Msangi aitembelea TBC

0

Jeshi la Polisi Nchini limejipanga kudhibiti vitendo vya uhalifu katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka za Krismasi na Mwaka Mpya na kuwaomba Watanzania wote kushirikiana na Jeshi hilo ili kuwafichua  wahalifu kwenye maeneo mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, – Ahmed Msangi alipofanya ziara ya kutembelea ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) eneo la Mikocheni jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa Jeshi hilo lipo imara katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, kufuatia elimu ya usalama barabarani inayotolewa na Jeshi hilo mara kwa mara,  ajali za barabarani zimepungua kwa kiasi kikubwa kuanzia mwezi Januari hadi Oktoba mwaka huu na kutaka kuzingatiwa kwa sheria za usalama barabarani kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu za mwisho wa mwaka .

Ziara hiyo ya Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini katika Shirika la Utangazaji Tanzania, ilikua na lengo la kujitambulisha baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.

Wadau wa afya wakutana Dar es salaam

0

Chuo Kikuu cha Aga Khan kina mpango wa kuandaa mapendekezo yatakayowasilishwa kwenye mamlaka husika ili kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto katika maeneo mbalimbali nchini.

Hayo yamebainika jijini Dar es salaam wakati wa mkutano ulioshirikisha wadau mbalimbali wa afya ya uzazi, mkutano uliokua na lengo la kuandaa mapendekezo hayo.

Akizungumza kando ya mkutano huo, Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan Dkt Lucy Hwai ameiomba serikali kuhakikisha madaktari bingwa wa masuala ya uzazi wanapelekwa katika maeneo ya vijijini ambako kuna vifo vingi vya mama na mtoto ili kusaidia kupunguza vifo hivyo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa afya ya uzazi na mtoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,  -Makuwami Mohamed amesema kuwa ushirikiano baina ya sekta binafsi na serikali ni muhimu katika kupunguza vifo hivyo vya mama na mtoto.

Rais Magufuli afanya uteuzi

0

Rais Dkt. John Magufuli amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa taasisi za umma.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema walioteuliwa ni  Pius Msekwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya na Zakia Meghji kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho.

Halikadhalika Rais Magufuli amemteua Profesa Esnati Chaggu kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira –NEMC, Dkt. Samwel Gwamaka kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC.

Wengine walioteuliwa ni Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa –STAMICO, Profesa Gaspar Mhinzi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli – PURA.

Uteuzi wa viongozi hawa umeanza leo tarehe 06 Desemba, 2018.

Benki ya Azania yafungua tawi Dodoma

0

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji amezitaka Benki nchini kushusha viwango vya riba za mikopo ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi wakiwemo wakulima kunufaika na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi hizo kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Dkt Kijaji ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifungua rasmi Benki ya Azania tawi la Sokoine na kusisitiza kuwa benki zina nafasi kubwa ya kuisaidia nchi kufikia azma yake ya kuwa ya viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa kukuza mitaji ya wananchi.

Amesema kuwa hivi karibuni Serikali imechukua hatua madhubuti za kiutawala na kisera ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo katika soko zinapungua.

Amezitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na serikali kuwa ni kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara, kushusha riba kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0 na kupunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0, hatua ambazo zimesaidia kupunguza riba katika soko kutoka wastani wa zaidi ya asilimia 20 hadi asilimia 17.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, – Charles Itembe amesema kuwa benki hiyo imeendelea kufanya vizuri katika soko kwa kupata faida na kwamba imejipanga kutoa mikopo na huduma za kifedha kwa wananchi mkoani Dodoma kwa viwango vya juu.

Rais Magufuli ateta na Mwang’onda

0

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu Mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa Apson Mwang’onda Ikulu jijini Dar es salaam.

Baada ya mazungumzo hayo, Mwang’onda amemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali ombi lake la kumuona na kuzungumza nae na amempongeza kwa uongozi mzuri unaochochea kasi ya maendeleo hususani katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Mwang’onda ameitaja baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa chini ya serikali ya Rais Magufuli kuwa ni ule wa uzalishaji wa umeme katika mto Rufiji na ujenzi wa madaraja na barabara ambazo licha ya kurahisisha usafiri zitasaidia kuondoa msongamano wa magari katika jiji la Dar es salaam.

“Mabadiliko ni makubwa sana ambayo yametokea, kuna miradi mikubwa mingi inafanyika sasa hivi, kwa hiyo mabadiliko ni makubwa kusema kweli na yote hayo ni kwa manufaa ya nchi, kwa hiyo nachoweza kusema amefanya kazi kubwa kwa maendeleo ya nchi”, amesema Mkurugenzi Mkuu huyo Mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Apson Mwang’onda.

Ametoa wito kwa Watanzania wote kushirikiana na serikali ili iweze kutekeleza mipango yake kwa ufanisi na kwa manufaa ya Taifa.

Myanmar kuridhia uwepo wa Casino

0

Nchi ya Myanmar iko katika hatua za mwisho za kuridhia maeneo ya starehe maarufu kama Casino, ambako vitendo mbalimbali vinavyowahusu watu wazima peke yako vinaruhusiwa kufanyika.

Awali maeneo ya Casino yalikuwa ni marufuku nchini humo, lakini hivi sasa ujenzi wa majengo yatakayokuwa yakitumiwa kwa shughuli za Casino yanaendelea kujengwa kwa kasi na huenda yakafunguliwa wakati wowote kuanzia sasa.

Wajenzi wa Casino hizo ni kutoka nchini China na baadhi ya raia wa Myanmar wamesema kuwa zitawapatia matumaini mapya ya ajira, kwani ajira ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayolikabili taifa hilo.

Wakimbizi wasubiri kuingia Marekani

0

Wakimbizi kutoka nchi za Amerika ya Kati hasa Honduras walioko njiani kwenda Marekani kutafuta maisha mazuri wamesema kuwa, wana matumaini ya kupata ridhaa ya kuingia nchini humo licha ya vikwazo vingi.

Wakimbizi hao wamesema kuwa matumaini yao yote yako nchini Marekani, kwani katika nchi wanazotoka wamekatishwa tamaa na mambo mbalimbali wakiwa hawana njia nyingine ya kujikimu.

Mkimbizi mmoja mwanamke mwenye mtoto mdogo, yeye amebainisha kuwa alikuwa akilazimishwa kuuza dawa za kulevya katika baa ili aweze kujitafutia maisha, la sivyo maisha yake yangekuwa hatarini.

Ameongeza kuwa amekuwa akiishi maisha ya kubahatisha na kwamba hata kama zoezi la kuingia nchini Marekani litakuwa refu atasubiri.

 

Mawaziri wa DRC na Uganda wakutana

0

Mawaziri wa afya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Uganda wamekutana  kwa dharura kwa lengo la  kujadili namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola ambao tayari umesababisha vifo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Wakati wa mazungumzo yao yanayofanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Mawaziri hao pamoja na mambo mengine wanajadili namna ya kukabiliana na mlipuko mpya wa ugonjwa huo.

Tayari serikali ya Uganda imechukua hatua kwa kuanza kuwapatia chanjo wahudumu wa afya walioko mpakani mwa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Uganda imeamua kuwapatia chanjo wahudumu wake wa afya baada ya Umoja wa Mataifa kusema kuwa ugonjwa huo unaweza kusambaa hadi katika nchi zinazopakana na Jamhuri hiyo ya Kidemokrasi ya Kongo.

Hadi sasa, watu mia mbili na sitini na nane wamekufa baada ya kuugua Ebola  katika Jamhuri hiyo.