Mkutano wa 13 wa Bunge waanza Dodoma

0

Mkutano wa 13 wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaendelea jijini Dodoma.

Mkutano huo wa wiki mbili umeanza kwa Spika wa Bunge Job Ndugai kuwaapisha wabunge wanne ambao watatu kati yao wanakula kiapo kwa mara ya pili ndani ya Bunge la 11.

Wabunge hao ni Mwita Waitara wa jimbo la Ukonga Jijini Dar es salaa, Julius Kalanga wa jimbo la Monduli mkoani Arusha na Zuberi Kuchauka wa jimbo la Liwale mkoani Lindi ambao ndio wamekula kiapo kwa mara ya pili na mwingine ni Thimotheo Mzava wa jimbo la Korogwe Vijijini mkoani Tanga.

Mbunge Waitara, Kalanga na Kuchauka wamechaguliwa katika majimbo yao baada ya kujiuzulu na kuhama kutoka vyama vyao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kisha kushiriki katika uchaguzi mdogo wa ubunge, na Mzava amechukua nafasi hiyo baada ya kufariki dunia kwa Steven Ngonyani aliyekua akishikilia kiti hicho.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Bunge imesema kuwa jumla ya maswali 125 ya kawaida yataulizwa wakati wa mkutano huo wa 13 na maswali mengine 16 ya papo kwa papo yataulizwa kwa Waziri Mkuu.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa Wabunge wengine wapya ambao tayari wamepita bila kupingwa na wengine watakaochaguliwa wataapishwa wakati wa mkutano wa 14 wa Bunge hilo unaotarajiwa kufanyika mwezi Januari mwaka 2019.

Zaidi ya watoto 70 watekwa Cameroon

0

Takribani watu 80 wengi wao wakiwa watoto wametekwa katika mji wa Bamenda Magharibi mwa Cameroon.

Kikundi cha watu wanaozungumza lugha la Kiingereza nchini Cameroon wamedai kuhusika na tukio hilo ambapo watoto hao walikuwa ni wanafunzi wa bweni.

Nchi ya Cameroon imekuwa na maandamano ya mara kwa mara wakimpinga Rais wa nchi hiyo Paul Biya.

Bunge kuanza Novemba sita

0

Mkutano wa kumi na tatu wa bunge la kumi na moja unatarajiwa kuanza kesho jijini Dodoma ambapo wabunge wateule wanne watakula kiapo cha uaminifu huku wabunge wengine waliopita bila kupingwa hivi karibuni wakisubiri kuapishwa katika mkutano wa bunge wa kumi na nne.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma Spika wa bunge Job Ndugai amesema bunge hilo litapokea na kujadili wasilisho la mpango wa taifa unaokusudiwa kutekelezwa mwaka 2019/2020.

Spika Ndugai ameongeza kuwa miswada sita ya sheria itasomwa kwa mara ya kwanza na muswada wa sheria ya huduma ndogo za fedha wa mwaka 2018 ambao utasomwa kwa mara ya kwanza na hatua zake zote baada ya kupelekwa bungeni kwa hati ya dharura kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Magufuli.

Aidha bunge hilo litapitia na kuridhia maazimio matatu ikiwa ni pamoja na azimio la kuridhia itifaki ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu kulinda hati miliki za aina mpya za mbegu za mimea, azimio la kuridhia mkataba wa kimataifa wa kuzuia matumizi ya silaha za kibaiolojia na sumu na azimio la kuridhia mkataba wa takwimu wa Afrika.

Mitihani kidato cha nne yaanza nchini

0

Mitihani ya kidato cha nne na mitihani ya maarifa –QT imeanza nchini kote huku hali ya ulinzi na ukimya vikiwa vimetawala.

Mwandishi wa TBC amepita katika shule mbalimbali za sekondari jijini Dar Es Salaam na kushuhudia hali ya ulinzi ikiwa imeimarishwa.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania –NECTA, Dkt. Charles Msonde ameiambia TBC kuwa mitihani hiyo imeanza vizuri kwa kuwa mitihani ilifika kwa wakati katika maeneo yote kunakofanyika mitihani.

Kamati yakamilisha kazi yake TBC

0

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt Ayub Rioba amewataka wafanyakazi wa shirika hilo kufanya kazi wa weledi na kuwatumikia wananchi kwa kutanguliza maslahi ya shirika.

