Walionusurika kwenye vita Ivory Coast wadai fidia

0

Baadhi ya watu walionusurika kufa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory Coast, vita iliyosababisha Rais Laurent Gbagbo kuondoka madarakani, wanaitaka serikali ya nchi hiyo iwalipe fidia.

Watu hao wamefikisha shauri lao mahakamani na kusema kuwa wanatamani kuona wahusika na mauaji hayo pamoja na vitendo vingine vya ukatili wakati wa miaka saba ya vita hiyo wanachukuliwa hatua za kisheria.

Wamesema kuwa wanapatwa na hasira wanapowaona wahalifu wa vita hiyo wakiendelea kuishi kwa amani bila ya kuchukuliwa hatua yoyote.

Vita hiyo ilizuka kati ya askari waliokuwa wakimtii rais wa zamani wa nchi hiyo Laurent Gbagbo dhidi ya wafuasi wa Alassane Dramane Ouattara ambaye alitangazwa mshindi wa kiti cha Urais.

Takribani watu elfu tatu waliuawa wakati wa vita hiyo.

Moto waendelea kuitesa California

0

Uongozi wa jimbo la California nchini Marekani umethibitisha kuwa idadi ya watu waliokufa kutokana na moto wa msituni imefikia 31 huku wengine zaidi ya mia mbili wakiwa hawajulikani walipo.

Maelfu ya watu katika jimbo hilo la California wamelazimika kuyakimbia makazi yao baada ya nyumba nyingi kuteketea kwa moto huo.

Habari zaidi kutoka katika jimbo hilo zinasema kuwa baadhi ya watu waliokufa, wamekufa wakiwa ndani ya magari yao walipokuwa wakijaribu kuukimbia moto huo.

Vikosi vya zimamoto katika jimbo la California vimesema kuwa kazi ya kuuzima moto huo wa msituni ni ngumu na haijawahi kutokea katika historia ya jimbo hilo.

Wamesema kuwa inaweza ikachukua muda wa wiki nzima ili kuweza kuuzima moto huo ambao unaendelea kuathiri uoto wa asili pamoja na makazi ya watu.

Upepo mkali na ukame vimetajwa kuwa ni moja kati ya vitu vinavyochochea moto huo wa msituni katika jimbo la California.

Kambi ya Stars yaongeza nguvu

0

Wachezaji watu wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, wameshajiunga na kambi ya timu ya taifa ya soka ya Tanzania – Taifa Stars iliyoko nchini Afrika Kusini.

Wachezaji walioripoti kambini ni walinzi Abdi Banda anayecheza soka kwenye timu ya Baroka FC ya nchini Afrika Kusini, Hassan Kessy anayecheza soka nchini Zambia kwenye timu ya Nkana Ranger pamoja na mshambuliaji Rashid Mandawa anayecheza soka nchini Botswana.

Wachezaji wengine wanaocheza soka nje ya nchi wanaotarajiwa kujiunga na kambi hiyo ni nahodha Mbwana Samatta wa Genk ya Ubelgiji, nahodha msaidizi Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva anayecheza soka nchini Morocco kwenye timu ya Hassan Difa El Jajida na mshambuliaji Shaaban Idd Chilunda anayecheza soka nchini Hispania kwenye timu ya Tenlif.

Hii ni wiki ya pili tangu Stars iweke kambi nchini Afrika kusini kwenye mji wa Bloemfontein uliopo kwenye jimbo la Free State kwa lengo la kujiandaa na mchezo muhimu wa kufuzu kwa michuano ya Afrika (AFCON) dhidi ya Lesotho.

Mchezo huo utachezwa jumapili ijayo kwenye mji mkuu wa Lesotho, – Maseru ambapo Taifa Stars inatakiwa kushinda mchezo huo ili kufuzu kwa mara ya pili kwenye michuano hiyo ya mataifa ya Afrika.

Manchester City mbabe kwa Man U

0

Manchester City imeibuka kidedea mbele ya wapinzani wao wa mji mmoja Manchester United kwa mabao matatu kwa moja kwenye mchezo wa ligi kuu ya England.

Magoli ya Manchester City yametiwa kimiani na David Silva, Sergio Kun Aguero na Iga Gundogan na lile ya kufutia machozi la Manchester United limefungwa na Anthon Martial.

Katika michezo mingine, Liverpool imepata ushindi wa mabao mawili kwa bila dhidi ya Fulham huku Chelsea ikitoka sare ya bila kufungana na Everton.

Arsenal yenyewe imetoka sare ya bao moja kwa moja na Wolverhampton Wanderers.

Serikali kununua korosho kwa sh 3,300

0

Rais John Magufuli ametangaza kuwa, serikali itanunua korosho za wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara kwa shilingi elfu 3, 300 kwa kilo muda wowote kuanzia hivi sasa.
Rais Magufuli ametoa tangazo hilo Ikulu Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kuwaapisha Mawaziri wawili na Naibu Mawaziri wanne aliowateua hivi karibuni.

