Watendaji wa serikali wapatiwa mafunzo kuhusu tafiti

0

Mkurugenzi  Mtendaji  wa Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa Umaskini Nchini (REPOA) Dkt Donard Mmary amesema  kuwa matokeo ya utafiti ndio yanayoweza kusaidia kuandaa sera na mipango ya kuleta maendeleo kwa  haraka kwa wananchi  na Taifa ikiwemo  kufikia   uchumi  wa  viwanda.

Dkt Mmary  ametoa kauli hiyo mjini Morogoro mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tano, yanayoshirikisha watendaji wa ngazi  ya kati wa serikali  wanaohusika na mipango pamoja na sera.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo washiriki wa namna ya kutumia matokeo ya tafiti  mbalimbali zinazofanywa na wataalamu wa kiuchumi ili kuharakisha maendeleo ya Taifa.

Dkt Mmari ameongeza kuwa kwa sasa tafiti nyingi zinazofanywa na wataalamu wa kiuchumi wazawa zimekuwa na faida kubwa kwa kuwa zimekua zikitumika katika kuharakisha maendeleo .

Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wanolewa

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefungua mafunzo yanayoshirikisha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini na kusema kuwa serikali inatarajia viongozi hao watasimamia nidhamu katika utumishi wa umma na wao wenyewe watakuwa kioo cha utumishi wa umma mara baada ya mafunzo hayo.

Akizungumza na viongozi hao mara baada ya kufungua mafunzo hayo jijini Dodoma, mafunzo yanayoendeshwa na Taasisi ya Uongozi nchini, Waziri Mkuu Majaliwa amewaagiza Wakuu hao wa mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini kuzingatia mipaka ya madaraka yao na kwamba hatua watakazozichukua katika uongozi na utendaji wao zizingatie sheria, kanuni na taratibu za nchi.

“Mkadumishe uhusiano mwema baina yenu na watumishi walio chini yenu, kwa kuzingatia kuwa kila mtumishi ana mchango katika kuboresha utendaji kwenye kituo chake cha kazi, nina matarajio makubwa kuwa mtadumisha uhusiano mzuri kikazi na viongozi wa juu na pia uhusiano wa diplomasia ya heshima na viongozi wengine ndani ya mihimili yetu mitatu”, amesisitiza Waziri Mkuu.

Pia amewaagiza kusimamia suala la amani na utulivu kwenye mikoa yao ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote, kwa kuwa amani na utulivu ndiyo itaiwezesha nchi iendelee kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Nchini, Profesa Joseph Semboja amesema  kuwa mafunzo hayo ya wiki moja yanazingatia maeneo makuu matatu ambayo ni pamoja na kuimarisha uwezo wa washiriki katika kufanya maamuzi ya kimkakati yanayozingatia mahitaji na manufaa mapana ya sasa na ya baadae kwa jamii.

Fury alalamikia maamuzi mabovu

0

Bondia Tyson Fury wa nchini Uingereza amesema kuwa dunia inatambua bingwa wa dunia wa uzito wa juu (WBC) ni nani, na anaamini sare aliyoipata Deontay Wilder wa Marekani dhidi yake ilikuwa ni maamuzi ya zawadi kwa Mmarekani huyo.

Fury mwenye umri wa miaka 30 alitoka sare kwenye pambano la kuwania ubingwa wa WBC kati yake na Wilder ingawa mabondia wengi wa Kimataifa wanasema kuwa Fury alishinda katika mpambano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Stapeles mjini Los Angeles, – Califoirnia.

Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya pambano hilo,  Fury amesema kuwa hajawahi kushuhudia maamuzi mabovu ya mchezo wa masumbwi katika maisha yake kama maamuzi yaliyotelewa kwenye mpambano huo na kuongeza kuwa hajui majaji walikuwa wakiangalia pambano la aina gani.

