Shambulio laua 21 Yemen

0

Watu 21 wameuawa na wengine kumi kujeruhiwa baada ya muungano wa vikosi vya kijeshi ukiongozwa na Saudi Arabia kushambulia eneo moja la soko nje ya mji wa Hodeida nchini Yemen.

Shambulio  hilo la bomu limefanywa zikiwa zimepita siku sita  tu tangu vikosi hivyo kufanya shambulio jingine katika soko la samaki lililopo kwenye mji huohuo wa Hodeida.

Mratibu wa shughuli za kibinadamu kutoka Umoja wa Mataifa nchini Yemen, – Lisa Grande ameelezea kusikitishwa na mashambulio yanayoendelea kufanywa na muungano wa vikosi hivyo vya kijeshi ukiongozwa na Saudi Arabia ambayo yamekua yakisababisha vifo vya raia  wengi wasio na hatia.

Mpaka sasa, maafisa wa Saudi Arabia hawajatoa taarifa yoyote kuhusu mashambulio hayo.

Saudi Arabia yakiri kupangwa kwa mauaji ya Khashoggi

0

Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Saudi Arabia, – Saud Al-Mojeb amesema kuwa mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi yalipangwa.

Taarifa  ya Al-Mojeb inakinzana na ile iliyotolewa awali kwamba Khashoggi aliuawa kwa bahati mbaya akiwa kwenye ubalozi mdogo wa Saudia Arabia mjini Instanbul nchini Uturuki.

Katika taarifa hiyo ya awali, maafisa wa Saudi Arabia pia walidai kwamba Khashoggi aliingia na baadaye aliondoka katika ubalozi huo mdogo.

Kauli hiyo ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Saudi Arabia inaashiria kuwa watuhumiwa wa mauaji ya Khashoggi walifanya kitendo hicho kwa kudhamiria.

Habari zaidi kuhusu mauaji hayo ya Kashoggi zinasema kuwa Kansela wa Ujerumani, -Angela Merkel amezungumza na mwana mfalme wa Saudi Arabia, – Mohammed Salman na kulaani mauaji hayo.

Merkel ametaka kufanyika kwa uchunguzi wa haraka, wa wazi na wenye kuaminika kuhusu tukio hilo na wahusika wote wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

China na Japan kuimarisha uhusiano

0

China na Japan zimekubaliana kuimarisha uhusiano wa kiuchumi katika kipindi hiki ambapo China iko kwenye mzozo wa kibiashara na Marekani.

Hayo yamebainika wakati wa hafla ya kutiliana saini makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi hizo mbili wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Japan, – Shinzo Abe nchini China.

Waziri Mkuu huyo wa Japan akiwa na mwenyeji wake ambaye ni Waziri Mkuu wa China, -Li Keqiang amewaambia waandishi wa habari nchini China kuwa masuala mengine waliyokubaliana ni pamoja na kushirikiana ili kuondoa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea Kaskazini.

Maeneo mengine ni katika teknolojia ya kisasa, ulinzi wa haki miliki na  biashara ya kubadilisha sarafu katika nyakati zinapotokea dharura za kifedha.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa China, –  Li Keqiang amesema kuwa nchi hizo ni majirani muhimu na kwamba amani, urafiki na ushirikiano ni masuala ya msingi kwa pande zote.

Hiyo  ni ziara ya kwanza kufanywa na Waziri Mkuu wa Japan nchini China katika kipindi cha miaka saba.

Elimu ya soko la mitaji yahitajika kwa Watanzania

0

Mhitimu wa kozi ya utendaji katika soko la mitaji la viwango vya kimataifa Ahmed Masumai kutoka benki ya  CRDB amesema kuwa ataitumia elimu aliyoipata katika kuelimisha Watanzania namna ya kuunganishwa na soko la mitaji.

Masumai  ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam kando ya hafla ya kutoa zawadi kwa washindi wa shindano la  kuandika Insha, maswali  na majibu  kuhusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.

