Hornets watamba NBA

0

Charlotte Hornets wamewanyuka Atlanta Hawks alama 113 kwa 102 kwenye ligi ya kulipwa ya mpira wa kikapu ya nchini Marekani maarufu kama NBA.

Nyota wa Hornets, mlinzi Kemba Walker amefunga alama 29 huku Marvin Williams akifunga alama 20 na kuchagiza ushindi huo muhimu kwa timu yao ambayo imekuwa na matokeo ya mchangayiko msimu huu.

Katika matokeo mengine, Dallas Mavericks wamewatungua Washington Wizards alama 119 kwa 100 huku Phoenix Suns wakiangukia pua kwa kufungwa na Brooklyn Nets alama 104 kwa 82.

Nao Portland Trail Blazers wameendeleza wimbi la matokeo mazuri kwenye ligi hiyo baada ya kuwanyuka Milwauckee Bucks alama 118 kwa 103 katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Moda Center mjini Portland, -Oregon.

Chaneli ya Utalii TBC mbioni kuzinduliwa

0

Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Susan Mlawi ameelezea kuridhishwa na hatua iliyofikiwa ya uanzishwaji wa chaneli maalum ya Utalii ya shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Mlawi ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati wa kikao maalum cha Makatibu wakuu wa sekta zinazohusika na masuala ya utalii na menejimenti ya TBC na kuongeza kuwa chaneli hiyo itazinduliwa mwezi Disemba mwaka huu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa hatua iliyofikiwa ya uanzishwaji wa chaneli hiyo maalum ya utalii ni kubwa na ya kuridhisha.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt Salehe Yusuf Mnemo ambaye amewaeleza washiriki wa kikao hicho kuwa suala la utalii ni la kitaifa na likipewa kipaumbe litakua na faida kubwa kwa Taifa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBC, – Dkt Ayub Rioba amesema kuwa chaneli hiyo itakayojulikana kama TANZANIA SAFARI itakuwa ni maalum kwa ajili ya kutangaza maliasili, utalii, vivutio na tamaduni zilizopo nchini .

Dkt Rioba ametoa wito kwa Watanzania wote hasa waandishi wa habari, kuandika na kutangaza mambo mazuri ya kimaendeleo ya Taifa ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya raia wa mataifa ya nje kuwa Bara la Afrika linatawaliwa na vita na njaa.

Mwezi Mei mwaka 2017 alipoitembelea TBC, Rais John Magufuli aliliagiza shirika hilo kuanzisha chaneli maalum itakayotangaza mambo mazuri na ya kuvutia yanayopatikana Tanzania, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini kila mwaka.

Vituo vya afya vyasisitizwa kutumia mashine za kielektroniki

0

Mkurugenzi wa manispaa ya Kigamboni mkoani Dar es salaam, -Ng’wilabuzu Ludigiji amesema kuwa kuna umuhimu kwa vituo vya afya nchini kutumia mashine za kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato.

Ludigiji amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kudhibiti upotevu wa mapato na hivyo kuboresha utoaji wa huduma bora za afya kwa wagonjwa.

Mkurugenzi huyo wa manispaa ya Kigamboni ametoa kauli hiyo wakati akipokea msaada wa vitanda vya kulalia wagonjwa pamoja na vya kujifungulia vitakavyotumiwa na wagonjwa wanaolazwa katika kituo cha afya cha Kigamboni.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa NMB Kanda ya Dar es salaam, – Badru Iddi amesema kuwa benki hiyo ipo tayari kutoa mashine hizo za kielekroniki ili kuvisaidia vituo vya afya katika ukusanyaji mapato.

Tayari serikali imetoa shilingi milioni mia nne kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya akina mama katika kituo hicho cha afya cha Kigamboni, ujenzi ambao umefikia hatua ya kuezeka na itakapokamilika itasaidia akina mama wengi zaidi wanaofika katika kituo hicho kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Miss Tanzania kutumia lugha ya kiswahili

0

Mrembo wa Tanzania kwa mwaka 2018 Queen Elizeberth Makune amesema kuwa atatumia lugha ya kiswahili kwenye shindano la kumtafuta mrembo wa dunia pamoja na kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii ili kuwavutia watalii wengi kutoka nchini China kuitembelea Tanzania.

Akizungumza jijini Dar es salaam baada kupewa tuzo ya pongezi na Chuo Cha Uhasibu ambapo yeye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu, Queen Elizeberth amesema kuwa amejiandaa vizuri ili kurejea na taji la dunia.

