China kupiga stop harusi za kifahari

0

China ina mpango wa kudhibiti ongezeko la harusi za kifahari ambazo zimekuwa zikishamiri katika miaka ya hivi karibuni.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya China imesema kuwa harusi nyingi zinazofanyika nchini humo hivi sasa zimekua sio tu za gharama kubwa, bali pia zinaenda kinyume na misingi ya kijamaa ya nchi hiyo.

Habari zaidi kutoka nchini China zinasema kuwa, harusi zinazofanyika hivi sasa nchini humo zimekua zikifungwa kimila na kuambatana na sherehe kubwa ambazo serikali inadai kuwa zimekuwa zikifanyika kwa kutumia fedha nyingi.

Raia wengi wa China kama walivyo wa nchi nyingine duniani, wamekuwa wakishindana katika kuandaa sherehe kubwa za harusi.

Plate walalamikia mtanange kufanyika Santiago Bernabeu

0

Mtendaji Mkuu wa klabu ya River Plate, –  Marcelo Gallardo amesema  kuwa kitendo cha mchezo wa fainali ya pili ya michuano ya ligi ya mabingwa Barani Amerika ya Kusini baina yao na mahasimu wao wakubwa Bocca Juniors maarufu kama Copa Libertadores kuhamishiwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu jijini Madrid nchini Hispania ni ukatili kwa mashabiki wa klabu hiyo.

Mchezo wa fainali ya kwanza uliowakutanisha wababe hao wa soka la Argentina,  ulimalizika kwa sare ya mabao  mawili kwa mawili na mchezo wa marudiano uliahirishwa mara mbili baada ya mashabiki wa River Plate kuwashambulia wachezaji wa Bocca Juniors na kuwasababishia majeraha.

Akizungumza baada ya River Plate kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Gimnasia La Plata  kwenye mchezo wa ligi uliofanyika Jumatatu Disemba tatu, Gallardo amesema kuwa mchezo huo kuchezwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu sio uungwana kwani kunawanyima faida ya kucheza nyumbani na kamwe hawatasahau tukio hilo.

Katika mchezo huo wa marudiano utakaochezwa Jumapili Disemba Tisa, kila timu itapewa tiketi  Elfu 25 lakini tiketi Elfu Tano tu kati ya hizo ndio zitauzwa kwa mashabiki nchini Argentina ukiwa ni mpango wa kudhibiti vurugu zinazoweza kuandaliwa na mashabiki kutoka nchini humo.

Serikali ya Argentina imesema kuwa inashirikiana kwa karibu na serikali ya Hispania ili kuhakikisha hakuna uwezekano wa kutokea vurugu zozote kwenye mchezo huo.

Modric ashinda tuzo ya Ballon D’or

0

Luka Modric ameshinda tuzo ya Mwanasoka bora duniani ya Ballon D’or na kuwa mchezaji wa kwanza kushinda tuzo hiyo mbele ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Croatia ameshinda mataji matatu mfululizo ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya akiwa na klabu yake ya Real Madrid na kisha kuisaidia nchi yake kufika fainali ya kome la FIFA la dunia mwezi Julai mwaka huu huko Russia.

Mshambuliaji wa Juventus, – Cristiano Ronaldo ameshika nafasi ya pili huku nyota wa FC Barcelona, – Lionel Messi akishika nafasi ya tano nyuma ya nyota wa Atletico Madrid , – Antoine Griezmann na mshambuliaji kinda wa PSG, – Kylian Mbappe ambao kwa pamoja waliisaidia Ufaransa kunyakua ubingwa wa dunia.

Luka Modric amesema tuzo hiyo ni kwa ajili ya wachezaji wote waliostahili kushinda, lakini waliikosa katika kipindi cha miaka kumi iliyotawaliwa na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ambapo mchezaji wa mwisho kushinda tuzo hiyo kabla ya utawala wa wawili hao alikuwa mshambuliaji wa AC Milan, – Ricardo Kaka mwaka 2007.

Modric ameongeza kuwa inawezekana katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kuna baadhi ya wachezaji walistahili kushinda tuzo ya Ballon D’or akiwemo Xavi Hernandes, Andres Iniesta na Wesley Sneijder, lakini watu sasa wanamshuhudia mtu mwingine.

Kiungo huyo wa Real Madrid amesema kuwa ni vigumu kuelezea hisia alizonazo baada ya kushinda tuzo hiyo kwani ni kitu cha kipekee kwake huku akiwataja Ronaldo na Messi kama wachezaji wa kipekee na kwamba kushinda tuzo hiyo mbele yao kunaonesha alifanya jambo la maana uwanjani kwa mwaka huu.

Naye mshambuliaji wa Olympic Lyon na timu ya Taifa ya Norway, – Ada Hegerberg amekuwa mwanamke wa kwanza kushinda tuzo ya Ballon D’OR ambayo kwa mara ya kwanza imetolewa kwa wanawake huku Kylian Mbappe akiwa mchezaji wa kwanza kinda kushinda tuzo hiyo kwa wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 21, tuzo inayopigiwa kura na nyota waliowahi kushinda tuzo ya Ballon D’OR miaka iliyopita.

