Mashindano ya Taifa ya Baseball yaanza Dar es salaam

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza mchezo wa Baseball uwe katika mfumo rasmi na kuchezwa katika mashindano mbalimbali ya Kitaifa nchini yakiwemo mashindano ya michezo kwa shule za msingi UMITASHUMTA na ya shule za sekondari  UMISSETA.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo jijini Dar es salaam wakati akizindua uwanja  na mashindano ya Taifa ya Baseball katika viwanja vya shule ya sekondari ya Azania.

Kwa upande wake waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison  Mwakyembe amesema kuwa wizara yake na idara zilizo chini yake kwa kushirikiana na wizara nyingine zinazohusika na Elimu, watahakikisha kufikia mwaka 2019 mchezo huo wa Baseball unarasimishwa na kuwa katika mfumo rasmi nchini.

Uwanja huo wa mashindano ya Taifa ya Baseball uliopo katika viwanja vya shule ya sekondari ya Azania, umejengwa kwa msaada wa serikali ya Japan kwa gharama ya zaidi ya Dola Elfu 80  za Kimarekani ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 180 za Kitanzania.

Mashindano hayo ya Taifa ya Baseball yanafanyika kuanzia leo Disemba Sita hadi  Tisa kwenye viwanja hivyo vya shule ya sekondari ya Azania ambapo timu 14 kutoka mikoa 11 nchini zinashiriki.

Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha Baseball na Softball nchini Hellen Sima, mashindano hayo yatatumika kupata wachezaji nyota wa Timu ya Taifa ya wanaume na wanawake, watakaopeperusha bendera ya Taifa katika kampeni ya kusaka tiketi ya kufuzu michuano ya Olimpiki ya mwaka  2020 itakayofanyika nchini Japan.

Mourinho awasifu wachezaji wake

0

Kocha wa timu ya Manchester United, – Jose Mourinho amesema kuwa wachezaji wa timu hiyo walijituma kwa kiwango cha juu katika mchezo wao dhidi ya Arsenal uliomalizika kwa sare ya mabao mawili kwa mawili.

Amesema kuwa mchezo  huo  katika Ligi Kuu ya England uliopigwa kwenye dimba la Old Trafford ulikua ukisubiriwa kwa hamu kubwa  na mashabiki kote duniani, hivyo ilikua ni lazima kucheza kufa na kupona ili kuweza kupata matokeo mazuri.

Kwa siku kadhaa kabla ya mpambana huo, mashabiki wa pande zote mbili za timu ya Manchester United na Arsenal walikua wakitambiana ambapo kila upande ulijinasibu kushinda.

Arsenal ndio walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza katika dakika ya 26 kupitia kwa mchezaji wake  Shkodran Mustafi na dakika nne baadae Man U wakasawazisha kupitia kwa mchezaji Anthony Martial ambapo  hadi dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza zinamalizika timu hizo zilitoka sare ya bao  moja kwa moja.

Katika kipindi cha pili,  mchezaji Alexandre Lacazette wa Arsenal  alifunga goli la pili kwenye dakika 68, lakini ndani ya dakika moja mchezaji wa Jesse Lingard akasawazisha.

Kwa sare hiyo, Arsenal imefikisha alama 31 ikiwa nafasi ya tano huku Man U ikifikisha alama 23 na kuwa nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu England inayoongozwa na Manchester City.

Nayo Wolverhampton Wanderers imeiduwaza Chelsea baada ya kuitandika mabao mawili kwa moja.

Chelsea ndiyo ilikuwa ya kwanza kupachika bao kupitia kwa Ruben Loftus-Cheek katika  dakika ya 18 mchezo huo.

Wolves walipambana katika kipindi cha pili ambapo walisawazisha dakika ya 59 kupitia kwa Raul Jimenez,  lakini Diogo Jota akapeleka kilio Chelsea  katika dakika ya 63  baada ya kupachika goli la ushindi.

Liverpool nao wakiwa ugenini wameendeleza wimbi la ushindi baada ya kuitandika Burnely magoli matatu kwa moja.