Miss Tanzania huyo wa mwaka 2018, – Queen Elizeberth , ametembelea Chuo hicho cha Uhasibu kwa lengo la kuwapa Wanafunzi moyo wa kusoma na Wafanyakazi wa chuo hicho moyo wa kufanya kazi kwa bidii.

Mrembo huyo anatarajiwa kuondoka nchini Ijumaa wiki hii kuelekea nchini China kushiriki shindano la urembo la dunia litakalofanyika Disemba nane mwaka huu

Washikiliwa kwa mauaji Mwanza

0

Jeshi la polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu watano akiwemo Rahel Matalaka mkazi wa kijiji cha Ikelege wilayani Misungwi kwa tuhuma za kumpiga hadi kusababisha kifo cha mtoto wake Maliatabu Constantine, mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Ikelege.

Kamanda wa polisi wa mkoa Mwanza, – Jonathan Shanna amesema kuwa Rahel anatuhumiwa kumpiga Maliatabu sehemu mbalimbali za mwili  kwa kutumia fimbo, baada ya kufikishiwa malalamiko kuwa ameiba maembe kwa jirani.

Kamanda Shanna ameongeza kuwa baada ya kusababisha kifo cha mtoto wake, Rahel alimtundika mtoto wake juu ya mwembe kwa kutumia kipande cha kanga ili kupoteza ushahidi.

Facebook yakubali shutuma za Umoja wa Mataifa

0

Mtandao wa kijamii wa Facebook umekubali shutuma zilitolewa na Umoja wa Mataifa kuwa mtandao huo ulishindwa kuzuia mazingira yaliyosaidia kuchochea ghasia nchini Myanmar.

Taarifa iliyotolewa na mtandao huo imesema kuwa habari zilizokua zikichapishwa na kusambazwa na raia wa Myanmar kupitia Facebook zilikua zikiunga mkono ukiukwaji wa haki za binadamu na hatimaye kuzusha ghasia.

Facebook imetoa taarifa hiyo kufuatia kuenea kwa ghasia nchini Myanmar dhidi ya kabila la Rohingya linaloonekana kama ni la wahamiaji nchini humo, ghasia zilizosababisha mauaji ya watu wengi.

Wakati ukitoa shutuma hizo, Umoja wa Mataifa uliitaka Facebook kufanya jitihada za kuzuia kutokea kwa ghasia kama hizo nchini humo, nchi yenye zaidi ya watumiaji milioni 18 hasa wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2020.

Facebook imesisitiza kuwa tayari imefanya jitihada kubwa ili kuzuia jambo hilo lisitokee tena, lakini inahitaji kufanya jitihada zaidi.

Nadal kukosa fainali za ATP

0

Mchezaji tenisi Rafael Nadal atakosa fainali za ATP huko London nchini Uingereza kutokana na kuwa katika upasuaji wa kifundo cha mguu kinachomsumbua toka mwezi Oktoba mwaka huu.

Nadal alijiondoka mwezi huo wa Oktoba katika mashindano ya Paris Masters kutokana na kuwa majeruhi na nafasi yake ikachukuliwa na mchezaji namba moja kwa ubora duniani Novak Djokovic.

Mchezaji huyo wa tenisi mwenye umri wa miaka 32 amesema kuwa amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu na ameamua kutibiwa kwanza kwa kufanyiwa upasuaji.

Baada ya kujitoa kwa mchezaji huyo, nafasi yake sasa imechukuliwa na mchezaji John Isner .

Van Der Vaart atangaza kustaafu soka

0

Kiungo Rafael Van Der Vaart aliyewahi kuchezea vilabu vya Tottenham na Real Madrid ametangaza kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 35.

Vaart ambaye ni Mholanzi, aliichezea timu yake ya taifa katika fainali za kombe la dunia mwaka 2010 na amedumu katika soka kwa muda wa miaka 18 akianza kuchezea timu ya Ajax.

Vaart amesema kuwa haikuwa kazi rahisi kutangaza kuachana na soka kwa kuwa anaipenda zaidi .

Mchezaji huyo alijiunga na timu ya Real Madrid mwaka 2008, kisha akaondoka na kujiunga na klabu ya Spurs akiichezea kwa muda wa miaka miwili ambako alicheza mara 67 na kufunga magoli 24 na kisha akajiunga na Hamburg mwaka 2012