Maeneo yenye miradi ya serikali kulipwa fidia

0

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali italipa fidia kwa wananchi katika maeneo ambayo miradi ya serikali imepita.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo wakati akiwahutubia wakazi wa Manerumango wilayani Kisarawe mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku sita mkoani humo.

“Nataka niwahakikishie wananchi wote kila kipande cha ardhi cha mtu kinachochukuliwa kwa ajili ya maendeleo ya serikali basi kipande kile kitalipiwa fidia, tutalipa fidia kwa viwango ambavyo sheria zetu zinaruhusu nataka niwaambie hakuna mtu atanyimwa haki yake, haki zote na fidia zote zitalipwa”, amesema Makamu wa Rais.

Akiwa wilayani Kisarawe, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pia amepokea msaada wa vifaa mbalimbali vya kituo cha afya cha Manerumango kutoka benki ya NMB, vifaa vyenye thamani ya shilingi Milioni 15.

Serikali kuendelea kushirikiana na sekta binafsi

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali inathamini uwepo wa sekta binafsi nchini na kwamba inaendelea kushirikiana nayo.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam alipokutana na bodi mpya ya Taasisi ya Sekta Binafsi nchini, ambayo ilikwenda kujitambulisha.

Amempongeza Mwenyekiti wa taasisi hiyo Salum Shamte na wajumbe wa bodi hiyo mpya kwa kuchaguliwa kuingoza taasisi hiyo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

“Serikai inadhamira ya dhati ya kushirikiana na taasisi hii kwa sababu ndio muwezeshaji wa kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025,” amesema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya Sekta Binafsi Nchini Salum Shamte amesema kuwa sekta hiyo inatambua juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya biashara nchini.

“Sisi tupo tayari kushirikiana na serikali kwa kuwabana wafanyabiashara ambao wanaenda kinyume na maadili na sheria, ila tunaomba serikali ishirikiane nasi katika utekelezaji wake,”ameongeza Shamte.

Pia ameiomba serikali iendelee kutoa vivutio kwa biashara zinazoanza ili kuhamasisha uwekezaji kwa kuwa baadhi yake zimeonesha gharama kubwa za uzalishaji.

CCM yashinda Uwakilishi Jang’ombe

0

Mgombea wa nafasi ya Uwakilishi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Jang’ombe Kisiwani Unguja, -Ramadhan Hamza Chande ameibuka mshindi wa nafasi hiyo kufuatia uchaguzi mdogo uliofanyika Jumamosi Oktoba 27 kisiwani Unguja.

Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Jang’ombe, -Mwanapili Khamis Mohamed amesema kuwa Chande ameshinda baada ya kupata kura 6,581 ambazo ni sawa na asilimia 90.5 ya kura zote halali zilizopigwa ambazo ni 7,274.

Baadhi ya wawakilishi kutoka vyama mbalimbali vilivyoshiriki kwenye uchaguzi huo wamesema kuwa ulikuwa huru na wa haki.

Uchaguzi huo mdogo katika jimbo la Jang’ombe Kisiwani Unguja umefanyika baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo hilo kupoteza sifa za uanachama.

Rais Magufuli afanya uteuzi

0

Rais Dkt. John Magufuli amefanya uteuzi wa wenyeviti nane wa bodi za taasisi za Serikali na Mtendaji Mkuu mmoja baada ya waliokuwepo katika nyadhifa hizo kumaliza muda wao.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu imesema walioteuliwa ni Profesa Joyce Kinabo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Profesa Costa Mahalu kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Ardhi –ARU, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Sauda Mjasiri kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Rufani za Zabuni za Umma – PPAA, Profesa Elifas Bisanda kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo –SIDO.

 

Wengine walioteuliwa ni Dkt. Selemani Majige kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Puma Energy Tanzania, Julius Ndyamukama kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini –GPSA, Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori –TAWA, Profesa Romanus Ishengoma kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Misitu Tanzania –TAFF.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Leonard Kapongo kuwa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma – PPRA. Kapongo anachukua nafasi ya Dkt. Laurent Shirima ambaye amemaliza muda wake.

Uteuzi wa wenyeviti hawa umeanza leo.

Watu kadhaa wahofiwa kufa katika ajali mkoani Pwani

0

Watu kadhaa wanahofiwa kufa na wengine kujeruhiwa baada ya gari la abiria aina ya Costa kugongana uso kwa uso katika eneo la Vigwaza mkoani Pwani.

Kamanda wa polisi mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa amesema ajali hiyo imetokea hivi punde na kwamba yuko njiani kuelekea eneo la tukio.

Wizara ya Kilimo yatakiwa kujitathmini

0

Rais John Magufuli ameitaka Wizara ya Kilimo ijitathmini kutokana na suala la mauzo ya zao la korosho linavyoendelea pamoja na utendaji wa Bodi ya Korosho Nchini.

Waziri Mkuu Majaliwa pia ameiagiza Wizara ya Kilimo kumrudisha wizarani Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Nchini (CBT) Profesa Wakuru Magigi baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo katika kikao chake na wakuu wa mkoa inayolima zao la korosho kilichofanyika mkoani Lindi.

“Haturidhishwi na utendaji wa bodi ambao umekiuka maelekezo ya msingi ya Serikali katika kusimamia mfumo mzima wa zao la korosho uliopelekea kuvurugika kwa minada,” ameongeza Waziri Mkuu.

