Italia na Afrika kushirikiana katika sekta mbalimbali

0

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Italia na Afrika wamekubaliana kukuza na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali hasa zile za biashara na uwekezaji, lengo likiwa ni kuleta maendeleo barani Afrika.

Mawaziri hao wamefikia makubaliano hayo wakati wa mkutano wa pili wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa Italia na Afrika uliofanyika katika mji wa Farnesina, -Italia na kuhudhuriwa na mawaziri kutoka zaidi ya nchi arobaini akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Dkt Augustine Mahiga.

Mawaziri hao walikutana kwa lengo la kujadili kwa pamoja changamoto zinazohusu usalama, uhuru, amani, demokrasia na namna wadau wa Italia watakavyoweza kushiriki katika kukuza uchumi barani Afrika hasa katika sekta ya uwekezaji na biashara.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliofunguliwa na Rais wa Italia, -Sergio Mattarella, Waziri Mahiga amesisitiza suala la amani na kuongeza kuwa ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi Barani Afrika.

Pamoja na kuhudhuria mkutano huo, Waziri Mahiga pia alipata fursa ya kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, – Enzo Moavero na Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), – Gilbert Houngbo.

Katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia wamekubaliana kuandaliwe hati ya makubaliano kati ya Tanzania na Italia ya kufanya majadiliano ya mara kwa mara yenye lengo la kukuza ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, elimu na utamaduni.

Balozi Mahiga amesema kuwa katika mazungumzo yake na Rais huyo wa IFAD wamekubaliana kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Mfuko huo kwenye maeneo makuu manne ambayo ni huduma za kifedha kwa wakulima wadogo, kuwajengea uwezo vijana ili waweze kufanya kilimo kama sehemu ya ajira, kuboresha sekta ya mifugo pamoja na masuala ya lishe bora.

Houngbo amemuahidi Waziri Mahiga kuwa IFAD itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye miradi inayoendelea ikiwemo ile ya programu ya miundombinu ya masoko, uongezaji wa thamani na kuwawezesha wakulima wadogo wa vijijini kifedha.

Zia ahukumiwa kifungo cha miaka saba jela

0

Waziri Mkuu wa zamani wa Bangladesh na kiongozi wa upinzani nchini humo Khaleda Zia amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na vitendo vya rushwa.

Tayari Zia anatumikia kifungo baada ya mahakama kumpata na hatia ya kutumia vibaya mali ya umma.

Zia amesema kuwa kesi dhidi yake zimehamasishwa kisiasa kwa lengo la kumzuia asishiriki katika uchaguzi mkuu wa Bangladesh unaotarajiwa kufanyika mwezi Disemba mwaka huu.

Waendesha mashitaka wa Saudi Arabia wawasili Uturuki

0

Waendesha mashitaka wa umma wa Saudi Arabia wamewasili mjini Istanbul nchini Uturuki kwa ajili ya majadiliano na serikali ya nchi hiyo kuhusiana na kifo cha mwandishi wa habari Jamal Kashoggi.

Waendesha mashitaka hao wanatarajiwa kuwasilisha ushahidi wa watu kumi na wanane wanaotuhumiwa kuhusika na kifo cha Kashoggi.

Serikali ya Uturuki inataka watuhumiwa wote kumi na wanane wanaotuhumiwa kupanga na kisha kutekeleza mauaji ya Kashoggi warejeshwe nchini Uturuki ili washitakiwe.

Serikali ya Saudi Arabia imekataa mpango huo wa Uturuki na kusisitiza kuwa watuhumiwa hao watashitakiwa na kuchukuliwa hatua za kisheria wakiwa nchini mwao.

Ndege yaanguka ikiwa na watu 188 Indonesia

0

Ndege ya abiria inayomilikiwa na Shirika la Lion Air la nchini Indonesia imeanguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege mjini Jakarta ikiwa na watu 188.

Ndege hiyo aina ya Boeing 737 – MAX 8 ilikuwa ikisafiri kutoka katika mji huo mkuu kwenda jiji la Pangkal Pinang lililopo kwenye visiwa vya Bangka Belitung.

