Viongozi wa mikoa watakiwa kusimamia nidhamu

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini kusimamia  kikamilifu nidhamu na maadili katika maeneo yao ili dhamira ya serikali kuendelea  kutoa huduma bora kwa wananchi itimie kwa wakati.

Akifunga mafunzo kwa  viongozi hao  jijini Dodoma, Waziri Jafo amesema kuwa jukumu la Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini ni kuhakikisha kuwa agenda ya serikali na ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatekelezwa kikamilifu kutokana na usimamizi wa nidhamu na uadilifu kote nchini.

“ Wakuu wa Mikoa kawekeni mkazo katika kusimamia masuala yanayolenga kuleta mageuzi katika maisha ya wananchi kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora zinazoendana na dhamira ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo”, amesisitiza Waziri Jafo.

Amesema kuwa dhamira ya serikali ni kuendelea kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa barabara katika majiji ya Arusha, Dar es salaam, Mwanza, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kuimarisha na kuongeza tija katika majiji husika kutokana na kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara.

Waziri Jafo pia amewataka viongozi hao kuhakikisha kuwa kero za wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati badala ya kusubiri viongozi wa kitaifa wafanye ziara katika maeneo husika na kutoa ufumbuzi .

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi   Profesa  Joseph Semboja  amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kujenga timu za utendaji na kuimarisha uwezo wa Wakuu hao wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini katika ngazi ya mikoa.

Amesema kuwa  viongozi hao wamejengewa uwezo ili waweze kuleta mageuzi makubwa katika utendaji wao na maeneo yao.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na kuratibiwa na Taasisi ya Uongozi pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa wakuu hao wa mikoa  na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini yamefanyika kwa muda wa siku tano Jijini Dodoma.

Mada mbalimbali zimewasilishwa wakati wa mafunzo hayo ikiwemo ile inayohusu dawa za Kulevya na namna serikali inavyofanya kazi.

 

 

 

 

Uturuki na Marekani kuimarisha uhusiano

0

Mkuu wa Shirika la Ujasusi la nchini  Uturuki, –  Hakan Fidan amekutana na kufanya mazungumzo na Wabunge wa  Bunge la Marekani pamoja na maafisa wa kijasusi wa nchi hiyo.

Lengo la mkutano huo ni kuimarisha uhusiano uliozorota mwaka 2017 baina ya Uturuki na Marekani, nchi ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya nchi za Magharibi (NATO).

Fidan ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki  amekutana na Wabunge hao wa Bunge la Marekani na kujadili masuala yanayohusu NATO na pia alitarajiwa kukutana na maafisa wa kijasusi  wa nchi hiyo.

Mauaji ya mwandishi wa habari wa Saudi Arabia, – Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo nchini Uturuki,  ni miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika mkutano huo wa Mkuu wa Shirika la Ujasusi la nchini  Uturuki  na Wabunge wa  Bunge la Marekani pamoja na maafisa wa kijasusi wa nchi hiyo.

Wabunge wa Bunge la Marekani wanataka kuiadhibu Saudi Arabia kwa mauaji hayo ya Khashoggi, licha ya uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani kuikingia kifua Saudia Arabia, nchi ambayo ni mshirika wake wa  muda mrefu.

 

Amnesty International yashutumu adhabu ya kifo kwa watoto

0

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu  la Amnesty International kuhusu adhabu ya kifo nchini Sudan Kusini imesema kuwa,  watoto ni miongoni wafungwa wanaonyongwa nchini humo.

Shirika hilo limesema kuwa watu saba  akiwamo mtoto mmoja  wamenyongwa na serikali ya Sudan katika kipindi cha kuanzia mwaka huu hadi hivi sasa,  idadi ambayo ni kubwa nchini humo tokea kuasisiwa kwake mwaka 2011.

Kwa mujibu wa Amnesty International, wafungwa wawili ambao walikuwa watoto walipohukumiwa walinyongwa mwaka 2017.

Kwa muda mrefu, Sudan Kusini imekua katika vita ya wenyewe kwa wenyewe hadi kulipofikiwa makubaliano ya amani hivi karibuni.

Makundi mbalimbali ya Wanamgambo nchini humo yalikuwa yakitumia maelfu ya watoto kama Askari, hali iliyosababisha watoto hao kukabiliwa na makosa mbalimbali.

