Rais Magufuli akutana na madaktari wa moyo wa Israel

0

Uamuzi wa serikali wa kufungua ubalozi wa Tanzania nchini Israel umeanza kuzaa matunda, baada ya timu ya madaktari na wataalamu wa matibabu ya moyo 30 kutoka nchini Israel kuja nchini kwa lengo la kuokoa maisha ya watoto 51 wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es salaam.

Timu ya madaktari na wataalamu hao wakiwemo wawili kutoka nchi za Marekani na Canada ambao wanatoka shirika la Save a Child’s Heart la nchini Israel, wamekutana na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Profesa Mohamed Janabi ambaye amesema kuwa kati ya watoto 51 wanaopatiwa matibabu katika kampeni maalum, kumi watafanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na ishirini watafanyiwa upasuaji kwa kutumia tundu dogo.

Profesa Janabi amefafanua kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, JKCI imetoa matibabu ya moyo kwa wagonjwa 254,881 ambapo kati yake 799 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua, 2,056 wamefanyiwa upasuaji kwa kutumia tundu dogo na wengine wamepatiwa matibabu mengine ya moyo.

Ameongeza kuwa ushirikiano wa JKCI na wataalamu kutoka nje ya nchi umesaidia kuwawezesha wataalamu wa Tanzania kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na pia kuokoa gharama kubwa zilizokuwa zikitumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi, ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu Tanzania imetumia shilingi bilioni 22 ikilinganishwa na shilingi bilioni 87.8 ambazo zingetumika kutoa matibabu hayo nje ya nchi.

Wakizungumza wakati wa mkutano huo, viongozi wa timu hiyo ya madaktari na wataalamu wa matibabu ya moyo kutoka nchini Israel wamemshukuru Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa ambao wameupata kutoka serikali na wameahidi kuendelea kushirikiana na serikali ili kuokoa maisha ya watoto.

Kwa upande wake Rais Magufuli amewashukuru madaktari na wataalamu hao kwa kuja nchini kuokoa maisha ya watoto na pia amemshukuru Waziri Mkuu wa Israel, – Benjamin Netanyahu kwa kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Israel.

Rais Magufuli amemuandikia barua ya shukrani Waziri Mkuu Netanyahu na kuikabidhi kwa balozi wa Israel nchini Noah Gal Gendler ambapo pamoja na kushukuru kwa msaada wa matibabu pia amemshukuru kwa ushirikiano katika sekta nyingine.

“Israel ni marafiki zetu wa siku nyingi, tunasaidiana na kushirikiana kwa mengi, ndio maana niliona tufungue ubalozi wetu kule Israel ili kurahisha masuala haya muhimu ya ushirikiano na yenye manufaa kwa watu wetu” amesisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amemuomba balozi huyo wa Israel nchini na wataalamu hao kuwahamasisha wawekezaji wanaoweza kujenga viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini na kuwahakikishia kuwa serikali itanunua dawa na vifaa hivyo, na pia watakuwa na uhakika wa soko la Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Pia Rais Magufuli amewapongeza madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kuokoa maisha ya Watanzania na amewahakikishia kuwa serikali inatambua juhudi hizo na itaendelea kuwajengea mazingira bora ya kazi.

Wakati huohuo, Rais Magufuli amefanya mazungumzo na balozi wa Israel nchini Noah Gal Gendler na baada ya mazungumzo hayo Gendler amesema kuwa Israel imetoa nafasi za masomo kwa Watanzania 150 watakaogharamiwa na serikali ya Israel kwa ajili ya kujifunza utaalamu wa kilimo cha kisasa kwa muda wa miezi 11.

Hati za kusafiria za wanaharakati wa kigeni zashikiliwa

0

Idara ya Uhamiaji nchini imekiri kushikilia hati za kusafiria za Wanaharakati wawili wa Kamati Maalum ya Kuwalinda Waandishi wa Habari Dunini (CPJ) ambao waliingia nchini kwa lengo la kukutana na taasisi mbalimbali za habari ili kufahamu kiwango cha uhuru wa vyombo vya habari.

