Wema afikishwa mahakamani

0

Msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam kusomewa makosa yanayomkabili ya kusambaza picha zisizo na maadili kwenye mitandao ya kijamii.

Habari zinasema kuwa Wema amefikishwa mahakamani na Mamlaka ya  Mawasiliano Nchini (TCRA).

Hivi karibuni Wema aliwaomba radhi mashabiki wake pamoja na Watanzania wote kufuatia kusambaa kwa picha zake hizo  ambazo hazina maadili zilizosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Lampard apoteza mchezo wake wa kwanza

0

Frank Lampard amepoteza mchezo wake wa kwanza aliporejea kwenye dimba la Stamford Bridge mbele ya timu yake ya zamani ya Chelsea akiwa kocha wa timu ya Derby Country kwenye michuano ya kombe la Ligi.

Magoli mawili ya kujifunga  ya wachezaji wa Derby Country na goli moja lililotiwa kimiani na Cesc Fabregas yalitosha kabisa kuipa ushindi Chelsea wa bao tatu kwa mbili na kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Magoli yote matano kwenye mchezo huo yalifungwa kwenye kipindi cha kwanza cha mchezo huo ambao ulikuwa na kila aina ya mvuto hasa kwa mashabiki wa Chelsea ambao walimshangilia mno Frank Lampard ambaye aliichezea timu yao kwa miaka 13 kwa mafanikio makubwa.

Katika michezo mingine, Arsenal imesonga mbele baada ya kuilaza Blackpool bao mbili kwa moja,Tottenham Hotspurs imeiondosha West Ham United baada ya kuifunga bao tatu kwa moja na Middlesbrough ikaifunga Crystal Palace bao moja kwa bila.

Kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo  ya kombe la Ligi, Arsenal itapambana na Tottenham, Chelsea itacheza na FC Bournemouth, Middlesbrough  itakipiga na  Burton Albion na Leicester au Southampton  itapepetana na  Manchester City au  Fulham.

 

Kombe la dunia mwaka 2022 kuwa na timu 48

0

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limesema kuwa ongezeko la timu kwenye michuano ya kombe la dunia inaweza kuanza kwenye michuano ya mwaka 2022 badala ya mwaka 2026 kama ilivyotarajiwa hapo awali.

Tayari maamuzi yameshapitishwa kuhusu kuongeza timu kutoka 32 hadi 48 na ilipangwa kuanza kwenye michuano ya mwaka 2026 itakayofanyika katika nchi za Marekani,Mexico na  Canada lakini sasa inavyoelekea ongezeko hilo litaanza kwenye michuano ijayo itakayofanyika nchini Qatar.

Rais wa FIFA, -Gianni Infantino amesema kuwa hilo linawezekana na sasa wako kwenye majadiliano na Qatar pamoja na washirika wao wengine ili kuona hilo linafanikiwa.

Infantino amesema kuwa FIFA itafanya kila linalowezekana ili kuona suala hilo linafanikiwa ili timu 48 zishiriki michuano hiyo ya kombe la Dunia ya mwaka 2022.

Pia Rais huyo wa FIFA amezungumzia mpango wake wa kuboresha michuano ya kombe la Dunia ya vilabu ambapo amesema kuwa anataka kuifanya michuano hiyo kuwa bora zaidi na inayopendwa na vilabu vyote duniani.

 

 

Askari waomba rushwa Lushoto kikaangoni

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemkabidhi mkuu wa mkoa wa Tanga, – Martine Shigela orodha ya askari wa usalama barabarani wanaodaiwa kuwaomba rushwa madereva wa noah wilayani Lushoto.

Majina ya askari hao wanaodaiwa kuomba rushwa kwa madereva wa noah wanaofanya kazi ya kusafirisha abiria ndani ya wilaya ya Lushoto yamewasilishwa kwa Waziri Mkuu Majaliwa kupitia mabango, wakati Waziri Mkuu akiendelea na ziara yake mkoani Tanga.

Baada ya kumkabidhi majina hayo mkuu wa mkoa wa Tanga, Waziri Mkuu amemtaka afanye uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazowakabili askari hao na kisha awasilishe taarifa kwake leo Novemba Mosi.

Mbali ya wananchi kuwasilisha malalamiko hayo, Pia mbunge wa Lushoto, -Shaaban Shekilindi amemuomba Waziri Mkuu awasaidie kutatua kero hiyo ya askari wa usalama barabara kuwa na tabia ya kuomba rushwa.

Awali, Waziri Mkuu Majaliwa alizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Lushoto na kuwasisitiza kufanya kazi kwa bidii.

Amesema kuwa serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli haina msamaha na mtumishi wa umma asiyetaka kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia weledi.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, watumishi wa umma wanatakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili ya utumishi ili waweze kutimiza lengo la serikali la kuwahudumia wananchi kwa kutumia taaluma zao.