Mabingwa wa zamani wa dunia akiwemo Floyd Mayweather, Lennox Lewis, Tony Bellew na Carl Froch wanaamini kuwa Fury alishinda pambano hilo ambalo baada ya raundi ya 12 majaji waliamua limalizike kwa sare.

Jaji wa kwanza alimpa Wilder ushindi wa alama115 kwa 111 huku jaji wa pili akimpa ushindi wa alama 114 kwa 112 na  jaji wa tatu akatoa alama 113 kwa kila mmoja.

Hata hivyo, muandaaji wa pambano hilo Frank Warren amesema kuwa yeye pamoja na bodi ya usimamiaji wa mchezo wa masumbwi nchini Uingereza wataandika barua kwa WCB kuomba mtanange huo urudiwe.

 

Mshindi Ballon D’or kutangazwa leo

0

Mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka 2018 ya Ballon D’or atatangazwa baadaye hii leo katika hafla itakayofanyika jijini Paris nchini Ufaransa.

Nahodha wa timu ya Taifa ya  Croatia anayechezea Real Madrid, – Luka Modric anapigiwa chapuo kubwa ya kutwaa tuzo hiyo na kumaliza utawala wa nyota wawili Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ambao wamekuwa wakipokezana tuzo hiyo kwa kipindi cha miaka kumi mfululizo.

Nahodha wa FC Barcelona, – Lionel Messi na mshambuliaji wa Juventus, – Cristiano Ronaldo wameshinda tuzo hiyo katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kila mmoja akishinda mara tano ambapo mchezaji wa mwisho kushinda tuzo hiyo kando ya wawili hao alikuwa Ricardo Kaka aliyeshinda tuzo hiyo mwaka 2007 akiitumikia AC Milan ya Italia.

Hata hivyo,  Luka Modric anapewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo hiyo baada ya mwezi Septemba mwaka huu kushinda tuzo ya mchezaji bora wa kiume wa FIFA, tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya na tuzo ya mchezaji bora wa fainali za kombe la FIFA la dunia zilizofanyika mwezi Juni hadi Julai mwaka huu nchini Russia.

Tangu mwaka 1956 , Jarida la France Football limekuwa likitoa tuzo hiyo yenye thamani kubwa zaidi duniani kwa mchezaji bora wa kiume kila mwaka na mwaka huu wameongeza tuzo kwa upande wa mchezaji bora wa kike na mchezaji bora kijana.

Shabiki wa Spurs mbaroni kwa ubaguzi

0

Shabiki mmoja wa Tottenham Hotspurs ametiwa mbaroni kwa kitendo cha kumrushia ganda la ndizi mshambuliaji wa Arsenal, -Pierre-Emerick Aubameyang wakati akishangilia bao la kwanza kwenye mchezo uliowakautanisha mahasimu hao wa Kaskazini mwa jiji la London.

Picha kutoka kwenye dimba la Emirates zinaonesha ganda la ndizi likiwa kwenye uwanja,  eneo alilosimama Aubameyang baada ya mshambuliaji huyo kwenda kushangilia bao lake la mkwaju wa penati katika dakika ya kumi mbele ya mashabiki wa Spurs.

Chama cha Soka cha England (FA) kimesema kuwa kinachunguza tukio hilo hata kama halikujumuishwa kwenye ripoti ya mwamuzi wa mchezo huo Mike Dean na polisi wa Metropolitan wamesema kuwa walimkamata shabiki huyo usiku wa Disemba pili kwa kufanya kitendo hicho ambacho hakikuabliki.

Kwa upande wao Spurs kupitia kwa msemaji wao wamesema kuwa kitendo alichofanya shabiki huyo kamwe hakikubaliki,  hivyo watamfungia shabiki huyo kutokana na vitendo hivyo vya kibaguzi na kwamba klabu hiyo haitamvumilia shabiki yoyote atakayefanya vitendo visivyokubalika kwenya mchezo wa soka.