Mtihani wa kidato cha pili Zanzibar wafutwa

0

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imefuta mtihani wa kidato cha Pili ulioanza leo baada ya kubaini udanganyifu uliosababisha kuvuja kwa mitihani hiyo.

Waziri wa Elimu Zanzibar Riziki Pembe Juma amesema wizara imefikia uamuzi huo kufuatia taarifa za kuaminika za kuvujishwa kwa baadhi ya mitihani ya kidato cha Pili na tayari baadhi ya wahusika wameanza kushikiliwa na vyombo vya dola.

Amesema kutokana na udanganyifu huo serikali imeingia hasara ya zaidi ya shilingi milioni 250 na kwamba tarehe ya kufanyika tena kwa mtihani wa kidato cha Pili itatangazwa hapo baadae.

Wanawake wapatiwa mafunzo ya ujasiriamali

0

Wanawake 150  wajane na wanaoishi katika mazingira magumu katika wilaya ya Temeke jijini Dar Es Salaam wamejikwamua kiuchumi kupitia mradi wa kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi –IWAPOA.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake jijini Dar Es Salaam, Meneja mradi huo Vivian Komba amesema baadhi ya wanawake hao wameanzisha shughuli za ujasiriamali na wengine wamejiunga katika vikundi vya kifedha- VICOBA.

Amesema mradi huo umetekelezwa katika kata sita za wilaya ya Temeke na wanawake hao wamepewa mafunzo ya jinsi ya kuanzisha shughuli za ujasiriamali na kazi za mikono.

Mazingira bora ya biashara yasisitizwa

0

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu -Sera na Uratibu – Profesa Faustin Kamuzora amesema suala la kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na uwekezaji ni la lazima kwa sababu serikali ina hisa katika kila biashara inayoanzishwa nchini.

Akizungumza baada ya kikao cha kwanza cha kamati ya mazingira ya biashara  jijini Dar Es Salaam, Profesa Kamuzora ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati hiyo amesema mazingira bora ya biashara yataiwezesha sekta binafsi kuanzisha biashara nyingi na serikali kuongeza mapato.

Naye kaimu katibu mtendaji wa baraza la taifa la Biashara- TNB- Oliva Vegula amesema ni muhimu kwa sekta ya umma na sekta binafsi kushikamana na kushirikiana katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Mfanyakazi TRA Dodoma asimamishwa kazi

0

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA kumsimamisha kazi mfanyakazi wake mmoja katika Ofisi ya TRA mkoa wa Dodoma, kupisha uchunguzi wa kuhusika kwake na tuhuma zinazomkabili za kumbughudhi mfanyabiashara mmoja jijini humo.

Dkt. Kijaji, ametoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwenye mitaa ya jiji la Dodoma baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mfanyabiashara mmoja kwamba amekuwa akipokea simu za vitisho kutoka kwa mfanyakazi huyo akishirikiana na watu wengine wakimdai shilingi laki saba za kulipia mashine ya kutolea stakabadhi za kielektroniki -EFD la sivyo angefungiwa biashara yake.

Amewataka watendaji wa TRA nchini kote kufanya kazi kwa kuzingatia maadili yao ya kazi, kukadiria kodi kwa haki,  watumie lugha nzuri kwa wateja wao na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa wafanyabiashara katika masuala ya kodi badala ya kuwakadiria kodi kubwa.

Meneja wa TRA mkoa wa Dodoma, Thomas Masese ameahidi kutekeleza maagizo hayo na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai hayo.

Watanzania wasisitizwa kuthamini utamaduni

0

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe ameendelea kusisitiza kuwa lugha ni kielelezo na sehemu muhimu ya utambulisho wa Taifa lolote duniani.

Dkt Mwakyembe ametoa kauli hiyo jijini Dodoma katika hafla ya kuwatunuku vyeti vya utambuzi wataalamu 67 wa lugha ya kiswahili waliofuzu mafunzo ya muda mfupi yaliyoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).

“Taifa lolote lisilo na utamaduni wake ni taifa mfu, na sisi tunajivunia kwa kuwa na utamaduni hai ikiwemo lugha yetu ya Kiswahili”, amesema Dkt Mwakyembe.

Ameongeza kuwa lugha ya Kiswahili ni kitambulisho cha utamaduni wa Mtanzania , kwa kuwa ndiyo lugha inayowaunganisha watu katika shughuli mbalimbali za Kijamii, Kisiasa na kiuchumi.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa Consolata Mushi amesema kuwa mpaka sasa Baraza hilo limefanikiwa kutoa mafunzo kwa wataalamu 350 wa lugha ya Kiswahili ambapo jumla ya wataalamu 198 tayari wametunukiwa vyeti na wengine 98 wanatarajiwa kutunukiwa vyeti hivyo mwezi Disemba mwaka huu.

Amesema lengo la BAKITA ni kuwapa fursa wataalamu hao ili waweze kusajiliwa katika mfumo wa kanzi data ambayo tayari imesajili wataalamu 380 kwa ajili ya kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wageni ndani na nje ya nchi.