Zitto ashikiliwa na polisi

0

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar Es Salaam linamshikilia mbunge wa Kigoma Mjini Kabwe Zitto.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania – TBC, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar Es Salaam, Liberatus Sabas amesema jeshi hilo linamshikilia mbunge huyo kwa mahojiano kufuatia kauli anazodaiwa kutoa hivi karibuni.

Jumanne Oktoba 30 mwaka huu, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma Martin Ottieno alimtaka mbunge huyo kuwasilisha ushahidi wa taarifa alizozitoa kuwa jeshi hilo limewaua watu mia moja wa jamii ya wafugaji katika operesheni ya kuwaondoa wavamizi wa maeneo ya ranchi ya NARCO wilayani Uvinza mkoani Kigoma.

Shehena ya mafuta ya kula yakamatwa Pwani

0

Jeshi la polisi mkoani Pwani limekamata lori moja lililokuwa linasafirisha shehena ya mafuta ya kula yaliyoingizwa nchini kinyume cha sheria kupitia bandari zisizo rasmi zilizopo katika wilaya ya Bagamoyo.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Pwani, – Wankyo Nyigesa amesema kuwa lori hilo aina ya Fuso lenye namba za usajili T 336 CVF limekamatwa katika kijiji cha Miono likiwa na watu wawili waliokuwa wakisafirisha mafuta hayo.

Kamanda Nyigesa amesema kuwa lori hilo limekamatwa baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema na baada ya polisi kulifuatilia waliweza kulikamata likiwa limebeba madumu 328 ya mafuta ya kula ambayo hayajalipiwa ushuru.

Ameongeza kuwa kukwamatwa kwa lori hilo ni sehemu ya msako unaofanywa na jeshi la polisi mkoani Pwani kwa lengo la kudhibiti bidhaa za magendo zinazoingizwa nchini bila kulipiwa ushuru kupitia bandari 15 sizizo rasmi zilizopo katika wilaya ya Bagamoyo.

Amesema kuwa katika msoko huo, polisi pia wamekamata mifuko 50 ya sukari.

Serikali kuendelea kuboresha sekta ya afya

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo halmashauri ya wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.

Amesema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya chenye uwezo wa kutoa huduma muhimu hasa zile za maabara, upasuaji na mama na mtoto.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Malindi wilayani Lushoto baada ya kutembelea jengo la soko la mboga la Malindi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Tanga.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa serikali imejipanga vizuri katika kuboresha sekta ya afya ndio maana imeongeza bajeti ya kununulia dawa kutoka shilingi bilioni 31 kwa mwaka hadi kufikia shilingi bilioni 269.

“Hatutaki tena kusikia mgonjwa anaenda hospitali na kukosa dawa biashara hiyo tumeimaliza, Rais Dkt. John Magufuli ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa”, amefafanua Waziri Mkuu.

Amesema kuwa katika wilaya ya Lushoto, serikali imetenga shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya vituo vya afya vya kata za Kangagai, Mnazi na Mlola.

“Halmashauri wekeni mpango thabiti wa kujenga wodi mbili kati yake moja ya wanaume na nyingine ya wanawake, lengo la Serikali ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi”, amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizungumzia mradi huo wa ujenzi wa soko hilo la mboga la Malindi, Waziri Mkuu amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya huduma zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii nchini.

Waziri Mkuu ametaja huduma nyingine zinazotolewa na serikali kwa wananchi kuwa ni pamoja na afya, elimu na maji.

Hivyo, amewataka wakazi wa kata hiyo ya Malindi kutumia vizuri soko hilo ambalo linatoa fursa kwao kufanya biashara katika eneo zuri na kuwawezesha kuuza bidhaa zao zikiwa katika ubora.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto, -Ikupa Mwasyoge amesema kuwa kukamilika kwa soko hilo kutainufaisha halmashauri na wananchi.

Ikupa amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo la soko la ghorofa mbili lililojengwa kwa awamu mbili ulianza mwaka 2011 na umekamilika mwezi Septemba mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni 1.1.

Wanaojihusisha na magendo Karagwe waonywa

0

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Simon Sirro amesema kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi dhidi ya raia na askari wa jeshi hilo wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya magendo ya kahawa kwenda nchi jirani.

IGP Sirro ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake wilayani Karagwe mkoani Kagera.

Kufuatia kuendelea kwa biashara ya magendo ya kahawa mkoani Kagera, IGP Sirro amewataka watu wote wanaojihusisha na biashara hiyo kuacha mara moja kabla operesheni maalum ya kupambana na magendo haijawafikia.

Akiwa wilayani Karagwe, Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini pamoja na mambo mengine, ameweka jiwe na msingi la ujenzi wa jengo la idara ya upelelezi na lile la ujenzi wa idara ya usalama barabarani.

Ujenzi huo unasimamiwa na Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Karagwe, ambapo IGP Sirro ameahidi kuchangia shilingi milioni Tano ili kukamilisha ujenzi huo.