka Uturuki pamoja na Jumuiya ya kimataifa ikakiri kuwa aliuawa alipojaribu kupambana na baadae ikasema kuwa Kashoggi ameuawa katika operesheni isiyo rasmi.

 

AL Ahly sasa kumenyana na Esperance

0

Bingwa wa kihistoria wa ligi ya mabingwa Barani Afrika, – AL Ahly ya Misri imetinga fainali ya ligi hiyo na itamenyana na Esperance ya Tunisia kwenye mchezo wa fainali baada ya usiku wa Oktoba 23 mwaka huu timu zote mbili kusonga mbele katika michezo yao ya marudiano ya hatua ya nusu fainali.

Esperance ndio walikuwa wa kwanza kutinga fainali baada ya kupindua matokeo ya kichapo cha bao moja kwa sifuri walichokipata nchini Angola kutoka kwa wapinzani wao Premeiro Agosto.

Wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani mjini Rades, -Esperance wamewatandika Agosto mabao manne kwa mawili na kutinga fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao manne kwa matatu.

AL Ahly wao licha ya kufungwa mabao mawili kwa moja na Entente Setif ya Algeria, timu hiyo imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao matatu kwa mawili kufuatia ushindi wa mabao mawili kwa nunge ilioupata kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza wakiwa nyumbani.

Mchezo wa kwanza wa fainali utachezwa wikiendi ya Novemba mbili au tatu, huku mchezo wa marudiano ukichezwa wikiendi itakayofuata.

Timu hizo mbili zina kumbukumbu ya kukutana kwenye fainali ya mwaka 2012 ambapo AL Ahly iliishinda Esperance.

Mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuanza leo

0

Mzungumzo wa 11 wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaanza hii leo kwa kuchezwa michezo Sita.

Moja kati ya michezo itakayochezwa ni wabishi wa jiji la Mwanza,- Mbao FC watakaokuwa wenyeji wa Lipuli kutoka Iringa katika mchezo utakaowakutanisha makocha wawili waliohudumu katika kikosi kimoja cha timu ya Lipuli msimu uliopita, ambao ni Amri Saidi ambaye kwa sasa ni kocha wa Mbao FC na Suleiman Matola ambaye ni kocha wa Lipuli FC.

Kocha mkuu wa Mbao FC, – Amri Said amesema kuwa licha ya wachezaji wanne muhimu katika kikosi chake kuukosa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi, anaamini atapata matokeo mazuri.

Mbali na mchezo huo wa Mbao FC dhidi ya Lipuli, pia JKT Tanzania watawakaribisha Azam FC, Ruvu shooting Stars wakiwa wenyeji wa Singida United na Coastal Union wakiwa Mkwakwani Tanga watawakaribisha Kagera Sugar.

Pale katika dimba la kumbukumbu ya Sokoine mkoani Mbeya, wenyeji wa dimba hilo Tanzania Prisons watawaalika African Lyon na bingwa mtetezi wa ligi hiyo Simba atakuwa mwenyeji wa Alliance FC ya Mwanza, mchezo utakaochezwa katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam kuanzia saa moja jioni na kutangazwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia kituo chake cha redio cha TBC Taifa.

Watoto wa familia moja wauawa kikatili Kagera

0

Miili ya watoto wawili ambao ni ndugu wa familia moja imeokotwa ikiwa imetenganishwa kichwa na kiwiliwili katika shamba la migomba  kwenye kijiji cha Mashule kata ya Kyamulaile wilayani Bukoba mkoani Kagera.

Kufuatia tukio hilo,  Mkuu wa wilaya ya Bukoba, –  Deodatus Kinawiro ameliagiza Jeshi la polisi  wilayani Bukoba kufanya uchunguzi wa haraka na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo.

Watoto hao waliouawa ni Auson Respicius mwenye umri wa miaka Saba na ndugu yake Aristidia Respicius mwenye umri wa miaka Mitano.

Tayari ya jeshi la Polisi mkoani Kagera linawashilikia watu tisa kwa kuhusika na tukio hilo ambalo linahusishwa na imani za kishirikina.

SIDO yatakiwa kubuni teknolojia na mitambo rafiki

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Nchini (SIDO) kujielekeza katika kubuni teknolojia na mitambo rafiki inayolenga kutatua changamoto za wajasiriamali kulingana na mazingira yao.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akifungua maonesho ya SIDO kitaifa yanayofanyika kwenye viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi mkoani Simiyu na kuhudhuriwa na wajasiriamali takribani mia tano.

Amesema  kuwa serikali inaendelea kuimarisha shughuli za SIDO lakini bado kuna  changamoto za wajasiriamali wadogo ambazo lazima zishughulikiwe kwa kasi kubwa ili kufungamanisha shughuli za shirika hilo na uchumi wa viwanda

Waziri Mkuu ameongeza kuwa, ili kufikia uchumi wa kati inambidi kila Mtanzania mahali alipo afanye kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu.

“Tusipoteze wakati kwa kufanya mambo yasiyo na tija, tuzingatie falsafa ya serikali ya awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu, fano kwa hapa Bariadi, tunatarajia SIDO watuletee teknolojia na mitambo inayoweza kurahisisha ukamuaji wa mafuta yanayotokana na mbegu za alizeti na pamba, kwa Dodoma teknolojia na mitambo kwa ajili ya kuchakata zabibu,”ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesisitiza kuwa ili nchi iweze kupata mafanikio, SIDO inatakiwa iwaunganishe wajasiriamali na taasisi mbalimbali za fedha ili wapate mikopo yenye masharti nafuu.

Pia, Waziri Mkuu Majaliwa amewasihi wajasiriamali wanaoshiriki maonesho hayo kutumia fursa hiyo kujifunza namna nzuri ya kuboresha viwango vya bidhaa zao na kubadilishana ujuzi na uzoefu, kupanua masoko na kubaini teknolojia zitakazorahisisha uzalishaji wa bidhaa.

Awali, Waziri Mkuu alitembelea mabanda mbalimbali ya washiriki wa maonesho hayo yakiwemo ya taasisi za Serikali zinazotoa huduma katika sekta ya viwanda na biashara ambazo ni pamoja na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini  (TFDA) na  Wakala wa Vipimo Nchini (WMA).

Waziri Mkuu ametoa wito kwa taasisi hizo kuhakikishe zinafanya kazi kwa kushirikiana, ujuzi na weledi ili kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kuendesha shughuli zao kwa viwango vinavyotakiwa.