Akizungumza kwa njia ya simu na TBC, msemaji wa Idara ya Uhamiaji nchini Ally Mtanda amesema kuwa wanaharakati hao ni Angela Quintal ambaye ni raia wa Afrika Kusini na Muthoki Mumo ambaye ni raia wa Kenya.

Mtanda ameiambia TBC kuwa Wanaharakati hao wa Kamati Maalum ya Kuwalinda Waandishi wa Habari Dunini wamehojiwa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa saa kadhaa kabla ya kuachiliwa.

Kwa mujibu wa Mtanda, wanaharakati hao watakabidhiwa hati zao za kusafiria wakati wowote, pindi uchunguzi utakapokamilika.

Waraka kwa waliohamishiwa Dodoma watolewa

0

Serikali imetoa waraka kuzuia watumishi wa umma waliohamishiwa Dodoma wakitokea Dar es salaam kurejea Dar es salaam mpaka watumishi hao waishi mkoani Dodoma kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma  Dkt Laurean Ndumbaro na kuongeza kuwa, waraka huo umetolewa kufuatia ofisi hiyo kupokea barua zisizopungua mbili kila siku kutoka kwa watumishi waliohamishiwa Dodoma wakitokea Dar es salaam kuomba kurejea jijini Dar es salaam.

Dkt Ndumbaro ametaja baadhi ya sababu ambazo zimekuwa zikitolewa na watumishi wanaoomba kurejea jijini  Dar es salaam kuwa ni kufuata matibabu.

Katibu Mkuu huyo wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma amewahakikishia wafanyakazi wote waliopo mkoani Dodoma kuwa, mkoa huo una hospitali ya Benjamini Mkapa inayoweza kutoa huduma zote kibingwa.

Tanzania na Kuwait kuimarisha ushirikiano

0

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumza na Balozi mpya wa Kuwait nchini Mubarak Mohammed Faleh Alsehaijan.

Balozi Alsehaijan alifika ofisini kwa Makamu wa Rais jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha.

Wakati wa mazungumzo yao, viongozi hao wamesisitiza kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Kuwait kwa manufaa ya nchi zote mbili na watu wake.

Waliotekwa Cameroon waachiliwa

0

Waasi nchini Cameroon wameliachia kundi la wanafunzi 74 waliowatekwa wakiwa shuleni Novemba tano mwaka huu.

Mbali na wanafunzi hao, watu wengine waliotekwa na waasi hao ni walimu kadhaa waliokuwa wakiwafundisha wanafunzi hao pamoja na dereva wa basi la shule.

Kasisi mmoja wa kanisa Katoliki nchini Cameroon aliyekuwa akisimamia mazungumzo kati ya waasi hao na serikali, mazungumzo yaliyosaidia kuchiliwa kwa wanafunzi hao amesema kuwa bado waasi hao wanamshikilia mkuu wa shule na mwalimu mmoja wa shule ya sekondari wanaposoma wanafunzi hao.

Ulipo mwili wa Kashoggi bado kitendawili

0

Zikiwa zimepita siku kadhaa tangu kuuawa kwa mwandishi wa habari wa Saudi Arabia katika mazingira ya kutatanisha ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul,- Uturuki, bado mwili wake haujulikani ulipo.

Licha ya serikali ya Saudi Arabia kukiri kuwa mwandishi huyo wa habari aliuawa ndani ya ubalozi huo na kisha mwili wake kukatwa vipande vipande, imeshindwa kuthibitisha mahali mwili wake ulipo.

Saudi Arabia imesema kuwa ipo tayari kuilipa fidia familia ya Kashoggi pamoja na mchumba wake aliyekuwa akitarajia kumuoa hivi karibuni, fidia kutokana na kifo hicho.

Stars mazoezini AfrikaKusini

0

Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) inaanza mazoezi leo Novemba saba kwenye kambi yake iliyoweka huko mjini Bloomfontein nchini Afrika Kusini ikiwa ni sehemu ya kujiwinda na mchezo wa kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya wenyeji Lesotho.

Kikosi cha Stars kiliwasili nchini Afrika Kusini Novemba sita mwaka huu kikiwa na wachezaji wanaocheza soka hapa nchini ambao wataanza mazoezi kabla ya kuungana na wale wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi katika kambi hiyo ya Afrika Kusini.

