Man City yaendelea kushika usukani Ligi Kuu

0

Ligi Kuu ya England imeendelea usiku wa Disemba Nne mwaka huu  kwa kuchezwa michezo minne ambapo Manchester City  wameendelea kushikilia usukani baada ya kuifunga timu ya Watford mabao mawili kwa moja.

Mabao  hayo mawili yamefungwa na Leroy Sane na Riyad Mahrez na kuiwezesha Man City kuendelea kuongoza ligi hiyo kwa alama tano mbele ya Liverpool yenye alama 36.

Watford wakiwa nafasi ya 11 na alama 20, walifunga goli la kufutia machozi katika dakika za lala salama kabla ya mchezo kumalizika.

Katika  uwanja wa London,  timu ya Westham United ikiwa nyumbani,  imeitandika Cardiff City mabao matatu kwa moja.

Mchezaji Lucas Perez aliyengia kipindi cha pili alifunga mabao mawili kwenye dakika za  49 na 54,  huku goli la tatu likifungwa na mchezaji Michail Antonio  katika dakika ya 61 na Cardiff City yenyewe ilipata goli moja kwenye dakika za nyongeza kabla ya mchezo kumalizika.

Katika mchezo mwingine, timu ya Brighton imeibuka na ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Crystal Palace na AFC Bournemouth ikaitandika Huddersfield Town mabao mawili kwa moja.

 

SSRA yaendelea kutoa ufafanuzi kuhusu mafao ya watumishi

0

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) Dkt Irene Isaka amesema kuwa mkanganyiko unaotokea juu ya kanuni ya kukokotoa asilimia 25 ya mafao ya mkupuo kwa mtumishi baada ya kustaafu unatokana na lugha ya kitalaamu inayotumiwa kutoa elimu kwa wananchi na hivyo kutoeleweka kwa haraka.

Akitoa ufafanuzi huo jijini Dar es salaam, Dkt  Isaka amesema kuwa asilimia hiyo inatokana na mshahara wa mtumishi na siyo michango yake.

Kuhusu kipindi cha malipo kwa mtumishi aliyestaafu, Dkt Isaka amesema kuwa  mtumishi huyo atalipwa mafao yake kwa muda wote wa maisha yake.

Siku za hivi karibuni,  kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu kanuni maalumu inayotumika kukokotoa mafao ya wastaafu.

 

Watumishi wazembe wa kituo cha ukaguzi Kibaha kuondolewa

0

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina ameagiza kuondolewa mara moja kwa watumishi wa wanaosimamia kituo cha ukaguzi kilichopo Kibaha mkoani Pwani kwa kushindwa kusimamia rasilimali za sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Waziri Mpina ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati  wa kikao cha tathmini ya Operesheni Nzagamba awamu ya Pili iliyofanyika  kati ya mwezi Oktoba na Novemba mwaka huu kwa lengo la kuinua mchango wa sekta ya mifugo katika pato la Taifa.

Amesisitiza kuwa watumishi wasio waadilfu na wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao hawana nafasi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ndio maana ameagiza kuondolewa mara moja kwa watumishi wanaofanya kazi ya ukaguzi wa rasilimali katika kituo cha Kibaha.

Hata hivyo Waziri Mpina amewapongeza watumishi wote walioshiriki katika Operesheni Nzagamba awamu ya Pili  kwa kufanya kazi kubwa na kwa uzalendo , na kwamba wameonesha kuwa na uwezo wa kusimamia rasilimali za Taifa ili zitoe mchango stahiki katika pato la Taifa.

Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi pia ametumia kikao hicho cha tathmini ya Operesheni Nzagamba awamu ya Pili, kuwaasa Watumishi wa wizara hiyo na wa halmashauri nchini kuhakikisha wanasimamia kwa makini utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zote zinazosimamia biashara ya Mifugo na Mazao yake hususani mabadiliko ya Kanuni mpya iliyotolewa mwezi Agosti mwaka huu.

Watanzania watakiwa kushiriki kuimarisha Utawala Bora

0

Watanzania wametakiwa kushiriki katika kuimarisha Utawala Bora ili kutoa mchango wenye tija kwa maendeleo ya Taifa,  badala ya kuviachia jukumu hilo vyombo vinavyosimamia masuala ya utawala bora.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika wakati akizindua maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za binadamu kitaifa jijini Dodoma.

