Milwaukee waendeleza ushindi NBA

0

Milwaukee Bucks wameendeleza wimbi la ushindi kwenye Ligi ya kulipwa ya mpira wa kikapu nchini Marekani baada ya kuilaza Sacramento Kings alama 144 kwa 109 katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Fiserv mjini Milwaukee , – Wisconsin.

Licha ya Justin Jackson kuifungia Kings alama 22, bado hazikutosha kuwapa ushindi mbele ya Bucks ambao tangu kuanza kwa msimu huu wamepoteza mchezo Mmoja na kushinda michezo nane.

Katika matokeo mengine Portland Trail Blazers wameinyuka Minasota Timberwolves alama 111 kwa 81 wakati Memphis Grizilies wakinyukwa alama 102 kwa 100 na Phonix Suns.

Washngton Wizards wamechomoa na ushindi wa alama 108 kwa 95 dhidi ya New York Knicks na Philadelphoia 76’ERS wamelala kwa alama 122 kwa 97 mbele ya Brooklyn Nets.

Huko AT & T Center mjini San Antonio, -Texas, wenyeji San Antonio Spurs wameshindwa kutamba baada ya kutandikwa alama 117 kwa 110 na Orlando Magic katika mchezo ambao Aaron Gordon amefunga alama 26.

Huo unakuwa mchezo wa tatu kati ya tisa kwa Spurs kupoteza kwa msimu huu wakati Magic wakipata ushindi wao wa sita katika michezo tisa waliyocheza mpaka sasa.

Rekodi ya haki za binadamu Saudi Arabia kupitiwa

0

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinakutana mjini Geneva nchini Uswisi kupitia rekodi ya haki za binadamu ya Saudi Arabia katika kipindi hiki ambapo taifa hilo linakabiliwa na shutuma juu ya mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.

Mkutano huo unaofanyika chini ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu ukiwa umepita takribani mwezi mmoja tangu mwandishi huyo wa habari ambaye alikua ni mkosoaji wa ufalme wa Saudi Arabia kuuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia Arabia mjini Istanbul nchini Uturuki.

Mkutano huo ambao unawakutanisha wawakilishi kutoka nchi zote 193 Wanachama wa Umoja wa Mataifa, pia unajadili wajibu wa Saudi Arabia kwenye vita vya Yemen, nchi ambayo mwaka 2015 pamoja na washirika wake waliingilia kijeshi vita hiyo ili kumuunga mkono Rais Abedrabbo Mansour Hadi baada ya waasi wanaoungwa mkono na Iran kuchukua udhibiti wa mji mkuu wa Sanaa.

Ujumbe wa Saudi Arabia katika mkutano huo unaongozwa na Bandar Al Aiban ambaye ni mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu ya nchi hiyo, ujumbe ambao utawasilisha ripoti ya namna nchi hiyo inavyojitahidi kuheshimu haki za binadamu za kimataifa na pia utajibu maswali na maoni kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu rekodi yao.

Tayari Uingereza, Austria na Uswisi zimewasilisha orodha ya maswali yatakayoulizwa kwenye mkutano huo kuhusu mauaji ya Khashoggi yaliyotokea Oktoba pili mwaka huu.
Saudi Arabia ina rekodi ya kuendelea kutumia adhabu ya kifo, kuwa na ongezeko la adhabu ya kunyonga pamoja na matumizi ya sheria ya kupambana na ugaidi inayolalamikiwa kuwa inatumika vibaya.

Marekani kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Iran

0

Marekani imeanza kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Iran katika sekta za mafuta na fedha.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, – Mike Pompeo amedai kuwa vikwazo hivyo ni vikali kuwahi kuwekwa na nchi hiyo dhidi ya Iran.

Wataalamu wa masuala ya kiuchumi wamesema kuwa, vikwazo hivyo huenda vikaathiri moja kwa moja kampuni mbalimbali zinazofanya biashara na Iran.

Mwezi Mei mwaka huu, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuiondoa nchi yake katika mkataba wa kimataifa wa nyuklia na Iran.

Cavaliers yaendelea kufanya vibaya NBA

0

Cleveland Cavaliers imeendelea kupepesuka kwenye ligi ya kulipwa ya mpira kikapu nchini Marekani maarufu kama NBA baada ya kuambulia kichapo cha alama 110 kwa 91 mbele ya Denver Nuggets.

Juan Hernangomez amefunga alama 23 huku Paul Millsap akifunga alama 16 kwa upande wa Nuggets na kuwapa wakati mgumu Cleveland Cavaliers wanaoonekana kuikosa huduma ya nyota Lebron James aliyetimkia Los Angeles Lakers.

Cavaliers wanaburuza mkia kwenye kanda ya mashariki wakiwa wamepata ushindi mmoja tu kwenye michezo nane waliyoshuka dimbani kucheza.

Kwenye matokeo mengine, Philadelphia 76ERS wamewabugiza Los Angeles Clippers alama 122 kwa 113, Charlotte Hornets wamenyukwa na Oklahoma City Thunder alama 111 kwa 107 huku Atlanta Hawks wakibugizwa alama 146 kwa 115 na Sacramento Kings.

Nao Boston Celtics wamepta ushindi mwembamba wa alama 117 kwa 113 za Milwauckee Bucks ambao wamepoteza mchezo wao wa kwanza msimu huu wa NBA kwa kanda ya mashariki huku mchezo mwingine ukiwashuhudia Portland Trail Blazers wakiwafunga New Orleans Pelicans alama 132 kwa 119.