Watoto 72 wapatiwa matibabu JKCI

0

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es salaam kwa kushirikiana na mradi wa Little Hearts wa nchini Saudi Arabia ambao ni moja ya miradi ya Afya iliyo ndani ya Taasisi ya Msaada ya Muntada yenye makao Makuu yake mjini London nchini Uingereza, wamefanya matibabu ya moyo kwa watoto 72.

Matibabu hayo yamefanyika katika kambi maalum ya siku Saba ya matibabu ya moyo kwa watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni pamoja na matundu na mishipa ya damu ya moyo kutopitisha damu vizuri.

Katika kambi hiyo iliyoanza Disemba Mosi mwaka huu, kati ya watoto 72 waliopatiwa matibabu, 43 wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na 29 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na hali zao zinaendelea vizuri.

Taarifa iliyotolewa na Taasisi hiyo ya Moyo Jakaya Kikwete imesema kuwa madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wamefanya upasuaji huo kwa kurekebisha valvu, kuziba matundu, kurekebisha mishipa ya moyo ambayo imekaa vibaya na kurekebisha mfumo wa uzungukaji wa damu katika moyo.

Taarifa hiyo imewataka wazazi na walezi nchini kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wao kwa kuwa magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni.

Uchaguzi wa Ubunge Temeke kufanyika Januari 2019

0

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Temeke mkoani Dar es salaam na kwenye kata 46 za Tanzania Bara.

Akitangaza kufanyika kwa uchaguzi huo,  Mwenyekiti wa NEC Jaji Semistocles Kaijage amesema kuwa uchaguzi huo utafanyika Januari 19 mwaka 2019 na fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kuanzia Disemba 14 hadi 20  mwaka huu.

“Uteuzi wa Wagombea utafanyika tarehe 20 Desemba mwaka huu, kampeni za uchaguzi zitafanyika kati ya tarehe 21 Desemba hadi tarehe 18 Januari mwaka 2019 na siku ya uchaguzi itakuwa ni tarehe 19 Januari mwaka 2019,” amesema Jaji Kaijage.

Ametoa wito kwa vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi nchini kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha uchaguzi huo mdogo.

Jaji Kaijage ameongeza kuwa uchaguzi huo mdogo katika nafasi ya udiwani utafanyika ndani ya halmashauri 28 zilizopo kwenye mikoa 14 ya Tanzania Bara.

Uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Temeke mkoani Dar es salaam unafanyika kufuatia kujiuzulu uanachama wa Chama Wananchi (CUF) kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo Abdalla Mtolea.

Rais Magufuli awatakia heri Watanzania siku ya Uhuru

0

Rais John Magufuli ametuma salamu kwa Watanzania wote katika kuadhimisha miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara, siku ya Jumapili Disemba Tisa.

Katika salamu zake, Rais Magufuli amewashukuru na kuwapongeza Wazee wote, wakiongozwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kufanikisha kupatikana kwa Uhuru wa Tanzania Bara na kwa Watanzania wote kwa kutimiza miaka hiyo 57 ya Uhuru wakiwa wamoja na nchi ikiwa na amani.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa Disemba Tisa itakuwa ni siku ya mapumziko na kwa kwamba shilingi bilioni moja zizotengwa hapo awali kwa ajili ya maadhimisho hayo zitatumika  kujenga hospitali ya Uhuru katika Jiji la Dodoma kama ilivyotangazwa na Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa na kuwataka Watanzania wote waitumie  siku hiyo kutafakari Uhuru uliopo, mahali walipotoka, walipo sasa na wanapoelekea.

Ameongeza kuwa amefarijika kuona katika kipindi cha miaka mitatu aliyokaa madarakani, serikali imefanikiwa kudumisha Amani, Umoja na Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar na juhudi za kukuza uchumi zikiendelea na kuiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi Tano ambazo uchumi wake unakua kwa kasi Barani Afrika.

Katika kuadhimisha miaka hiyo  57 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Rais Magufuli kwa mujibu wa Mamlaka aliyopewa,  ametoa msamaha kwa wafungwa 4,477,  ambapo kati yao 1,176 watatoka siku ya maadhimisho ya  siku ya Uhuru.

Msamaha huo unawahusu wafungwa wagonjwa, wazee kuanzia miaka 70 na zaidi, wafungwa wa kike walioingia gerezani wakiwa wajawazito, na waliongia na watoto wanaonyonya au wasionyonya pamoja na wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili.

