Ripoti ya uchunguzi wa ajali ya MV Nyerere yakamilika

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea ripoti ya uchunguzi wa  ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza kutoka kwa kamati iliyoundwa na serikali kwa ajili ya kuchunguza ajali hiyo.

Waziri Mkuu amepokea ripoti hiyo  jijini Dar es salaam aliyokabidhiwa na Mwenyekiti wa Kamati  hiyo ambaye ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu Jenerali George Waitara.

Mara baada ya kupokea ripoti hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa ameishukuru kamati hiyo kwa niaba ya Rais John Magufuli kwa kazi kubwa waliyoifanya ambayo imethibitisha umakini wao.

Pia ameipongeza kamati hiyo kwa namna walivyotumia muda wao vizuri kwa kufanya kazi hiyo na kutoa mapendekezo kwa serikali juu ya mambo waliyoyabaini.

“Nimepokea taarifa kwa niaba ya Serikali, Serikali itafanya mapitio ya taarifa yote na viambatisho vyake na itapitia kwa kina mapendekezo mliyoyatoa ambayo yote yatafanyiwa kazi,” amesema Waziri Mkuu.

Amesema kuwa serikali inaamini mambo yote yaliyosheheni katika ripoti hiyo ni yale ambayo Watanzania wanasubiri kuona yakifanyiwa kazi.

Kivuko cha MV Nyerere kilipinduka na kuzama Septemba Ishirini mwaka huu katika ziwa Viktoria ambapo zaidi  ya watu Mia Mbili walikufa maji na wengine zaidi ya arobaini kuokolewa.

Kufuatia ajali hiyo, Septemba 24 mwaka huu,  Waziri Mkuu Majaliwa  alitangaza kamati ya kuchunguza ajali hiyo, Kamati  yenye wajumbe saba na kuitaka kukamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

 

Palestina yaahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania

0

Palestina imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo za afya na kilimo.

Ahadi hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na balozi wa Palestina nchini Hamdi Mansour Abdu Ali wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.

Amesema kuwa kukua kwa  uchumi wa Palestina kwa kiasi kikubwa kumetokana na shughuli za kilimo,  hivyo nchi hiyo ina nafasi kubwa ya kuisaidia Tanzania katika sekta ya kilimo.

Kwa mujibu wa balozi Hamdi,  Palestina pia inaandaa utaratibu wa kuwasaidia wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania kutoka sekta binafsi ili waweze kupata uzoefu kutoka nchini humo.

Balozi  Hamdi  ametumia mkutano huo na waandishi wa habari kumpongeza Rais John Magufuli  kutokana na kutekeleza sera zenye lengo la kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa viwanda.

 

Salman azungumzia kifo cha Kashoggi

0

Kwa mara ya kwanza mwana wa mfalme wa Saudi Arabia, – Mohammed Salman anayetuhumiwa kupanga mauaji ya mwandishi wa habari wa nchi hiyo Jamal Kashoggi, amezungumzia kifo cha mwandishi huyo.

Akizungumza katika mkutano wa wafanyabiashara mjini Riyadh, – Salman amesema kuwa Kashoggi amekufa kifo cha kusikitisha na serikali yake itafanya kila iwezalo kuwatia hatiani wale wale wote waliohusika na tukio hilo.

Oktoba 24 mwaka huu, mwana huyo wa mfalme pamoja na baba yake walikwenda kuwapa pole watoto wa kiume wa Kashoggi nchini Saudi Arabia, jambo ambalo pia liliwatia mashaka watu wengi.

Maafisa usalama Marekani wapongezwa

0

Aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais nchini Marekani katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliopita Hilarry Clinton amewapongeza maafisa usalama nchini humo kwa kubaini milipuko iliyokuwa imelengwa kumuangamiza.

Hillary amesema kuwa maafisa usalama nchini humo wamefanya kazi kubwa ya kuokoa maisha yake na ya familia yake baada ya kutumiwa kifurushi ambacho kilibainika kuwa na vitu vyenye milipuko.

