Treni yapata ajali

0

Treni ya abiria inayomilikiwa na Kampuni ya Reli nchini (TRC) inayofanya safari zake kati ya Pugu na Stesheni jijini Dar es salaam imepata ajali  asubuhi ya leo na kusababisha watu tisa kujeruhiwa.

Akizungumza na Mwandishi wa TBC, Kamanda wa  Polisi Kikosi cha Reli, – David Mnyambuga amesema kuwa ajali hiyo imetokea katika eneo la  Pugu nje kidogo ya jiji la Dar es salaam wakati ikielekea Stesheni huku chanzo chake bado hakijajulikana.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ilala, –  Sophia Mjema amewatoa hofu wananchi wanaotumia treni hiyo kwa kusema kuwa usafiri huo bado ni salama licha ya kutokea kwa ajali hiyo.

Baadhi ya watu walioshuhudia ajali hiyo wamesema kuwa,  dereva wa treni hiyo alifanya jitihada kubwa kuzuia treni hiyo isitoke katika njia yake ili kuepusha madhara zaidi.

Taasisi na mashirika yatakiwa kuvutia wawekezaji

0

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) Geoffrey Mwambe ametoa wito kwa taasisi na mashirika ya umma kutathmini mifumo yao ya utendaji kazi na kuangalia maeneo muhimu ya kuyafanyia kazi ili kuharakisha juhudi za kuvutia wawekezaji.

Mwambe ametoa wito huo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ambapo alikua akizungumzia kongamano la uwekezaji lililofanyika mwezi Oktoba mwaka huu huko Geneva, – Uswisi na kuhudhuriwa na wakuu wa nchi na viongozi wakuu wa taasisi za uwekezaji, kongamano lililoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Biashara(UNCTAD).

Amesema kuwa kila taasisi na shirika la umma nchini lina maeneo muhimu kwa ajili ya kuvutia wawekezaji, hivyo juhudi za dhati zinahitajika katika kuimarisha maeneo hayo ambayo yataimarisha uchumi wa Taifa.

“Kila wizara, kila idara na kila taasisi ya serikali itambue inahitaji kufanya nini ili kuweza kuvutia uwekezaji, kila sekta ijitathmini inafanya nini katika kurekebisha mfumo wao ili  kuvutia wawekezaji, watu wengi wanadhani suala la uwekezaji ni la wizara ya viwanda na Biashara tu,wengine wanadhani ni suala la Kituo cha uwekezaji tu,hapana ni la kila wizara na la kila mtu,  hivyo ni lazima sekta zote zifanye juhudi za kuvutia uwekezaji”, amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TIC.

Amesisitiza kuwa TIC inafanya jitihada nyingi za kuhamasisha wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza nchini, lakini kumekua na baadhi ya watendaji wa serikali wamekua wakikwamisha juhudi hizo, jambo ambalo halikubaliki.

“Jamani huko Duniani tunanyang’anyana wawekezaji, hata nchi zilizoendelea zinahamasisha wawekezaji waende kuwekeza kwao,sisi hapa kwetu tunahamasisha waje na wakija kuna baadhi ya watendaji wa serikali wanawakwaza, hili halikubaliki”, amefafanua Mwambe.

Ameongeza kuwa wakati wa kongamano hilo,  UNCTAD imetoa mwenendo wa uwekezaji kwa nchi  mbalimbali duniani, ambapo kwa mwaka 2016 kwenye nchi za Afrika Mashariki, Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji  kwa kupata  uwekezaji wa shilingi  bilioni 1.565  ikifuatiwa na Uganda kwa shilingi milioni 580.

 

 

 

Serikali yaagiza kiwanda cha Mponde kianze kazi

0

Serikali imemaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya wakulima wa chai wa wilaya za Lushoto na Korogwe zilizopo mkoani Tanga  na kampuni ya Mponde Tea Estate uliosababisha kufungwa kwa kiwanda cha chai cha Mponde na kuagiza kiwanda hicho kianze kazi mara moja.

Uamuzi huo wa serikali umetangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Kweminyasa kata ya Mponde wilayani Lushoto baada ya kutembelea kiwanda hicho.