Burnely ndio walikuwa wa kwanza kupachika goli la kuongoza kwenye dakika ya 54 kupitia kwa mchezaji Jack Cork.

Liverpool wakapambana kuondoa aibu wakasawazisha kupitia kwa Roberto Firmino  na magoli ya mawili ya ushindi yakafungwa na wachezaji James Milner  na Xherdan Shaqiri.

Liverpool wanaendelea kushikilia nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya  England wakiwa na alama 39.

Tanzania kinara kwa kuvutia wawekezaji

0

 

Tanzania imeendela kuweka rekodi ya  kuvutia wawekezaji kwa nchi zilizopo ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa na mtaji wa uwekezaji wa Dola Bilioni 1.18 za Kimarekani ikifuatiwa na Uganda wenye uwekezaji wa Dola Milioni 700 za Kimarekani.

Akizungumza na waandishi wa habari  Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu  wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) Godffrey Mwambe amesema kuwa Kenya inashika nafasi ya Tatu ikiwa na uwekezaji wa Dola Milioni 670 za Kimarekani.

Mwambe amesema kuwa Tanzania inaongoza kwa kuvutia wawekezaji kutokana  na mapinduzi makubwa yaliyofanywa na serikali ambapo hadi sasa imewekeza jumla ya miradi mipya 905 katika sekta mbalimbali, miradi ambayo itatengeneza ajira 115,055 kwa watanzania na kuleta tija na manufaa kwa Taifa.

Ametolea mfano miradi mikubwa iliyowekezwa nchini kuwa ni pamoja na kiwanda cha Goodwill Ceremics Ltd kilichopo Mkuranga mkoani Pwani kinachojihusisha na utegenezaji vigae ambacho kimewekeza jumla ya Dola milioni 53 za Kimarekani na kutoa ajira za moja kwa moja 1500 kwa Watanzania na ajira zisizo za moja kwa moja 3,000.

“Viwanda vingine ambavyo vimeiwezesha Tanzania kuwa kinara wa kuvutia wawekezaji ni KEDA (Twyford) Tanzania ceramic Ltd pia ni cha kutengeneza marumaru na hiki ni kikubwa zaidi kina mtaji wa Dola za kimarekani milioni 56, kimetoa ajira  za moja kwa moja zipatazo 2,000 kwa watanzania na  ajira zisizo za moja kwa moja 4,000” amesema Mwambe.

Mkurugenzi Mkuu  huyo wa Kituo cha Uwekezaji Nchini ametaja nchi zinazoongoza kwa kuwekeza Tanzania kuwa ni pamoja na China, Uingereza  na Marekani.

Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi wakutana Dodoma

0

Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini wametakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na kuwa wazalendo na wabunifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Rai hiyo imetolewa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji wakati akifungua Kongamano la Tisa la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini.

Amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa kuna viashiria vya rushwa kwenye miradi ya umma, na hivyo kuwataka wataalamu wa manunuzi na ugavi kuepuka vitendo hivyo.

Dkt Kijaji amesema kuwa program na miradi mingi ya serikali haiwezi kufanyika bila kuhusisha ununuzi na ugavi na kuwataka wataalamu hao kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa ujuzi na weledi.

Kuhusu ujenzi wa Tanzania ya viwanda, Dkt Kijaji amesema kuwa viwanda vitachochea utoaji wa ajira, ongezeko la pato la Taifa, pato la mtu mmoja mmoja na kufanya maisha ya Watanzania kuwa bora zaidi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini  Dkt Hellen Bandiho amesema kuwa hadi kufikia Disemba Mosi mwaka huu, Bodi hiyo imesajili jumla ya wataalamu 10,863 katika ngazi mbalimbali za ununuzi na ugavi.

Kongamano  hilo la Tisa la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini linafanyika kwa muda wa siku tatu  na kuhudhuriwa na washiriki kutoka mikoa yote ya Tanzania.

 

 

Sakata la mauaji ya Kashoggi laendelea

0

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Uturuki amewasilisha ombi la hati ya kukamatwa kwa viongozi wawili wa ngazi za juu nchini Saudi Arabia kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha mwandishi wa habari maarufu wa  Saudi Arabia, – Jamal Kashoggi.