Federer na Djokovic watinga robo fainali

0

Nguli wa mchezo wa tenisi Roger Federer na Novak Djokovic wametinga robo fainali ya michunao ya tenisi ya Paris Masters.

Roger Federer anayeshika nafasi ya tatu kwenye viwango vya ubora wa mchezo huo amemuondosha Fabio Fognin wa Italia kwa ushindi wa seti mbili kwa bila za 6-4 na 6-3 katika mchezo uliodumu kwa saa moja na dakika 13.

Kwa upande wake Novak Djokovic anayeshika nafasi ya pili kwenye viwango vya ubora wa mchezo wa tenisi, yeye ametinga robo fainali baada ya mpinzani wake Damir Dzumhur wa Bosnia kushindwa kumaliza mchezo huo baada ya kupata maumivu ya mgongo.

Djokovic atachuana na Marin Cilic wa Croatia kwenye mchezo wa robo fainali ambapo Cilic amemuondosha Grigor Dimitrov wa Bulgaria kwa ushindi wa seti mbili kwa sifuri za 7-5 na 6-4.

 

Al Ahly na Esperance uso kwa uso

0

Timu za Al Ahly ya Misri na Esperance ya Tunisia zinacheza mchezo wa kwanza kati ya miwili ya fainali ya ligi ya mabingwa Barani Afrika katika mchezo unaofanyika jijini Alexandria nchini Misri.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya tatu kwenye msimu huu baada ya kucheza mara mbili kwenye hatua ya makundi ambapo Al Ahly ilishinda bao moja kwa sifuri nchini Tunisia na kutoka suluhu kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa nchini Misri.

Mjumbe wa bodi ya Al Ahly, –  Khaled Mortagy amesema kuwa wanatarajia michezo hiyo miwili ya fainali itakuwa migumu kutokana na matokeo ya hatua ya makundi zilipokutana timu hizo ambapo amewataka wachezaji wa kikosi hicho kusahau matokeo ya michezo iliyopita na kupambana ili kutwaa taji hilo.

Jambo zuri kwa Al Ahly ni kurejea kwa mfungaji wao bora Walid Azaro, – raia wa Morocco aliyekuwa anauguza majeraha aliyoyapata kwenye mchezo dhidi ya Entente Setif ya Algeria kwenye mchezo wa nusu fainali.

Mabingwa wa kihistoria Al Ahly wenye makombe nane ya ligi ya mabingwa Barani Afrika, wanaingia kulisaka taji la tisa kwenye michuano hiyo huku Esperance wakiliwinda taji la tatu.

 

Zimbabwe kuwa na mafuta na gesi asilia

0

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ametangaza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa mafuta na gesi asilia kaskazini mwa nchi hiyo.

Amesema kuwa kampuni ya uchimbaji madini ya Invictus Energy ya nchini Australia kwa kushirikiana na serikali ya Zimbabwe inatarajiwa kuanza utafiti ili kubaini iwapo mafuta hayo yanaweza kuchimbwa na kuuzwa kibiashara.

Rais Mnangagwa amesema kuwa kisima cha mafuta kitachimbwa na kampuni hiyo ya Invictus Energy kwenye wilaya ya Muzarabani katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

“Tumeshauriwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Invictus Energy kwamba matokeo ya utafiti huo yana matumaini makubwa na yanaashiria kupatikana kwa mafuta na gesi asilia katika eneo hilo” amesema Rais Mnangagwa.

Kisima hicho cha mafuta kitachimbwa takribani kilomita 240 kaskazini mwa mji mkuu wa Zimbabwe, – Harare kwa gharama ya dola milioni 20 za kimarekani.

Mazungumzo ya simu kuhusu Kashoggi yanaswa

0

Baadhi ya majarida nchini Marekani yameandika habari inayosema kuwa Mwana wa mfalme wa Saudi Arabia, – Mohammed bin Salman aliwahi kuiambia Marekani kuwa mwandishi wa habari wa Saudi Arabia aliyeuawa Jamal Khashoggi ni mwanachama wa kikundi kimoja cha Kiislam.
Majarida hayo ya Washington Post and New York Times yamedai kuwa Salman alitoa kauli hiyo kwa njia ya simu alipozungumza na maafisa wa Ikulu ya Marekani Oktoba Tisa mwaka huu ikiwa ni wiki moja tangu kutoweka kwa Khashoggi.
Kwa mujibu wa majarida hayo, kauli ya Mwana wa mfalme huyo wa Saudi Arabia aliitoa kabla nchi hiyo haijakiri kuwa mwandishi huyo wa habari aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo huko Istanbul,- Uturuki.
Katika mazungumzo hayo Salman alieleza kuwa Kashoggi alikua mwanachama wa kikundi cha Muslim Brotherhood na kuiomba Marekani kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Kufuatia kutolewa kwa taarifa za mazungumzo hayo ambayo yalifanyika kwa njia ya simu, familia ya mwandishi huyo wa habari nayo imetoa tamko na kusema kuwa Kashoggi hakuwa mwanachama wa Muslim Brotherhood na kwamba katika uhai wake aliwahi kukanusha jambo hilo mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni.
Habari zaidi zinasema kuwa kauli ya Mwana wa mfalme huyo wa Saudi Arabia inatofautiana na ile aliyoitoa mara baada tu ya mauaji hayo, ambapo alisema kuwa Kashoggi amekufa kifo cha kusikitisha na kwamba nchi hiyo itafanya kila iwezalo kuwatia hatiani wale wote waliohusika na tukio hilo.
Kashoggi aliyefahamika kama mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, anadaiwa kuuawa oktoba pili mwaka huu na mwili wake haujpatikana hadi hivi sasa.