Taifa Stars watakuwa wageni wa Mamba wa Lesotho Novemba 18 mwaka huu katika uwanja wa Setsoto mjini Maseru kwenye mchezo muhimu wa Kundi L ambapo inahitaji ushindi ili kufuzu kwa fainali za AFCON kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 38.

Liverpool yapata kichapo

0

Timu ya Liverpool imepata kichapo cha tatu mfululizo kwa mara ya kwanza katika historia yake kwenye michezo ya ugenini ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya baada ya kunyukwa mabao mawili kwa nunge na Red Star Belgrade kwenye mchezo wa kundi C.

Msimu uliopita Liverpool ilinyukwa mabao manne kwa mawili na AS Roma kwenye mchezo wa pili wa nusu fainali ya ligi hiyo ambapo pamoja na kufungwa, ilitinga fainali kwa faida ya ushindi wa mabao matano kwa nunge ilioupata kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Msimu huu wameuanza kwa kichapo kwenye mchezo wa ugenini walipokubali kipigo cha bao moja kwa sifuri jijini Naples walipocheza na Napoli huku mchezo wa tatu ukiwa ni wa usiku wa kuamkia leo Novemba saba waliopoteza mbele ya Red Star Belgrade ya Serbia.

Mabao mawili ya mshambuliaji Milan Pavkov wa Red Star katika dakika za 22 na 29 yamewazamisha majogoo hao wa jiji na kulifanya kundi lao la C kuwa wazi kwa kila timu kusonga hatua ya mtoano baada ya Napoli na PSG kutoshana nguvu.

Napoli wao wakiwa nyumbani kwenye dimba la San Paolo walilazimika kutoka nyuma ili kusawazisha bao la Juan Bernet wa Paris Saint Germain aliyefunga katika dakika ya 45 huku Lorenzo Insigne akiisawazishia Napoli kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 63.

Katika matokeo ya michezo mingine iliyochezwa Novemba sita, Monaco imeendelea kupepesuka msimu huu licha ya kuwa na kocha mpya, ambapo katika mchezo wao dhidi ya Club Brugge ya Ubelgiji wameambulia kichapo cha mabao manne kwa nunge na kuwafanya waendelee kuburuza mkia kwenye kundi A wakiwa na alama moja kwenye michezo minne iliyocheza.

Nao Atletico Madrid wamewabugiza Borussia Dortmund mabao mawili kwa nunge ambapo timu hiyo inafikisha alama tisa sawa na Dortmund na hivyo ushindi huo wa Atletico unaiondoa rasmi Monaco kwenye ligi ya mabingwa msimu huu.

Kwingineko kwenye kundi B, FC Barcelona imejihakikishia kusonga mbele kwa hatua ya mtoano baada ya kulazimisha sare ya kufungana bao moja kwa moja na Inter Milan ya Italia.

Barcelona imefikisha alama 10 ambazo zinaweza kufikiwa na Inter Milan yenye alama saba na Tottenham Hotspur yenye alama nne ambapo miamba hiyo ya Hispania imebakiza michezo miwili dhidi ya PSV Eindhoven na mwingine ni dhidi ya Tottenham.

Katika kundi D, FC Porto imeinyuka Locomotiv Moscow mabao manne kwa moja huku Schalke 04 ikiibugiza Galatasaray mabao mawili kwa bila.

Leo Novemba saba, inapigwa michezo mingine nane ya makundi E mpaka H, ambapo kwenye kundi E Bayern wenye alama saba wanawaalika vibonde wa kundi lao AEK Athens na Benfica wanakipiga na Ajax.

Olympique Lyon ya Ufaransa inakipiga na TSG Hoffenheim ya Ujerumani huku Manchester City ikiialika Shakhtar Donetsk katika michezo ya kundi F huku CSKA Moscow watapepetana na AS Roma wakati Viktoria Plzen wakiwaalika mabingwa watetezi Real Madrid kwenye michezo ya kundi G.

Na Valencia wanapepetana na Young Boys huku kibibi kizee cha Turin, Juvetus wakiwa wenyeji wa mashetani wekundu kwenye michezo ya kundi H.