Idara ya usalama nchini Marekani pia imethibitisha kifurushi kingine alichotumiwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Barack Obama pamoja na bilionea mmoja nchini humo, vyote vilikuwa na vitu vyenye milipuko.

Kifurushi kingine kama hivyo kilitumwa katika ofisi za kituo cha televisheni cha CNN nchini Marekani.

Rais Donald Trump wa Marekani amewalaumu wale wote waliohusika na matukio hayo na kusema kuwa hayawezi kuvuruga amani na demokrasia nchini humo.

Sahle Rais mpya Ethiopia

0

Sahle-Work Zewde amekuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais nchini Ethiopia baada ya bunge la nchi hiyo kuidhinisha uteuzi wake.

Sahle anachukua madaraka baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, – Abiy Ahmed kufanya mabadiliko makubwa katika baraza lake la mawaziri.

Sahle ni mwanadiplomasia na analazimika kuachia wadhifa wake katika ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alikokuwa akifanya kazi kwa sasa.

Makamu wa Rais aendelea na ziara yake Pwani

0

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameziagiza halmashauri  zote nchini kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji  ili kudhibiti vyanzo hivyo visiharibiwe na watu wanaoendesha shughuli za kibinadamu.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo wilayani Bagamoyo  mkoani Pwani wakati akikagua  mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Chini unaofanywa kwa pamoja na ujenzi wa tanki kubwa  ambalo litatumika kusambaza maji kwenye mji wa Bagamoyo na vijiji jirani.

Amesema kuwa serikali imetumia gharama kubwa kutekeleza mradi huo ili kuondoa kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika miji ya Bagamoyo na Dar es salaam, hivyo ni vema halmashauri nchini zikaweka utaratibu mzuri wa kutunza vyanzo hivyo.

Akiwa katika wilaya hiyo ya Bagamoyo ikiwa ni  sehemu ya ziara yake ya siku sita mkoani Pwani, Makamu wa Rais amewaomba Watanzania wote kutunza  miundombinu ya maji inayojengwa katika maeno yao.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amemueleza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa huo imeongezeka hadi kufikia asilimia 51 kwa maeneo ya mijini na asilimia 62 kwa maeneo ya vijijini.

Mazungumzo ya kutafuta amani Burundi yaendelea

0

Awamu ya tano ya mazungumzo ya kutafuta amani nchini Burundi yanafanyika hii leo jijini Arusha, chini ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mzee Benjamini Mkapa.

Mazungumzo hayo yalikua yafanyike jana Oktoba 24 lakini yaliahirishwa kwa kile kilichodaiwa na upande wa upinzani kuwa ni kuishinikiza serikali kutuma washiriki katika mazungumzo hayo.

Makundi ya upinzani yanayoshiriki mazungumzo hayo yamesema kuwa mazungumzo hayo hayatakua na maana yoyote ikiwa serikali ya Burundi haitatuma wawakilishi na kwamba sababu zilizotolewa na serikali za kutotuma wawakilishi si za msingi.

Tangu mazungumzo ya kutafuta amani ya Burundi yaanze miaka mitatu iliyopita, pande zinazopigana hazijawahi kukutana ana kwa ana na badala yake msuluhishi wa mgogoro huo Mzee Mkapa amekuwa akikutana na pande hizo kwa nyakati tofauti.

Wahalifu kuendelea kusakwa

0

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro amesema kuwa jeshi hilo litaanzisha operesheni ya kuwasaka watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha za moto na kusababisha mauaji kwa watu wasiokuwa na hatia pamoja na kuwajengea hofu wananchi.

IGP Sirro ametoa kauli hiyo katika tarafa ya Nguruka wilayani Uvinza mkoani Kigoma kufuatia tukio la kushambuliwa na kuuawa kwa askari wawili na mwingine mmoja kujeruhiwa wakiwa katika operesheni ya kuwaondoa watu waliovamia eneo linalomilikiwa na  Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO)  na kuendesha shughuli za kilimo kinyume cha sheria.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini pia ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kushirikiana na jeshi hilo ili kuwafichua watu wanaojihusisha na matukio ya uhalifu yakiwemo yale ya mauaji  ili wachukuliwe hatua za kisheria.