Wakati huo huo mashabiki wengine sita wametiwa mbaroni wakiwemo wawili wa Arsenal,  kwa kosa la kuwasha miale ya moto iliyoambatana na moshi mzito baada ya timu yao kutoka nyuma kwa mabao mawili na kuibuka na ushindi wa mabao manne kwa mawili.

 

Buhari ajitokeza, asema atawania tena Urais

0

Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria amejitokeza hadharani na kukanusha uvumi kuwa amefariki dunia, uvumi uliokua ukienea katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwa miezi kadhaa sasa.

Buhari ambaye atakuwa anawania kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa Urais nchini Nigeria mwezi Februari mwaka 2019, alikuwa nchini  Uingereza kwa  muda mrefu akipatiwa matibabu ya maradhi ambayo hayajawekwa wazi.

Kumekuwa na uvumi kuwa Rais  Buhari amefariki dunia na nafasi yake imechukuliwa na mtu anayefanana naye, ambaye anatoka nchini Sudan.

Buhari amesisitiza kuwa anayeiongoza  Nigeria ni yeye na kwamba hivi karibuni atakuwa anaadhimisha mwaka wake wa 76 wa kuzaliwa.

Buyoya apinga waranti wa kukamatwa

0

Rais wa zamani wa Burundi, -Pierre Buyoya amepinga waranti wa kukamatwa kwake uliotolewa na serikali ya nchi hiyo kwa madai ya kuhusika katika mauaji ya rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa kidemokrasia, – Melchior Ndadaye na kusema kuwa hizo ni sababu za kisiasa.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Burundi ilitoa waranti wa kimataifa wa kukamatwa kwa Buyoya, maafisa wengine 11 wa zamani  wa nchi hiyo na raia  watano waliokuwa karibu naye kwa madai hayo ya kuhusika na  mauaji ya Ndadaye mwaka 1993.

Katika taarifa yake, Rais huyo wa zamani wa Burundi, – Pierre Buyoya  amesema kuwa ushahidi unaonyesha siasa ndizo zilizotumika katika kutoa waranti hiyo ili kuuficha mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo kwa sasa.

Kwa sasa Buyoya ni mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Mali na ni mtu anayeheshimika sana Barani Afrika pamoja na nchi nyingine nje ya bara hilo.

Buyoya anayetokea kabila la Watutsi aliingia madarakani mwaka 1987 kwa kusaidiwa na jeshi la Burundi na aliachia wadhifa huo baada ya Ndadaye ambaye ni Mhutu kuchukua madaraka mwaka 1993.

Hata hivyo, Ndadaye aliuawa miezi minne baadae katika jaribio la mapinduzi lililofanywa na Wanajeshi wa Kitutsi wenye itikadi kali.

 

Ubelgiji wataka ulinzi zaidi wa mazingira

0

Maelfu ya raia wa Ubelgiji wameandamana katika mitaa mbalimbali ya mji mkuu wa nchi hiyo Brussels wakitaka kuwekwa kwa mikakati zaidi ya kulinda mazingira.

Raia hao wameandamana wakati ambapo mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (COP 24) ukianza rasmi katika mji wa Katowice nchini Poland

Polisi nchini Ubelgiji wamesema kuwa karibu watu elfu 65 wameandamana mjini Brussels  wakiitaka serikali ya nchi hiyo na za nchi  nyingine za Ulaya kuweka hatua kali za kulinda utoaji wa gesi ya ukaa.

Wamesema kuwa ni kwa njia hiyo tu ulimwengu utaweza kupunguza kiwango cha joto duniani kwa Sentigredi 1.5 na kuyafikia malengo ya mkataba wa mazingira wa Paris wa mwaka 2015.

Maandamano kama hayo kuhusiana na masuala ya mazingira yamefanyika kwenye miji mingine ya nchi za Ulaya ikiwa ni pamoja na Berlin na Cologne nchini Ujerumani.