“Waziri Mwijage na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Profesa  Siza Tumbo hakikisheni kazi ya kukagua kiwanda na mitambo inafanyika haraka na kubaini mitambo ipi ni mizima na ipi ina hitilafu ili ukarabati ufanyike na kiwanda kianze kazi mara moja,”ameagiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa mwaka 1999 serikali iliamua kuwapa wakulima wa chai kiwanda hicho  kwa ajili kuwawezesha kuwa na sehemu ya kuchakata chai yao, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi na hivyo imeamua kukirudisha serikalini baada ya kuwepo kwa migogoro iliyoathiri uzalishaji.

“Serikali imeamua kukichukua kiwanda hiki ambacho awali ilikikabidhi kwa wakulima wa chai na kwamba itahakikisha lengo lake la kuboresh kilimo linafanikiwa na  wakulima wanaendelea kulima zao la chai, hatutaki kusikia masuala ya Utega wala Mponde hapa si mahali pake,”amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa anayeendelea na ziara yake mkoani Tanga.

Kuhusu suala la madeni ya watumishi, ameagiza watafutwe na madai yaorodheshwe kwa ajili ya malipo, na amewahakikisha wananchi hao kuwa ajira zilizopotea baada ya kiwanda hicho kufungwa zitarudi kwa kuwa serikali inataka kuona kiwanda hicho cha chai cha Mponde kinafanya kazi.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, wakulima hao wa chai wa wilaya za Lushoto na Korogwe walikosea kwa kuunda Umoja wa Wakulima wa Chai (UTEGA) ambapo katika kusajili badala ya kuanzisha ushirika wao walisajili kama NGO ambayo ilikuwa na wanachama wake, huku kiwanda kikiwa kimeanzishwa kwa ajili ya wakulima wote, jambo ambalo lilisababisha mgogoro baina ya wakulima na viongozi wa UTEGA.

Ameongeza kuwa wakati mgogoro huo ukiendelea kati ya UTEGA na wakulima wa chai wasiokuwa wanachama wa NGO hiyo, uliibuka mgogoro mwingine baina ya wakulima wote pamoja na mwekezaji ambaye ni kampuni ya Mponde Tea Estate baada ya kukabidhiwa kiwanda hicho  na uongozi wa UTEGA bila ya wao kushirikishwa.

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makam wa Rais Muungano na Mazingira, –  January Makamba alisema kuwa mgogoro huo wa kiwanda cha Mponde ulianza mwaka 1999 na ilipofika mwezi Mei mwaka 2013, wananchi walimlalamikia kwa kushindwa kutatua tatizo hilo.

Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli pia  ameiomba serikali iwasaidie wakulima wa zao la chai  kwa kuwapa miche mipya pamoja na pembejeo kwa ajili ya kufufua zao hilo na kukiwezesha kiwanda cha chai cha MPonde kupata malighafi kama ilivyokuwa hapo awali.

Akizungumza  kiwandani hapo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji  Charles Mwijage amesema kuwa  tayari wataalam kwa ajili ya kukagua mashine zote zilizopo kiwandani hapo wamekwishafika kiwandani ili mchakato wa kuziwasha mashine hizo uanze  mara moja.

 

Kisanduku cheusi cha ndege iliyoanguka Indonesia chapatikana

0

Wapigambizi nchini Indonesia wamekipata kisanduku cheusi kinachorekodi mwenendo wa ndege cha ndege ya nchi hiyo iliyoanguka baharini Jumatatu wiki hii na kusababisha vifo vya abiria wote 189 waliokuwa ndani ya ndege hiyo.

Ndege hiyo ilianguka dakika kumi mara baada ya kuruka kutoka katika uwanja wa ndege wa Jarkata, ikiwa imepoteza mawasiliano na mnara wa kuongoza ndege kwenye uwanja huo.

Hata hivyo, mapema rubani wa ndege hiyo alisikika akiomba ridhaa ya kurejea tena katika uwanja huo wa ndege wa Jarkata.

Kifaa cha kuwasaidia waliopooza chagunduliwa

0

Wanasayansi nchini Uswisi wamegundua kifaa maalum kinachotumia umeme ambacho kinatarajiwa kuwasaidia watu waliopooza viungo mbalimbali vya mwili hasa uti wa mgongo kupona na kurejea katika hali ya kawaida.

Kifaa hicho kina uwezo wa kusisimua misuli ya mgongo na kuunganisha ufahamu katika ubongo wa binadamu ili hatimaye kurejesha mawasiliano yaliyokatika kati ya ubongo na uti wa mgongo.

Hata hivyo zoezi hilo sio rahisi, kwa kuwa mgonjwa anapaswa kupitia katika mazoezi mengi, wakati mwingine kuhisi maumivu makali, lakini mwisho ni kumsaidia kurejea katika maisha yake ya kawaida.