Kufuatia hali hiyo, amesema kuwa serikali imesitisha minada yote ya korosho nchini kuanzia Oktoba 26 na kuwataka wakulima wawe watulivu wakati suala hilo likishughulikiwa.

Kaimu Mkurugenzi huyo wa Bodi ya Korosho nchini analalamikiwa kwa kufanya kazi bila ya kushirikisha ushirika wa zao la korosho na kutotambua mamlaka zilizowekwa kisheria ikiwa ni pamoja mkuu wa mkoa.

Mbali na malalamiko hayo, Kaimu Mkurugenzi huyo wa Bodi ya Korosho Nchini pia anadaiwa kuendesha operesheni kwa kutumia silaha na askari dhidi ya viongozi wa ushirika kinyume cha taratibu za nchi.

Kutokana na malalamiko hayo, Waziri Mkuu Majaliwa amewaagiza Makamanda wa Polisi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kuhakikisha gari lenye namba T 814 DDM pamoja na dereva wake linatafutwa popote lilipo.

Waziri Mkuu amefafanua kuwa gari hilo ndilo linalodaiwa kutumika katika kuwakamata viongozi wa ushirika waliokuwa wanawasimamia wananchi waliokataa kuuza korosho kwa bei ndogo.

Amesisitiza kuwa baada ya dereva wa gari hilo kukamatwa ahojiwe na aeleze askari hao alikuwa anawatoa wapi na nani aliyemtuma na kwamba askari wote waliohusika watafutwe.

“Bodi imekuwa ikiwatisha na kuwalazimisha wakulima na viongozi wa ushirika kukubali kuuza korosho kwa bei ya chini jambo ambalo Serikali haiwezi kulikubali,” amesema Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, serikali haiwezi kulifumbia macho suala hilo kwa sababu limekuwa likiipaka matope kwa kuwa Kaimu Mkurugenzi huyo wa Bodi ya Korosho Nchini alikua akiingiza askari katika mikoa hiyo bila ya mamlaka kuwa na taarifa.

Kadhalika Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Kilimo kutokaa kimya pindi zinapotokea changamoto kama hizo na badala yake watoe taarifa mapema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Rais John Magufuli amewapongeza wakulima wa korosho kwa uamuzi wao wa kukataa kuuza korosho kwa bei ndogo na kwamba yuko pamoja nao.

“Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Kilimo ijitathmini katika suala la mauzo ya zao la korosho linavyoendelea,” amesema Waziri Mkuu.

Pia Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Magufuli ana taarifa kwamba kuna baadhi ya watendaji serikalini wanatumia vibaya jina lake na kwamba ni lazima wahusika wote watachukuliwa hatua.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, – Gelasius Byakanwa na Mkuu wa mkoa wa Lindi, – Godfrey Zambi walilalamikia kitendo cha Profesa Magigi kuvuruga mfumo wa uuzaji wa korosho.

Pia walisema licha ya kumshauri kiongozi huyo juu ya namna bora ya kuendesha minada ya uuzaji wa korosho hakuwasikiliza na kwamba hakuwa tayari kushirikiana nao na pia alikuwa akidharau mamlaka zao.

Pia alikuwa akiingiza askari na kuwatisha na kukamata viongozi wa ushirika bila ya wao kujua jambo ambalo walisema limezua taharuki kwa watendaji wa ushirika.

Waziri Mkuu akutana na wakuu wa mikoa iliyoanza kuuza korosho

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana  na kufanya mazungumzo na wakuu wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani  na  Ruvuma, pamoja na watendaji wa Bodi ya Korosho Nchini  kwa lengo la kujadili bei ya korosho.

Mkutano huo ulioshirikisha wakuu hao wa mikoa ambao mikoa yao imeanza kuuza korosho, pia umehudhuriwa na Wenyeviti wa vyama vikuu vya Ushirika katika mikoa hiyo na Naibu Waziri wa Kilimo Omari Mgumba.

 

Mtendaji Mkuu wa Pride Tanzania atakiwa kujisalimisha

0

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  Nchini (TAKUKURU) imemtaka aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa taasisi iliyokuwa ikijishughulisha na utoaji mikopo ya Pride Tanzania, – Rashid Malima kujisalimisha kufuatia tuhuma za ubadhilifu wa shilingi bilioni moja nukta nane ambazo ni fedha za taasisi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo amesema kuwa Malima amekimbilia nchini Marekani na kuwaomba watanzania wanaoishi nchini humo na wenye taarifa kamili kuhusiana na mtu huyo waziwasilishe katika taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mbungo, TAKUKURU pia inamtafuta Josephat Machiwa aliyekuwa afisa mikopo wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Kitivo cha Elimu (DUCE) kwa madai ya kukimbia na fedha za ada za wanafunzi wa chuo hicho.

Katika hatua nyingine Brigedia Jenerali Mbungo amesema kuwa TAKUKURU imewakamata wafanyabiashara kadhaa katika eneo la  Kariakoo jijini Dar es salaam ambao wamekuwa wakiibia serikali kwa kutoa risiti za kielektroniki ambazo hazilingani na thamani ya fedha za manunuzi.

Amewakumbusha Watanzania wote kuwa kitendo chochote cha kutumia nyaraka zenye lengo la kuidanganya serikali kinahesabiwa kama rushwa chini ya kifungu cha 22 cha sheria ya TAKUKURU na hivyo kuwataka kutokubali kupokea risiti ambayo haiendani na thamani ya fedha za manunuzi ya bidhaa.