 

Halikadhalika, Rais Magufuli ameamua wafungwa waliotumikia robo ya adhabu zao, wapunguziwe robo ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa kwenye Kifungu cha  49 (1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58.

Hata hivyo, msamaha huo hautawahusu wafungwa wanaotumikia baadhi ya adhabu zikiwemo za kunyongwa, kifungo cha maisha, biashara ya dawa za kulevya na binadamu, makosa ya unyang’anyi, kukutwa na viungo vya binadamu, makosa ya kupatikana na silaha, risasi, milipuko isivyo halali, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka, kulawiti na makosa  kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Wafungwa wengine ambao hawahusiki na msamaha huo wa Rais ni wale wa makosa ya uhujumu uchumi, rushwa, ubadhirifu, ujangili, waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msamaha wa Rais, wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole, wenye makosa ya kutoroka au kujaribu ama kusaidia kutoroka chini ya ulinzi halali, walioingia gerezani baada ya Disemba Mosi mwaka huu  au waliowahi kufungwa na kurudi tena gerezani pamoja na wenye makosa ya kinadhamu magerezani.

 

 

 

Jumuiya ya Sharjah yakaribishwa kuwekeza Zanzibar

0

Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein ameikaribisha Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Sharjah kuzichangamkia fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar.

Dkt Shein ametoa kauli hiyo Ikulu mjini Zanzibar alipofanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Sharjah,  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Al Rawabi, – Abdallah Sultan Owais akiwa pamoja na baadhi ya viongozi wa Jumuiya hiyo.

Wakati wa mazungumzo hayo, Dkt  Shein amemueleza Mwenyekiti huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), tayari imeweka mazingira mazuri ya kuwekeza huko Zanzibar na kusisitiza kuwa milango ya uwekezaji iko wazi.

 

Amesema kuwa Zanzibar ina fursa nyingi za kuwekeza katika sekta mbalimbali,  ikiwemo ile utalii, viwanda, ufugaji na nyinginezo ambazo Jumuiya hiyo  ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Sharjah ina uzoefu.

Mbali ya kuitaka Jumuiya hiyo kuwekeza Zanzibar, Rais Shein pia amesisitiza umuhimu wa  kuwepo kwa ushirikiano na Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Zanzibar na kusisitiza kuwa Zanzibar iko tayari kufanya kazi na Jumuiya hiyo.

Ametumia fursa hiyo kupongeza mafanikio yaliofikiwa Jumuiya hiyo ya Sharjah ambayo aliitembelea mwezi Januari mwaka huu wakati alipokuwa katika ziara yake kwenye nchi za Jumuiya ya Falme za Kiarabu (UAE).

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Sharjah, – Abdallah Sultan Owais ameeleza kuvutiwa na mazingira ya Zanzibar na amemuahidi Rais Shein kuwa Jumuiya hiyo itahakikisha inaimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria baina ya pande hizo mbili.

 

 

Waziri Mkuu asisitiza Korosho zote zitanunuliwa

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia wakulima wa korosho nchini kuwa korosho zao zote zitanunuliwa.

Akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha korosho cha Terra kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani akiwa njiani kuelekea mkoani Dodoma,  Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza kuwa serikali kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko Nchini itanunua korosho zote na hakuna korosho za wakulima ambazo zitabaki bila ya kununuliwa.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Bodi hiyo ya Mazao Mchanganyiko Nchini  inaendelea kufanya tathmini na kujiridhisha kama kweli korosho hizo zimezalishwa nchini na kuangalia viwango vya ubora.

amesema kuwa hadi sasa zaidi ya Tani  Laki Moja na Elfu Themanini  za korosho  zimekwishakusanywa, na hivyo kuwataka wakulima wa zao hilo nchini waendelee kuiamini serikali kuwa itaendelea kununua korosho zao.

Akiwa katika kiwanda hicho cha korosho cha Terra kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani, Waziri Mkuu Mkuu Majaliwa  ameupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuunga mkono jitihada za serikali za kukuza uchumi kwa kupitia sekta viwanda.

Meneja Utawala wa kiwanda cha Korosho cha Terra, – Peter Ngwale amemweleza Waziri Mkuu kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kubangua Tani  Elfu Sita za korosho kwa mwaka.