Habari kutoka nchini Indonesia zinasema kuwa ndege hiyo ilitoweka kwenye mitambo ya rada dakika 13 baada ya kupaa ilipokuwa inavuka bahari.

Maafisa wa anga nchini Indonesia wamesema kuwa wakati ajali hiyo inatokea, ndege hiyo ambayo ni mpya ilikuwa imebeba abiria 181, marubani wawili na wahudumu watano.

Katika taarifa yake, shirika hilo la ndege la Lion Air ndege limesema kuwa chanzo cha kuanguka kwa ndege hiyo bado hakijajulikana na kwamba vyombo vya baharini viko katika eneo ilipotokea ajali hiyo.

Hadi sasa hakuna taarifa za mtu yeyote aliyenusurika katika ajali hiyo na jitihada za uokoaji zinaendelea.

Gamba kuzikwa Jumatano Bunda

0

Mwili wa Mtangazaji wa Tanzania aliyekuwa akifanya kazi katika Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW) , – Isaac Gamba unaagwa hii leo jijini Dar es salaam.

Mwili wa Gamba unaagwa baada ya kuwasili nchini usiku wa kuamkia hii leo ukitokea nchini Ujerumani.

Mara baada ya ibada pamoja na kukamilika kwa shughuli ya kuaga  katika eneo la Lugalo, mwili wa Gamba utasafirishwa kwenda mkoani Mara kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Jumatano Oktoba 31.

Gamba aliyekuwa mtangazaji wa michezo na burudani katika Idhaa hiyo ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani  alikutwa akiwa amefariki dunia mjini Bonn nchini Ujerumani Oktoba 18 mwaka huu baada ya kutoonekana ofisini kwa muda wa siku mbili.

Hali ya kutoonekana ofisini iliwashtua wafanyakazi wenzake ambao waliamua kutoa taarifa polisi ambao walifika nyumbani kwake na kuvunja mlango na ndipo walimkuta amekwishafariki dunia.

Gamba aliyezaliwa mwaka 1970 wilayani Bunda, ni mtoto wa 12 kati ya watoto 13 na alijiunga na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani mwaka 2015 akitokea kwenye kituo cha ITV na Radio One nchini Tanzania.

Rais Magufuli atoa msimamo kuhusu bei ya korosho

0

Rais John Magufuli amekutana na wanunuzi wa zao la korosho na kutoa msimamo wa serikali kuhusu bei ya zao la korosho kufuatia kuwepo kwa mvutano wa bei ya zao hilo kati ya wanunuzi na wakulima.

Rais Magufuli amekutana na wanunuzi hao katika mkutano wa majadiliano uliokuwa ukiendelea kati ya wanunuzi hao wa korosho na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

Katika msimamo huo Rais Magufuli amesema kuwa serikali inaungana na msimamo wa wakulima kukataa bei zilizotolewa na wanunuzi katika mnada uliofanyika hivi karibuni ambapo kampuni za ununuzi wa korosho zilitangaza kununua korosho kwa bei ya kati ya shilingi 2,717 na shilingi 1,900 kwa kilo ikiwa imeshuka kutoka zaidi ya shilingi 3,600 ya msimu uliopita.

Rais Magufuli amesema kuwa endapo wanunuzi hao hawatakuwa tayari kununua korosho kwa bei isiyopungua shilingi 3,000 kwa kilo, serikali ipo tayari kununua korosho kwa bei yenye maslahi kwa wakulima na kutafuta masoko yenye bei nzuri.

“Kama hamtanunua korosho kwa bei yenye maslahi kwa wakulima, serikali itanunua korosho kwa bei nzuri kwa wakulima na tutaihifadhi, nipo tayari hata kutumia majeshi yetu kununua korosho na tutatafuta masoko ya uhakika ili tuuze kwa bei nzuri” amesisitiza Rais Magufuli.

Wakizungumza katika mkutano huo, wanunuzi hao wa korosho wamekubali kununua korosho kwa bei isiyopungua shilingi 3,000 kama ilivyoelekezwa na serikali na wameomba baadhi ya tozo zinazosababisha kupungua kwa bei ya zoa hilo kwa mkulima ziondolewe pamoja na kuruhusiwa kusafirisha korosho kupitia bandari ya Dar es salaam ambako wanaweza kupata meli zinazotoza gharama nafuu za usafirishaji wa korosho kwenda kwenye masoko ya nje ya nchi.