Akitoa tangazo hilo, Rais Magufuli amesema kuwa serikali imeachana na kampuni 13 ambazo zimejitokeza hadi asubuhi ya leo kuonyesha nia ya kununua korosho hizo baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Rais Magufuli amesema kuwa serikali imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa, kampuni hizo hazina nia njema na wakulima wa zao hilo la korosho la lengo lao ni kuendelea kuwanyonya.

Amewataka viongozi hao aliowaapisha hii leo ambao ni pamoja na wa wizara nyeti za Kilimo na Viwanda, Bishara na Uwekezaji kufanya jitihada za kutafuta soko la korosho kwa kuwa kwa sasa jitihada hazijafanyika ipasavyo.

Pia ametumia hafla hiyo kuiagiza wizara inayohusika na Benki ya Maendeleo ya Kilimo kumthibitisha kwenye nafasi ya Ukurugenzi aliyekua akikaimu nafasi hiyo.

Awali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alieleza kuwa hadi kufikia asubuhi ya leo, kampuni 13 zimejitokeza zikithibitisha kuwa zitanunua korosho kwa bei elekezi iliyotolewa na serikali baada ya kuwapatia muda wa siku nne kuthibitisha jambo hilo.

Waziri Mkuu pia amewataka viongozi wote walioapishwa, kujifunza kwa haraka majukumu yao na kutekeleza majukumu hayo kwa uadilifu na nidhamu

Serikali yatoa tamko kuhusu korosho

0

Serikali imetoa siku nne kwa wanunuzi wote 35 waliojiandikisha kununua korosho kupeleka barua katika Ofisi ya Waziri Mkuu wakionesha  kiasi cha tani wanazohitaji na lini watazichukua.

Akitoa tamko la serikali kuhusu ununuzi wa zao la korosho mjini Dodoma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema wanunuzi waliojiandikisha wakiwemo wale wote ambao wamekuwa wananunua kwenye minada lakini kwa kiasi kidogo, wahakikishe ndani ya siku hizo nne kuanzia leo Ijumaa hadi Jumatatu saa 10 alasiri wanawasilisha barua zao.

Amesema baada ya siku hizo kupita serikali italazimika kufuta usajili kwa wote waliojisajili kununua zao hilo kwa sababu walikubaliana kwenda kununua.

Makamu wa Rais ziarani Kilimanjaro

0

Makamu wa Rais Samia Hassan Suluhu leo anaanza ziara ya siku tano mkoani Kilimanjaro.

Akiwa mkoani humo pamoja na mambo mengine, Makamu wa Rais atatembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri zote za mkoa huo.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, – Anna Mghwira ametoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kujitokeza katika maeneo yote ambayo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan atayatembelea.

Wakulima wa korosho watakiwa kuwa wavumilivu

0

Serikali imewataka wakulima wa zao korosho nchini kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kuzungumza na wanunuzi wakubwa wa korosho kutoka maeneo mbalimbali duniani, lengo likiwa ni kupata soko la uhakika la zao hilo.

Kauli hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, ambapo Mbunge wa Mtwara Mjini, -Maftaha Nachuma alitaka kupata kauli ya serikali kuhusu bei ya korosho ambayo imeshuka katika msimu wa mwaka huu na kusababisha wakulima kugomea baadhi ya minada.

“Tunaendelea kuzungumza na wanunuzi wakubwa ili tujue ni nani atanunua korosho na kwa kiasi gani, hivyo tunawaomba wakulima waendelee kuwa watulivu, serikali inajitahidi kuhakikisha zao hilo linatafutiwa masoko, Korosho zitanunuliwa tu,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema kuwa serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya ujenzi wa viwanda vya mbolea.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum, Neema Mgaya aliyetaka kujua serikali ina mpango gani katika kuwahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza katika viwanda vya mbolea ili wakulima waweze kuipata kwa gharama nafuu.

Ameongeza kuwa viwanda vya mbolea vilivyopo nchini ni vichache na havitoshelezi mahitaji, hivyo kwa sasa kuna utaratibu wa kujenga viwanda vingine viwili, kimoja wilayani Kilwa mkoani Lindi na kingine kitajengwa mkoani Mtwara.

Kuhusu suala la wakulima wa mahindi kukosa soko, amesema kuwa ruhusa ya kuuza mahindi nje ya nchi ilishatolewa na jambo hilo lilikwishatolewa ufafanuzi na Wizara ya Kilimo.

Waziri Mkuu Majaliwa amefafanua kuwa licha ya kuwepo kwa ruhusa hiyo ya kuuza mahindi nje ya nchi, ni lazima serikali itambue kiasi gani kinachotolewa kwa ajili ya kuuza nje ya nchi, hivyo muuzaji anatakiwa awasisilishe taarifa zake kwa wakuu wa wilaya.