Ameongeza kuwa elimu aliyoipata itaongeza chachu ya uelewa kwa Watanzania wengi kuhusu masuala ya masoko, mitaji na dhamana, masuala ambayo Watanzania wengi hawayafahamu.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt  Philip Mpango ameishauri  Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Nchini (CMSA) kuendelea kutoa elimu na ujuzi kwa wanafunzi wa elimu ya juu kuhusu masoko ya mitaji ili waweze kuwa wawekezaji wa baadae katika biashara ya hisa.

Amesema kuwa elimu ya masoko ya mitaji kwa watanzania bado ipo chini,  hivyo elimu hiyo itasaidia kuongeza ujuzi na weledi wa kiwango cha kimataifa katika utendaji wa sekta ya masoko ya mitaji hapa nchini.

Kwa upande wake afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, – Nicodemus Mkama amesema kuwa wameanza kuwashirikisha wanafunzi wote zaidi ya elfu 15  walioshiriki katika shindano hilo kwa kuwapatia elimu zaidi.

Amefafanua kuwa washiriki ishirini kati ya  washiriki hao zaidi ya elfu 15 wameibuka washindi ambapo mshindi wa kwanza amepata zawadi ya shilingi milioni moja na laki nane, mshindi wa pili shilingi milioni moja na laki nne,mshindi wa tatu ameibuka na shilingi laki nane na  mshindi wa nne amepata shilingi shilingi laki tano.

Kwa mujibu wa Mkama, washindi 12 kati ya ishirini watapatiwa ufadhili wa kimasomo nchini Mauritius, nchi inayofanya vizuri kwenye sekta ya masoko ya mitaji  ili kuongeza uwezo wa kiteknolojia katika sekta hiyo.

Shindano la kuandika Insha, maswali na majibu kuhusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini  lilikua na lengo la kupima uelewa wao katika masuala ya masoko ya mitaji na uwekezaji wa pamoja kwa kutumia njia za kielektroniki na lilifunguliwa Mei 22  na kufungwa Septemba 15 mwaka huu.

 

 

Loftuscheek aweka rekodi kwa Hat Trick

0

Ruben Loftuscheek ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Uingereza kuifungia Chelsea  mabao matatu yaani Hat Trick katika mashindano ya vilabu Barani Ulaya tangu Septemba 29 mwaka 1971 pale Peter Osgood alipofunga mabao matano na Tommy Baldwin akiweka mengine matatu kwenye michuano ya kombe la washindi dhidi ya  Jeunesse Hautcharage ya Luxemborg.

Loftuscheek amefunga mabao hayo katika dakika ya pili, ya nane na 53 na kuifanya Chelsea kushinda michezo yake mitatu ya mwanzo ya hatua ya makundi kwenye michuano ya vilabu Barani Ulaya kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2010/2011 walipofanya hivyo kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya.

Mpaka sasa Chelsea haijapoteza mchezo wowote chini ya kocha Maurisio Sarri ambaye amesema lengo lake ni kufuzu hatua inayofuata mapema huku wakimaliza wakiwa vinara wa kundi lao.

Sarri ameongeza kuwa walicheza vema kwa dakika 65 na hakupenda waliporuhusu bao,  kwa kuwa alitaka wamalize mchezo  huo wakiwa hawajafungwa.

Kuhusu mchezo wao unaofuata wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Burnley, – Sarri amesema kuwa anajua utakuwa mgumu na huenda akafanya mabadiliko ya wachezaji sita mpaka saba kwani Burnley ni timu ngumu na ameshuhudia michezo yao mingi msimu uliopita,  hivyo inawabidi kupamabana kupata matokeo.

Katika matokeo mengine ya michuano ya ligi ya Yuropa, mabao mawili ya nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, – Mbwana Samatta yametosha kuipa ushindi wa ugenini wa mabao manne kwa mawili timu yake ya Genk dhidi ya miamba ya  Uturuki timu ya Besiktasi.

Samatta amefunga mabao hayo katika dakika za 23 na 70 kabla ya Diumerki Ndongala na Jakub Piotroski kuongeza mengine kwenye dakika za 81 na 83 huku mabao ya kufutia machozi kwa Besiktas yakifungwa na Sandro Vagner katika dakika za 74 na 86.