Dkt Rioba ameyasema hayo jijini Dar es salaam baada ya kupokea taarifa ya kamati ya uchunguzi wa mianya ya rushwa na upotevu wa mapato ya TBC aliyoiunda kwa lengo la kuchunguza mali na mapungufu ndani ya shirika hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo Aloysia Maneno amesema kuwa katika uchunguzi wao pamoja na mambo mengine wamebaini changamoto kadhaa zinazolikabili shirika hilo.

Kamati hiyo ya kuchunguza mianya ya rushwa na upotevu wa mapato ya TBC ilikuwa na wajumbe wanane na imefanya kazi kwa muda wa takribani wiki mbili kwa kutafuta taarifa kwa wafanyakazi na wasio wafanyakazi katika kanda ya kati Dodoma na kanda ya kaskazini katika mkoa wa Tanga.

Serikali kuendeleza mageuzi ya kiuchumi

0

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi ametoa taarifa inayohusu mafanikio ya kijamii na kiuchumi yaliyofikiwa na serikali katika kipindi cha miaka mitatu.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Dkt Abbasi amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli imeendeleza mageuzi ya kiuchumi yenye lengo la kuwaletea Watanzania maendeleo.

Amesema kuwa ndani ya kipindi hicho cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Magufuli, uchumi wa nchi umeendelea kukua kwa kasi inayokubalika duniani, mbali na changamoto kadhaa zinazojitokeza.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, mambo yanayosimamiwa na serikali ya awamu ya tano ni pamoja na ukusanyaji wa mapato, ufufuaji wa mashirika ya umma, mapambano dhidi ya rushwa na usimamiaji wa miradi ya maendeleo.

Rooney ndani ya mtanange wa England na Marekani

0

Mshambuliaji wa kimataifa wa England, – Wayne Rooney atarejea dimbani kuitumikia timu ya taifa hilo katika mchezo maalum wa kumuaga dhidi ya Marekani baadae mwezi huu.

Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 33, anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika taifa hilo akiwa amefunga mabao 53.

Mara ya mwisho kuitumikia timu ya taifa ya England ilikuwa mwezi Novemba mwaka 2016, ambapo timu hiyo ilipata ushindi wa mabao matatu kwa bila dhidi Scotland.

Mchezo huo utakaochezwa Novemba 15 mwaka huu kwenye dimba la Wembley jijini London utakuwa wa 120 kwa Rooney kuitumikia timu ya taifa na tayari mechi hiyo imepewa jina la taasisi ya kimataifa ya Wayne Rooney yaani The Wayne Rooney Foundation international.

Chama Cha Soka cha England (FA)  kimesema kuwa hiyo ni nafasi pekee ya kumuaga kwa heshima nguli huyo na kwamba uwanja wa Wembley utapambwa kwa rangi za dhahabu zilizopo kwenye taasisi hiyo ya kimataifa ya Rooney.

Kwa upande wake Rooney amesema kuwa anajisikia fahari kuichezea tena timu ya taifa na kumshukuru kocha wa kikosi hicho Gareth Southgate pamoja FA kwa kumuita kwenye mchezo huo.

Messi kuikabili Inter Milan

0

Lionel Messi amejumuishwa kwenye kikosi cha FC Barcelona kinachosafiri hadi mjini Milan nchini Italia kuikabili Inter Milan kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa barani ulaya.

Kujumuishwa kwa Messi kwenye kikosi hicho kumewashangaza wengi hasa baada ya ripoti ya daktari kuonyesha kuwa nyota huyo angekuwa nje ya dimba kwa kipindi cha majuma matatu baada ya kuumia mkono katika ushindi wa mabao manne kwa mbili dhidi ya Sevilla wiki mbili zilizopita.

Messi tayari amekosa michezo kadhaa ukiwemo ule wa ushindi wa mabao matano kwa moja dhidi ya Real Madrid na mchezo dhidi ya Inter Milan ambao walishinda mabao mawili kwa moja.

Kocha wa Barcelona, – Ernesto Valverde amesema kuwa hajamuondoa Messi kwenye kucheza, bali anafikiria kumrudisha kikosini mapema.

Barcelona ndiyo vinara wa kundi B wakiwa na alama tisa baada ya kushinda mechi zao zote tatu huku wapinzani wao Inter Milan wakiwa katika nafasi ya pili wakiwa wamepoteza mchezo mmoja tu dhidi ya miamba hiyo ya Hispania.