Miongoni mwa watu wanaotuhumiwa kuhusika na kifo cha Kashoggi, na ambaye ameorodheshwa katika hati hiyo ya kukamatwa ni aliyekuwa mkuu wa masuala ya Kiintelijensia wa Saudi Arabia, Ahmed Al Siri na mshauri wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo  Saud Al Kathani.

Watu hao wanatuhumiwa kupanga mauaji ya Kashoggi mwezi Oktoba mwaka huu mjini Istanbul nchini Uturuki kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia.

 

Houthi wasema wako tayari kwa mazungumzo

0

Wawakilishi wa Wanamgambo wa Houthi wa nchini Yemen wamewasili nchini Sweden kwa ajili ya mazungumzo ya amani ya nchi yao.

Wawakilishi hao wamesema kuwa wako tayari kujadiliana kuhusu masuala kadhaa ya nchi yao ikiwa ni pamoja na kutafuta njia zitakazowezesha misaada ya kibinadamu kuwafikiwa walengwa wakati Yemen ikiwa katika vita.

Wanamgambo hao  wa Houthi wanashikilia sehemu kubwa ya nchi ya Yemen, wakati serikali iliyoko madarakani ikiendesha shughuli zake uhamishoni.

 Majeshi ya Saudi Arabia yakishirikiana na majeshi ya nchi washirika yamekuwa yakiwashambulia Wanamgambo hao wa  Houthi kwa lengo la kuisaidia serikali iliyopo madarakani.

Serikali yatoa kipaumbele matumizi ya TEHAMA

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za serikali za kila siku.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya utoaji tuzo za mashindano ya TEHAMA yaliyoandaliwa na kampuni ya HUAWEI upande wa Tanzania kupitia programu yake ya Seed of the Future.

Ametumia hafla hiyo kuwaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii nchini na kuwataka Watanzania wote kutumia vizuri  mitandao hiyo kwenye shughuli za maendeleo.

“Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache,  ni vema wakatumia mitandao hiyo kwa kuhamasishana mambo mema zikiwemo shughuli mbalimbali za maendeleo, na kwa wataokiuka sheria ipo na inaendelea kufanya kazi,”amesisitiza Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, matumizi ya TEHAMA yataongeza ufanisi katika kuwahudumia ipasavyo wananchi, mfano katika sekta ya elimu  ambapo mwalimu mmoja anaweza kufundisha wanafunzi wengi kutoka katika shule tofauti kwa wakati mmoja.

Amesema kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kutekeleza kwa vitendo azma ya kuwapatia wananchi maendeleo hususani waishio maeneo ya vijijini huduma bora na kwa wakati.

Ameipongeza kampuni  hiyo ya HUAWEI kwa uzinduzi wa program hiyo ya Seed of the Future ambayo inalengo la kuwajengea uwezo wa TEHAMA wanafunzi mbalimbali nchini katika hatua za awali.

Mashindano hayo ya TEHAMA ya HUAWEI yalianzishwa mwaka 2015 na baadaye mwaka 2016 yakazinduliwa Afrika Kusini, ambapo hadi kufikia mwaka 2017, wanafunzi  Elfu 40  walikua wameshiriki.

Kwa upande wa Tanzania mashindano hayo yamezinduliwa mwaka huu, ambapo wanafunzi 500 walishiriki na baadaye kubaki 50.

Miongoni mwa wanafunzi hao 50, saba ndio waliokabidhiwa tuzo, na watatu   kati yao wamepata fursa ya kushiriki hatua inayofuata ya mashindano hayo nchini Afrika Kusini.

 

Mzee Mwinyi alazwa hospitalini, Rais amjulia hali

0

Rais John Magufuli amemtembelea na kumjulia hali Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi ambaye amelazwa hospitalini.

Pamoja na kumjulia hali, Rais Magufuli pia  ameshiriki dua ya kumuombea afya njema iliyoongozwa na familia ya Mzee Mwinyi.