Watanzania watakiwa kudumisha maadili mema

0

Mufti wa Tanzania, – Sheikh Abubakar Zubeir amewataka waumini wa dini ya Kiislam nchini na Watanzania wote kudumisha maadili mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mufti amesema kuwa hakuna dini yoyote duniani inayoruhusu vitendo vya mmomonyoko wa maadili, hivyo ni vema jamii ikatenda matendo mema na kuwalea watoto katika maadili ya kupendeza.

Akizungumzia sherehe za Maulid za kuzaliwa kwa Mtume Muhammad, Mufti wa Tanzania amesema kuwa sherehe hizo kitaifa zitafanyika wilayani Korogwe mkoani Tanga Novemba 19 mwaka huu na Baraza la Maulid litasomwa tarehe ishirini mwezi huu.

Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir pia ametumia mkutano wake na waandishi wa habari, kuzungumzia maadhimisho ya miaka hamsini ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), maadhimisho yatakayofikia kilele chake Disemba 17 mwaka huu na kuwataka waumini wa dini ya kiislam nchini kujitokeza na kushiriki katika maadhimisho hayo.

Mchezo kati ya Kenya na Sierra Leone wafutwa

0

Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limethibitisha kufutwa kwa mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwaka 2019 nchini Cameroon, kati ya Kenya na Sierra Leone.

CAF imesema kuwa mchezo huo wa kundi F uliokuwa uchezwe Jumapili ya wiki hii jijini Nairobi, umefutiliwa mbali kutokana na Sierra Leone kuendelea kutumikia adhabu ya kufungiwa kwa muda usiojulikana na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Tayari CAF imeviandikia barua vyama vya soka vya nchi zote mbili kuviarifu juu ya mchezo huo kufutwa ikiwa ni maagizo kutoka FIFA ambayo ndiyo mamlaka ya juu zaidi ya soka duniani.

Mwezi oktoba mwaka huu, bodi ya CAF ilifuta michezo miwili kati ya Sierra Leone na Ghana iliyokuwa ichezwe nyumbani na ugenini na kuondoa kabisa uwezekano wa mechi hizo kuchezwa hata kama adhabu ya Sierra Leone itaondolewa.

Hata hivyo CAF bado haijaweka wazi nini kitaendelea baada ya kufutwa kwa mchezo huo na kwa kiasi gani utaathiri kampeni za mataifa husika katika kundi hilo kwenye kufuzu kwa michuano ya AFCON.

Mpaka sasa Kenya wanaongoza kundi F wakiwa na alama saba wakati Ghana, Ethiopia na Sierra Leone kila mmoja wakiwa na alama moja.

 

Michuano ya Challenge kutofanyika mwaka huu

0

Baraza la Vyama Vya Soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limethibitisha kutofanyika kwa michuano ya kombe la Challenge kwa mataifa wanachama kwa mwaka 2018 kutokana na sababu zilizo nje ya baraza hilo.

Katibu Mkuu wa CECAFA, – Nicholas Musonye amesema kuwa wamefanya kila linalowezekana kupata nchi muandaaji baada ya Kenya kujitoa bila mafanikio.

Kenya walipewa uenyeji wa michuano hiyo kwa mara ya pili baada ya mwaka 2017 kuifunga Zanzibar kwa changamoto ya mikwaju ya penati kwenye mchezo wa fainali na kunyakua taji hilo.

Musonye ameongeza kuwa wamejaribu kutafuta nchi mbadala ya kuandaa bila mafanikio, lakini muda pia umekuwa finyu kutokana na ratiba ya mashindano ya vilabu Barani Afrika ambapo sasa itaanza mwezi Novemba hadi Disemba mwaka huu kwenye hatua za awali.

Katika hatua nyingine, Musonye amethibitisha kufanyika kwa mashindano ya CECAFA kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka ishirini kuanzia Disemba 15 hadi 23 nchini Uganda.

 

Kamata kamata yaendelea Ethiopia

0

Ethiopia imewakamata zaidi ya watu sitini kwa tuhuma za ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu, wakiwemo maafisa wa upelelezi, askari na wafanyabiashara.

Watu hao wamekamatwa kufuatia amri iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, – Abiy Ahmed na wamekamatwa baada ya kufanyika kwa uchunguzi uliodumu kwa miezi kadhaa kuhusu makosa mbalimbali yaliyotokea chini ya utawala wa watangulizi wake.

Ofisi ya mwendesha mashtaka nchini Ethiopia imesema kuwa baadhi ya watu waliokamatwa wanashutumiwa kuwatesa wafungwa huku wakiwalazimisha kukiri makosa yao, kuwadhalilisha watu, kuwatesa watuhumiwa wa uhalifu kwa kutumia nyaya za umeme na hata kuwaua.

Tangu alipoingia madarakani mwezi Aprili mwaka huu, Abiy amewaachilia huru maelfu ya wafungwa na kufanya mageuzi mengine makubwa ya kisiasa nchini Ethiopia.

