Kima cha chini cha mshahara chaongezwa Ufaransa

0

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametangaza kushusha kodi na kuongeza kiwango cha kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi kwa kiasi cha Euro 100 kwa mwezi.

Akitangaza hatua hiyo katika hotuba yake ya kwanza tangu maandamano  yaanze nchini humo Macron amesema malipo kwa watumishi wanaofanya kazi kupita saa za kazi yataongezwa pamoja na kuboresha maslahi ya wastaafu.

Waziri Mkuu wa Ufaransa Eduado Phillipo ametangaza kusitishwa kwa maandamano hayo na kuweka ulinzi katika maeneo yote ya Paris.

May akutana na viongozi wa EU

0

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amekutana na baadhi ya viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya – EU kwa mazungumzo rasmi kuisaidia Uingereza kutoka katika Umoja huo.

May amekutana na Waziri Mkuu wa Holland Mark Rutte na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel baada ya kuahirisha kura ya kujitoa katika Umoja huo iliyokuwa ifanyike hii leo.

May amekuwa akipata shinikizo kutoka kwa wabunge wa bunge la Ulaya  kuhusu hatua yake ya kujitoa katika Umoja huo huku baadhi wakionyesha wazi kuwa watampinga wakati wa kura hiyo ya maoni.

Kampuni ya uchimbaji madini yapigwa stop

0

Naibu Waziri wa Madini Dotto Biteko ameiagiza kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya MMC inayofanya kazi katika kijiji cha Mangae na Mtipule wilayani Mvomero mkoani Morogoro kusimamisha uzalishaji hadi hapo watakapokamilisha taratibu za kisheria za madini.

Akikagua kazi zinazofanyika katika mgodi huo Naibu Waziri Biteko amesema kampuni hiyo inapaswa kuwalipa fidia wananchi walioondolewa katika eneo hilo.

Halikadhalika amewaonya baadhi ya watanzania wanaoingia mikataba na wawekezaji kutoka nje ambao hawafuati taratibu za nchi.

Mkuu wa wilaya ya Mvomero Mohamed Utali ameahidi kusimamia utekelezaji wa ulipwaji fidia wananchi huku mwakilishi wa kampuni ya MMC Daniel Augustino akisema watazifanyia kazi changamoto zilizojitokeza.

Madereva wanaotumia barabara za mwendokasi waonywa

0

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar Es Salaam limewatahadharisha madereva wanaotumia vyombo vya moto kuacha mara moja kutumia barabara za mabasi ya mwendo kasi ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.

Tahadhari hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar Es Salaam, Lazaro Mambosasa baada ya jeshi hilo kuwashikilia madereva wa pikipiki 20 kwa tuhuma za kulishambulia basi la mwendokasi na kusababisha uharibifu.

Kamanda Mambosasa pia amesema jeshi hilo linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kukutwa na vipande 20 vya meno ya tembo vyenye thamani ya shilingi Milioni 87.

Rais Magufuli atoa vitambulisho vya wajasiriamali

0

Rais Dkt. John Magufuli ametoa vitambulisho 670,000 maalum kwa wajasiriamali wadogo nchini ambao wana biashara zenye mtaji usiozidi shilingi milioni nne na kusema kupitia vitambulisho hivyo hakuna mtu atakayewanyanyasa wafanyabiashara wadogo.

Rais Magufuli amekabidhi vitambulisho hivyo jijini Dar es Salaam kwa wakuu wa mikoa na kuonya wafanyabiashara kuacha kufanya shughuli zao katika sehemu zitakazosababisha usumbufu kwa wengine.

Vitambulisho hivyo vimetolewa katika mkutano maalum baina ya Rais Magufuli na uongozi wa Mamlaka ya Mapato Nchini – TRA ambapo vitambulisho hivyo vimetolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI na vitatumika kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2019.

Watanzania waadhimisha miaka 57 ya Uhuru

0

Watanzania leo wanaadhimisha miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Uhuru uliopatikana Disemba Tisa mwaka 1961.