Mjini Milan, miamba ya Italia, – AC Milan wakiwa kwenye dimba la San Siro wamekubali kipigo cha mabao mawili kwa moja kutoka kwa Real Betis, Manyambizi wa Manyano Villareali wamesambaratisha Rapid Vien kwa kipigo kizito cha mabao matano kwa bila wakati Rangers wakishindwa kutamba nyumbani na kulazimishwa suluhu na Spartak Moscow.

Arsenal waendeleza ushindi

0

Arsenal wameendeleza wimbi la ushindi baada ya usiku wa kuamkia leo kuweka rekodi ya kushinda mchezo wa 11 mfululizo katika mashindano yote kwa kuinyuka Sporting Lisborn ya Ureno bao moja kwa bila kwenye mchezo wa michunao ya Yuropa League.

Washika bunduki hao wa jiji la London wameendeleza rekodi hiyo ya ushindi tangu mwezi Oktoba mwaka 2007 waliposhinda michezo 12 mfululizo na ushindi wa jana unakuwa wa kwanza wa ugenini dhidi ya timu za Ureno baada ya kushindwa kushinda katika michezo sita iliyopita wakipoteza mitatu na kutoka sare mitatu.

Bao pekee kwa Arsenal limepachikwa kimiani na Danny Welbeck katika dakika ya 77 na kumfanya kuhusika kwenye mabao matano katika michezo mitano aliyoanza kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal kwa msimu huu katika mashindano yote.

Mchezo wa jana ni wa kwanza kwa Arsenal kucheza bila kuruhusu timu pinzani kupiga shuti hata moja lililolenga lango lao kwenye michuano ya Ulaya ambapo mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa mwaka 2015 dhidi ya Monaco kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa Barani Ulaya.

Katika hatua nyingine kocha wa kikosi hicho Unai Emery ameendelea kuwa mfalme wa michuano ya Yuropa akiweka rekodi ya kupoteza mchezo mmoja kati ya 21 ya hatua ya makundi kwenye michuano hiyo ambapo ameshinda michezo 12 huku akitoka sare katika michezo nane.

NBA yapamba moto

0

Kwenye ligi kuu ya kulipwa ya mpira wa kikapu nchini Marekani – NBA, alfajiri ya leo imechezwa michezo minne.

Cleveland Cavaliers wameendelea kuwa pombe ya ngomani baada ya kutandikwa alama 110 kwa 103 na Detroit Pistons kwenye mchezo uliochezwa katika dimba la Little Sizaz mjini Detroit, -Miami.

Licha ya Kyle Korver kupambana na kufunga alama 21,  bado hazikutosha kuwapa Cavaliers ushindi mbele ya Pistons waliokuwa wakiongozwa vyema na Blake Griffin na Andri Drammond ambao kwa pamoja wamefunga alama 52 na kucheza mipira iliyorudi yaani rebounds 32.

Huko Amway Center mjini Orlando –  Florida,  wenyeji Orlando Magic wamekiona cha moto kwa kutandikwa alama 128 kwa 114 na Portland Trail Blazers katika mchezo ambao Damian Lilard amefunga alama 41 na kucheza rebounds saba.

Katika mchezo mwingine Boston Celtics wakiwa ugenini kwenye dimba la Shezapeake Energy mjini Oklahoma wamewanyuka wenyeji Oklahoma City Thunder alama 101 kwa 95.

Jayson Tatam, Marcus Morris na AL Horford kwa pamoja wamefunga alama 64 zilizotosha kuliamisha jahazi la Thunder waliokuwa wakitegemea zaidi huduma ya Paul George aliyefunga alama 22 na kucheza rebounds nane.

Watano wafa ajalini Lindi

0

Watu watano wamekufa na mmoja kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha lori na gari dogo la abiria katika kata ya Kitomanga wilayani Lindi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Lindi Pudenciana Protas amesema ajali hiyo imetokea mapema leo baada ya dereva wa lori la Kampuni ya saruji ya Dangote kupoteza mwelekeo na kuligonga gari dogo la abiria.

Miili ya watu wanne imekwishatambuliwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi amewataka madereva hasa wanaosafiri usiku kupata muda wa kutosha wa kupumzika ili kuepusha ajali zinazotokana na uchovu na usingizi.