 

Tshisekedi na Kamerhe wabatilisha uamuzi

0

Viongozi wawili wa vyama vya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wamejitoa katika makubaliano ya kumuunga mkono mgombea mmoja wa upinzani, makubaliano yaliyofikiwa mjini Geneva, – Uswisi Jumapili iliyopita.

Felix Tshisekedi kutoka Chama Cha UDPS na Vital Kamarhe kutoka UNC walikuwa ni miongoni mwa viongozi wa upinzani waliotia saini makubaliano ya kumuunga mkono Martin Fayulu kuwa mgombea wa pamoja wa upinzani katika uchaguzi wa urais utakaofanyika Disemba 23 mwaka huu katika Jamhuri hiyo ya Kidemokrasi ya Kongo.

Wafuasi wa upinzani katika Jamhuri hiyo wameandamana katika mitaa mbalimbali ya mji mkuu wa Kinshasa kupiga hatua ya viongzoi hao wawili kujiondoa kwenye makubaliano hayo.

Awali wafuasi hao waliamini kuwa makubaliano hayo ya kumuunga mkono mgombea mmoja wa upinzani, yangeweza kuusaidia upinzani chini ya mgombea wao Fayulu kuchuana vikali na Emmanuel Ramazani Shadary, mgombea anayeungwa mkono na Rais Joseph Kabila.

Taarifa iliyotolewa na Chama Cha UDPS imesema kuwa Tshisekedi ameondoa saini yake kwenye makubaliano ya Geneva kufuatia shinikizo la wanachama wa chama hicho, uamuzi uliotangazwa na Kamerhe baada ya saa chache.

Mapigano makali yaendelea Gaza

0

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kusitishwa kwa mapigano yanayoendelea kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo wa Hamas wa Palestina katika ukanda wa Gaza.

Umoja huo umesema kuwa mapigano kati ya pande hizo mbili ni makali zaidi kuwahi kutokea katika eneo hilo tangu mwaka 2014.

Mapigano hayo kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo wa Hamas yamezuka baada ya Wanamgambo hao kurusha makombora 370 ndani ya Israel na hivyo kuifanya nchi hiyo kulipiza kisasi kwa kufanya mashambulio ya anga.

Kwa sasa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika ukanda huo wa Gaza, – Nickolay Mladenov anashirikiana na Misri pamoja na pande zote zinazohusika katika mapigano hayo kwa lengo la kurejesha hali ya utulivu.

Hapo jana, ndege za Israel ziliyashambulia maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu na kuharibu kituo cha televisheni kinachomilikiwa na wanamgambo wa Hamas na kuwaua raia watatu wa Palestina.

Habari zaidi kutoka eneo hilo zinasema kuwa kumekua na mapigano usiku wote wa kuamkia hii leo.

Wimbo wa Mwanza wapigwa stop na BASATA

0

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA ) limeufungia rasmi wimbo unaojulikana kama Mwanza ulioimbwa na msanii wa lebo ya Wasafi, -Raymond Mwakyusa maarufu kama Rayvanny na kumshirikisha mwanamuziki mwenzake Naseen Abdul maarufu kama Diamond Platinumz.

Katibu Mtendaji wa BASATA, – Geofrey Mngereza amesema kuwa wameamua kuufungia wimbo huo kutokana na ukiukaji wa maadili ya Kitanzania kwa msanii Rayvanny ambaye ametumia maneno ya udhalilishaji.

Pamoja na kuufungia wimbo huo, BASATA pia imewataka wasanii, vyombo vya habari na mtu yoyote kutoutumia, kutoucheza ama kuusambaza kwa namna yoyote ile.

BASATA imewataka msanii Rayvanny, Diamond pamoja na uongozi wa kampuni ya Wasafi Limited kufuata sheria, kanuni na taratibu wakati wa kuandaa kazi za sanaa.

Kampuni hiyo ya Wasafi imeagizwa kuuondoa wimbo huo kwenye mitandao ya kijamii mara moja kabla ya saa 12 kamili jioni Novemba 12 mwaka huu.

Umoja wa Mataifa kuchunguza umaskini Uingereza

0

Baadhi ya watu walionusurika kufa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory Coast, vita iliyosababisha Rais Laurent Gbagbo kuondoka madarakani, wanaitaka serikali ya nchi hiyo iwalipe fidia.

Watu hao wamefikisha shauri lao mahakamani na kusema kuwa wanatamani kuona wahusika na mauaji hayo pamoja na vitendo vingine vya ukatili wakati wa miaka saba ya vita hiyo wanachukuliwa hatua za kisheria.

Wamesema kuwa wanapatwa na hasira wanapowaona wahalifu wa vita hiyo wakiendelea kuishi kwa amani bila ya kuchukuliwa hatua yoyote.

Vita hiyo ilizuka kati ya askari waliokuwa wakimtii rais wa zamani wa nchi hiyo Laurent Gbagbo dhidi ya wafuasi wa Alassane Dramane Ouattara ambaye alitangazwa mshindi wa kiti cha Urais.

Takribani watu elfu tatu waliuawa wakati wa vita hiyo.