Katika kuadhimisha siku hiyo, Rais  John Magufuli kwa mujibu wa Mamlaka aliyopewa,  ametoa msamaha kwa wafungwa 4,477,  ambapo 1,176 kati yao wanatoka hii leo.

Msamaha huo unawahusu wafungwa wagonjwa, wazee kuanzia miaka 70 na zaidi, wafungwa wa kike walioingia gerezani wakiwa wajawazito, na waliongia na watoto wanaonyonya au wasionyonya pamoja na wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili.

Halikadhalika, Rais Magufuli ameamua wafungwa waliotumikia robo ya adhabu zao, wapunguziwe robo ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa kwenye Kifungu cha  49 (1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58.

Hata hivyo, msamaha huo hauwahusu wafungwa wanaotumikia baadhi ya adhabu zikiwemo za kunyongwa, kifungo cha maisha, biashara ya dawa za kulevya na binadamu, makosa ya unyang’anyi, kukutwa na viungo vya binadamu, makosa ya kupatikana na silaha, risasi, milipuko isivyo halali, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka, kulawiti na makosa  kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Wafungwa wengine ambao hawahusiki na msamaha huo wa Rais ni wale wa makosa ya uhujumu uchumi, rushwa, ubadhirifu, ujangili, waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msamaha wa Rais, wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole, wenye makosa ya kutoroka au kujaribu ama kusaidia kutoroka chini ya ulinzi halali, walioingia gerezani baada ya Disemba Mosi mwaka huu  au waliowahi kufungwa na kurudi tena gerezani pamoja na wenye makosa ya kinadhamu magerezani.

Serikali yaagiza kubanguliwa kwa korosho inazonunua

0

Serikali imeagiza korosho zote inazonunua kwa wakulima kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kuanza kubanguliwa nchini.

Agizo hilo la serikali limetolewa mkoani Mtwara na Waziri wa Kilimo, – Japhet Hasunga wakati akizungumza kwenye mkutano wa wamiliki wa viwanda vya kubangua korosho.

Waziri Hasunga amesema kuwa mkakati wa serikali ni kuwanufaisha wakulima nchini,  hivyo maamuzi ya kununua korosho ni sehemu ya maamuzi mema kwa manufaa ya wakulima wote.

Amesema kuwa wakati serikali inaendelea kukamilisha uhakiki wa wakulima wa korosho pamoja na kuendelea na malipo ya wakulima,  mpaka sasa tayari wakulima 77,380 wamekwishalipwa,  hivyo hakuna korosho itakayoruhusiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi bila utaratibu maalumu na badala yake korosho zote zitabanguliwa nchini.

Waziri huyo wa Kilimo amesisitiza kuwa korosho zitakazoruhusiwa kusafirishwa  nje ya nchi ni zile Tani 2,000 pekee zilizonunuliwa mnadani na kampuni mbili kwa utaratibu uliokuwa ukitumika awali.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Joseph Kakunda amesema kuwa serikali imedhamiria kuimarisha uchumi wa viwanda,  hivyo haitakubali kuhujumiwa inapoendelea kuboresha uwekezaji, uanzishaji na uendelezaji wa viwanda.

 

 

 

Sita wafa kwa kukanyagana Italia

0

Watu sita wamekufa na wengine hamsini wamejeruhiwa baada ya kukanyagana kufuatia kuzuka kwa taharuki katika tamasha la muziki wa kufokafoka kwenye klabu moja ya usiku nchini Italia.

Maafisa wa uokoaji na zimamoto nchini Italia wamesema kuwa tukio hilo limetokea alfajiri ya Jumamosi Disemba nane mwaka huu  katika klabu ya Lanterna Azzurra iliyopo kwenye mji wa Corinaldo.

Habari zaidi kutoka nchini Italia zinasema kuwa, watu hao waliokufa ni vijana wenye umri wa chini ya miaka 18 na kwamba wengi wa waliojeruhiwa hali zao ni mbaya.

Sababu za watu hao kukanyagana katika klabu hiyo ya usiku ya Lanterna Azzurra bado hazijafahamika, lakini taarifa za awali zinasema kuwa walikuwa wakijaribu kukimbia baada ya mtu mmoja kupuliza gesi ya kutoa machozi.