May kuungana na viongozi wa EU

0

Waziri Mkuu wa Uingereza, -Theresa May anatarajiwa kuungana na viongozi wa nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) huko Brussels nchini Ubelgiji kuhudhuria mkutano maalum wa kilele wa viongozi hao.

Akiwa Brussels , pamoja na mambo mengine, May anararajiwa kuwashawishi viongozi hao wa nchi Wanachama wa EU kulegeza msimamo wao kuhusu mchakato wa Uingereza wa kujiondoa kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit.

May anaungana na viongozi hao zikiwa zimepita saa kadhaa baada ya kunusurika katika kura ya kutokuwa na imani naye kutoka kwa wabunge wa chama chake cha Conservative baada ya kupata kura 200 dhidi ya 117.

Wabunge hao 200 wamepiga kura ya kumuunga mkono May ili aendelee kuwa kiongozi wa chama hicho  na Waziri Mkuu wa Uingereza.

Hata hivyo hali hiyo inamaanisha kuwa May amepoteza uungwaji mkono wa theluthi moja ya Wabunge kutoka chama chake na hivyo kuashiria bado anakabiliwa na changamoto kubwa katika kutekeleza mpango wake kuhusu mchakato wa Uingereza wa kujiondoa kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Kabla ya kura hiyo, May aliwaahidi wabunge wa chama chake cha Conservative kuwa hatawania tena muhula mwingine wa kukiongoza chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2022.

Kwa sasa May hawezi kukabiliwa na kura nyingine ya kutokuwa na imani naye kutoka kwenye chama chake kwa kipindi cha mwaka mmoja, lakini iwapo atashindwa katika kura ya wabunge wote 650 wa Uingereza mwezi Januari mwaka 2019, serikali yake inaweza kukabiliwa na kura ya kutokuwa na imani naye.

May aapa kutetea wadhifa wake

0

Waziri Mkuu wa Uingereza Thereza May amesema kuwa yuko tayari kupambana na changamoto zozote zitakazojitokeza wakati wa utawala wake.

Akihutubia Taifa kupitia vyombo vya habari nchini Uingereza, May amesema kuwa hakutakuwa na mpango wa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye wakati wa uongozi wake.

Kiongozi huyo wa Uingereza ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo kwa tetesi kuwa huenda Wabunge wa Bunge la nchi hiyo wakapiga kura ya kutokuwa na imani naye.

May ameapa kufanya kila linalowezekana kupigania kura  hiyo isipigwe na kwamba atabaki mjini London kupigania wadhifa wake na kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi ambayo amejitolea kuifanya.

Baadhi ya Wabunge wa Bunge la Uingereza wamekasirishwa na rasimu iliyotolewa na kiongozi huyo ya nchi yao ya kujitoa rasmi katika Umoja wa nchi za Ulaya.

Zaidi ya wabunge 48 wa chama chake Coservative wamewasilisha barua za kutokuwa na imani naye.

 

Rais Shein ataka kuenziwa kwa Kiswahili

0

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohammed Shein amesema kuwa kongamano la Kiswahili linaloendelea Mjini Zanzibar lina mchango mkubwa katika kuendeleza historia, maendeleo ya kiswahili pamoja na kuitambulisha Zanzibar kimataifa.

Akifungua kongamano la pili la Kimataifa la Kiswahili mjini Zanzibar, Dkt Shein amesema kuwa kongamano hilo linatoa fursa ya kuendeleza uhusiano kati ya wataalamu wa lugha hiyo ya kiswahili popote walipo duniani.

Amesema kuwa Zanzibar inatambulika duniani kote kuwa ndio chimbuko la lugha ya kiswahili fasaha kinachotokana na lahaja ya Kiunguja mjini ambayo ilipitishwa mwaka 1930, hivyo ni vema kongamano hilo likatumika kuiendeleza historia hiyo.

Amesisitiza kuwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume walikuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha lugha ya kiswahili, ndio maana kwa nyakati tofauti lugha hiyo ilitangazwa kuwa rasmi ya Taifa na Zanzibar mwaka 1964, pamoja na lugha ya Taifa la Tanzania mwaka 1967.

Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohammed Shein, ametumia ufunguzi wa kongamano hilo la pili la Kimataifa la Kiswahili, kutoa wito kwa vijana nchini wanaosoma masomo ya kiswahili katika vyuo vikuu mbalimbali nchini kuchangamkia fursa za ajira zilizopo katika nchi za Afrika Mashariki.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Dkt Mohamed Seif Khatib amesema kuwa ni wakati muafaka kwa serikali kusisitiza matumizi fasaha ya lugha ya kiswahili kwa kutambua kuwa ni bidhaa yenye thamani kubwa kiuchumi na kiutamaduni.

Kongamano hilo la pili la Kimataifa la Kiswahili linalofanyika kwa muda wa siku mbili, limeandaliwa na BAKIZA na kushirikisha wataalamu na mabingwa wa lugha ya kiswahili, watunzi wa vitabu, waandishi wa riwaya, tamthilia na mashairi, pamoja na wapenzi wa lugha ya kiswahili kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Serikali yataka mradi kukamilika kwa wakati

0

Serikali za Tanzania na Misri zimetiliana saini makubaliano ya ujenzi wa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa Megawati Elfu Mbili na Mia Moja katika maporomoko ya mto Rufiji.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutiliana saini makubaliano hayo Ikulu Jijini Dar es salaam, Rais John Magufuli ametoa wito kwa wadau wote wa mazingira nchini kuunga mkono mradi huo kwa kuwa ni muhimu katika utunzaji wa mazingira.

Amesisitiza kuwa moja ya mambo yaliyozingatiwa wakati wa uanzishwaji wa mradi huo ni kuhakikisha hakuna uharibifu wowote wa mazingira unaoweza kujitokeza na kwamba kama kuna taarifa zozote zilizosema kuwa mradi huo unasababisha uharibifu wa mazingira hazina ukweli wowote.

Rais Magufuli ameongeza kuwa mradi huo wa uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto Rufiji utakapokamilika, utasaidia nchi kuwa na umeme wa uhakika na kwa bei nafuu na hivyo kuchochea ukuaji wa viwanda nchini.

Amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ambaye ni Kampuni ya Arab Contractors kutoka nchini Misri kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliopangwa ambao ni miezi 36 na hata ikiwezekana kuufupisha muda huo.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, mara kwa mara amekua akizungumza kwa njia ya simu na Rais Abdel Fatah Al-Sisi wa Misri ambaye amemuhakikishia kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.

Rais Magufuli ametumia fursa hiyo kuiomba serikali ya Misri kujenga miradi mingine ya kuzalisha umeme katika maeneo mbalimbali nchini, kwa kuwa bado Tanzania ina vyanzo vingi kwa ajili ya kuzalisha umeme na inahitaji umeme zaidi.

Timu ya mazungumzo ya uanzishwaji wa mradi huo kwa upande wa Tanzania inaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Uchukuzi Dkt Leonard Chamuriho ambapo Rais Magufuli ametangaza kuwaongezea muda wa kustaafu wajumbe wote wa timu hiyo waliokua wastaafu mwaka huu na hivyo watastaafu baada ya kukamilika kwa mradi huo.

Dola Bilioni 2.9 za Kimarekani ambazo ni zaidi ya Shilingi Trilioni Sita za Kitanzania zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Hafla ya utiaji saini mkataba huo wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto Rufiji imehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Misri Dkt Mostafa Madbouly, Spika wa Bunge Job Ndugai na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma.

Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini akiwemo Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mtume na Nabii Josephat Mwingira wa Kanisa la Epatha na Sheikh Mohamed Rafik wamehudhuria hafla hiyo na kufanya sala.

Mkataba ujenzi wa mradi wa kufufua umeme wa maji kusainiwa

0

Mkataba wa ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa maji katika maporomoko ya mto Rufiji unasainiwa hii leo Ikulu jijini Dar Es Salaam.

Kabla ya utiaji saini mkataba huo viongozi wa dini mbalimbali akiwemo Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Mwingira wa Kanisa la Epatha, Sheikh Mohamed Rafik Turki wamefanya sala.

