Marekani kulinda mpaka wake na Mexico

0

Marekani  imetangaza mpango wake wa  kuwatuma zaidi ya askari elfu tano kwenda  kusaidia kulinda maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Mexico, baada ya maelfu ya wahamiaji kutoka mataifa ya Amerika ya Kati kujiunga na msafara wa wahamiaji wanaotaka kuingia nchini Marekani.

Mpango huo umetangazwa na Rais Donald Trump, huku baadhi ya wachambuzi wa masuasa ya kiuchumi wakisema kuwa idadi hiyo ya askari wanaotumwa kulinda  maeneo hayo ni kubwa kuliko ilivyotarajiwa.

Habari zaidi kutoka nchini Marekani zinasema kuwa tayari askari mia nane wameishaelekea katika jimbo la Texas ambalo nalo ni eneo la mpaka wa nchi hiyo na mexico na wengine  katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na majimbo ya California na Arizona.

Wakati marekani ikitangaza mpango huo, mamia ya wahamiaji kutoka Honduras wamevuka mto kuingia  nchini Mexico, likiwa ni kundi jipya la wahamiaji wanaoelekea nchini Marekani.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa,  zaidi ya wahamiaji  elfu saba wako njiani kuelekea nchini Marekani hivi sasa.

Maafisa wa uhamiaji  nchini Marekani wamesema kuwa katika kipindi cha wiki tatu zilizopita,takribani wahamiaji elfu moja na mia tisa wamekua wakivuka mpaka kinyume cha sheria kila  siku  na kuingia nchini humo.

 

Kamati Kuu ya CCM yakutana

0

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Rais John Magufuli ameongoza kikao cha Kamati Kuu ya CCM.

Kikao hicho kimefanyika katika ofisi ndogo za CCM zilizopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es salaam.

Waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Makamu wa Rais,- Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, – Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, Makamu Mwenyekiti wa CCM – Bara, – Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM Dkt Bashiru Ally.

Mahrez amlilia Vishai

0

Winga wa Manchester City, – Riyad Mahrez amesema kuwa mmiliki wa klabu ya Leicester City  marehemu Vishai  Rivahanapraha  alikuwa kama baba kwake na ilimuwia vigumu kupata usingizi kabla ya mchezo wa hivi karibuni dhidi ya Tottenham.

Mahrez amesema kuwa goli pekee na la ushindi aliloifungia  City dhidi ya Spurs ni kwa ajili ya marehemu Vishai na kwamba Bilionea huyo alikuwa mtu wa kipekee kwake na katika kipindi cha miaka minne na nusu alichokuwa Leicester wamefanya mambo mengi ambayo yanabaki kuwa kumbukumbu isiyofutika katika kichwa chake.

Nyota huyo wa kimataifa wa Algeria aliitumikia Leicester katika michezo 179 kati ya mwaka 2014 hadi 2018 na kuwasaidia kutwaa taji la ligi kuu ya England mwaka 2016 ambapo pia alitangazwa kuwa mchezaji bora.

Kwa mujibu wa Mahrez, habari za kifo cha Vishai na wenzake zimemuumiza sana na anaungana na klabu hiyo pamoja na wote walioguswa katika kipindi hiki cha majonzi.

Mahrez aliifungia City bao pekee na la ushindi katika dakika ya sita  katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Wembley,  ushindi unaowafanya City kukwea kileleni kwenye msimamo wa ligi ya England wakiwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga ambapo wamefikisha alama 26 sawa na Liverpool.

Katika hatua nyingine,  salamu za rambirambi zimeendelea kutolewa na watu mbalimbali mashuhuri kufuatia kifo cha  mmiliki huyo wa klabu ya Leicester City  kilichotokana na ajali ya helikopta Jumamosi iliyopita nje ya uwanja wa timu hiyo wa King Power.

Helikopta hiyo ambayo ni binafsi ilianguka muda mfupi baada ya kuruka kutoka kwenye uwanja huo ambapo mmiliki huyo wa timu ya Leicester City FC alikuwa akirejea nyumbani mara baada ya kutazama mchezo baina ya timu yake na West Ham United.

Manyoni kupata gari la wagonjwa

0

Serikali imeahidi kupeleka gari ya kubeba wagonjwa  katika hospitali ya wilaya ya Manyoni mkoani Singida ili kutatua tatizo linaloikabili wilaya hiyo hasa vifo vinavyotokana na uzazi.

Ahadi hiyo  ya serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile alipotembelea hospitali hiyo kwa lengo la kujionea hali ya utoaji huduma, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu mkoani humo.

Dkt Ndugulile amefikia uamuzi wa kutoa ahadi hiyo baada ya kusikiliza kero za wananchi wanaotumia hospitali hiyo ambao wamesema kuwa gari la wagonjwa lingeweza kuepusha vifo vya akina mama wajawazito na watoto pamoja na wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.