Rais Magufuli amekubali kuondolewa kwa utozaji ushuru wa mara ya pili wa ushuru wa halmashauri uliokuwa ukifanywa baada ya korosho kufikishwa Mtwara, kupunguza ushuru wa Bodi ya Korosho Nchini kutoka shilingi 17 kwa kilo hadi shilingi 10 kwa kilo na ameruhusu wafanyabiashara kununua magunia yao wenyewe kwa ajili ya korosho badala ya kuuziwa na vyama vya ushirika kwa bei kubwa.

Kuhusu bandari ya kusafirishia korosho, Rais Magufuli amekubali ombi la wanunuzi hao wa korosho la kutaka kusafirisha korosho kwa kutumia bandari ya Dar es salaam ambapo kilo moja inasafirishwa kwa shilingi 47 kwa kilo kwa kutumia meli ambazo zimebeba mizigo mingine ikilinganishwa na bandari ya Mtwara ambako kilo moja inasafirishwa kwa shilingi 203 kilo kwa kutumia meli zinazokodiwa kwa ajili ya kubeba korosho tu.

“Bandari ya Mtwara na bandari ya Dar es salaam zote ni bandari za serikali, mimi sina tatizo na kusafirisha korosho kupitia bandari ya Dar es salaam, lakini na nyinyi muwe tayari kutozidisha uzito kwenye magari mnaposafirisha kutoka Mtwara hadi Dar es salaam, kutotorosha korosho na pia kutimiza masharti ya usafirishaji”, amesisitiza Rais Magufuli.

Ameiagiza Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha usafirishaji wa korosho hizo kupitia bandari ya Dar es salaam kama ambavyo wanunuzi hao wameomba.

Aidha, Rais Magufuli amewataka wanunuzi hao kuwekeza viwanda vya kubangua korosho ama kuwahamasisha washirika wao kuwekeza katika viwanda hivyo na kwamba serikali itaunga mkono juhudi hizo ikiwa ni pamoja na kuweka vivutio vya kodi.

Makamu wa Rais akataa kufungua kituo cha mabasi cha Mailimoja

0

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amekataa kufungua kituo kipya na cha kisasa cha mabasi cha Mailimoja kilichopo Kibaha mkoani Pwani na kuagiza kituo hicho kisifunguliwe hadi hapo serikali itakapojiridhisha kuhusu mchakato uliotumika kujenga kituo hicho.

Akiwa katika ziara yake ya siku sita mkoani Pwani, Makamu wa Rais amesema kuwa amefikia uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko ya Wakazi wa Kibaha ambao wamelalamikia mchakato wa ujenzi wa kituo hicho.

Amesema kuwa serikali itatuma Kamati kwenda kuchunguza ubora wa kituo hicho, kiasi cha fedha kilichotumika na kama itajiridhisha mambo yote yapo sawa ndipo kituo hicho kipya na cha kisasa cha mabasi cha Mailimoja kitafunguliwa.

Kituo hicho kimejengwa na halmashauri ya mji wa Kibaha kwa thamani ya shilingi bilioni 3.4.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais kufungua kituo hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya mji wa Kibaha, – JENIFA OMOLO alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho cha mabasi cha kisasa cha Mailimoja umekamilika na kuanza kutumika, jambo lililosaidia kuongeza mapato.

Waliomuua Kashoggi kushitakiwa Saudi Arabia

0

Saudi Arabia imesema kuwa watuhumiwa wote wa mauaji ya mwandishi wa habari, -Jamal Khashoggi, mashtaka yao yatasikilizwa nchini humo.

Akizungumza wakati wa kikao cha kujadili suala hilo mjini Bahrain, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, -Adel Al-Jubeir pia amevishutumu vyombo vya habari vya magharibi kwa kuongeza vitu ambavyo havina ukweli wakati wa kuandika habari kuhusu mauaji ya Kashoggi.

Kauli ya Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia imekuja siku moja tu baada ya serikali ya Uturuki kutaka kuwahamisha watu 18 wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya Mwandishi huyo wa habari.