Amesema kuwa ili kuwa na utawala bora nchini, watanzania wote wanahusika, kwa maana ya wale waliopewa dhamana ya kusimamia utawala bora na wananchi wa kawaida, kwa kuwa wenye dhamana ya kusimamia utawala bora wanahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuchika, Mtanzania wa kawaida anatakiwa abadilike kimtazamo na kifikra kuhusu uzingatiaji wa maadili, nidhamu ya kazi, vita dhidi ya rushwa, haki za binadamu, uwazi na uwajibikaji, na kusisitiza kuwa mabadiliko hayo ndio yawe  utamaduni wa mtanzania wa kila siku.

Naye, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Mary Mwanjelwa ametoa wito kwa Watanzania kuwa wazalendo kwa kutanguliza maslahi ya umma kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Amesisitiza kuwa kupitia kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ya mwaka huu inayosema kuwa  Udhibiti wa Mgongano wa Maslahi, Nguzo Muhimu Kujenga Utawala Bora, ni vema kwa kila Mtanzania akatanguliza maslahi ya umma mbele badala ya maslahi binafsi ili kufikia lengo la uchumi wa kati wa viwanda kama inavyohimizwa na Rais John Magufuli.

Kwa upande wake Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Harold Nsekela amesema kuwa maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu kitaifa ni muhimu kwa kuwa yanahimiza na kukumbusha kuzingatia misingi ya maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, mapambano dhidi ya rushwa hasa kwa watumishi wa umma ambao jukumu lao kubwa ni kutoa huduma kwa wananchi.

Maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu kitaifa huratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lengo likiwa ni kuhamasisha uadilifu, uwazi, uwajibikaji na utawala bora nchini.

 

 

 

 

 

Rais Magufuli afanya teuzi

0

Rais Dkt. John Magufuli amemteua Balozi Luteni Jenerali Mstaafu Wyjones Kisamba kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumbu.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema Balozi Kisamba anachukua nafasi ya Profesa Burton Mwamila ambaye amemaliza muda wake.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amemteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza Mbaraka Semwanza kuwa Kamishna wa Utawala na Fedha katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Semwanza anachukua nafasi ya Michael Shija ambaye amestaafu.

Uteuzi wa viongozi hao umeanza leo.

Tume ya Utumishi wa Umma yapata viongozi

0

Rais John Magufuli amemteua Jaji Mstaafu Steven Bwana kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa kipindi cha miaka mitatu.

Pamoja na kumteua Mwenyekiti wa Tume, Rais Magufuli pia amewateua Makamishna watano wa Tume ya Utumishi wa Umma.

Walioteuliwa ni
George Yambesi, Balozi Mstaafu John Haule, Immaculate Ngwale, Yahaya Mbila na Balozi Mstaafu Daniel Ole Njoolay.

Uteuzi huo wa Mwenyekiti na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma umeanza Novemba 22 mwaka huu.

Ahmed Msangi sasa Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini

0

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,-Simon Sirro amefanya mabadiliko ndani ya jeshi hilo, lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi.

Miongoni mwa mabadiliko hayo,  IGP Sirro amemteua Ahmed Msangi kuwa msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini kuchukua nafasi ya Barnabas Mwakalukwa.

 

 

Ufaransa kutoongeza kodi ya mafuta

0

Waziri Mkuu wa Ufaransa, – Edouard Philippe anatarajiwa kutangaza uamuzi wa serikali ya nchi hiyo wa kubatilisha mpango wake wa kuongeza kodi kwenye mafuta, ongezeko lililokua lianze Januari Mosi mwaka 2019.

Uamuzi huo wa serikali ya Ufaransa umelenga kutuliza ghasia pamoja na maandamano ya takribani wiki mbili  yanayofanywa na wanaharakati ili kupinga ongezeko hilo la kodi.

Ghasia na maandamano  hayo nchini Ufaransa yalianza mwezi Novemba mwaka huu baada ya serikali ya nchi hiyo kutangaza azma yake ya kuongeza kodi ya mafuta ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupambana na mabadiliko ya Tabia Nchi.