“Naomba niwaahidi wananchi wa Manyoni, serikali imeagiza magari ya kubebea wagonjwa ambayo yanaweza kufika mwezi Disemba mwaka huu, hivyo nitahakikisha katika mgao wa magari hayo basi na hospitali hii ya wilaya  inapata gari moja kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wa hapa”, amesema Dkt Ndugulile.

Naye Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo ya wilaya ya Manyoni Dkt Atupele Mohamed amesema kuwa hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa majengo kikiwemo chumba cha huduma za uzazi ambapo uwezo wake kwa mwezi ni  kuzalisha akina mama 90 lakini kwa sasa wanazalisha  wastani wa akina mama 400.

 

Lopetegui atimuliwa Madrid

0

Klabu ya Real Madrid imemtimua kocha wake Julen Lopetegui ikiwa imepita miezi minne na nusu tangu alipopewa kibarua cha kukinoa kikosi hicho.

Mhispania huyo alirithi mikoba iliyoachwa na Zinedine Zidane mwezi June mwaka huu, lakini kipigo kizito cha mabao matano kwa moja kutoka kwa mahasimu zao FC Barcelona kwenye mchezo wa El Clasico kimeondoa uvumilivu wa mabosi wa miamba hiyo na kuamua kumtimua.

Uamuzi wa kumfungashia virago Lopetegui umekuja saa chache baada ya kikao cha bodi ya wakurugenzi wa timu hiyo chini ya Rais wa Real Madrid, –  Florentino Perez ambaye baada ya mchezo wa El Clasico alitoka uwanjani akiwa amekasirika.

Hii ni mara ya pili kwa kocha Lopetegui kufukuzwa kazi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya kuondoshwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania  kwenye kombe la Dunia huko Russia  siku mbili baada ya kugundulika kuwa yupo katika mazungumzo ya mwisho ya kupata kibarua cha kuinoa Real Madrid baada ya mashindano ya kombe la dunia kumalizika.

Nyota wa zamani wa Real Madrid ambaye anakinoa kikosi cha pili cha timu hiyo Santiago Solari ameteuliwa kuwa kocha wa muda wa Madrid baada ya mazungumzo na aliyekuwa kocha wa Chelsea, -Antonio Conte kuchelewa na kibarua chake cha kwanza kitakuwa Jumatano wiki hii atakapoiongoza Madrid kwenye mchezo wa kombe la mfalme dhidi ya Melilla.

NHC yapata viongozi wapya

0

Rais  John Magufuli amemteua Dkt Sophia Kongela kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Dkt  Kongela ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU).

Kufuatia uteuzi wa mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC uliofanywa na Rais Magufuli, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, – William Lukuvi amemteua Dkt Maulid Banyani kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa.

Kabla ya uteuzi huo Dkt Banyani alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU).

Uteuzi wa viongozi hao umeanza leo Oktoba 30.

 

 

 

Uteuzi FCC

0

Rais John Magufuli amemteua Profesa Humphrey Moshi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ushindani nchini (FCC).

Profesa Moshi ni Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Uteuzi wa Profesa Moshi unaanza leo Oktoba 30.

Maonesho wiki ya viwanda yafunguliwa Pwani

0

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameushauri uongozi wa mkoa wa Pwani kuwaomba wawekezaji mkoani humo kukifanyia marekebisho Chuo cha Ufundi cha mkoa huo ili kitumike kuwafundisha vijana mambo mbalimbali yatakayowawezesha kuajiriwa katika viwanda vilivyopo katika mkoa huo.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wilayani Kibaha wakati akifungua maonesho wiki ya viwanda kwa mkoa wa Pwani na kutahadharisha kuwa endapo vijana hao hawatapata elimu, fursa za ajira mkoani humo zitachukuliwa na vijana kutoka mikoa ya jirani.

Pia amezitaka taasisi zinazohusika na maslahi ya wafanyakazi kutembelea maeneo ya viwandani ili kuona namna maslahi ya wafanyakazi hao yanavyoshughulikiwa.

Maonesho hayo ya viwanda mkoani Pwani yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba, yana lengo la kutoa fursa za masoko na kutangaza bidhaa za wajasiriamali wa mkoa huo.

Akiwa katika viwanja hivyo, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mambo mengine ametembelea mabanda ya kampuni mbalimbali ili kujionea bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais kufungua maonesho hayo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, – Charles Mwijage amesema kuwa serikali inajenga uchumi wa kitaifa na lengo ni kufikia pato la dola elfu tatu za kimarekani kwa mwananchi ifikapo mwaka 2025.

Maonesho ya wiki ya viwanda mkoani Pwani yana kauli mbiu inayosema kuwa Viwanda vyetu, Uchumi wetu, Kwani tumeweza, Tunatekeleza na Tunakuza uchumi wa viwanda.