 

Khan ashutumu maandamano Pakistan

0

Waziri Mkuu wa Pakistan, – Imran Khan ameshutumu maandamano yanayoendelea nchini humo kwa mwamvuli wa dini ya kiislamu, yanayopinga hatua ya mahakama nchini humo kubatilisha hukumu ya kifo dhidi ya mwanamke mmoja.

Khan amesema kuwa serikali yake haitaruhusu ghasia zenye mwamvuli wa dini kuondoa amani nchini humo, kwani wananchi wanapaswa kuheshimu vyombo ya dola ikiwemo mahakama.

Kumekuwa na maandamano makubwa ya vitisho nchini Pakistan, baada ya mahakama kuu nchini humo kubatilisha hukumu ya kifo dhidi ya mwanamke huyo Asia Bibi kutoka dini ya kikristo aliyekuwa ametiwa hatiani kwa kosa la kukufuru dini ya kiislam.

Khan amesema kuwa waandamanaji hao hawawakilishi uislamu, bali hisia zao na amewataka wananchi kudumisha amani na kujiepusha katika mikusanyiko isiyofaa, kwa kuwa serikali haitaendelea kuwavumilia.

Mwanamke huyo ambaye ni mama mwenye watoto wanne, alipatikana na hatia baada ya kuchota maji ya kunywa katika chombo chake na kuwapatia wanawake wa kiislamu ili wanywe maji hayo.

Wanawake hao walikasirishwa na hatua hiyo na kudai kuwa Asia amemkufuru mtume, kwani hakupaswa kuwapatia maji akitumia chombo chake.

Asia alitiwa mbaroni miaka minane iliyopita, baada ya wanawake hao kutaka ahukumiwe kifo.

Viwanda zaidi vyaendelea kujengwa

0

Serikali imesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu zaidi ya viwanda elfu tatu na sitini vimejengwa na hivyo kutoa fursa kwa Watanzania wengi.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Rais John Magufuli wakati wa kongamano la hali ya Uchumi na Siasa nchini lililoandaliwa na Chuo Kikuu Cha Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Rais Magufuli ameongeza kuwa pamoja na serikali kufanya jitihada kubwa za kujenga viwanda vipya, pia ina mpango wa kuvichukua viwanda ilivyovibinafsisha na ambavyo havizalishi kama ilivyotarajiwa.

Kuhusu  hali ya uchumi nchini, Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania ni miongozni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi na kwamba hadi sasa umekua kwa asilimia Saba, huku mfumuko wa bei ukiimarika.

Amesisitiza kuwa nchi ina fedha za kutosha na hadi sasa ina akiba ya dola bilioni 5.4 za Kimarekani, akiba ambayo haijawahi kuwepo toka uhuru na inayoweza kutosheleza kwa muda wa miezi sita.

Rais Magufuli ameahidi serikali yake kuyashughulikia mambo yote yaliyowasilishwa kupitia mada mbalimbali, kwa maana yana mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.

Miongozi mwa watoa mada katika kongamano hilo la hali ya Uchumi na Siasa nchini, lililohudhuriwa na washiriki kutoka sekta mbalimbali ni Profesa Humphrey Mushi, Profesa Rwekaza Mukandala na Profesa Kitila Mkumbo.

 

 

 

Waliodanganya umri Benin watupwa jela

0

Wachezaji kumi wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 nchini Benin na Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini humo Anjorin Moucharafou wamehukumiwa kifungo jela kwa kosa la kudanganya umri.

Mahakama ya mji wa Cotonou imewakuta na hatia wachezaji hao baada ya vipimo vya MRI kubaini umri wao sahihi.

Mwezi Septemba mwaka huu,  wachezaji hao  kumi wa timu ya vijana  ya Benin walikwenda nchini Niger kushiriki michuano ya awali ya kufuzu kwa michuano ya Afrika ya vijana na walipopimwa walikutwa wamezidi umri na hivyo nchi hiyo kuondoshwa kwenye michuano hiyo.

Wachezaji hao kumi watatumikia kifungo cha miezi sita jela na kuzuiliwa kucheza soka kwa kipindi cha miezi mitano.

Kwa upande wake Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini Benin, – Anjorin Moucharafou  atatumikia kifungo cha miezi 12 jela na amefungiwa kujihusisha na masuala ya soka kwa kipindi cha miezi kumi.