Mkandarasi kutoka nchini Misri anatarajiwa kujenga mradi huo.

Hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi huo imehudhuriwa na Rais Dkt. John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Misri Dkt. Mostafa Madbouly na viongozi wengine mbalimbali.

Machinga wajitokeza kupata vitambulisho

0

Zoezi la utoaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo maarufu Machinga limeanza jijini Dar Es Salaam ambapo limeonyesha mafanikio.

Katika awamu ya kwanza wajasiriamali wadogo elfu moja wamepatiwa vitambulisho hivyo katika wilaya za Kinondoni na Ilala huku matarajio yakiwa ni kuwafikia wajasiriamali zaidi ya elfu kumi na tano kila wilaya.

Wilayani Kinondoni Mkuu wa wilaya hiyo Daniel Chongolo amezindua vitambulisho hivyo kwa kuwasajili na kugawa vitambulisho hivyo kwa wafanyabiashara wadogo mia tano huku akisema wilaya hiyo imepanga kutoa  vitambulisho elfu kumi na nane ili kuwafikia wamachinga walioko  katika Manispaa ya Kinondoni.

Chongolo ametoa tahadhari kwa wafanyabiashara wakubwa watakaobainika  kufanya udanganyifu kwa lengo la kukwepa kodi.

Zoezi hili pia limeendelea katika wilaya ya Ilala jijini Dar Es Salaam ambapo katika wilaya hizo za jiji la Dar Es Salaam wajasiriamali wameonekana kujitokeza kwa wingi kupata vitambulisho hivyo.

Hapo jana Desemba 10 mwaka huu Rais John Magufuli alikabidhi vitambulisho 670,000 vya wajasiriamali wadogo kwa wakuu wa mikoa ili vigawanywe kwa wajasiriamali lengo ikiwa ni kuwawezesha kufanya kazi zao bila bugudha na kuwezesha serikali kupata kodi.

Wasimamizi wa uchaguzi watakiwa kuzingatia sheria

0

Tume ya Taifa ya Uchaguzi –NEC imewataka wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia kanuni, sheria  na miongozo ya uchaguzi wanaposimamia na kutekeleza majukumu ya uchaguzi.

Hayo yameelezwa na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Mery Longway katika ufunguzi wa mafunzo kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi yaliyofanyika mkoani Dodoma.

Amewakumbusha wasimamizi hao wa uchaguzi kuwa uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatiwa ndio msingi wa Uchaguzi kuwa huru wa haki na kupunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa Uchaguzi na hivyo kupunguza kesi mahakamani baada ya Uchaguzi.

Amesema kuwa pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo kuwa wazoefu katika kuendesha Uchaguzi washiriki hao wametakiwa kuhakikisha wanazingatia maelekezo watakayopewa na wakufunzi wa Tume, haitokuwa vyema kutekeleza majukumu hayo kwa mazoea bali wanatakiwa kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria na Kanuni zinazosimamia zoezi la Uchaguzi.

Washiriki wa Mafunzo hayo ni Wasimamizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo , Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo, Wasimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata ambao watasimamia Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Temeke na Udiwani katika kata 46  unotarajiwa kufanyika Januari 19 mwaka 2019.

Wajasiriamali waanza kupata vitambulisho

0

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewahakikishia wajasiriamali wadogo kupata vitambulisho vilivyotolewa na Rais John Magufuli na kuwataka wakuu wa wilaya na maafisa biashara kusimamia zoezi la ugawaji huku akionya dhidi ya udanganyifu wowote.

Mtaka amesema hayo wakati akikabidhi vitambulisho vya wajasiriamali wadogo kwa wakuu wa wilaya za mkoa wa Simiyu.

Amesema kuwepo kwa vitambulisho hivyo kutajenga uthubutu na ujasiri na kuwaibua wajasiriamali wapya huku akisisitiza kwamba mkoa wa Simiyu umejipanga kuwafikia wajasiriamali wanyonge kama ilivyokusudiwa na Rais Magufuli.

Baadhi ya wajasiriamali wamemshukuru Rais Magufuli kwa vitambulisho hivyo na kusema vitawaondolea adha waliyokuwa wakiipata.